MOJA ya mada zinazotawala
vyombo vya habari huko nyumbani ni zoezi linaloendelea la bomoabomoa. Zoezi
hilo limepokelewa kwa hisia tofauti huku baadhi ya wananchi wakiliunga mkono
(hususan wasioguswa nalo) huku wengine wakiilaumu (hususan waathirika wa zoezi
hilo)
Kwa upande mmoja serikali
na mamlaka husika zipo sahihi kutekeleza zoezi hilo kwa vile suala hilo licha
ya kuwa la muda mrefu lakini pia limekuwa na gharama kubwa, kwa serikali na
mamlaka husika, kwa maana ya kuwakwamua wakazi wa mabondeni kila yanapojiri
mafuriko, na kwa wakazi hao kukumbwa na hasira kubwa kila msimu wa masika.
Kwa maana hiyo, ilikuwa
lazima kwa serikali kufika mahala kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo.
Na kwa kiasi kikubwa, hakukuwa na njia ya mkato au ufumbuzi rahisi. Na vyovyote
ambavyo ingeamuliwa, ilikuwa lazima wakazi hao wa mabondeni waondoke, aidha kwa
hiari yao wenyewe au kwa serikali na mamlaka husika kuwaondosha.
Tayari baadhi ya watu
wameanza kuhusisha zoezi la bomoa bomoa na upungufu wa Rais Dk. John Magufuli.
Sidhani kama wanamtendea haki. Sawa, tunatambua kuwa kubomolewa makazi na
kukosa makazi mbadala si kitu kizuri. Lakini hata hivyo, si Dk. Magufuli au
serikali yake iliyowashauri wakazi wa mabondeni kuendelea kuishi katika
mazingira hatarishi.
Na kama nilivyoeleza
awali, mara nyingi wakazi hao wanapokumbwa na mafuriko, serikali hulazimika
kuingia gharama ili kunusuru maisha yao. Kwa hiyo, katika mazingira ya kawaida
tu, kwa minajili ya kuepusha gharama hizo, ilikuwa lazima kwa serikali kuchukua
hatua stahili.
Lakini pia serikali ina
jukumu la kuhakikisha usalama wa raia wake. Kuendelea kuwaachia wakazi wa
mabondeni kuishi katika mazingira hatarishi kungekuwa ni sawa na serikali hiyo
kuzembea kutekeleza jukumu hilo la msingi, yaani jukumu la kuhakikisha usalama
wa raia.
Hata hivyo, pamoja na
dhamira nzuri ya serikali katika utekelezaji wa zoezi hilo, pengine ni muhimu
kuupa nafasi ubinadamu. Kimsingi, makosa yaliyosababisha uwepo wa makazi
hatarishi mabondeni ni ya pande zote mbili: serikali na mamlaka husika, kwa
upande mmoja, na wakazi hao, kwa upande mwingine.
Si kwamba siku moja
tuliamka na kukuta nyumba zimejengwa mabondeni au kwenye hifadhi za barabara.
Misingi ya nyumba ilichimbwa, matofali na vifaa vingine vya ujenzi vililetwa,
na ujenzi ukafanyika, na hatimaye wakazi hao kuhamia maeneo hayo, na muda wote
huo, serikali na mamlaka husika walikuwepo na hawakuchukua hatua stahili. Japo
sio kisingizio mwafaka kwa wakazi hao, lakini kwa serikali na mamlaka husika
kutozuia ujenzi huo wakati huo inaweza kuwa ilichangia sio tu kuwafanya
waliokwishajenga hapo kudhani wana ruhusa isiyo rasmi bali pia kuliwavuta
wengine wasio na mahala pa kujenga.
Sasa, kama wasemavyo
waswahili yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo, la muhimu kwa sasa
ni kupata ufumbuzi utakaozinufisha pande zote mbili.
Kwa vile ujumbe
umekwishafika, kwa maana ya wakazi waliosalia mabondeni wamekwishaona
yaliyowakuta wenzao, basi sidhani kama kuna ubaya wa kutoa muda wa kutosha na
wa kiuhalisia wa kuwaagiza wakazi hao kuhama kwa hiari yao. Kumpa mtu wiki moja
ahame sehemu aliyoishi kwa miaka kadhaa sio kuzingatia uhalisia.
Kama iliwezekana kuwapa
wakwepa kodi matajiri siku kadhaa walipe madeni, licha ya ukweli kuwa kukwepa
kodi ni kosa la jinai, na matokeo yake (tunaambiwa) wengi walitekeleza agizo
hilo, basi kwa nini tusijaribu njia hiyo hiyo kwa wakazi wa mabondeni?
Kwa upande mwingine, japo
ujenzi wa mabondeni sio tu ni kinyume cha sheria lakini pia unahatarisha maisha
ya wakazi husika, madhara yake kwa jamii sio makubwa kama matatizo mengine ya
dharura yanayohitaji kushughulikiwa haraka, hususan biashara ya dawa ya kulevya.
Ndio, makazi mabondeni
yanahatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo, lakini angalau hayahatarishi
uhai wa wasiokaa mabondeni. Vipi kuhusu dawa za kulevya? Yanapoteza uhai wa
vijana wetu kila kukicha huku yakichangia uhalifu kwa kiwango kikubwa. Naam, mtumia
dawa za kulevya akikosa fedha ya kununulia dawa hizo, njia ya mkato ni kufanya
uhalifu.
Kwa maana hiyo biashara
ya dawa ya kulevya ina madhara makubwa kwa jamii kuliko makazi ya mabondeni.
Lakini kinachoanza kuvunja moyo ni ukimya wa serikali katika kushughulikia
suala hilo ambalo lilipewa kipaumbele cha hali ya juu na Rais Dk. Magufuli
alipotangaza dira ya serikali yake wakati anazindua Bunge jipya.
Sambamba na suala la dawa
za kulevya ni suala la ufisadi. Ndio, ziara za kushtukiza zimezaa matunda lakini
kumekuwa na ukimya kidogo hapa katikati, na sio wa ziara hizo tu bali pia hata
utekelezaji wa uanzishwaji wa mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za
ufisadi.
Siku chache zilizopita
nilikutana na habari kuhusu Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe,
kuwa amebaini kuna rushwa katika Mahakama. Hilo sio suala geni, na binafsi
nilishangaa kusikia Waziri Mwakyembe amebaini sasa ilhali ripoti mfululizo za
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikiitaja
Mahakama kama miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa rushwa. Je, Waziri
Mwakyembe hakuwa akizisoma au kuzisikia habari hizo?
Lakini kilichonikera
zaidi ni ukweli kwamba wakati wa mjadala wa ufisadi wa Tegeta-Escrow,
zilipatikana taarifa zilizoonyesha majina ya baadhi ya majaji waliopokea mgao
uliotokana na ufisadi huo. Hadi leo, majaji hao hawajachukuliwa hatua.
Kadhalika, ziliwahi kupatikana taarifa zilizowataja majaji waliotuhumiwa
kuwasaidia watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya. Hata hao wanasubiri kuundwa
kwa mahakama za ufisadi?
Na tuwe wakweli, hivi
kuunda mahakama za ufisadi kunahitaji muda gani hasa ilhali tayari tuna mfumo
wa mahakama unaoshughulikia kesi za jinai?
Rais Dk. Magufuli
alituasa tumsaidie katika vita dhidi ya maovu mbalimbali yanayoikabili nchi
yetu. Kumsaidia si kwa kupiga vigelegele pekee zinapofanyika ziara za
kushtukiza au fulani anapofukuzwa kazi bali pia kukosoa pale inapobidi.
Matarajio ya wananchi bado yapo juu, na hii ni muhimu sana kwa mafanikio ya
mapambano dhidi ya uozo mwingi unaohitaji kushughulikiwa. Kasi hafifu ya
kushughulikia matatizo ya ufisadi na uhalifu – kama biashara ya dawa za kulevya
– sio tu yaweza kupunguza ari ya wananchi lakini pia yaweza kutoa mwanya kwa
wahusika kubuni mbinu mpya, sambamba na kuvutia wahalifu wapya (hususan wale
wanaobaini kuwa Shamba la Bibi limefungwa).
Nimalizie makala hii kwa
kukumbushia haja ya kuitumia vizuri fursa hii kuikwamua Tanzania yetu kutoka
kwenye lindi la umasikini, unaochangiwa na ufisadi na uhalifu mwingine,
sambamba na kuweka vipaumbele vyetu sawia kwa kushughulikia matatizo ya haraka
badala ya yale yanayoweza kushughulikiwa taratibu. Ndio, Waingereza wanasema
“two wrongs don’t make a right,” yaani kufanya kosa la pili hakulifanyi kosa la
kwanza kuwa jambo sahihi, na kwa maana hiyo sina maana kuwa kutochukuliwa hatua
dhidi ya ‘wauza unga’ kunahalalisha kutofanya bomoa bomoa. Hata hivyo, haja ya
kuwashughulikia wahalifu ni ya dharura mno kuliko ya wakazi wa mabondeni.