21 May 2016


Nianze makala hii kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua aliyochukua jana ‘kumtumbua’ aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kwa kosa la kuingia Bungeni akiwa amelewa.

Kadhalika, ningependa kutumia fursa hii kumshukuru kwa kuwa kiongozi msikivu. Binafsi, ‘nilikomalia’ sana kuhusu uwaziri wa Kitangwa hasa kutokana na tuhuma kuwa ni mhusika katika skandali ya Lugumi (na tetesi kuwa alikuwa mlevi - japo sikuwahi kuongelea ishu hiyo ya ulevi kwa vile niliona kama suala binafsi, alimradi haliathiri utendaji wake wa kazi). 

Kwa ‘mtaani’ hatua hiyo ya Rais Magufuli inaweza kuonekana ni ya kawaida tu, yaani kiongozi aliyefanya uteuzi wa mtu flani, hatimaye kuamua kuteungua uteuzi huo. Lakini kwa hakika, hatua hiyo ya Rais Magufuli haikuwa rahisi. 

Kwa mujibu wa taarifa, Rais Magufuli na Kitwanga wamekuwa marafiki wa muda mrefu. Wajuzi wa mambo wanaeleza kuwa hata uamuzi wa kumteua Kitwanga kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ulitokana na imani ya Rais Magufuli kwa rafiki yake huyo. Ikumbukwe kuwa wizara hiyo ni moja ya wizara nyeti ambazo kwa kiasi kikubwa hukabidhiwa kwa watu wanaoaminika mno kwa rais husika. 

Kuna kipande cha video kilichosambaa mtandaoni siku za nyuma ambacho kilikuwa kinamwonyesha Rais Magufuli kabla hajawa rais wala mgombea wa CCM, akiwa na Kitwanga, na katika maongezi yao, Kitwanga anasikika akimwambia Magufuli agombee urais (japo ni katika hali ya utani). 

Lakini pia inaelezwa kuwa hata kabla Rais Magufuli hajatangaza baraza lake la mawaziri, Kitwanga alikuwa akijigamba kuwa angepewa wizara nyeti, mara baada ya Magufuli kutangaza kabineti yake, na wizara nyeti ya mambo ya ndani ya nchi akapewa baada ya kutangazwa kabineti hiyo. 

Hata hivyo, suala hili la Kitwanga linapaswa kuamsha maswali kuhuru Idara yetu ya Usalama wa Taifa na utaratibu wa ‘kuwatafiti wateule watarajiwa wa Rais,’ kitu kinachofahamika kitaalam kama ‘vetting.’ Nina uhakika wa asilimia 100 kuwa ‘dossier’ (kabrasha maalum kuhusu mtu maalum) la Kitwanga lilipaswa kueleza bayana kuhusu tabia yake ya ulevi. Je ilikuwaje sio tu akateuliwa kuwa waziri bali pia kuteuliwa kuwa waziri katika wizara nyeti kabisa kwa usalama wa raia na nchi. Je kulikuwa na mapungufu huko Idara ya Usalama wa Taifa au walieleza hilo kabla Kitwanga hajateuliwa lakini likapuuzwa? Ni vigumu kuwa na uhakika wa kipi kilitokea. 

Kwa kuwa lengo ni kwenda mbele na si kunyoosheana vidole tu bila kutoa uushauri au kuleta ufumbuzi, binafsi ninashauri wahusika waangalie wapi walijikwaa, ili wasirudie tena kosa hilo. Vetting ya wateuliwa watarajiwa ni muhimu mno kwa sababu licha ya kuiingiza gharama serikali pale inapolazimu uteuzi husika kutenguliwa, pia inahatarisha usalama wa taifa (watu wanaotimuliwa madarakani ni rahisi kuwa recruited na maadui wa taifa ili 'kulipa kisasi').

Tukiweka kando mapungufu hayo, kitendo cha Dkt Magufuli kumtumbua Kitwanga kinapeleka ujumbe mzito kwa kila mtumishi wa serikali. Kwanza, kinaashiria kuwa Rais anafanyia kazi taarifa anazoletewa (maana hakuwepo Bungeni Dodoma wakati Kitwanga akiwa 'bwii' mjengoni. 

Lakini pia kitendo hicho kinaashiria kuwa mfumo wa mawasiliano ndani ya serikali umerejea kama wa zama za Nyerere, pasipo 'taarifa kuvuja' kabla ya kufika mahali stahili. Hali hii itapelekea watendaji wa serikali ikiwa ni pamoja na mawaziri kuwa makini zaidi kwani hawajui nani anawachunguza au nini kinaripotiwa kwa Rais kuhusu wao.

Tukiweka hilo kando, binafsi nimefarijika sana baada ya kusikia taarifa za Kitwanga ‘kutumbuliwa’ kwa sababu nilipiga kelele za kutosha kuhusu uongozi usioridhisha wa mheshimiwa huyo. Nilianza kitambo kuhoji kuhusu utendaji kazi wa waziri huyo.

Suala la kwanza ‘kumshikia bango’ lilikuwa kauli zake za utata kuhusu kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Hili nililiandikia MAKALA HII. 







Baadaye, ikaibuka skandali ya Lugumi, na kwa hakika sikuchoka kupiga kelele, hususan kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kama inavyoonekana hapa chini 



Sambamba na kelele hizo hatimaye niliamua kuandika MAKALA HII 


Ni matarajio yangu makubwa kuwa makala hii itamhamasisha kila msomaji kuwa na msimamo, na kisha kusimama imara katika msimamo huo, sambamba na kuhakikisha kuwa anachosimamia ni sahihi, na kuendelea kuupigania hadi mafanikio yapatikane. Sio kazi rahisi lakini mara nyingi vitu vizuri, au vinavyodumu, huwa havipatikani kirahisi. 

Mwaka 2006, niliandika MAKALA HII kuhusu suala la mkataba wa kufua umeme, uliopelekea skendo ya Richmond, na nikaendelea kupiga kelele hadi mwaka Februari 2008 baada ya mhusika mkuu katika skendo hiyo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiuzulu. Hata hivyo, ishu hiyo ilinigharimu mno kimaisha. 

Na hivi majuzi, nilijaribu ‘kuwashikia bango’ wahusika wa Mamlaka ya Mawasiliano TCRA, na nikawatwanga MAKALA hii. 


Siku chache baadaye, bosi wa taasisi hiyo akatumbuliwa. 


Na majuzi tu, Ubalozi wetu hapa Uingereza ulitaka kutufanyia 'uhuni' katika ziara ya Waziri Mkuu, ambapo awali kulikuwa na mpango wa kumkutanisha Waziri Mkuu na kundi dogo tu la Watanzania wanaoishi hapa. Kelele nilizoshiriki kuibua zilisaidia, na hatimaye mkutano huo wa Waziri Mkuu ulifanywa kuwa wa wazi kwa kila Mtanzania mkazi wa hapa kuhudhuria. Nimeelezea kwa kirefu kuhusu sakata hili katika MAKALA HII.

Sitaki kujisifu kuwa kelele zangu pekee ndio zinapelekea hatua kusudiwa kuchukuliwa. Hapana. Ninachojaribu kuonyesha ni ushiriki wangu katika harakati za kudai mabadiliko kwa kupitia maandishi, “kelele zetu” iwe hapa bloguni, kwenye mitandao ya kijamii au kwa njia ya makala. Pia, kwa kuwaeleza wasomaji kuhusu mafanikio ya 'kelele zetu' inasaidia kuhamaisha watu wengi zaidi kutambua umuhimu wa harakati kama hizi katika kuleta mabadiliko kusudiwa


Mara nyingi tunapopiga kelele hizo tunaishiwa kukebehiwa, kuonekana vimbelembele, tusio na vitu muhimu vya kufanya katika maisha yetu binafsi, na shutuma kama hizo. Lakini pindi kelele zetu zinapozaa matunda, walewale waliokuwa wakitukebehi huwa mstari wa mbele “kusaka sifa.” 

Kimsingi, harakati hizi sio za kusaka ujiko au madaraka. Ni kile nilichoeleza awali: kuwa na msimamo na kusimama thabiti katika msimamo huo hadi ufumbuzi wa tatizo husika upatikane.

Nimalizie makala hii kwa kumpongeza sana Rais Magufuli kwa ‘kumtumbua’ Kitwanga. Wanaohisi kuwa kutambuliwa huko ni ‘kuficha kombe’ la ishu ya Lugumi, ombi langu kwao ni wavute subira. 

Sakata la Lugumi sasa litachukua sura mpya, na tusishangae kusikia watu wakiburuzwa mahakamani hivi karibuni. Pia suala hili la kutambuliwa Kitwanga linaweza kumpa fursa Rais Magufuli fursa ya kuwatumbua angalau mawaziri mawili hivi ambao mwenendo wao umekuwa wa kusuasua. Fursa ya kuwatumbua inatokana na kutambuliwa kwa Kitwanga ambako kutamlazimu Rais kufanya ‘reshuffle’ ndogo.

1 comment:

  1. Ndugu maneno uliyonena sawa kabisa tumuombe Mungu Rais aongoze serikali yenye nidhamu

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.