14 Jul 2015


Nitakuwa siwatendei haki kwa kusema ASANTE au SHUKRANI pekee. Kwa hakika ni vigumu sana kupata neno/ maneno sahihi yenye kuonyesha shukrani za dhati kwa wema mkubwa uliofanyiwa. Labda niseme hivi: nawaombea Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa upendo mkubwa na sapoti kubwa kabisa mliyonipatia mie na familia ya Marehemu Mzee Philemon Chahali.

Ninyi sasa ni familia ya Mzee Chahali kwa sababu wengi wenu mlishirikia kumfanyia sala/dua ili apone lakini bahati mbaya akafariki, na mkajitokeza kwa wingi wenu kumlilia kwa salamu zenu za rambirambi lukuki. Sidhani kama kuna upendo mkubwa zaidi ya huo. 

Kitu kimoja nina hakika nacho ni kwamba japo sasa ni marehemu, Mzee Chahali ametuacha akithamini sana upendo wenu usiomithilika. Dua/sala alipokuwa anaumwa na salamu za rambirambi zitoka kwa zaidi ya watu 850 kwa ujumla wenu. Inawezekana idadi ni kubwa zaidi ya hiyo kwa sababu nilishindwa kuhesabu watu wote.

Historia fupi ya marehemu Mzee Chahali ni kama ifuatavyo, Alizaliwa Ifakara tarehe 22/11/1930 na kupata elimu yake katika zama za Ukoloni, kitu kilichomfanya athamini sana elimu kwa sie wanae. Baadaye alifunga ndoa na marehemu mama yetu Adelina Mapngo, ndoa iliyodumu hadi mama alipofariki Mei 2008, ikiwa imedumu kwa miaka 53. Katika uhai wake, baba na mama walijaaliwa kupata watoto tisa, japo mmoja alitangulia mbele ya haki na kwa sasa tumebaki wanane, wanaume sita na wanawake wawili.

Moja ya mafanikio makubwa katika maisha ya marehemu baba ni kuwa mmoja wa mapostamasta wa kwanza wazalendo baada ya uhuru. Kwangu binafsi, moja ya legacies za baba ni kunifanya nipende habari. Kwa kawaida, alipokuwa akitoka kazini alikuja na rundo la magazeti, aliyasoma kisha kutusimulia kilichomo katika magazeti hayo. Vilevile alihakikisha hakosi kusikia taarifa ya habari ya Redio Tanzania zama hizo, na vituo vya redio vya kimataifa kama vile BBC Swahili , Sauti ya Ujerumani na Voice of Amerika kila ilipowezekana. Ile tabia ya kusoma/kusikikia habari kisha kutusimulia hatimaye ilihamia kwangu ambapo kwa hakika ninashindwa kujizuwia kukutana na habari kisha nisiishirikieshe jamii aidha katika blogu hii au kwenye makala za Raia Mwema au kwenye tweet au Facebook.

Baada ya ujio wa televisheni, Mzee alikuwa akitumia muda mwingi kufuatilia habari. Na kila mara nilipompigia simu alikuwa akiniulizia kuhusu habari za kimataifa. Hofu yake kubwa ilikuwa katika maeneo mawili. Kwanza alikuwa anapata wasiwasi sana akiona kwenye TV kuhusu matishio ya ugaidi yanayozikabili nchi za Magharibi ikiwa pamoja na hapa Uingereza ninapoishi. Kingine ilikuwa ni wasiwasi wake kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na makala zangu magazetini hasa pale nilipoonekana nina msimamo mkali. Baba alipatwa na hofu kubwa aliposikia kwamba kwa wakati flani maisha yangu yalikuwa hatarini kutokana na tishio lililotoka huko nyumbani. Nilijitahidi sana kumpa matumaini lakini kwa hakika alikuwa na hofu kubwa hasa kila nilipokosa kufanya mawasiliano nae japo kwa siku chache.

Miongoni mwa vitu ninavyobaki ninasikitika kwa maana ya 'kumwangusha' marehemu baba ni, kwanza, kutotimiza lengo lake la mie kuwa padre. Nilipomaliza darasa la saba nilichaguliwa kujiunga na seminari ya Kasita huko Morogoro lakini pia nilikuwa nimefaulu kujiunga na sekondari ya serikali. Nikafuata moyo wangu, sikwenda seminari nikajiunga na sekondari ya serikali. Hilo lilimuumiza sana baba, lakini kwa bahatio nzuri alifanikiwa kumshawishi mdogo wangu wa kike na kumwingiza kwenye usista ambao anautumikia hadi leo.

Kingine ni faragha kidogo, ila kwa kifupi, ilinigharimu miaka kadhaa kabla sijamfahamisha nilikuwa ninafanya kazi gani nilipokuwa mtumishi wa umma huko Tanzania. Nilipomjulisha na kumfahamisha kwanini sikumweleza mapema, alinielewa. Lakini hapohapo nikawa nimemwanzishia hofu mpya akidhani kuwa kazi hiyo ilikuwa ya roho mkononi. Na hata aliposikia kuwa 'nimeachana na kazi hiyo,' baba alifanya sala kwenye simu kumshukuru Mungu akinieleza kuwa ilikuwa ikimyima amani rohoni.

Mzee Chahali alifariki tarehe 8/7/15 kutokana na mchanganyiko wa maradhi lakini kubwa likiwa tatizo la moyo. Hata hivyo, baada ya mkewe wa miaka 53- marehemu mama - kufariki mwaka 2008, mzee aliyekuwa na takriban miaka 10 zaidi ya mama, alishindwa kabisa kukabiliana na ukweli kuwa mkewe amemtangulia. Mara kadhaa nilipoongea nae alikuwa akimkumbuka mkewe na kutamani kuwa nae. Kimsingi, marehemu baba na marehemu mama walikuwa zaidi ya mke na mume. Walikuwa marafiki pia hasa kwa vile Mzee Chahali alikuwa mkimya sana na mwenye marafiki wachache. 

Sijui niwaelezeje kuhusu kifo hiki kilivyoniathiri binafsi. Baada ya mama kututoka, mzazi pekee tuliyebakiwa nae alikuwa baba. Sasa tumabaki yatima. Kwa hakika inauma sana.  Lakini yote ni kazi yaMungu.

Mzee Chahali amezikwa kwa heshima zote, ambapo kwa mji wetu wa kidini sana, misa ya mazishi kuendeshwa na Askofu ni heshima kubwa sana, na kwa hakika tunalishukuru sana jimbo la Mahenge kwa kumthamini Mzee wetu kiasi hicho.

Lajkini sijui kama leo hii ningekuwa katika nafasi ya kuandika makala hii bila sapoti yenu kubwa mno. Kila nilipotupa jicho Facebooka au Twitter nilikuta rundo la salamu za kumwombea dua/sala baba alipokuwa mgonjwa, na rundo kubwa zaidi baada ya kuwatangazia taarifa za msiba. Ninawashukuru sana sana sana. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki mno na awazidishie upendo wenu.

Jana nilibandika Makala Maalumu ya Sauti lakini kwa kutambua kuwa si kila mmoja ana muda au access ya kuskiliza audio filela takriban dakika 30 nikaona ni bora niziwasilishe tena salamu hizi za shukrani kwa maandishi.

Ninaomba mniruhusu nisimtaje kila mmoja wenu kwa sababu sio tu mpo wengi sana bali pia ukweli kwamba shukrani za dhati huwa moyoni. Naweza kujibaraguza hapa na sante zangu nyiiingi lakini moyoni nina mawazo mengine. Ila kwa hakika Mungu ndo shahidi wangu. Ninathamini mno mchango wenu wa hali na mali katika kumuuguza baba na kushiriki katika mazishi yake kwa njia ya rambirambi.

ASANTENI SANASANA SANA. SINA MANENO SAHIHI YA KUWAAMBIA LAKINI NINAWAOMBEA BARAKA TELE KUTOKA KWA MWENYEZI MUNGU.

Mwisho, Pumziko la Milele Bwana Mungu ajmjaalie Mzee Chahali, na mwanga wa milele amwangazie apumzike kwa amni, Ameni

ASANTENI SANA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.