23 Sept 2016

NIANZE makala hii kwa kurudia salamu zangu za rambirambi kwa vifo vya Watanzania wenzetu 17 na pole kwa majeruhi 440 kutokana na tetemeko la ardhi maeneo ya Ukanda wa Ziwa, hususan mkoani Kagera.
Pia ningependa kutumia fursa hii kumshukuru Diwani William Rutta wa Kata ya Ishozi, wilayani Missenyi, mkoani Kagera, kwa kutumia muda wake kipindi hiki kigumu kunitumia barua pepe kuhusu janga hilo la tetemeko la ardhi lililoharibu nyumba 2,063 huku 14,081 zikiwa katika hali hatarishi, 9,471 zikiwa zimepata uharibifu mdogo na wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
Licha ya pongezi zake kwa makala yangu katika gazeti hili toleo la wiki iliyopita, Diwani huyo alielezea masikitiko yake kuona vyombo vya habari vikiitaja Wilaya ya Bukoba tu kuhusu tetemeko hilo ilhali waathirika wengi wapo wilayani Missenyi.
Kadhalika Diwani huyo alitoa wito kuwa tofauti zetu za kisiasa zisituondolee uzalendo na kutoa wito kwa watu na taasisi mbalimbali kuendelea kutoa michango ya hali na mali kwa waathirika wa tetemeko hilo, sambamba na kuhakikisha michango iliyokwishatolewa inawafikia walengwa.
Baada ya shukrani hizo, nigusie kuhusu mijadala ya chinichini inayoendelea, angalau katika mitandao ya kijamii ya Watanzania kuhusu kinachoelezwa kuwa ni ukimya wa Rais Dk. John Magufuli katika janga hilo la tetemeko la ardhi.
Katika kumtendea haki Rais Magufuli, ukweli ni kwamba hajawa kimya kama inavyoelezwa. Mara baada ya kupata taarifa ya janga hilo, rais alitoa salamu zake za rambirambi siku hiyo ya tukio kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Lakini binafsi ninawaelewa vema wanaohoji 'ukimya' wa Rais wetu kuhusu janga hilo. Kwamba Dk Magufuli sio tu ni Rais wetu bali pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na pengine anatarajiwa kusikika kwa 'maneno ya mdomo' (na sio tamko tu la maandishi) akizungumzia suala hilo. Na pengine wanaohoji 'ukimya' wake walitarajia angekwenda eneo la tukio (hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni 'mwenyeji' wa maeneo yaliyokumbwa na janga hilo). Hata hivyo, binafsi ninataraji kuwa rais atazuru huko hivi karibuni tu.
Kadhalika, kwa vile rais ndiye mkuu halisi wa serikali, taasisi yenye jukumu la usalama wa wananchi, basi huenda wanaohoji ukimya wake wanatarajia yeye kuongoza jitihada za serikali kuwapatia uhakika waathirika wa tetemeko hilo, sio tu kwa kuongoza jitihada za michango ya kuwasaidia wahusika bali pia kuonekana katika eneo la tukio.
Na vile vile, licha ya ukweli kwamba kuna kundi fulani ambalo limejiapiza kumkosoa Dk. Magufuli kwa kila atakalofanya, wanaohoji ukimya wake sio tu wanaruhusiwa na Katiba kufanya hivyo bali pia wanaweza kuwa wanamsaidia rais wetu ili kuepusha uwezekano wa lawama za upungufu wa kiuongozi katika nyakati za majanga.
Licha ya wanachokitafsiri kuwa ni ukimya wa rais, wanaozungumzia suala hilo pia wameonesha kuguswa na Rais Magufuli na watangulizi wake wawili, yaani marais wastaafu Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa kutojitokeza kwenye matembezi ya hiari yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kuwachangia waathirika wa tetemeko hilo la ardhi. Matembezi hayo yaliongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye kiumri ni mkubwa zaidi ya Dk Magufuli, Kikwete na Mkapa.
Binafsi nadhani pengine isingekuwa mwafaka kiusalama kwa rais aliyepo madarakani na watangulizi wake watatu kushiriki matembezi hayo kwa pamoja, japo ingewezekana baadhi yao au wote kumpokea mwenzao aliyeongoza matembezi hayo. Hata hivyo, sidhani kama suala hili ni muhimu zaidi ya ukweli kuwa matembezi hayo yaliyowezesha kupatikana zaidi ya shilingi bilioni moja zikiwa ni michango na ahadi.
Kama nilivyotanabaisha awali, kuna wenzetu ambao ni kama wamejiapiza kumkosoa Magufuli kwa lolote atakalofanya, hata liwe zuri kiasi gani. Kana kwamba hilo sio tatizo, kuna wenzetu wengine ambao kwa mtazamo wao, mtu yeyote anayemkosoa rais hata kama ni kwa sababu halali basi mtu huyo ni adui wa taifa. Makundi haya mawili yanafanya mijadala ya kitaifa kuwa migumu.
Nimalizie kwa kutoa pongezi kwa wote waliochangia na wanaochangia misaada kwa waathirika wa tetemeko hilo, hususan marais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya, mabalozi wa nchi mbalimbali nchini Tanzania, taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, washiriki katika matembezi ya kuwachangia waathirika wa tetemeko, pamoja na wanaofanya michango ya kiroho kwa njia ya sala au dua.
Mungu ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.