29 Dec 2016


ATIMAYE mwaka 2016 unafikia ukingoni ambapo siku nne zijazo tutaingia mwaka mpya 2017. Makala hii inafanya tathmini ya jumla ya matukio makubwa zaidi, hususan ya kisiasa, kitaifa na kimataifa.
Tukio kubwa zaidi kimataifa ni kuyumba kwa itikadi ya siasa za kiliberali katika nchi za Magharibi, suala lililokwenda sambamba na kukua kwa siasa za mrengo mkali wa kulia. Kadhalika, nchi kadhaa za Magharibi zinaendelea kushuhudia ujio wa zama mpya za siasa, zinazojulikana kama ‘post-truth,’ ambazo kwa tafsiri fupi ni ‘kupigia chapuo uongo, na upinzani dhidi ya ukweli.’
Ni katika mazingira hayo, kulijitokeza mshtuko mkubwa katika nchi hizi za Magharibi, na pengine duniani kwa ujumla, pale Uingereza ilipoamua kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) katika kura ya maoni iliyofanyika mwezi Juni. Kampeni za kura hiyo zilijenga msingi imara wa siasa za ‘post-truth.’
Miezi mitano baadaye, Marekani nayo ilikumbwa na wimbi hilo la siasa za ‘post-truth,’ pale mfanyabiashara bilionea, Donald Trump, aliyekuwa na kila sifa mbaya ya kumnyima japo ‘ujumbe wa nyumba kumi,’ alifanikiwa kumbwaga mwanasiasa mkongwe, Hillary Clinton. Trump na wafuasi wake walitumia kila aina ya hadaa huku wakisaidiwa na mlipuko wa habari zisizo za kweli hususan katika mitandao ya kijamii.
Kinachotisha kuhusu zama hizi za siasa za ‘post-truth’ ni ukweli kwamba zimekumbatiwa na vyama vya siasa na vikundi vyenye mrengo mkali kabisa wa kulia, pamoja na vyama/vikundi vya kibaguzi.
Kinachoendelea kusaidia ‘uongo kuwa muhimu kuliko ukweli’ ni ukweli kwamba tabaka la siasa, tabaka la uongozi, tabaka la wanataaluma na wataalamu, tabaka la wafanyabiashara, na makundi kama hayo, yanaangaliwa kama yaliyoweka pamba masikioni. Hayasikii vilio vya tabaka la watu wa chini, na hata wakisikia hawafanyii kazi vilio hivyo.
Ndio maana, watu ‘hatari’ kama vile Nigel Farage wa hapa Uingereza, Donald Trump huko Marekani, Marine Le Pen wa Ufaransa, Norbert Hofer wa Austria (ambaye almanusura ashinde urais wa nchi hiyo), Geert Wilders wa Uholanzi, Frauke Petry wa Ujerumani na kadhalika, wamemudu kutumia uongo na hadaa kwa ufanisi kutokana na ‘ukweli’ kupoteza maana yake.
Mashambulizi ya kigaidi huko Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani na kuendelea kuwepo kwa tishio la vitendo hivyo kumeongeza umaarufu wa siasa za mrengo mkali wa kulia ambazo zinahusisha ugaidi na sera za ukarimu kwa wahamiaji.
Mwaka 2017 unatarajiwa kushuhudia michuano mikali ya kisiasa barani Ulaya ambapo nchi zinazotupiwa jicho zaidi ni Ufaransa na Ujerumani zinazokabiliwa na hatari ya kuwa chini ya utawala wa wanasiasa wenye mrengo mkali kabisa wa kulia.
Kwa huko nyumbani, tishio kubwa halikuwa kwenye siasa bali ajali zinazoendelea kugharimu maisha ya Watanzania kwa idadi kubwa, japo janga hilo halionekani kuwasumbua wananchi na viongozi.
Kwenye ulingo wa siasa, Rais ‘mpya’ Dk. John Magufuli ndiye aliyetawala zaidi katika anga za siasa. Kwa upande mmoja, hali hiyo ilitokana na matumaini makubwa waliyonayo wananchi kwake, na kwa upande mwingine, udhaifu unaozidi kukua miongoni mwa vyama vya upinzani.
Hata hivyo, kwa kulinganisha kasi aliyoanza nayo na hali ilivyo sasa, yayumkinika kusema kuwa ‘kasi ya Magufuli imepungua.’ Huku ‘tumbua majipu’ ikizidi kuwa ya msimu (na baadhi ya utumbuaji ukituhumiwa kufanywa kutokana na majungu), sera iliyowapa matumaini makubwa, ya kuanzishwa kwa mahakama maalumu ya ufisadi iliyogeuka kuwa kichekesho ambapo tangu mahakama hiyo ianzishwe imeendesha kesi moja tu.
Na kituko kikubwa zaidi ni pale waziri mwenye dhamana ya mahakama hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, alipotuhadaa kuwa uchache wa kesi katika mahakama hiyo ni dalili ya mafanikio, yaani ufisadi umepungua.
Lakini kama kuna suala ambalo baadhi yetu tunapata shida mno kumwelewa Rais Magufuli ni ‘kutengeneza maadui wasio wa lazima.’ Hatua za kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya upinzani na kukatisha matangazo mubashara ya vikao vya Bunge ni hatua ambazo sio tu hazikuwa na tija bali hazikuwa na umuhimu wowote.
Matumizi ya sheria ya makosa ya mtandao pale tu rais anapotukanwa, huku maelfu kwa maelfu ya Watanzania wakiendelea kuwa waathirika wa matusi imetufanya baadhi ya ‘tulioupigia debe’ muswada wa kuanzisha sheria hiyo tujilaumu.
Jinsi serikali ilivyowatimua wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kana kwamba walijichagua wenyewe kujiunga na masomo, na kuwakashifu kuwa ni ‘vilaza,’ uamuzi wa kutishia ajira za mahakimu wasio na shahada za chuo kikuu, kupuuza jitihada za Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete za kuwashawishi Watanzania wa Diaspora kushiriki katika harakati za maendeleo huko nyumbani na badala yake ‘kuwaharamisha’ kwa kuwazuia kumiliki ardhi, na hatua kama hizo, ni baadhi ya mambo yaliyotawala zaidi mwaka huu katika siasa za Tanzania.
Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kurejesha nidhamu ya kazi, angalau kwa kujenga mwamko wa wananchi kutegemea kipato halali badala ya shughuli zilizo kinyume cha sheria. Na japo matukio ya ujambazi yameendelea kutawala, kumekuwa na dalili nzuri ya kupungua biashara ya dawa za kulevya na ujangili. Na kama tetesi kuhusu uwezekano wa mabadiliko ya baraza la mawaziri hivi karibuni ni za kweli, basi huenda ‘timu mpya’ ikaufanya mwaka ujao kuwa ‘mwema’ zaidi kwa Watanzania.
Nimalizie makala hii kwa kuahidi kuwaletea ubashiri wa mwenendo wa mambo mbalimbali kwa mwaka kesho katika makala ijayo.
Nawatakia heri ya mwaka mpya 2017

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali 

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube