14 May 2016


Jana nilibandika makala kuhusu manung'uniko ya Watanzania wengi wanaoishi hapa Uingereza ambao walikuwa hatarini kukosa fursa ya kuhudhuria mkutano na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye yupo nchini hapa kikazi.

'Kelele' hizo zimezaa matunda, na leo Waziri Mkuu Majaliwa atakutana na Watanzania wote wanaoishi nchini humu wanaoweza kumudu kufika ubalozini London saa kumi alasiri. Awali, maofisa husika katika ubalozi huo walialika kundi dogo tu la Watanzania kuhudhuria mkutano huo, hatua iliyotafsiriwa na wengi kama ubaguzi na pengine jitihada za kuficha majipu yanayoukabili ubalozi huo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imeandikwa kidiplomasia, ambapo kwa upande mmoja imejitoa lawama ya kuhusika na maandalizi ya mkutano huo (na hakuna aliyemlaumu Waziri Mkuu au Ofisi yake bali lawama zilielekezwa kwa ubalozi) .Kwa upande mwingine ni kama imekanusha 'madai ya watu' kuwa kuna watu maalum waliochaguliwa kuhudhuria mkutano huo (badala ya kuwa mkutano wa wazi kwa kila Mtanzania anayeishi hapa). Nimesema ni "lugha ya kidiplomasia" kwa sababu uthibitisho kwamba awali mpango wa ubalozi ulikuwa ni kama ulivyolalamikiwa jana , yaani kundi la watu kadhaa tu ndio wakutane na Waziri Mkuu, na uthibitisho huo unasikika katika audio hii ya mmoja wa maofisa wa ubalozi wetu anayetukebehi kwa kudai haki ya kukutana na Waziri Mkuu. Msikilize kwa kubonyeza play


Ni wazi kuwa laiti afisa ubalozi huyo ndio angekuwa na mamlaka ya mwisho basi ni wazi angebaki na hao watu wachache ambao awali ndio waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kana kwamba ni wa siri.

Badala ya kukiri kwamba ubalozi ulifanya makosa kuteua watu wachache tu, afisa huyo anaelekea kutuona kituko kwa kudai haki ya msingi ya kukutana na viongozi wetu wa kitaifa. Na badala ya kutumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania ratiba ya mkutano huo (tetesi zinasema utafanyika ubalozni mida ya saa 10 jioni) yeye ameamua kutunanga. Madaraka huwafanya baadhi ya wenzetu kujisahau sana.

Tukiweka kando lugha ya kidiplomasia ya Ofisa ya Waziri Mkuu na kebehi za afisa ubalozi, la muhimu ni kwamba sasa Watanzania wote wanaoishi hapa Uingereza wamepewa fursa ya kuhudhuria mkutano huo muhimu na Waziri Mkuu. Binafsi nimefarijika sana kwa sababu nilijitahidi kulipigia kelele suala hilo kwenye kundi la Whatsapp la jumuiya ya Watanzania ambayo ipo katika hatua za awali za kuundwa, japo mapokeo hayakuwa ya kuridhisha (watu wanahimiza umoja lakini walikalia kimya 'ubaguzi' uliotaka kufanywa na baadhi ya maafisa ubalozi wetu hapo London). 

"Kelele" zangu hazikutokana na mie kutopewa mwaliko, kwa sababu hata kama ningekuwa miongoni mwa watu hao takriban 40 walioalikwa bado nisingehudhuria (na leo sintohudhuria...kwa sababu zangu binafsi). Nilipiga kelele kwa maslahi ya walio wengi ambao pengine kwa namna moja au nyingine walishindwa kupiga kelele hizo wao wenyewe. Sie wengine tuna kumbi kama hii ya blogu au makala magazetini ambazo ni rahisi kupiga kelele na watawala kutusikia. Lakini si kila mtu ni blogs au mwandishi wa makala. Ni matumaini yangu kuwa 'kelele' hizi zitawahamasisha wengi kutambua kuwa 'kelele dhidi ya jambo lisilofaa' sio uchizi, kusaka umaarufu au ukorofi. Marehemu Kighoma Ali Malima aliwahi kutuusia kwamba "HAKI HAIPASWI KUOMBWA KAMA ZAWADI. HAKI HUDAIWA...KWA NGUVU IKIBIDI."

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube