12 Oct 2018NANI KAMTEKA MO DEWJI? UCHAMBUZI WA KIINTELIJENSIA KWA KUTUMIA MBINU YA 'CONTRARIAN' IJULIKANAYO KAMA DEVIL'S ADVOCATE

Changamoto kuu mbili katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia (intelligence analysis) ni, moja, kutambua taarifa stahili/mwafaka za kuzifa
nyia uchambuzi husika, na mbili, ni kitu kinachofahamika kama 'cognitive bias,' yaani kwa lugha nyepesi ni kama upendeleo/ubaguzi wa aina flani ambao unatokea akilini bila kuamua kwa makusudi.

Kwa mfano, mchambuzi ambaye ni kada wa CCM akipewa jukumu la kuchambua suala linalohusu Chadema, basi anaweza kuwa anaendeshwa na ubaguzi flani kichwani pasi yeye kukusudia.
Kwahiyo, hata katika uchambuzi huu wa kiintelijensia, huenda kukawa na cognitive bias, lakini hilo sio lengo langu, na ninadhamiria kuongozwa na taarifa zilizopo kuliko hisia zangu binafsi.

Kuna mbinu kadhaa za kufanya uchambuzi wa kiintelijensia, na miongoni mwa mbinu hizo ni "Contrarian Techniques" ambazo ni "Devil's Advocacy," "Team A/Team B," "High Impact/Low Probability Analysis" na "'What If' Analysis."

Katika uchambuzi huu, nitatumia mbinu ya Devil's Advocacy ambayo hutumika zaidi katika mazingira ambayo tayari kuna hisia flani 'kali' kuhusu suala husika.

Tukio ninalolifanyia uchambuzi wa kiintelijensia ni kama nilivyotanabaisha kwenye kichwa cha habari, nalo ni la kutekwa kwa Mkurugenzi wa kundi la Makampuni ya Mohamed Enterprises, Mohammed Dewji almaarufu 'Mo.' Tukio hilo lilitokea jijini Dar es Salaam jana alfajiri, katika eneo la ukumbi wa Colosseum.

Mbinu ya uchambuzi wa kiintelijensia ya Devil's Advocacy ni mwafaka katika tukio hili kwa sababu kuu moja: utafutaji wa taarifa za kiintelijensia uliofanywa tangu baada ya kupatikana taarifa za tukio hilo, kwa kutumia njia kuu moja ya ukusanyaji taarifa za kiintelijensia – Open Source Intelligence (OSINT) – unaonyesha kuwa serikali inatupiwa lawama kuwa ndiyo iliyohusika kwenye tukio hilo.

Na kama ilivyoelezwa awali, mbinu ya Devil's Advocacy ni mwafaka katika mazingira ambayo tayari kuna hisia flani 'kali' kuhusu suala husika, na hapa hisia hiyo kali ni uhusika wa serikali.

Katika kutumia mbinu hii, kuna hatua kadhaa zinazopaswa kufuatwa na mchambuzi, na miongoni ni kama ifuatavyo:

·        →Kuorodhesha hisia mbalimbali
·       → Kuchagua hisia kuu moja au mbili katika hizo mbalimbali, inayoonekana kuwa na uzito zaidi
·        →Rejea taarifa zilizopatikana kuhusiana na tukio husika
·        →Onyesha ushahidi unaoweza kufanya hisia husika kuwa na uzito zaidi.

Kwahiyo tuanze uchambuzi huu kwa kuorodhesha hisia mbalimbali kuhusiana na kutekwa kwa Mo Dewji. Hisia hizi zimekusanywa kwa kutumia ukusanyaji taarifa kupitia vyanzo vya wazi, yaani Open Source Intelligence (OSINT).

Hisia hizo ni kama ifuatavyo:

·        Mo Dewji ametekwa na serikali
·        Mo Dewji ametekwa na watu wanaohusiana na serikali lakini hawakutumwa na serikali (rogue elements)
·        Mo Dewji ametekwa na watu wanaotaka kuichafua serikali
·        Mo ametekwa na wahalifu
·        Mo ametekwa na washirika/maadui zake kibiashara
·        Mo hajatekwa, ni maigizo tu.

Tupitie kila hisia ili kuweza kubakiwa na hisia kuu moja au mbili.

Mo Dewji ametekwa na serikali:

Uzito wa hisia: Rekodi ya serikali sio nzuri katika usalama wa raia mbalimbali, kuanzia "kupotea" kwa kada wa Chadema Ben Saanane na kwa mwanahabari Azory Gwanda, na idadi isiyojulikana ya watu waliopotea huko MKIRU. Kadhalika, matukio yanayohusisha 'watu wasiojulikana' na shambulizi dhidi ya Mbunge Tundu Lissu yanaongeza uzito kwenye hisia hii. Vilevile ukweli kwamba eneo la Colosseum limezungukwa na nyumba mbalimbali za viongozi na taasisi muhimu zenye ulinzi mkali, na hakukuwa na jitihada za kukabiliana na watekaji, zinaweza kuashiria uhusika wa serikali.

Mapungufu ya hisia: Serikali haina incentive katika kumteka Mo Dewji. Kwamba kama kulikuwa na tatizo lolote kama ni kisiasa au kiuchumi basi angeweza tu kukamatwa au "kubebeshwa kesi ya kodi" na TRA au "kesi ya ufisadi" na TAKUKURU. Ieleweke kuwa Mo Dewji alijiweka mbali na masuala ya siasa, na yayumkinika kuamini kuwa hana maadui wa kisiasa. Kadhalika, high profile ya Mo Dewji ilitosha kuijulisha serikali kuwa lolote litakalomtokea mfanyabiashara huyo litakuwa na athari kubwa kwake.

Hitimisho: Mapungufu dhidi ya hisia hii ni makubwa zaidi ya uzito wake. Kwahiyo inaondolewa.

Mo Dewji ametekwa na rogue elements ndani ya serikali:

Uzito wa hisia hii: Kwa kurejea matukio mbalimbali hususan yanayohusishwa na Daudi Albert Bashite, yayumkinika kuhisi uwepo wa mkono wa rogue elements huko TISS au kwingineko. Uzito zaidi kwenye hoja hii unachangiwa na jinsi Bashite alivyojaribu kuwa mstari wa mbele kuelezea kuhusu suala hilo, badala ya kuwaachia polisi wafanye kazi yao.

Mapungufu ya hisia hii: Huenda mkakati huo ungefahamika mapema kwa taasisi kama TISS na hivyo kuweza kuzuiliwa kabla haijatekelezwa. Hata hivyo, kuna mapungufu katika hoja hii ambayo ni ishara zinazoashiria mapungufu makubwa ya kiutendaji ya TISS, kiasi kwamba inawezekana taarifa hizi hawakuzipata.

Hitimisho: Hisia hii ina mantiki, na itaendelea kuwepo katika uchambuzi huu

Mo Dewji ametekwa na watu wanaotaka kuichafua serikali

Uzito wa hisia hii: Uzito upo kwenye ukweli kwamba upinzani mkubwa dhidi ya serikali ya Rais John Magufuli upo zaidi ndani ya CCM kuliko nje ya chama hicho. Ikizingatiwa kuwa kuna takriban miezi 24 tu kabla ya uchaguzi mkuu ujao, wapinzani wa Magufuli wanaweza kufanya tukio hilo kwa minajili ya kumchafua, na pengine kujenga hoja ya kumwekea vikwazo kwenye kugombea urais mwaka 2020. Kwa kuzingatia incentives, wapinzani hao wana kila cha kunufaika na kidogo cha kupoteza (a lot to gain and only a little to lose).

Mapungufu ya hisia hii: Mkakati mkubwa kama huu ungeweza kunaswa kirahisi tu na vyombo vya dola kama vile TISS na hivyo kuweza kuudhibiti. Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwenye hisia iliyopita, kuna ishara za mapungufu ya kiutendaji kwa taasisi hiyo, hali ambayo inaweza kuwa iliruhusu mpango huu kutekelezwa.

Hitimisho: Hisia hii ina mantiki, na inaendelea kubaki kwenye uchambuzi huu.

Mo Dewji ametekwa na wahalifu:

Uzito wa hisia hii:  Kuna taarifa za uwepo wa magenge ya kihalifu ya kimataifa nchini Tanzania. Taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa watekaji ni 'wazungu' zinaweza kusaidia kuipa uzito zaidi hisia hii.

Mapungufu ya hisia hii: katika mazingira ya kawaida, wahalifu hao wasingependelea sehemu kama Colesseum kuwa eneo la utekaji kwa sababu kuna idadi kubwa na nyumba za viongozi na taasisi za serikali ambazo zina ulinzi mkali. Hata hivyo, yawezekana kuwa wahalifu hao walishafanya reconnaissance ya kutosha na kubaini mapungufu husika.

Hitimisho: Hisia hii japo ina mantiki lakini kiuhalisia inaonekana kuwa sio yenye nguvu. Kwahiyo inaondolewa.

Mo Dewji ametekwa na washirika/maadui wake kibiashara:

Uzito wa hisia hii: mfanyabiashara wa kimataifa kama Mo Dewji hawezi kukosa maadui. Lakini pia masuala ya biashara za kimataifa yanaweza kuzua migongano hata miongoni mwa washirika katika biashara husika. Kama ilivyokuwa kwenye hisia iliyotangulia, yawezekana watekaji hao walishasoma mapungufu ya kiusalama katika eneo la tukio.

Mapungufu ya hisia hii: Kama ilivyokuwa kwenye hisia iliyopita, mazingira ya eneo la tukio hayakuwa mwafaka kwa watu wenye lengo la kumdhuru mtu kuyatumia kutekeleza lengo hilo. Hata hivyo, yawezekana wahusika walishabaini mapungufu ya kiusalama katika eneo hilo.

Hitimisho: Hisia hii ina mantiki lakini uwezekano wa washirika/maadui wa Mo Dewji kumteka katika mazingira yalivyokuwa, haiingii sana akilini. Hisia hii inaondolewa kwenye uchambuzi huu.

Mo Dewji hajatekwa ni maigizo tu:

Uzito wa hisia hii: Kwa kuzingatia matukio ya huko nyuma, yawezekana tukio hili ni mchezo wa kuigiza tu.

Mapungufu ya hisia hii: Mchezo wa kuigiza ili iweje? Hakukuwa na tukio la muhimu ambalo jamii ilipaswa "kuzugwa na kutekwa kwa Mo Dewji." 

Hisia hii inaondolewa kutokana na kukosa mashiko.
Kwahiyo, hisia zinazosonga mbele ni mbili,
       Mo Dewji ametekwa na watu wanaohusiana na serikali lakini hawakutumwa na serikali (rogue elements)
       Mo Dewji ametekwa na watu wanaotaka kuichafua serikali

Hisia hizi mbili zinaweza kimsingi kuwa moja, kwa sababu watu wenye nia ya kuichafua serikali wanaweza kuzitumia rogue elements kufanya kazi hiyo. Lakini pia rogue elements hizo zinaweza kuwatumia watu wanaotaka kuichafua serikali kutekeleza azma hiyo.

Na kwa minajili ya kuweka rekodi sawia, kiongozi wa rogue elements hizo ni Daudi Albert Bashite, bila shaka. Na hili linaweza kuongezewa uzito na ukweli kwamba jana Bashite alijigeuza kama RPC au Mkuu wa Kanda Maalum ama sio msemaji wa Jeshi la Polisi. Je ni ile "mchawi aliyemroga marehemu hujifanya mwenye uchungu kuliko wafiwa"?

Uchambuzi wa kiintelijensia sio sayansi timilifu kwa asilimia 100 (it's not exact science), na kwa maana hiyo inawezekana kabisa sababu ikawa nyingine nje kabisa ya hizi nilizozichambua.

Ninachofanya hapa sio kujifanya mjuaji bali kuchangia kwenye 'body of knowledge,' sambamba na kuhamasisha mjadala kuhusu suala hili ambalo linaweza kuwa na athari kubwa kwa Tanzania.

Hitimisho: Ingependeza kuhitimisha makala hii kwa kutamka bayana kuwa "hisia kuu ni hii" lakini hisia mbili zilizoweza kuvuka mchujo zinabaki kuwa mtazamo ninaona ni mwafaka zaidi.
Je wewe una mawazo gani?


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube