6 Feb 2023

Watu wengi wanafahamu faida ya mazoezi ya viungo, na sehemu ambayo watu wengi hupendelea kwenda kufanya amzoezi hayo ni kwenye gym.

Kama ilivyo kwa viungo, ubongo nao unahitaji mazoezi. Na kuufanyisha ubongo mazoezi kunaelezwa kama “kuupeleka ubongo wako gym.”

Na kama ambavyo mazoezi ya viungo hayahitaji ushinde gym kutwa nzima, mazoezi ya ubongo nayo yanahitaji muda kidogo tu. Na kama ambavyo huwezi kupata “six packs” baada ya kuhudhuria gym siku chache tu, kuvuna matunda ya kuupelekea ubongo wako gym hakuwezi kutokea kwa muda mfupi tu.

Kwahiyo, kama ambavyo unahitaji ratiba ya mazoezi ya viungo, mazoezi ya ubongo pia yanahitaji ratiba.

Mazoezi hayo ni kama ifuatavyo

Kuupigisha ubongo push-ups

 1. Andika shukrani kuhusu kitu kimoja ulichofanya au ulichonacho. Kuna uthibitisho wa kisayansi kuwa shukrani zina faida kwa ubongo. Neno la kimombo ni gratitude.

 2. Fanya tahajudi. Zoezi rahisi kabisa la tahajudi ni kuvuta pumzi ndani kisha kuibana kwa sekunde chache kisha kutoa pumzi puani au hata mdomoni kisha kuibana tena. Unaweza kufanya raundi 4 au zaidi. Tahajudi kwa kiingereza ni meditation.

 3. Pima uwezo wako wa kukumbuka vitu. Andika vitu viwili vitatu kisha jaribu kuvikumbuka baada ya saa moja hivi bila kuangalia ulichoandika.

Jiandikie mwenyewe

 1. Chagua mada yenye umuhimu kwako.

 2. Andika bila kuwa na hisia kuwa unachoandika kitasomwa na mtu mwingine.

 3. Usijali kuhusu makosa ya sarufi au mpangilio wa unachoandika

Baada ya siku nne, unaweza kuacha zoezi hilo, na baadaye unaweza kurudi kusoma ulichoandika japo sio lazima. Umuhimu wa zoezi hili haupo katika ulichoandika bali kitendo cha kuandika.

Jifunze kitu kipya

Kuna faida lukuki za kujifunza kitu kipya.Tafiti zinaonyesha kuwa moja ya njia za kuufanya ubongo wako kuwa makini ni kujifunza kitu kipya. Vilevile, kukifunza kitu kipya husaidia kukabiliana na msongo wa mawazo.

Baadhi ya njia za kujifunza kitu kipya

 1. Soma kitabu

 2. Sikiliza podcast (haya ni maongezi yanayorekodiwa, yaani kama YouTube vile lakini ni ya sauti (audio). Mfano wa podcast ni hii ya Jasusi

 3. Jiunge na kozi ya mtandaoni. Unaweza kuanzia hapa “AdelPhil Online Academy” ambacho ni “chuo cha Jasusi”.

 4. Shiriki mdahalo.

 5. Jifunze lugha mpya.

 6. Angalia video za TED (haya ni maongezi ya watu mbalimbali - wengi ni maarufu - kuhusu mada muhimu).

 7. Jifunze ujuzi mpya.

 8. Mfunze mtu kitu flani (hii ni njia nzuri ya kumudu kitu hata kama unajifunza kuhusu kitu hicho. Kufundisha husaidia kukidumisha kichwani kitu unachofundisha).

Kuwa mbunifu

Sayansi inathibitisha kuwa shughuli za ubunifu kama muziki, kuchora, kuchonga, kufinyanga, kufuma, nk “hutekenya” ubongo. Uzuri ni kwamba kuna makundi mbalimbali mtaani au hata mtandaoni yanayojihusisha na shughuli za ubunifu.

Hitimisho

Endapo unahitaji msaada wa ziada katika eneo lolote kati ya hayo yaliyotanabaishwa hapo juu, wasiliana na kocha wako wako.0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.