29 Mar 2015Kwa muda mrefu, baadhi ya watumiaji wa mtandao wa kompyuta (Internet) wamekuwa na wakati mgumu kufuatia kushamiri kwa unyanyasaji mtandaoni, kwa kimombo CYBERBULLYING.

Kwa kiasi kikubwa, tatizo hili linaakisi tabia zetu nje ya mtandao. Mtu aliyezowea kunyanyasa wenzie mtaani, akiingia mtandaoni anaweza kuendeleza tabia hiyo kirahisi. Kadri mtandao unavyozidi kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku ,ndivyo unavyoakisi maisha yetu 'ya kawaida' nje ya mtandao. 

Kwa upande mwingine, mtandao unatoa fursa ya watu wenye tabia tofauti kukutana. Ndio maana si ajabu kukuta mtu mmoja akiweka bandiko kuhusu dini, mwingine akaweka bandiko kuhusu matusi.

Licha ya tabia, mtandao pia huwakutanisha watu wenye sifa tofauti: wapole na wakorofi, wapenda amani na wagomvi, wenye elimu na mbumbumbu, wenye aibu na wasio na mishipa ya aibu, nk. 

Kadhalika, mtandao unatoa fursa mbalimbali, nzuri na mbaya. Kwa mfano, mtandao unatuwezesha kuwa karibu na viongozi wa nyanja mbalimbali, kutoka mawaziri hadi viongozi wa taasisi binafsi.Uzuri wa fursa hiyo ni pamoja na kurahisisha mawasiliano baina ya watu wanaotoka 'madaraja' tofauti ya kijamii. Kadhalika, fursa hiyo inatuwezesha kujifunza kutoka kwao, sambamba na kufuatilia masuala mbalimbali ambayo kutokana na nafasi zao yanagusa maisha yetu binafsi au ya jamii kwa ujumla.

Fursa hiyo pia inatuwezesha kuwa karibu na watu mbalimbali, muhimu na wa kawaida. Katika mazingira ya kawaida, ni vigumu kufahamiana na Waziri, kwa mfano, labda kuwe na undugu, kufahamiana au mahusiano kikazi.

Hata hivyo, mtandao pia unatoa fursa 'mbaya.' Binadamu tupo tofauti, kuna wenzetu ambao wakiiona fursa wanaitumia kwa manufaa, lakini kuna wengine sio tu hawataki kujifunza 'mazuri' ya wenzao (ambayo wao hawana) pia hujenga chuki na jitihada za kuwachafua au kuwadhalilisha wenzao wenye 'mazuri.' Kwa mfano, unaweza kukutana na mtu ambaye hakubahatika kupata elimu ya kutosha, au hakusoma kabisa. Anapokutana na mwenye elimu kiasi au ya juu, badala ya kutumia fursa hiyo kama 'darasa nje ya shule' anaanzisha chuki na uhasama usio na manufaa.

Kama dunia ilivyo uwanja wa fujo, ndivyo ilivyo kwa mtandaoni. Kuna mazuri na mabaya. Kuna baadhi yetu ambao tumenufaika sana kwa uwepo wetu mtandaoni, kwa maana ya kutengeneza urafiki na watu muhimu, lakini pia kuna nyakati tumejikuta tukikutana na 'maadui.'

Ofkoz, mtandano sio sehemu ya kubadilisha mawazo, kujifunza au kuuliza maswali tu bali pia ni sehemu ya burudani. Utani ni ruksa lakini utani wenyewe usizidi kiwango. Na kanuni ya mtaani kuwa usimtanie mtu asiyekutania, ina-apply mtandaoni pia.

Kwa bahati mbaya kuna wenzetu ambao hulazimisha utani.Wengine huenda mbali zaidi kwa kulazimisha kumjua mtu zaidi ya anavyojijua yeye mwenyewe.

Kwa bahati nzuri, hatimaye serikali imesikia kilio dhidi ya unyanyasaji wa mtandaoni na Jumanne ijayo inatarajia kuwasilisha muswada kuhusu uhalifu wa mtandaoni ambao pamoja na mambo mengine unaharamisha unyanyasaji wa mtandaoni (cyberbullying) 

Katika muswada huo unajulikana kwa kimombo kama The Cyebrcrimes Act, 2015, ibara ya 23 inaharamisha unyanyasaji mtandaoni (cyberbullying) na kutaja adhabu husika. 

Muswada unafafanua maana ya cyberbullying, kwamba "mtu hataruhusiwa kuanzisha au kutuma mawasiliano ya kielektroniki kwa kutumia kompyuta kwa mtu mwingine kwa malengo ya 'kumsukuma kwa nguvu' (coerce), kumtisha, kumyanyasa au kumsababishia msongo wa mawazo, na mtu atakayekiuka kipengele hocho atakuwa anafanya kosa, na adhabu yake ni sio chini ya shilingi milioni tatu au kifungo cha sio chini ya mwaka mmoja au adhabu zote pamoja."  

Muswada kamili ni huu hapa chini (kwa bahati mbaya au makusudi, watawala wetu hawakuona umuhimu wa kuupatia tafsiri ya Kiswahili)Wakati muswada huu ni habari njema kwa wahanga wa unyanyaswaji mtandaoni, unatarajiwa pia angalau kupunguza kushamiri kwa matusi na picha zisizofaa mtandaoni. Sio siri kwamba baadhi ya mitandao ya kijamii, hususan Instagram, imegeuka uwanja wa matusi.

Kibaya zaidi, umahiri wa matusi umegeuka moja ya vyanzo vya umaarufu mtandaoni. Kama nilivyobainisha hapo juu,mtandao unatoa fursa 'mbaya' kwa wenzetu  wasio  na cha kuelimisha, kujadili au hata kujivunia hadharani, na matokeo yake ni kuwabughudhi watu wengine au kubandika picha zisizofaa kama mbinu ya kusaka sifa za kipuuzi.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbushana kuwa Tanzania yetu haina uhaba wa sheria.Tatizo kubwa ni katika kuziheshimu na kuzitekeleza. Twaweza kuwa na sheria kali dhidi ya uhalifu wa mtandaoni lakini utekelezaji ukiwa hafifu basi sheria hizo zitabaki maandiko tu vitabuni.

Kadhalika, ni muhimu kutahadharisha kwamba sheria hii ya uhalifu wa mtandaoni isitumiwe vibaya na serikali kuwanyima wananchi uhuru wa mawasiliano, au kibaya zaidi, kuitumia kwa minajili ya kuficha maovu na kuwalinda waovu. Sitarajii kuona sheria hii ikitumika iwapo chombo cha habari kitaibua utovu wa maadili wa kiongozi, kwa mfano.

Mwisho, ni matarajio yangu kuwa vitendo vya uhalifu wa mtandaoni, ikiwa ni pamoja na cyberbullying, vitapungua kufuatia sheria hii, iwapo itapitishwa na bunge. Angalau sasa, cyberbullies watafikiria mara mbili kabla ya kumwaga sumu zao kuwanyanyasa watu wasio na hatia.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.