Showing posts with label BABU WA LOLIONDO. Show all posts
Showing posts with label BABU WA LOLIONDO. Show all posts

9 Jun 2011


Mkala yangu katika toleo la wiki hii la jarida maridhawa la Raia Mwema inazungumzia suala la "tiba ya Babu wa Loliondo".Nimejaribu kuelezea kwanini kwa muda mrefu nimechelea kuzungumzia suala hilo,nikitanabaisha uwepo wa suala la imani katika "tiba ya Babu",nafasi ya tiba zisizo za kisayansi katika jamii (hususan nafasi ya waganga wa kienyeji) na uelewa wangu kitaaluma kama mwanafunzi wa zamani wa sosholojia ya dini.

Pamoja na makala hii,jarida la Raia Mwema limesheheni habari na makala nyingine mbalimbali zenye kiwango cha hali ya juu.Kwa sasa,soma makala husika hapa chini

RAIA MWEMA UGHAIBUNI

Vipi twawa tegemezi kwa tiba zisizo za kisayansi?

Evarist Chahali, Uskochi
Juni 8, 2011

PAMOJA na kuvuma kwa habari za “tiba ya Babu wa Loliondo”, nimekuwa nikichelea kuzungumzia suala hilo kwa sababu kadhaa za msingi. Kwa sasa yaweza kuelezwa kwamba Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kilutheri la Kiinjili Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile ni mmoja wa watu maarufu nchini Tanzania. Na kwa nini asiwe maarufu; ilhali kuna maelfu ya Watanzania wanaoamini kuwa Mchungaji huyo anaweza kuponya magonjwa kadhaa sugu ikiwemo upungufu wa kinga mwilini (ukimwi)?

Nimechelea kuzungumzia suala hili kwa sababu, kwanza, suala hili linagusa imani. Kwa mujibu wa maelezo ya “Babu”, uwezo wa kuponya magonjwa sugu alipewa na Mungu ndotoni. Mimi ni Mkristo, na katika imani yetu tunaamini kuwa Mungu anaweza kumpa binadamu kipawa cha kufanya miujiza ikiwa ni pamoja na kutibu magonjwa sugu.

Hata hivyo, pamoja na Ukristo wangu, sina ujuzi wa kutosha wa Maandiko Matakatifu japo huwa napata wasaa wa kuyasoma. Na miongoni mwa yanayoelezwa katika Biblia Takatifu ni jinsi Mungu alivyomtuma mwanaye Yesu Kristo katika ubinadamu wake kuwafunulia wanadamu kuhusu ukombozi wa kiroho. Na moja ya mengi aliyofanya Yesu ni miujiza ya uponyaji.

Kwa mantiki hiyo, uponyaji ni jambo linalowezekana katika imani ya Kikristo. Hata kabla ya habari za “Babu wa Loliondo” tulishawahi kusikia habari za “watumishi wa Mungu” waliodaiwa kufanya uponyaji. Majina kama Father Nkwera, Esther wa Mikocheni na wengineo, yamezoeleka masikioni mwa Watanzania wengi.

Kwa hiyo, kwa wanaoamini kwenye nguvu ya Mungu katika uponyaji kupitia watumishi wake, uwezekano wa Mchungaji Mstaafu Mwasapile kuponya sio jambo la ajabu sana. Hata hivyo, hadi hapa simaanishi kuwa madai ya Mchungaji huyo ni ya kweli au ni uzushi tu.

Kwa upande mwingine, ninatoka katika ukoo ambao mmoja wa ndugu zangu ni mganga maarufu. Nisingependa kumtaja jina lakini ana umaarufu mkubwa huko wilayani Kilombero. Baba yangu huyo mdogo alirithishwa uganga na bibi yake aliyekuwa akitembelewa katika makazi yake huko Malinyi (wilayani Ulanga, mkoani Morogoro) na watu kutoka sehemu mbalimbali za nchi yetu.

Ndugu yangu huyo ni Muislamu na anatibu kwa kutumia mitishamba na Maandiko Matakatifu ya dini yake. Kutokana na ukaribu wetu, nilipata fursa ya kudadisi mengi kutoka kwake. Kubwa nililojifunza katika utoaji wa huduma zake za tiba kwa watu wanaohitaji huduma yake, ni umuhimu wa imani katika ufanisi wa tiba hizo. Mara kadhaa alinieleza kuwa ili tiba anazotoa ziwe na ufanisi, ni lazima kwa mtumiaji wa tiba husika awe na imani sambamba na kufuata masharti ya tiba aliyopewa.

Ukaribu wangu na ndugu yangu huyo uliniwezesha pia kuifahamu jinsi jamii yetu ilivyo tegemezi kwa tiba zisizo za kisayansi! Kama ilivyo kwa “Babu wa Loliondo”, vigogo kadhaa walikuwa miongoni mwa wateja wakubwa wa baba yangu huyo mdogo.

Suala jingine lililosababisha nichelee kujadili “tiba ya Babu wa Loliondo” ni ukweli kwamba wakati ninasomea Shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilifanya kozi ya Sosholojia ya dini (Sociology of Religion). Na kwa bahati nzuri, mhadhiri wa kozi hiyo alikuwa pia ni Padre wa Kimarekani, Dokta Father John Sivalon wa Kanisa Katoliki jijini Dar (wakati huo).

Kimsingi, somo hilo lilihusu nafasi ya dini kwenye jamii; kwa maana ya jinsi dini husika inavyotendeka, historia yake, maendeleo yake na mada mbalimbali kuhusu dini husika duniani. Sosholojia ya dini haijihusishi na filosofia ya dini; kwa maana ya kupima ukweli wa imani katika dini husika. Kwa hiyo, uwepo wa Padre kama mwalimu wa somo hilo haukuathiri alichokuwa akifundisha. Kadhalika, katika nyakati tofauti, tulipata fursa ya kutembelewa na viongozi mbalimbali wa dini kutufundisha kuhusu imani za dini zao.

Kama sehemu ya kozi hiyo, mimi na wanafunzi wenzangu watatu tulifanya utafiti mdogo kuhusu vikundi vipya vya kidini. Utafiti wetu ulifanyika katika kanisa moja “jipya” jijini Dar es Salaam. Kwa kifupi, moja ya matokeo ya utafiti huo yalikuwa ufahamu kuwa wengi wa waliojiunga na kanisa hilo walikuwa na matatizo ya aina Fulani kama vile ya kazi, familia, afya nk.

Kadhalika, wengi kati ya tuliowahoji walibainisha kuwa waliamua kuachana na dini zao za awali baada ya dini hizo kushindwa kuwapatia ufumbuzi wa matatizo yao. Ikumbukwe kuwa asili ya dini (kisayansi jamii) ni katika harakati za mwanadamu kupata mahala pa kuelekeza matatizo yake. Kidini, asili ya dini ni habari tofauti na inatofautiana kati ya dini moja na nyingine.

Ili kuelewa kwa nini “njia za mkato” za matatizo ya mwanadamu katika jamii yetu, kwa misingi ya imani, zinapata umaarufu, ni muhimu kufahamu kwamba kabla ya ujio wa dini “kuu” nchini Tanzania, kilichokuwepo ni dini za kitamaduni za Kiafrika (African Traditional Religions).

Japo sensa zetu za idadi ya watu zimekuwa zikikwepa kuainisha mgawanyiko wa Watanzania kwa misingi ya imani zao za kidini, ukweli ni kwamba dini kuu tatu huko nyumbani Tanzania ni Ukristo, Uislamu na Upagani (ambao wanajumuisha pia wale wasio na dini). Na hadi sasa, Upagani umeendelea kuwa sehemu muhimu miongoni mwa Wakristo na Waislamu. Na ndio maana mila na desturi zetu zimeendelea kushamiri; licha ya jitihada za mapadre na mashehe kuzikemea; hususan pale zinapokinzana na mafundisho ya dini hizo.

Kwa hiyo, ninaamini kuwa hadi hapa utaelewa kwa nini nimekuwa na wakati mgumu kukemea au kuafiki habari za “tiba ya Babu wa Loliondo”. Lakini nafasi yangu inakuwa ngumu zaidi kutokana na ukweli kwamba kadri ninavyoelimika ninatarajiwa na jamii kuangalia mambo “kisomi” zaidi; kwa maana ya kuchambua mambo kwa misingi ya kanuni za sayansi au sayansi jamii.

Kisayansi au kisayansi jamii, kinachoitwa tiba ya Babu wa Loliondo ni sawa na tetesi tu; kwa vile hakuna uthibitisho wa kitaaluma kuwa “tiba” yake inaponya. Natambua kuwa kuna idadi ndogo ya watu wanaodai kupona baada ya kupata tiba hiyo, lakini kitakwimu idadi hiyo ni ndogo sana kuhalalisha hitimisho la uhakika.

Lakini kikubwa kinachozua wasiwasi kuhusu “tiba” hiyo ni kukosekana kwa ushuhuda wa waliopona baada ya kupewa “kikombe cha Babu”. Yayumkinika kuamini kuwa hadi sasa takriban Watanzania nusu milioni wameshapata “kikombe”. Hivi kweli hatungeweza kusikia japo wenzetu 1,000 wakitoa ushuhuda wa kupona kansa (hata kama kilichowapeleka “kwa Babu” ni ukimwi)? Kulikoni habari zinazovuma zaidi (hasa kwenye gazeti moja la kila siku), ni za halaiki ya wanaokwenda kupata “kikombe” na sio ya walioponyeshwa?

Nimelazimika kuandika makala hii baada ya kusoma habari kwamba idadi ya watu walikwishapoteza maisha (katika harakati za kupata tiba hiyo) hadi sasa inazidi 100. Nikiangalia hawa wenyeji wangu hapa Uingereza wanavyohangaika pindi kinapotokea kifo cha mtu mmoja tu, nafadhaika kuona Serikali yetu ikiendelea na “sintofahamu” katika suala hili la “tiba ya Babu wa Loliondo”.

Ni rahisi kuwalaumu Watanzania wanaohangaika kwenda kwa “Babu”, lakini ni muhimu kuelewa kuwa kama Serikali inaonekana kuafiki kuwa “tiba” hiyo ina ufanisi, kwa nini basi wananchi nao wasiamini? Unaposikia viongozi kadhaa wakifunga safari zao kwenda kupata “tiba ya Babu” huku taratibu za kiserikali zikitumika kana kwamba ni sehemu ya sera ya afya, mwananchi wa kawaida anaweza kabisa kushawishika kuamini habari za “tiba” hiyo.

Serikali yoyote makini duniani ingeshtushwa na taarifa kuwa zaidi ya watu 100 wameshapoteza maisha yao katika harakati zao za kupata “tiba ya Babu wa Loliondo”. Lakini tutegemee nini kutoka kwa serikali isiyoonekana kushtushwa na mamia ya wananchi wanaonyang’anywa maisha yao kutokana na ajali za barabarani ambazo kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na kushamiri kwa rushwa katika Jeshi la polisi kitengo cha Usalama Barabarani?

Siombei hili litokee, lakini ukweli ni kwamba jambo pekee litakaloiamsha serikali yetu kuchukua hatua stahili katika suala hili la “tiba ya Babu wa Loliondo”, ni pale kigogo mmoja atakapokumbwa na zahma katika harakati za kupata, au baada ya kutumia, “tiba ya babu”.

Kama ambavyo umeme wetu umekuwa ukitegemea kudra za Mwenyezi Mungu, inaelekea sasa sekta ya afya nayo imeachwa katika mikono ya akina “Babu wa Loliondo” na ndivyo pia Watanzania watakavyozidi kuzama katika utegemezi wa tiba zisizo za kisayansi.

Ni jambo la ajabu na la kushangazaa kwamba yote haya yanatokea wakati nchi yetu inajiandaa kusherehekea nusu karne tangu ipate uhuru! Ndiyo, miaka 50 ya Uhuru!

CHANZO: Raia Mwema

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.