Showing posts with label Charles Kitwanga. Show all posts
Showing posts with label Charles Kitwanga. Show all posts

27 May 2016


Makala hii imechapishwa katika toleo la wiki hii la gazeti la RAIA MWEMA lakini tovuti ya gazeti hilo haijaweka habari mpya, kwahiyo nimeonelea ni vema nikiitundika hapa (na sina hakika lini Raia Mwema wata-update tovuti yao). Kichwa cha habari cha makala hii gazetini kinaweza kuwa tofauti na hiki nilichotumia kwenye blogu. 

Ijumaa iliyopita itabaki kuwa siku ya kumbukumbu kwa muda mrefu katika siasa za nchi yetu na medani nzima ya uongozi wa taifa letu. Siku hiyo, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi mno, Rais wa nchi yetu alimtimua waziri wake mwandamizi ‘bila kuuma maneno’

Tukiweka kando zama za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, tangu tupate uhuru hadi alipong’atuka mwaka 1985, kipindi ambacho kutokana na urefu wake kilishuhudia majeruhi kadhaa wa kisiasa, kwa zaidi ya miaka 30 Tanzania yetu haijashuhudia kulichofanywa na Rais Dkt John Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita ‘alipomtumbua’ aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kwa kosa la kuingia bungeni akiwa amelewa.

Uzito wa hatua hiyo unatokana zaidi na mambo makuu matatu. Kwanza, Kitwanga ni rafiki wa muda mrefu wa Rais Magufuli, na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alimtambulisha kama mtu anayemfahamu vizuri, waliyesoma pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Bila kujali uzito wa kosa la Kitwanga, ilihitaji ujasiri mkubwa kwa Magufuli kumtimua ‘hadharani’ rafiki yake huyo.

Pili, uzito wa hatua hiyo unatokana na hicho nilichokiandika katika paragrafu iliyotangulia; katika miaka 10 ya utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, miaka 10 ya utawala wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, na miaka 10 iliyomalizika mwaka jana ya utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne, hakujawahi kutokea hatua kama hiyo aliyochukua Rais Magufuli.

Kila ilipojitokeza kasoro ya kiutendaji, marais waliotangulia waliishia aidha kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri pasipo maelezo ya kutosha kuwa “uwaziri wa flani umetenguliwa kwa sababu flani” au pengine waziri kutolewa wizara moja na kupelekwa wizara nyingine. Na hali hiyo ya ‘boronga hapa uhamishiwe kule’ ilikuwepo pia katika zama za Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Kwa kifupi, Dokta Magufuli amevunja mwiko wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu mno, na kwa hilo tu anastahili kila aina ya pongezi, sio tu kwa sababu ya kuandika upya historia ya taifa letu bali ukweli kwamba hatua hiyo inamtambulisha Rais wetu kama mtu anayeweka mbele zaidi maslahi ya taifa letu kuliko maslahi binafsi.

Tatu, miaka nenda miaka rudi, baada ya kuingia kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, marais wetu kama wenyeviti wa chama tawala CCM, wamekuwa wakijitahidi kadri wawezavyo kujifanya ‘viziwi’ kila zinapojitokeza ‘kelele’ kutoka vyama vya upinzani. Kabla ya ‘kutumbuliwa,’ baadhi ya vyama vya upinzani vilikuwa vikimlalamikia Rais Magufuli kuwa ‘anamlinda Kitwanga’ kuhusiana na kashfa ya ufisadi ya Lugumi, na vilikuwa vikipiga kelele kumtaka ‘amtumbue’ Kitwanga.

Sasa, katika mazingira ya kawaida tu, ingeweza kuwa vigumu kwa Dkt Magufuli kumtimua Kitwanga kwa kuhofia “kuwapa wapinzani ushindi wa bure” katika suala hilo. Kwamba, wapinzani wangeweza kujigamba kuwa shinikizo lao ndio limepelekea Rais ‘kumtumbua’ rafiki yake.

Na katika hilo, ni muhimu kutambua kuwa Dkt Magufuli “ana wabaya wake ndani ya CCM,” na angeweza kuchelewa kumtimua Kitwanga kwa vile “wabaya wake hao” wangeweza kutafsiri kitendo hicho kama udhaifu, kwa maana ya “kuendeshwa na kelele za Wapinzani.”

Kwa kiwango kikubwa, hatua hiyo ya Dkt Maguguli imepokelewa vizuri na Watanzania wengi, hasa ikizingatiwa kuwa licha ya ‘kumtumbua Kitwanga,’ suala zima la kuchukua hatua stahili pale inapohitajika ni kama kitu kigeni kwa wananchi wengi, ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa ikiongozwa kwa siasa za kulindana. Kwahiyo, ahadi za Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na baada ya kuapishwa kuwa rais, kwamba hatomwonea aibu mtu yeyote zimethibitika zaidi katika suala hilo la ‘kumtumbua’ Kitwanga.

Hata hivyo, Tanzania yetu imegawanyika kuliko wengi tunavyoiona. Na mgawanyiko mkubwa wa nchi yetu ni athari ya moja kwa moja ya uchaguzi mkuu uliopita. Kuna kundi kubwa tu la wenzetu ambao hadi dakika hii hawataki kuamini kuwa “mgombea wao alishindwa.” Hapa namzungumzia mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa. Sasa kwa wenzetu hao, Dkt Magufuli sio tu “hakushinda kihalali” bali pia ni “dikteta anayetumbua watu bila kuzingatia sheria, mwenye jazba, nguvu ya soda” na kila baya unaloweza kumuongelea kiongozi.

Waungwana hawa walikuwa wakipiga kelele mno kumtaka Rais amwajibishe ‘swahiba wake’ Kitwanga ili kuwezesha uchunguzi wa kashfa ya Lugumi ufanyike kwa ufanisi zaidi hasa kwa vile nafasi ya Kitwanga kama Waziri mwenye mamlaka juu ya Jeshi la Polisi ingeweza kuathiri uchunguzi huo.

Akina sie pia tulimshauri Rais afikiri kutengua uwaziri wa Kitwanga, lakini tunapopishana na wenzetu hao ni kwamba hata baada ya Rais “kusikiliza kilio cha kumtaka amtumbue Kitwanga” bado wanamlaumu. Baadhi wanadai kuwa “kumtumbua Kitwanga ili kuuwa suala la Lugumi.” Wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai “suala hilo ni mchezo wa kuigiza usioingia akilini.” Wanasema eti “Kitwanga ametolewa kafara ili kuwanusuru vigogo flani.”

Lawama kwa Dkt Magufuli hata baada ya kuweka kando urafiki na kuchukua hatua stahili dhidi ya swahiba yake, zinaweza kumvunja moyo. Tukumbuke, yeye ni binadamu kama sie. Na ni wazi, unapokubali lawama kutoka kwa mtu wako wa karibu ili tu kukidhi matakwa ya jamii, kisha ukaishia kulaumiwa na baadhi ya wanajamii, inavunja moyo. Hata hivyo, ninatumaini kuwa Dkt Magufuli hatoyumbishwa na lawama hizo. Kimsingi, zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo kwa sababu tatizo sio anachofanya bali imani fyongo ya “wenzetu” kuwa aliyepaswa kuwa rais ni yule “mtu wao.”

Kama kuna lawama au kasoro inayoweza kujadiliwa basi ni kuhusu utaratibu wa kiusalama uanaofahamika kama “vetting.” Kabla ya kuteuliwa, jina la Kitwanga lilipelekwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa ajili ya kufanyiwa vetting. Swali, je Idara hiyo ilishindwa kubaini kuwa “Kitwanga ana kasoro ya ulevi ambayo sio tu ingeweza kuathiri utendaji kazi wake bali pia ingeweza kuhatarisha usalama wa taifa”? Je inawezekana kuwa Idara hiyo ilitekeleza jukumu lake ipasavyo lakini ‘mfanya uteuzi’ akapuuzi ushauri wa mashushushu hao?

Huu sio muda wa kunyoosheana vidole. Kama Idara yetu ya Usalama wa Taifa ilizembea kwenye vetting basi na ijirekebishe haraka. Kama ‘mfanya uteuzi’ alipuuzia ushauri wa mashushushu hao basi ameshapata funzo muhimu.

Ikumbukwe kuwa hadi muda huu hatufahamu kuwa ‘tatizo la ulevi wa Kitwanga’ limeathiri vipi utendaji wake wa kazi kama Waziri wa wizara nyeti ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kiusalama, hakuna kitu majasusi kutoka nchi za nje wanaombea kama kukutana na mtendaji wa serikali katika eneo nyeti ambaye ana udhaifu kama huo wa ulevi. Na ninaamini kuwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa wanafahamu fika jinsi majirani zetu walivyojaza majasusi ndani ya Tanzania yetu, hususan baada ya ujio wa Dkt Magufuli unaoanza kuifanya nchi yetu kuwa tishio kiuchumi kwa majirani zetu.

Ni matumaini yangu makubwa kuwa kutafanyika uchunguzi wa kina kuhakikisha kuwa mapungufu ya Kitwanga hayakuathiri usalama wa taifa letu kwa maana ya kwamba hakuna aliyetumia ‘ulevi wake’ kum- “blackmail” ili atoe siri za serikali.

Kiu kubwa kwa Watanzania kwa muda huu ni kuona Bunge litachukua hatua gani dhidi ya ‘mwenzao.’ Hata hivyo, ishara mbaya zimeanza kuonekana baada ya Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, kunukuliwa akidai kuwa “hakuna kifungu chochote cha kanuni za Bunge kinachomzuwia mtu kuingia Bungeni akiwa amelewa.” Yaani hawa waheshimiwa wana kinga dhidi ya Kanuni za Utumishi wa Umma zinazokataza “tabia inayovunja heshima ya utumishi kwa umma hata nje ya mahali pa kazi” kwa mfano ulevi.

Lakini kubwa zaidi ni kuona kuwa ‘kutumbuliwa’ kwa Kitwanga haukuathiri uchunguzi wa suala tete la Lugumi. Kimsingi, kwa kutolewa uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamati Teule ya Bunge inayochunguza suala hilo sasa haina kisingizio chochote cha kutowapatia Watanzania kile wanachostahili: ukweli kamili kuhusu suala hilo.
Nimalizie makala hii kwa kumpongeza Rais Dkt Magufuli kwa kuwakumbusha watendaji wote wa serikali kuwa “zama za nchi kujiendesha yenyewe (autopilot) zimekwisha, na sasa ‘Hapa Ni Kazi Tu’.” Kwamba kiongozi atakayezembea atatumbuliwa bila kuonewa haya. Kadhalika, hongera nyingi kwa Rais wetu kwa kuweka mbele zaidi maslahi ya taifa kuliko maslahi binafsi, umekubali lawama kuliko fedheha. Mwenyezi Mungu akulinde katika utendaji kazi wako, wenye hila mbaya washindwe na uendelee kuwatumikia Watanzania kwa uwezo wako wote.

Mungu Mbariki Rais wetu Dkt John Magufuli.
Mungu Wabariki Watanzania wote wenye kuitakia mema nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania.

24 May 2016

Sakata la kutumbuliwa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, linazidi kutawala vichwa vya habari, huku maendeleo mapya yakiashiria kuwa kuna mengi yanayoweza kuwa yanaendelea 'nyuma ya pazia.'

Jana, watu waliojitambulisha kama 'wana-jimbo wa Misungwi' walitoa tamko kwa waandishi wa habari. Hebu ndugu msomaji mpendwa, fanya kulisoma tamko hilo kwanza, kisha bingirika nami kwa uchambuzi zaidi, and trust me, sintokuangusha haha!

First thing first, hawa 'wana-jimbo wa Misungwi' WAMETUMWA NA NANI? Ninauliza hivyo kwa sababu hisia yangu ya sita inanituma kuamini kuwa hawajajitolea wenyewe tu kutoa tamko hilo. Hawa wametumwa, no doubt about that. Lakini hatujui nani kawatuma.

Kwa kuitegemea tena hisia yangu ya sita, yayumkinika kuhisi kuwa hao 'wana-jimbo' ni wapambe tu wa Kitwanga. Twende mbali zaidi, ninahisi watu hao ni sawa na spika tu ya kumwezesha Kitwanga asikike.. 

Tetesi zinaeleza kuwa Kitwanga alikuwa 'mtu wa kinywaji' kitambo sasa. Na kwa wenzetu ambao hawajawahi kugusa kinywaji, ukweli upo hivi: hakuna mtu anayeitwa 'mnywaji wa muda mrefu.' Mtu wa aina hiyo ni MLEVI. Period. Na ulevi, japo si dhambi au kinyume cha sheria, una athari zake. Kuna mlolongo mrefu wa jinsi ulevi ulivyobomoa maisha ya watu mbalimbali. Kwahiyo, tukiafikiana kuwa Kitwanga ni mlevi, basi ilikuwa suala la muda tu kabla haijamlipukia. Kwa lugha nyingine, Bwana Kitwanga alikuwa kama time-bomb, muda wowote ule lingetokea la kutokea.

Mengi yameshaongewa tangu Kitwanga atumbuliwe na Rais Magufuli hapo juzi, makubwa zaidi yakiwa ni pamoja na madai kuwa ishu hiyo ni mcheoz wa kuigiza. Kwamba kutumbuliwa kwa Kitwanga ni mkakati wa makusudi wa kuiua ishu ya Lugumi. 

Siafikiani na mtazamo huo kwa sababu kama kweli Magufuli alikuwa anataka kumuokoa rafiki yake alikuwa na njia nyingi tu, moja ya wazi ikiwa ni 'kuziba masikio,' kwa maana ya kupuuza kelele za waliotaka Kitwanga atumbuliwe.

Wengine wanadai kuwa kweli Kitwanga alikuwa amelewa, lakini hakulewa kwa hiari yake bali 'kinywaji chake kilifanyiwa utaalam,' wakijaribu kutushawishi kuwa Kitwanga alihujumiwa. 

Hizi ni hisia tu zisizo na uthibithso wowote. Jamaa alikuwa 'chapombe,' na wanaomfahamu hawashangazwi na hilo tukio la majuzi au kutumbuliwa kwake. Pombe sio chai, siku ya siku lazima itamwadhiri mtu.

Madai mengine ambayo yanahusiana na hayo ya 'kinywaji cha Kitwanga kufanyiziwa' yanauhusisha utawala wa Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, ambako ndiko suala la Lugumi lilianzia. In fact, hizo tuhuma za 'kinywaji cha Kitwanga kufanyiziwa' zinawahusu baadhi ya watu waliokuwa karibu na utawala huo. 

Na kama msomaji ulivyoona katika 'tamko la wana-jimbo wa Misungwi' hapo juu, mmiliki wa Kampuni ya Lugumi, Said Lugumi na mtoto wa Rais Kikwete, Ridhiwani, wametajwa kuwa miongoni mwa wanaomhujumu Kitwanga.

Sawa, ishu ya ufisadi wa Lugumi ipo complex lakini kudai kuwa akina Lugumi na Ridhiwani ndo waliomfanyizia Kitwanga hadi akaishia kutimuliwa na Rais Magufuli ni hisia tu zisizo na mantiki. Haina mantiki kwa vile haiingii akilini jinsi gani hao jamaa wangemudu kumhujumu Kitwanga na wakati huohuo kumshinikiza Magufuli amchukulie hatua.

Kwa upande mwingine, Spika Job Ndugai, amejiingiza matatizoni 'kitoto' kwa kauli yake isiyo na busara ianyoashiria kuwa 'ulevi wa Kitwanga ni cha mtoto, kuna waheshimiwa wanavuta bangi na kubwia unga.' Really? Yaani Spika anawafahamu waheshimiwa wanaotenda makosa ya jinai lakini anawahifadhi!? 

Sasa, inasemekana baadhi ya wabunge wameamua kumkalia kooni awataje hao 'wabunge wavuta bangi na wala unga' na ajieleze kwanini hakuwaripoti kwa mamlaka husika.

Kadhalika, baadhi ya 'wazushi' wanamtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuonyesha uthibitosho kuwa kweli Kitwanga alikuwa 'njwii' siku ile pale Bungeni hadi Rais Magufuli kuchukua hatua ya kumtumbua. Nadhani hii inalenga kumpima ubavu tu Waziri Mkuu Majaliwa kwani kila aliyeona Kitwanga akijibu swlai pale Bungeni hatoshindwa kujua kuwa alikuwa amelewa

Anyway, blogu hii inaendelea kufuatilia ishu hiyo, pamoja na ishu nyingine mbalimbali katika jamii yetu. Pia, kesho, makala yangu katika toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema inajadili kwa kirefu kuhusu suala hilo la Kitwanga kutumbuliwa. Usikose kupata nakala yako.

21 May 2016


Nianze makala hii kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa hatua aliyochukua jana ‘kumtumbua’ aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kwa kosa la kuingia Bungeni akiwa amelewa.

Kadhalika, ningependa kutumia fursa hii kumshukuru kwa kuwa kiongozi msikivu. Binafsi, ‘nilikomalia’ sana kuhusu uwaziri wa Kitangwa hasa kutokana na tuhuma kuwa ni mhusika katika skandali ya Lugumi (na tetesi kuwa alikuwa mlevi - japo sikuwahi kuongelea ishu hiyo ya ulevi kwa vile niliona kama suala binafsi, alimradi haliathiri utendaji wake wa kazi). 

Kwa ‘mtaani’ hatua hiyo ya Rais Magufuli inaweza kuonekana ni ya kawaida tu, yaani kiongozi aliyefanya uteuzi wa mtu flani, hatimaye kuamua kuteungua uteuzi huo. Lakini kwa hakika, hatua hiyo ya Rais Magufuli haikuwa rahisi. 

Kwa mujibu wa taarifa, Rais Magufuli na Kitwanga wamekuwa marafiki wa muda mrefu. Wajuzi wa mambo wanaeleza kuwa hata uamuzi wa kumteua Kitwanga kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ulitokana na imani ya Rais Magufuli kwa rafiki yake huyo. Ikumbukwe kuwa wizara hiyo ni moja ya wizara nyeti ambazo kwa kiasi kikubwa hukabidhiwa kwa watu wanaoaminika mno kwa rais husika. 

Kuna kipande cha video kilichosambaa mtandaoni siku za nyuma ambacho kilikuwa kinamwonyesha Rais Magufuli kabla hajawa rais wala mgombea wa CCM, akiwa na Kitwanga, na katika maongezi yao, Kitwanga anasikika akimwambia Magufuli agombee urais (japo ni katika hali ya utani). 

Lakini pia inaelezwa kuwa hata kabla Rais Magufuli hajatangaza baraza lake la mawaziri, Kitwanga alikuwa akijigamba kuwa angepewa wizara nyeti, mara baada ya Magufuli kutangaza kabineti yake, na wizara nyeti ya mambo ya ndani ya nchi akapewa baada ya kutangazwa kabineti hiyo. 

Hata hivyo, suala hili la Kitwanga linapaswa kuamsha maswali kuhuru Idara yetu ya Usalama wa Taifa na utaratibu wa ‘kuwatafiti wateule watarajiwa wa Rais,’ kitu kinachofahamika kitaalam kama ‘vetting.’ Nina uhakika wa asilimia 100 kuwa ‘dossier’ (kabrasha maalum kuhusu mtu maalum) la Kitwanga lilipaswa kueleza bayana kuhusu tabia yake ya ulevi. Je ilikuwaje sio tu akateuliwa kuwa waziri bali pia kuteuliwa kuwa waziri katika wizara nyeti kabisa kwa usalama wa raia na nchi. Je kulikuwa na mapungufu huko Idara ya Usalama wa Taifa au walieleza hilo kabla Kitwanga hajateuliwa lakini likapuuzwa? Ni vigumu kuwa na uhakika wa kipi kilitokea. 

Kwa kuwa lengo ni kwenda mbele na si kunyoosheana vidole tu bila kutoa uushauri au kuleta ufumbuzi, binafsi ninashauri wahusika waangalie wapi walijikwaa, ili wasirudie tena kosa hilo. Vetting ya wateuliwa watarajiwa ni muhimu mno kwa sababu licha ya kuiingiza gharama serikali pale inapolazimu uteuzi husika kutenguliwa, pia inahatarisha usalama wa taifa (watu wanaotimuliwa madarakani ni rahisi kuwa recruited na maadui wa taifa ili 'kulipa kisasi').

Tukiweka kando mapungufu hayo, kitendo cha Dkt Magufuli kumtumbua Kitwanga kinapeleka ujumbe mzito kwa kila mtumishi wa serikali. Kwanza, kinaashiria kuwa Rais anafanyia kazi taarifa anazoletewa (maana hakuwepo Bungeni Dodoma wakati Kitwanga akiwa 'bwii' mjengoni. 

Lakini pia kitendo hicho kinaashiria kuwa mfumo wa mawasiliano ndani ya serikali umerejea kama wa zama za Nyerere, pasipo 'taarifa kuvuja' kabla ya kufika mahali stahili. Hali hii itapelekea watendaji wa serikali ikiwa ni pamoja na mawaziri kuwa makini zaidi kwani hawajui nani anawachunguza au nini kinaripotiwa kwa Rais kuhusu wao.

Tukiweka hilo kando, binafsi nimefarijika sana baada ya kusikia taarifa za Kitwanga ‘kutumbuliwa’ kwa sababu nilipiga kelele za kutosha kuhusu uongozi usioridhisha wa mheshimiwa huyo. Nilianza kitambo kuhoji kuhusu utendaji kazi wa waziri huyo.

Suala la kwanza ‘kumshikia bango’ lilikuwa kauli zake za utata kuhusu kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Hili nililiandikia MAKALA HII. 







Baadaye, ikaibuka skandali ya Lugumi, na kwa hakika sikuchoka kupiga kelele, hususan kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kama inavyoonekana hapa chini 



Sambamba na kelele hizo hatimaye niliamua kuandika MAKALA HII 


Ni matarajio yangu makubwa kuwa makala hii itamhamasisha kila msomaji kuwa na msimamo, na kisha kusimama imara katika msimamo huo, sambamba na kuhakikisha kuwa anachosimamia ni sahihi, na kuendelea kuupigania hadi mafanikio yapatikane. Sio kazi rahisi lakini mara nyingi vitu vizuri, au vinavyodumu, huwa havipatikani kirahisi. 

Mwaka 2006, niliandika MAKALA HII kuhusu suala la mkataba wa kufua umeme, uliopelekea skendo ya Richmond, na nikaendelea kupiga kelele hadi mwaka Februari 2008 baada ya mhusika mkuu katika skendo hiyo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujiuzulu. Hata hivyo, ishu hiyo ilinigharimu mno kimaisha. 

Na hivi majuzi, nilijaribu ‘kuwashikia bango’ wahusika wa Mamlaka ya Mawasiliano TCRA, na nikawatwanga MAKALA hii. 


Siku chache baadaye, bosi wa taasisi hiyo akatumbuliwa. 


Na majuzi tu, Ubalozi wetu hapa Uingereza ulitaka kutufanyia 'uhuni' katika ziara ya Waziri Mkuu, ambapo awali kulikuwa na mpango wa kumkutanisha Waziri Mkuu na kundi dogo tu la Watanzania wanaoishi hapa. Kelele nilizoshiriki kuibua zilisaidia, na hatimaye mkutano huo wa Waziri Mkuu ulifanywa kuwa wa wazi kwa kila Mtanzania mkazi wa hapa kuhudhuria. Nimeelezea kwa kirefu kuhusu sakata hili katika MAKALA HII.

Sitaki kujisifu kuwa kelele zangu pekee ndio zinapelekea hatua kusudiwa kuchukuliwa. Hapana. Ninachojaribu kuonyesha ni ushiriki wangu katika harakati za kudai mabadiliko kwa kupitia maandishi, “kelele zetu” iwe hapa bloguni, kwenye mitandao ya kijamii au kwa njia ya makala. Pia, kwa kuwaeleza wasomaji kuhusu mafanikio ya 'kelele zetu' inasaidia kuhamaisha watu wengi zaidi kutambua umuhimu wa harakati kama hizi katika kuleta mabadiliko kusudiwa


Mara nyingi tunapopiga kelele hizo tunaishiwa kukebehiwa, kuonekana vimbelembele, tusio na vitu muhimu vya kufanya katika maisha yetu binafsi, na shutuma kama hizo. Lakini pindi kelele zetu zinapozaa matunda, walewale waliokuwa wakitukebehi huwa mstari wa mbele “kusaka sifa.” 

Kimsingi, harakati hizi sio za kusaka ujiko au madaraka. Ni kile nilichoeleza awali: kuwa na msimamo na kusimama thabiti katika msimamo huo hadi ufumbuzi wa tatizo husika upatikane.

Nimalizie makala hii kwa kumpongeza sana Rais Magufuli kwa ‘kumtumbua’ Kitwanga. Wanaohisi kuwa kutambuliwa huko ni ‘kuficha kombe’ la ishu ya Lugumi, ombi langu kwao ni wavute subira. 

Sakata la Lugumi sasa litachukua sura mpya, na tusishangae kusikia watu wakiburuzwa mahakamani hivi karibuni. Pia suala hili la kutambuliwa Kitwanga linaweza kumpa fursa Rais Magufuli fursa ya kuwatumbua angalau mawaziri mawili hivi ambao mwenendo wao umekuwa wa kusuasua. Fursa ya kuwatumbua inatokana na kutambuliwa kwa Kitwanga ambako kutamlazimu Rais kufanya ‘reshuffle’ ndogo.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.