27 Sept 2016

Naomba anayefahamiana na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dkt Charles Kimei, amfikishie ujumbe huu kwa njia yoyote mwafaka.

Ndugu Dkt Kimei,

Nakuandikia barua hii ya wazi nikiwa na masikitiko makubwa kutokana na huduma zisizoridhisha za benki unayoiongoza. Nimekuwa mteja wa benki yenu kwa zaidi ya miaka kumi sasa, nikitumia huduma ya Tanzanite Account, maalum kwa ajili ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi.

Tarehe 20/09/2016 nilitumiwa barua pepe ikieleza kuwa uboreshaji (upgrade) wa huduma za kibenki kwa kutumia intaneti ulikamilika tarehe 19/09/2016 na kuwa tayari kwa matumizi saa 12 jioni (kwa saa za Tanzania). Hata hivyo, kulijitokeza matatizo ya kiufundi, na licha ya kuomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza, alifahamisha kuwa wateja wangejulishwa pindi matatizo hayo yakitatuliwa 
Siku moja baadaye, tarehe 21/09/2016 nilitumia barua-pepe nyingine yenye maelezo ya jinsi ya kuingia kwenye akaunti yangu. Nilielezwa pia kuwa tarakimu za siri (one time key) za kuniwezsha kuingia kwenye akaunti yangu zimeshatumwa kwa SMS kwa namba yangu ya simu inayoishia na namba ***2957, na kama sijapata tarakimu hiyo ya siri basi niwasiliane na benki kwa barua-pepe [email protected]


Nilipoangalia SMS zangu sikuona ujumbe wowote kutoka Tanzania. Nikadhani kwamba labda SMS hiyo itakuja mara baada ya kufuata maelekezo ya kuingia kwenye akaunti yangu. Nikafanya hivo, hakuna SMS iliyotumwa kwangu. Baada ya hapo nikatuma barua pepe kwa anwani [email protected] Hiyo ilikuwa tarehe 21/09/2016Kuonyesha kuwa wahusika huko CRDB sio watu makini, katika jibu lao kwangu wakaniomba niwapatie namba yangu ya simu japo awali walieleza kuwa nitapata tarakimu ya siri kwa namba niliyosajili kwa benki hiyo. 


Sijawahi kuitaarifa CRDB kuwa nimebadili namba yangu ya simu, sasa ni kituko kusikia wakiniomba niwapatie namba yangu ya simu. Je walipoteza namba yangu niliyoisajili kwao? Sidhani, kwa sababu katika email ya awali walieleza kuwa tarakimu ya siri ingetumwa kwa namba yangu yenye kuishia namba ***2957. Kama wanayo, kwanini waombe tena niwatumie namba yangu? Je hii haitoshi kumpa hofu mteja kuhusu usalama wa habari (data) zake katika benki hiyo?


Sikujibiwa. Nikawaandikia tena na tena na tena, lakini sijajibiwa hadi wakati ninaandika makala hii


Baadaye nikasema labda nijaribu kuwasiliana na benki hiyo kupitia akaunti yao katika mtandao wa kijamii wa Twitter, lakini ilikuwa kazi bure kama sehemu ya maongezi yetu inavyoonyesha hapo chini. Pia nilijaribu kutumia huduma ya mwasiliano ya maongezi (chat service) kwenye tovuti ya benk hiyo lakini nilitumia zaidi ya masaa mawili bila kupata mtu wa kuongea nami. Pia nilijaribu kutumua SMS kwa namba ya huduma kwa wateja, sikujibiwa. Nikajaribu kutuma ujumbe kwa Whatsapp, pia sikujibiwa.Nilichobaini baada ya kujaribu kuwasiliana na CRDB huko Twitter ni kwamba kuna wananchi kadhaa ambao pia hawaridhishi na huduma za benki hiyo. Kwa lugha nyingine, mie sio mwathirika pekee wa huduma za kiwango cha chini za benki hiyo.

Sasa naomba nilikabidhi suala hili kwako Dokta Kimei. Haikubaliki kabisa kwa mteja wenu kunyimwa huduma za kibenki katika intaneti (internet banking) kwa takriban wiki nzima sasa kwa sababu ya uzembe tu. 

Kwenu wasomaji wa makala hii, ninaomba kuwafahamisha kuwa kama kuna mtu yeyote amekumbana na huduma mbovu iwe kwa hawa jamaa wa CRDB au huduma yoyote ile - na ana ushahidi - basi naomba uwasiliane nami ili angalau tuwafikishie ujumbe wa husika hadharani namna hii, na pengine kuwaumbua kwa uzembe wao au huduma zao mbovu.  Kukalia kimya huduma mbovu ni sawa na kuridhika nazo. Huduma bora kwa mteja sio suala la fadhila bali haki na stahili ya mteja.

UPDATE: Hatimaye tatizo langu limetatuliwa kwa jithada kubwa za Msimamizi wa Huduma za benki kwa intaneti, Bi Sarah Nzowa. Ninamshukuru kwa msaada mkubwa alionipatia

1 comment:

  1. Ndugu chahali , pole kwa changamoto hiyo uliyoipata , lakini bila shaka tatizo lako limekwisha tatuliwa na wahusika wa huduma ya internet banking .

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube