30 May 2016

Mitandao ya jamii imeturahisishia maisha kwa kiasi kikubwa. Sasa tunaishi katika dunia kama kijiji ambapo tukio likotokea sehemu moja ya dunia linafahamika sehemu nyingine muda huohuo bila kutegemea radio, runinga au gazeti pekee. Kadhalika, mitandao ya kijamii imetuwezesha kufahamiana na watu wengi popote walipo duniani bila kukutana ana kwa ana.

Pamoja na mazuri mengi ya mitandao ya kijamii, kuna upande wa pili usiopendeza kuhusu mitandao hiyo ya kijamii. Licha ya kutupatia fursa ya kufahamiana na watu mbalimbali muhimu, mitandao hiyo pia imetoa fursa kwa watu waovu wanaoitumia kwa minajili ya kufanya maovu yao.

Katika makala hii ninaongelea kuhusu tishio kubwa na lililotapakaa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, ambapo watu waovu huweka hufungua akaunti feki na kuweka profile feki zinazoambatana na picha za warembo wa kuvutia. Watu hawa wanaweza kuwa aidha wanawake au wanaume lakini hiyo haijalishi kwa sababu lengo lao sio zuri.

Wanachofanya ni rahisi. Wanafungua akaunti feki kwa maana ya jina na taarifa husika, kisha wanaweka picha kadhaa za msichana mrembo. Picha zinazotumika zaidi ni za warembo wa Afrika Kusini. Kama wengi wetu tunavyofahamu, mabinti wengi wa nchi za Kusini mwa Afrika wamejaliwa shepu zenye mvuto. Kwahiyo, tapeli husika anaweka picha kama tano hivi kwa kuanzia, nyingi au zote zikiwa katika pozi za kuvutia kama sio kutamanisha.

Baada ya hapo wanaanza kuomba urafiki (friend requests) kwa kasi ya kimbunga. Kwa makadirio ya chini, mara baada ya kukamilisha profiles zao feki, matapeli hao hutuma friend requests kati ya 100 hadi 300 kwa mkupuo.

Jinsi ya kuwatambua sio ngumu sana. Cha muhimu nikuzingatia kanuni muhimu ya matumizi ya mtandao (Internet) yaani "ukiona ni kizuri kupita maelezo, basi kitlie shaka," wanasema "if it is too good to be true, them may be it is not true." Kanuni hiyo pia ina umuhimu mkubwa katika matumizi ya barua-pepe. Ukipata email kutoka kwa mtu usiyemjua anayedai ana mamilioni ya dola na anataka kuweka kwenye akaunti yako, huyo ni tapeli tu. Hakuna mtu mwenye akili timamu, hata awe tajiri kiasi gani, ambaye yupo tayari kumpatia mtu japo dola 10 tu (achilia mbali hayo mamilioni) mtu asiyemjua.

Kwahiyo, ukipata friend request kutoka kwa binti mrembo kupindukia ilhali hamjuani, basi washa king'ora cha tahadhari. Kitu cha kwanza kabisa ni kuangalia profile husika. Angalia mtu huyo amejiunga lini na Facebook. Pili angalia idadi ya marafiki wapya. Ukikutana na profile inasema "X amekuwa friends na Y na watu 100 au zaidi (kwa mkupuo)" basi uwezekano mkubwa ni kwamba huyo ni tapeli 'anakulia taimingi..'

Kingine ni kuangalia aina ya marafiki zake, Mara nyingi matapeli wa aina hiyo hujifanya wa jinsia ya kike lakini friends wao wengi kabisa kama sio wote ni wanaume. Sio dhambi wala kosa la jinai kwa mwanamke kuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike lakini 'unapaswa kuchezwa na machale.'

Lakini ili kupata uthibitisho zaidi, unaweza ku-save moja ya picha za mtu huyo kwenye computer yako kisha nenda kwenye ukurasa wa kutafuta utambulisho wa picha kwenye Google. 

Ngoja nikuelekeze jinis ya kutumia tovuti hiyo inayoitwa Google Image.

1. Kwanza, ni rahisi zaidi kuitumia Google Image kutafuta utambulisho wa picha kwenye computer kuliko kwenye simu au tablet. Kwahiyo maelezo ninayotoa hapa ni ya kutumia Google Image kwa computer na sio simu au tablet. Andika anwani hii https://images.google.com 


2. Ukishaingia hapo, bonyeza hapo kwenye alama ya kamera kwa ajili ya ku-search kama ilivyo pichani3. Ukishabonyeza hapo, bonyeza palipoandikwa 'upload an image' kama inavyoonekana pichani,4. Kisha bonyeza palipoandikwa 'choose file.'5. Baada ya kubonyeza hapo, nenda sehemu uliyo-save ile picha unayohisi ni feki.6. Upload picha hiyo7. Angalia matokeo 

Njia hiyo hapo juu ni muhimu sana sio kwa ajili ya kuangalia kama picha ni feki kwenye Facebook tu bali kwa kuhakiki picha mbalimbali unazokutana nazo mtandaoni.

Hata hivyo, wakati mwingine matokeo ya Google Images search yanaweza yasikupe jibu unalotarajia. Ushauri wangu ni kuzingatia tahadhari nilizotoa awali. Na kumbuka, "if it is too good to be true, may it is not true."

Waweza ku-accept friend request na kusubiri kama huyo 'binti' ataanzisha maongezi nawe. Mara nyingi, akianzisha maongezi, anaweza kukuomba namba ya simu au ya  Whatsapp. Ukimwomba yake atakwambia simu imeharibika aua imeibiwa. Sasa katika mazingira ya kawaida tu, waweza kushawishika kusema "basi nitakununulia simu mpya" au "nitakutumia simu mpya." Hapo utakuwa umeshajigeuza ATM.

Hata hivyo, haina maana kuwa kila binti mrembo atakaye-request friendship kwenye Facebook ni tapeli. Na sio kila friend atakayekuomba msaada kwa Facebook ni tapeli. Kuna watu wanaomba misaada ya dhati. Cha muhimu ni "kuwa na machale."

Ni muhimu kutambua kuwa ushauri niliotoa hapo juu haumaaniishi kwamba 'matapeli wa Facebook' ni mabinti au wanawake pekee. Tunaishi zama za ajabu kabisa ambapo kuna ' vijana wengi tu wa kiume au wanaume wazima wanaowinda akinadada au kinamama wa kuwalea au kuwatapeli.' Kwahiyo ushauri huo ni kwa jinsia zote. 

Kwa akinadada au kinamama , ukikutana na 'handsome boy' mwenye dalili kama hizo hapo juu, basi ni muhimu kuskilizia 'machale' yako. Ndio kuna akina Brad Pitt kibao ambao bado wapo single na wanatafuta marafiki wa kike au wenza, lakini wengine ni matapeli tu.

Endelea kutembelea blogu hii kwa makala mbalimbali kama hii na nyinginezo. Na ususahau ku-share na mwenzio kwa sababu SHARING IS CARING.

1 comment:

  1. Suala hapo kwa wengi na ndio hata mimi natamani niwe hivyo kwa kiwango cha juu ni uwezo wa machale...nifanyeje (nitumie mbinu gani ili kujijengea uwezo mzuri wa machale?)

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube