Showing posts with label MSIBA. Show all posts
Showing posts with label MSIBA. Show all posts

14 Jul 2015


Nitakuwa siwatendei haki kwa kusema ASANTE au SHUKRANI pekee. Kwa hakika ni vigumu sana kupata neno/ maneno sahihi yenye kuonyesha shukrani za dhati kwa wema mkubwa uliofanyiwa. Labda niseme hivi: nawaombea Mwenyezi Mungu awabariki sana kwa upendo mkubwa na sapoti kubwa kabisa mliyonipatia mie na familia ya Marehemu Mzee Philemon Chahali.

Ninyi sasa ni familia ya Mzee Chahali kwa sababu wengi wenu mlishirikia kumfanyia sala/dua ili apone lakini bahati mbaya akafariki, na mkajitokeza kwa wingi wenu kumlilia kwa salamu zenu za rambirambi lukuki. Sidhani kama kuna upendo mkubwa zaidi ya huo. 

Kitu kimoja nina hakika nacho ni kwamba japo sasa ni marehemu, Mzee Chahali ametuacha akithamini sana upendo wenu usiomithilika. Dua/sala alipokuwa anaumwa na salamu za rambirambi zitoka kwa zaidi ya watu 850 kwa ujumla wenu. Inawezekana idadi ni kubwa zaidi ya hiyo kwa sababu nilishindwa kuhesabu watu wote.

Historia fupi ya marehemu Mzee Chahali ni kama ifuatavyo, Alizaliwa Ifakara tarehe 22/11/1930 na kupata elimu yake katika zama za Ukoloni, kitu kilichomfanya athamini sana elimu kwa sie wanae. Baadaye alifunga ndoa na marehemu mama yetu Adelina Mapngo, ndoa iliyodumu hadi mama alipofariki Mei 2008, ikiwa imedumu kwa miaka 53. Katika uhai wake, baba na mama walijaaliwa kupata watoto tisa, japo mmoja alitangulia mbele ya haki na kwa sasa tumebaki wanane, wanaume sita na wanawake wawili.

Moja ya mafanikio makubwa katika maisha ya marehemu baba ni kuwa mmoja wa mapostamasta wa kwanza wazalendo baada ya uhuru. Kwangu binafsi, moja ya legacies za baba ni kunifanya nipende habari. Kwa kawaida, alipokuwa akitoka kazini alikuja na rundo la magazeti, aliyasoma kisha kutusimulia kilichomo katika magazeti hayo. Vilevile alihakikisha hakosi kusikia taarifa ya habari ya Redio Tanzania zama hizo, na vituo vya redio vya kimataifa kama vile BBC Swahili , Sauti ya Ujerumani na Voice of Amerika kila ilipowezekana. Ile tabia ya kusoma/kusikikia habari kisha kutusimulia hatimaye ilihamia kwangu ambapo kwa hakika ninashindwa kujizuwia kukutana na habari kisha nisiishirikieshe jamii aidha katika blogu hii au kwenye makala za Raia Mwema au kwenye tweet au Facebook.

Baada ya ujio wa televisheni, Mzee alikuwa akitumia muda mwingi kufuatilia habari. Na kila mara nilipompigia simu alikuwa akiniulizia kuhusu habari za kimataifa. Hofu yake kubwa ilikuwa katika maeneo mawili. Kwanza alikuwa anapata wasiwasi sana akiona kwenye TV kuhusu matishio ya ugaidi yanayozikabili nchi za Magharibi ikiwa pamoja na hapa Uingereza ninapoishi. Kingine ilikuwa ni wasiwasi wake kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na makala zangu magazetini hasa pale nilipoonekana nina msimamo mkali. Baba alipatwa na hofu kubwa aliposikia kwamba kwa wakati flani maisha yangu yalikuwa hatarini kutokana na tishio lililotoka huko nyumbani. Nilijitahidi sana kumpa matumaini lakini kwa hakika alikuwa na hofu kubwa hasa kila nilipokosa kufanya mawasiliano nae japo kwa siku chache.

Miongoni mwa vitu ninavyobaki ninasikitika kwa maana ya 'kumwangusha' marehemu baba ni, kwanza, kutotimiza lengo lake la mie kuwa padre. Nilipomaliza darasa la saba nilichaguliwa kujiunga na seminari ya Kasita huko Morogoro lakini pia nilikuwa nimefaulu kujiunga na sekondari ya serikali. Nikafuata moyo wangu, sikwenda seminari nikajiunga na sekondari ya serikali. Hilo lilimuumiza sana baba, lakini kwa bahatio nzuri alifanikiwa kumshawishi mdogo wangu wa kike na kumwingiza kwenye usista ambao anautumikia hadi leo.

Kingine ni faragha kidogo, ila kwa kifupi, ilinigharimu miaka kadhaa kabla sijamfahamisha nilikuwa ninafanya kazi gani nilipokuwa mtumishi wa umma huko Tanzania. Nilipomjulisha na kumfahamisha kwanini sikumweleza mapema, alinielewa. Lakini hapohapo nikawa nimemwanzishia hofu mpya akidhani kuwa kazi hiyo ilikuwa ya roho mkononi. Na hata aliposikia kuwa 'nimeachana na kazi hiyo,' baba alifanya sala kwenye simu kumshukuru Mungu akinieleza kuwa ilikuwa ikimyima amani rohoni.

Mzee Chahali alifariki tarehe 8/7/15 kutokana na mchanganyiko wa maradhi lakini kubwa likiwa tatizo la moyo. Hata hivyo, baada ya mkewe wa miaka 53- marehemu mama - kufariki mwaka 2008, mzee aliyekuwa na takriban miaka 10 zaidi ya mama, alishindwa kabisa kukabiliana na ukweli kuwa mkewe amemtangulia. Mara kadhaa nilipoongea nae alikuwa akimkumbuka mkewe na kutamani kuwa nae. Kimsingi, marehemu baba na marehemu mama walikuwa zaidi ya mke na mume. Walikuwa marafiki pia hasa kwa vile Mzee Chahali alikuwa mkimya sana na mwenye marafiki wachache. 

Sijui niwaelezeje kuhusu kifo hiki kilivyoniathiri binafsi. Baada ya mama kututoka, mzazi pekee tuliyebakiwa nae alikuwa baba. Sasa tumabaki yatima. Kwa hakika inauma sana.  Lakini yote ni kazi yaMungu.

Mzee Chahali amezikwa kwa heshima zote, ambapo kwa mji wetu wa kidini sana, misa ya mazishi kuendeshwa na Askofu ni heshima kubwa sana, na kwa hakika tunalishukuru sana jimbo la Mahenge kwa kumthamini Mzee wetu kiasi hicho.

Lajkini sijui kama leo hii ningekuwa katika nafasi ya kuandika makala hii bila sapoti yenu kubwa mno. Kila nilipotupa jicho Facebooka au Twitter nilikuta rundo la salamu za kumwombea dua/sala baba alipokuwa mgonjwa, na rundo kubwa zaidi baada ya kuwatangazia taarifa za msiba. Ninawashukuru sana sana sana. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awabariki mno na awazidishie upendo wenu.

Jana nilibandika Makala Maalumu ya Sauti lakini kwa kutambua kuwa si kila mmoja ana muda au access ya kuskiliza audio filela takriban dakika 30 nikaona ni bora niziwasilishe tena salamu hizi za shukrani kwa maandishi.

Ninaomba mniruhusu nisimtaje kila mmoja wenu kwa sababu sio tu mpo wengi sana bali pia ukweli kwamba shukrani za dhati huwa moyoni. Naweza kujibaraguza hapa na sante zangu nyiiingi lakini moyoni nina mawazo mengine. Ila kwa hakika Mungu ndo shahidi wangu. Ninathamini mno mchango wenu wa hali na mali katika kumuuguza baba na kushiriki katika mazishi yake kwa njia ya rambirambi.

ASANTENI SANASANA SANA. SINA MANENO SAHIHI YA KUWAAMBIA LAKINI NINAWAOMBEA BARAKA TELE KUTOKA KWA MWENYEZI MUNGU.

Mwisho, Pumziko la Milele Bwana Mungu ajmjaalie Mzee Chahali, na mwanga wa milele amwangazie apumzike kwa amni, Ameni

ASANTENI SANA

10 Jun 2013


Bloga mwenzangu Lilly Melody amefiwa na mama yake. Bado sina taarifa za kutosha kuhusu tukio hili la kuhudhunisha mno.Kwa wakti huu ninawaomba wasomaji wa blogu tuungane kumwombea marehemu na kumfariji mfiwa.

Pumziko la milele, umpe ee Bwana na Mwanga wa milele umwangazie apumzike kwa amani Amen.

Pole sana Lilly

27 Apr 2013



Watanzania wanaoishi New Jersey na New York City. Wanasikitika kutangaza kifo cha mtanzania mwenzao Adolph aka Brian aka Thadeo Lwakajende kilichotokea tarehe 24 mwezi wa 4, 2011 hapa New Jersey, USA. Mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu inaendelea huko New Jersey. Ili kufanikisha mipango hiyo wanawaomba watanzania wote popote pale walipo wajiunge nao kusaidia kuchangisha hela za shughuli hiyo. Unaweza kutuma hela kwa kutumia paypal [email protected] au katika site hii ya Adolf sending home fund http://dt.tl/adolfsendhomecost.
Kwa mawasiliano ya shughuli hizi wasiliana na 

Peter Luangisa (917) 681-6971

Rashidi Kamugisha (973) 703-4596

Bernard Kivugo (973) 580-7166

William Vedasto (973) 551-2916

Tunatanguliza shukurani zetu za dhati. 

--
Thanks
--
******************************
Sara (Admin/Writer/ Editor)
http://www.tanzanianblogawards.com
Skype Id: Bongoblogawards
Twitter Id: Bongoblogawards
******************************



7 Feb 2013



Habari zilizotufikia hivio punde kutoka Jijini Arusha zinaarifu kuwa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Ask Thomas Laizer amefariki dunia.

Taarifa hizo zinadai kuwa Ask. Laizer amefikwa na umauti alasiri ya leo katika Hospitali ya Rufaa ya Selelian ya Mjini Arusha.


Jana Februari 6, 2013 Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alimtembelea  na kumjulia hali Askofu Thomas Laizer wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati.

Taarifa zilipasha kuwa Askofu Laizer alilazwa Hospitalini hapo kwa zaidi ya mwezi mmoja, na hakuna daktari wala ndugu aliye tayari kusema ugonjwa unaomsibu.

Pinda alikwenda hospitalini hapo jana saa 9 alasiri na kukaa zaidi ya nusu saa, huku waandishi wa habari wakizuiwa kuingia katika chumba alimolazwa cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu.

Hata hivyo, baada ya kutoka katika chumba hicho kama ilivyo ada ya viongozi kuzungumzia hali ya mgonjwa, Pinda hakuzungumza na waandishi wa habari na kulikuwa na ulinzi mkali ambapo pia waandishi wa habari walizuiwa kuzungumza naye.

Awali ilisemekana kuwa Askofu Laizer amehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya watu wengi kumiminika Selian kutaka kumwona, lakini jana ilidhihirika kuwa, amelazwa hospitalini hapo.

 FK Blog inatoa pole kwa Waumini na washarika wote wa KKKT nchini kote kufuatia msiba huo mzito ulilolikumba Kanisa la Kilutheri hasa wakati huu ambao kuna mgongano kati ya waumini na Viongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati.



15 Jul 2012
































Marehemu Patrin Kibelloh aliefariki ghafla siku ya Jumanne July10,2012. alizikwa Ijumaa july13 huka kwenye makaburi ya Gardner, West Roxbury ,Massachusset. Nchini Marekani 



  
Baadhi ya ndugu na marafiki waliohudhuria katia msiba huko nyumbani kwake Saugus, Boston Massachusset.


Marehemu Patrin Kibelloh amepata mafunzo katika Institute proffesional & Restaurant mjini Boario nchini ITALY alizaliwa April 25,1963 huko Tanzania ameacha mke wa Watoto wawili akiwa na umri wa miaka 49. (Picha zote na swahilivilla.blogspot.com)

         Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi!


11 Apr 2012

18 Jan 2012













Picha zote kwa hisani ya Jamii Forums

14 Jan 2012



TANZIA


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepatwa na majonzi makubwa na kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa, Mheshimiwa Regia Mtema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema amefariki leo tarehe 14 Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu darajani.


Habari za kusikitisha zilizopatikana kwenye mtandao wa jamii wa Twitter na ukumbi wa mijadala ya mtandaoni wa Jamii Forums zinaeleza kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema,Regia Mtema,amefariki kwa ajali ya gari iliyotokea daraja la mto Ruvu.

Licha ya kifo cha Regia kuwa pigo na pengo kubwa kwa Chadema pia ni msiba mkubwa kwa sie wazawa wa wilaya ya Kilombero,mahali alipozaliwa marehemu na ambapo alipatumikia kwa nguvu zake zote.

Tutawaletea taarifa zaidi kadri zinavyopatikana.

Bwana Ametoa Bwana Ametwaa,Jina lake lihimidiwe Milele.Amen.





2 Nov 2011


KWA NIABA YANGU BINAFSI NA  WASOMAJI WA BLOGU NINATOA SALAMA NYINGI ZA POLE KWA PRODUCER WA SPORAH SHOWSOPHIA MWANAUTA, KWA MSIBA MKUBWA WA KUONDOKEWA NA MDOGO WAKE MPENDWA.

HAKUNA MANENO MWAFAKA TUNAYOWEZA KUKUPA KATIKA KIPINDI HIKI KIGUMU LAKINI MAANDIKO YANATUFUNDISHA KUWA SOTE NI WAJA WA MUUMBA NA HUTUCHUKUA KATIKA MUDA NA WAKATI ATAKAO YEYE.LAKINI KWA VILE MWENYEZI MUGNU NI MWINGI WA HURUMA NA UPENDO BASI SIO TU ATAWALIWAZA WAFIWA KATIKA KIPINDI HIKI KIGUMU LAKINI PIA ATAMJAALIA MAREHEMU PUMZIKO LA AMANI

YEYE NDIYE MUUMBA,ANAPOMCHUKUA MMOJA WETU NI KWA VILE LICHA YA KUWA TULIMPENDA MAREHEMU LAKINI MOLA ALIMPENDA ZAIDI NA KUAMUA KUMCHUKUA.

POLE SANA SANA SOPHIA.MOLA AKUJAALIE WEWE BINAFSI NA FAMILIA,NDUGU NA JAMAA NGUVU NA MOYO WA KUSTAHILIMILI MAJONZI MLIYONAYO

INNA LILLAHI WA INNA ILAYHI RAJI'UN

من المؤكد أننا ننتمي إلى الله وإنا إليه راجعون يجب

SURELY WE BELONG TO ALLAH AND TO HIM SHALL WE RETURN



12 Oct 2011

MSIBA WA MTANZANIA MWENZETU MZEE SAID MUHAMMAD SIKAMKONO

Tunaskitika kuwataarifu kuhusu kifo cha Mtanzania mwenzetu Mzee Said Muhammad Sikamkono kilichotokea jana tarehe 11/10/2011 mchana katika hospitali ya Queen Elizabeth, Woolwich, London.
Mipango ya mazishi inaendelea na mtaendelea kujulishwa. Kwa wakati huu ambao tutakuwa tunasubiri kupata taarifa ya mazishi, mwenye kuweza kuchangia chochote au mwenye kuhitaji kujua zaidi kuhusu msiba huu, tunaomba awasiliane na;
Sheikh Ayub kwa namba; 07944930708
AU
 Said Surur kwa namba; 07538063536
AU
Mr. Haruna Mbeyu kwa namba; 07813539025.

“MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU SAID MUHAMMAD SIKAMKONO MAHALI PEMA.  MUNGU AMETOA NA MUNGU AMETWAA, JINA LAKE LIBARIKIWE”

7 Jul 2008

Jamaa yangu mmoja mkazi wa Kwa Jongwe (Zimbabwe) kanitumia fedha hii kama rambirambi rambi yake kwa msiba ulionikumba hivi karibuni.

3 Jun 2008

NINASIKITIKA KUWATANGAZIA KIFO CHA MAMA YANGU MZAZI ADELINA MAPANGO KILICHOTOKEA IFAKARA MOROGORO TAREHE 29/05/2008 NA MAZISHI YALIKUWA JANA TAREHE 02/06/2008 KATIKA MAKABURI YA UKOO WA CHAHALI HAPA IFAKARA.NAWASHUKURU NYOTE AMBAO KWA NAMNA MOJA AU NYINGINE MLIUNGANA NAMI KATIKA KUMUOMBEA MAMA APONE LAKINI BWANA AMEMPENDA ZAIDI NA HATIMAYE KUMREJESHA KWAKE.UKOO WA CHAHALI NA MAPANGO UNAWASHUKURU SANA KWA USHIRIKIANO WENU.BWANA AMETOA BWANA AMETWAA,JINA LA BWANA LIHIMIDIWE MILELE.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.