
Ndani ya tofauti zao bao
Waingereza wamtukuza Malkia Elizabeth wa Pili
Tangu Ijumaa iliyopita, Uingereza
imekuwa katika shamrashamra za maadhimisho ya miaka 60 ya utawala wa Malkia
Elizabeth wa Pili. Sherehe hizo za siku tano mfululizo zinaweza kusaidia sana
kuonyesha ni jinsi gani kiongozi huyo wa heshima wa taifa hili
anavyowaunganisha Waingereza, licha ya tofauti zao za hapa na pale.
Kama nilivyoeleza katika makala yangu
ya toleo lililopita, ‘muungano’ unaounda nchi iitwayo The United Kingdom of Great
Britain (England, Uskochi na Wales) and
Northern Ireland unakabiliwa na upinzani unaoweza kutishia uhai wake huko mbeleni.
Pia nilieleza jinsi ‘chama tawala’ hapa Uskochi, SNP, chini ya uongozi wa
Waziri wa Kwanza (mithili ya Waziri Mkuu), Alex Salmond, kilivyoanza mchakato
wa kuhamasisha kura ya ‘ndiyo’ kwenye referendum ya kuamua kama Uskochi
ijitenge na Uingereza.
Japo sherehe hizo za miaka 60 ya
utawala wa Malkia Elizabeth hazijapata msismko mkubwa sana kwa huku Uskochi
lakini ukweli unabaki wazi kuwa Malkia huyo anabaki kuwa kiungo muhimu kwa nchi
hii. Na pengine sherehe hizo zinaweza kutoa picha nzuri kwa Salmond na chama
chake kuhusu ugumu unaowakabili katika azma yako ya kuifanya Uskochi iwe ‘nchi
huru.’
Kwa sie wageni katika nchi hii,
sherehe hizo na jinsi zilivyoonekana kuwa na umuhimu wa kipekee kwa Waingereza
wengi kunatupa fundisho moja la msingi: uwepo wa mtu au itikadi inayolifanya
taifa lishikamane.
Kwa huko nyumbani tulibahatika kuwa
na Baba wa Taifa, Marehemu Mwalimu Julius Nyerere ambaye licha ya kuwa muumini
mkubwa wa umoja na mshikamano, pia alifanya jitihada kubwa ya kueneza imani
hiyo ndani na nje ya Tanzania, hususan kusini mwa Bara la Afrika.
Kwa mujibu wa mila zetu za Kiafrika
si vema kumlaumu marehemu. Kwa msingi huo kuna ugumu wa kutosha katika
kuzungumzia mapungufu au makosa ya Mwalimu. Lakini kwa vile Mwalimu aliipenda Tanzania,
angetamani kuona jitihada zake zikienziwa kwa namna moja au nyingi, basi
ninaamini hata angekuwa hai asingechukia kumjadili kwa minajili ya ustawi wa
taifa letu.
Moja ya mapungufu machache aliyofanya
Baba wa Taifa ilikuwa kutomwandaa mrithi wake wakati wa utawala wake na hata
baada ya kung’atuka. Ni vigumu kuwa na sababu sahihi ya kwanini Nyerere
hakutaka au hakuona umuhimu wa kuandaa mrithi wake lakini moja ya sababu za
kufikirika inaweza kuwa labda hakuona mwanasiasa mwenye sifa stahili za
kukabidhiwa jukumu hilo.
Inawezekana pia kuwa labda kwa vile
Mwalimu hakupenda ubaguzi wa aina yoyote ile basi huenda ingekuwa vema
kutoandaa mrithi bali mwenendo wa kisiasa upewe fursa ya kutoa viongozi
wanaostahili.
Kwa bahati mbaya (au makusudi?) mengi
ya mazuri aliyofanya Nyerere yalianza kuhujumiwa muda mfupi tu baada ya yeye
kuondoka madarakani. Kubwa zaidi lilikuwa kile kinachoitwa Azimio la Zanzibar
ambalo inaelezwa kwamba lilisimamiwa na mtangulizi wa Baba wa Taifa, Rais wa
Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Wakitumia ‘upole’ wa Mwinyi, baadhi
ya wanasiasa waliokuwa wakisubiri kwa hamu Nyerere aachie ngazi katika uongozi
wa serikali na chama walishinikiza Azimio hilo la siri (hadi sasa sijawahi
kuona chapisho rasmi la CCM kuhusu Azimio hilo) na kuua Azimio la Arusha. Kwa
lugha nyingine, Azimio hilo lilivunja itikadi ya Ujamaa iliyowezesha umoja na mshikamano wa Watanzania
.
Pengine Nyerere angeweza kupambana na
‘uhuni’ huo lakini nadhani aliamua kutumia busara kutopingana na wana-CCM
wenzie hasa ikizingatiwa kuwa kufanya hivyo kungeweza kuzua hisia kwamba ana
tamaa ya madaraka na anaingilia kazi za marais waliomtangulia.
Kwa hilo ninaweza kumlaumu tena
Mwalimu kwa sababu katika mazingira ya kawaida tu huwezi kumwachia mtu abomoe
kitu ulichotumia miongo kadhaa kukijenga. Licha ya hilo, ni wazi kuwa Baba wa
Taifa alifahamu kuwa watu aliowaamini kuwa ni wafuasi wake wazuri walikuwa
mithili ya mbwa mwitu waliojivika ngozi ya kondoo: wanasiasa waliosimama
majukwaani kuhubiri umoja na usawa lakini mioyoni walikuwa wakisubiri fursa ya
kujitajirisha kupitia migongo ya Watanzania wenzao masikini.
Nimejaribu kutoa nadharia hapo juu
kuhusu sababu ambazo pengine zilimkwaza Nyerere kuandaa mrithi wake. Lakini
Azimio la Zanzibar lilipaswa kumtahadharisha kuwa kuondoka kwake madarakani
kunaweza kabisa kuipeleka Tanzania kusikostahili. Kwa maana hiyo, kama
angetaka-na kwa vile hata baada ya kung’atuka serikalini na kwenye chama
aliendelea kuwa na nguvu na mvuto mkubwa-angeweza kufanya jitihada binafsi
kuipatia Tanzania kiongozi mwenye sifa ambazo angalau zinakaribiana naye.
Katika stadi zinazohusu hali ya mambo
ilivyo sasa huko nyumbani, na zile zinazobashiri hali itakavyokuwa huko mbeleni,
kuna mwafaka wa kitaaluma kwamba kukosekana kwa itikadi ya kuwaunganisha
Watanzania ni moja ya matishio makubwa kwa umoja na ustawi wa taifa letu.
Itikadi ya Ujamaa sio tu ilifanikiwa
kwa kiasi kikubwa kutufanya Watanzania tujione kitu kimoja lakini pia ilimudu
kwa kiasi kikubwa kuzuwia nyufa kama za udini na ukabila kuhatarisha umoja
wetu.
Sasa tumebaki kama watoto yatima,
hatuna mwelekeo unaoeleweka na wengi wa Watanzania wanaogopa kufikiria nchi
yetu itakuwaje, kwa mfano, miaka 50 kutoka sasa. Na hatuwezi kuwalaumu
wanaoogopa, kwa sababu wakati mwingine inalazimu kuangalia wakati uliopo tu
hasa pale ambapo hakuna namna ya kuufanya wakati ujao uwe bora kuliko sasa.
Leo hii ukiwauliza Watanzania
wanafikiri mwanasiasa gani ndani ya chama tawala anafaa kumrithi Rais Jakaya
Kikwete atakapomaliza muda wake mwaka 2015, uwezekano mkubwa ni kupata jibu
hili la kukatisha tamaa, “sioni mwanasiasa yeyote yule anayeweza kutuondoa
katika lindi hili la umasikini linalorutubishwa na vitendo vya ufisadi.”
Wananchi wengi wamekata tamaa hasa
baada ya kushuhudia nyingi ya ahadi za kutia matumaini zilizotolewa kwenye kila
Awamu zikiishia kubaki ahadi tu pasipo kuleta mabadiliko kusudiwa.
Pengine kukata tamaa huko kunaweza
kuwa na faida kwa vyama vya upinzani iwapo vitaweza kujitambulisha vya kutosha
kwa wananchi na kuwahakikishia kuwa vina jipya zaidi ya CCM.Kwa vile chama
hicho tawala ni sababu muhimu ya wananchi wengi kukata tamaa, wapinzani wakionyesha
kuwa wanaweza kutekeleza yake yaliyoshindikana kwa CCM basi hakuna sababu ya
wao kutochukua hatamu za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Ukiangalia vurugu zinazoendelea huko
Zanzibar ni rahisi kubaini kuwa ukosefu wa itikadi inayotuunganisha unachangia
kutokuwepo kwa hatua mwafaka za kushughulikia na hatimaye kumaliza matatizo ya
Muungano na kudhibiti kuchipuka kwa hisia za ubaguzi wa kidini.
Kufanya hali mbaya kuwa mbaya zaidi,
ukosefu huo wa itikadi ya kutuunganisha unakuwa tatizo kubwa zaidi
unapojumlishwa na kutokuwa na mwanasiasa “anayeweza kusema na akasikilizwa”
mithili ya Nyerere: yaani hatuna kitu wala mtu wa kutuunganisha.
Ndio maana wakati Waingereza
wanasherehekea miaka 60 ya utawala wa Malkia Elizabeth na jinsi
unavyowaunganisha, sie tusio na mtu wala itikadi ya kutuunganisha tunakuwa
katika wakati mgumu sana: kutamani tusichokuwa nacho na hapohapo kuvunjwa
matumaini kwa vile hakuna dalili za tatizo hilo kupatiwa ufumbuzi (angalau
ndani ya chama tawala).
Lakini licha ya ukweli huo wa
kuumiza, kuna habari ya kuleta matumaini: uzalendo. Katika mazingira
tuliyonayo, Kinachohitajika zaidi si mtu au itikadi (japo ni muhimu) bali kiu
kwa kila anayeipenda Tanzania kutimiza wajibu wake kwa maslahi ya nchi yetu.
Tukiweza kuweka kando ubinafsi na kuepuka unafiki na tabia isiyopendeza ya
kufanya mambo kwa minajili ya kupata fedha au sifa, tunaweza kwa umoja wetu wa
kizalendo kuwa sio tu warithi wa Nyerere bali pia umoja wetu huo kuweza kuondoa
ombwe linalotokana na ‘kifo’ cha itikadi ya Ujamaa.
Tunaweza kuendelea kumlaumu Nyerere
kwa kutotuandalia mrithi wake, na tunaweza kuendelea kuwalaani milele walioua
itikadi ya Ujamaa, lakini kwa bahati mbaya lawama na laana haziwezi kubadili chochote.
Mkoloni hakutupa uhuru kwa sababu tulimlaumu kwa kututawala pasipo ridhaa yetu,
na Nduli Idi Mani hakusalimu amri kwa vile tu tulimlaani kwa kila namna.
Kilichomwondoa mkoloni ni jitihada za kizalendo za kudai uhuru wetu na
kilichomtimua Amin ni umahiri na ujasiri wa majeshi yetu chini ya uongozi
thabiti wa Nyerere.
Kwa kuwa kila Mtanzania mwenye akili
timamu anataka tuendelee kuishi kwa amani pasipo kubaguana kwa misingi ya dini
au kabila, na hakuna anayetaka kuona Wabara wakiambiwa wahame Zanzibar (na
majuzi tumesikia kuna vipeperushi vinavyowataka Wapemba waondoke Unguja), na
hakuna anayefurahia umasikini wetu licha ya raslimali lukuki tulizonazo, basi
uzalendo ni jukumu la kila Mtanzania. Nia tunayo, sababu tunayo, na njia tunayo
(uzalendo), kinachohitajika sasa ni utekelezaji kwa vitendo.
Yes
we can!