12 Apr 2015

Wakati mitandao mbalimbali ya kijamii ikiendelea mjadala kuhusu sheria ya kudhibiti uhalifu wa mtandaoni (Cyber Crime Act 2015), ukweli mchungu unabaki kuwa uhalifu huo upo, na unaendelea kuwaathiri watu kila siku.

Jamii inaweza kuendelea kubishana hata kwa miaka 100 kama twahitaji sheria hiyo au la, lakini wahalifu wa mtandaoni wanaendelea kutusumbua kila kukicha. Wakati sheria hiyo haiwezi kumaliza kabisa tatizo la uhalifu wa mtandaoni, angalau kwa kiasi flani itasaidia kumfanya mhalifu atafakari mara mbili kuhusu madhara ya uhalifu wake pindi akikamatwa.

Na kama kuna eneo ambalo wahalifu wa mtandaoni hulipendelea zaidi ni wizi wa nywila, au kwa kimombo PASSWORD. Lakini kinachowafanya wahalifu hao kupendelea wizi wa nywila sio kwa vile wakifanikiwa kuiba watakuwa na 'control' ya akaunti yako bali pia ukweli kwamba watu wengi hufanya makosa wakati wanapofungua akaunti mtandaoni kwa kuchagua nywila dhaifu.

Pengine ushamsikia shushushu mmoja maarufu kabisa duniani aitwaye EDWARD SNOWDEN. Kama hujawahi kumsikia, basi ngoja nikuhabarishe.Huyu jamaa alikuwa anafanya kazi kama mchambuzi katika moja ya taasisi kubwa za ushushushu nchini mMarekani, inayojulikana kakma NSA, yaani National Security Agency. Hawa jamaa kazi yao ni kunasa mawasiliano- iwe ya email, simu au njia nyingine yoyote ile. Sasa Bwana Snowden, kwa kukerwa na ukiukwaji wa haki za binadamu uliokuwa unafanywa na mwajiri wake, akaamua kumwaga siri hadharani.Akawapatia wanahabari, hususan wa gazeti la Guardian la hapa Uingereza, data kibao zilizokuwa zikionyesha jinsi NSA ilivyokuwa ikiwapeleleza Wamarekani na watu wengike kibao duniani.

Sasa, kama ilivyo kawaida kwa taasisi za ushushushu, ukiweka hadharani madhambi yao unakuwa adui yao.Hivyo ilimlazimu Bwana Snowden kutoroka Marekani, na kwa sasa amepata hifadhi ya ukimbizi nchini Russia.

Siku nafasi ikiniruhusu nitaelezea kwa kirefu kuhusu mkasa wa shushushu huyu.Ila kwa leo nitazungumzia ushauri alioutoa hivi karibuni kuhusu nywila imara, itakayowapa kibarua wahalifu wa mtandaoni kuihujumu.

Snowden akiongea katika mahojiano na mtangazaji wa televisheni na mchekeshaji, John Oliver, alieleza kuwa nywila za watu wengi ni dhaifu mno kiasi kwamba inamgharimu mhalifu wa mtandaoni chini ya sekunde moja kuhujumu nywila yenye tarakimu nane.

"Nywila yangu ina tarakimu tano," alieleza Oliver. "Huo sio utani.Kwahiyo hiyo ni mbaya,sawa?" Snowden alikubaliana nae kwamba hiyo ni mbaya sana.

Kwahiyo watu wafanyeje kuhusu nywila zao? Wakati pendekezo la Oliver kuwa na nywila kama 'limpbiscuit4eva' lilionekana halifai,Snowden alikuwa na ushauri mzuri.Sahau kuhusu nywila zinazotumia maneno ya kawaida na badala yake tumia maneno marefu (paraphrases) ambayo ni rahisi kuyakumbuka, kwa mfano 'margaretthatcheris110%SEXY.' Mhalifu wa mtandaoni hawezi kuhisi neno kama hilo na wakati huohuo wewe utabaki na kumbukumbu ya neno hilo refu.


Kwa sie tunaotumia Kiswahili, ushauri wangu ni kujaribu kutumia mchanganyiko wa majina ya ndugu katika familia yenu na namba flani, bila kusahau herufi kubwa japo moja na tarakimu zisizo namba au herufi kama vile £ au % au $.

Unaonaje kama baada ya kusoma makala hii ukibadili nywila yako kuwa imara zaidi na hivyo kukuwezesha kukabiliana na jitihada za wahalifu wa mtandaoni kuihujumu nywila yako?0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.