Showing posts with label EXCLUSIVE INTERVIEW. Show all posts
Showing posts with label EXCLUSIVE INTERVIEW. Show all posts

25 Apr 2010




Kama nilivyoahidi siku chache zilizopita kuwa blogu yako ingekuletea mahojiano mengine exclusive kutoka kwa mmoja wa Watanzania wanaotuwakilisha vema,leo natimiza ahadi hiyo kwa kuwaletea exclusive interview na msanii mahiri wa Bongoflava,anayefahamika kama Mzee wa Commercial.Huyo si mwingine bali ni Ambwene Yesaya,au AY kama anavyofahamika na wengi.Kama ilivyokuwa katika mahojiano ya Mwana FA,interview hii itapatikana pia katika sura ya Kiingereza (English version).Tuaanza kwanza na WASIFU wa AY kabla ya kuingia kwenye mahojiano kamili.Pata vitu:


MSANII TANGU UTOTONI:
AY alianza kijihusisha na fani ya muziki tangu udogoni.Alipokuwa shule ya msingi alishiriki katika mashindano mbalimbali ya kutafuta vipaji na pia alitumbuiza katika hafla mbalimbali.Mwaka 1996 akiwa high school aliunda kundi la S.O.G lililojumisha wasanii watatu (akiwemo AY) na walirekodi albamu yao ya kwanza mwaka 2000.

KUKUA KISANII:
Mwaka mmoja baadaye,AY aliamua kufanya kazi za kisanii peke yake (solo) na kufyatua albamu yake ya kwanza iliyokwenda kwa jina ‘Raha Kamili’.Wimbo wa kwanza kutambulisha albamu hiyo, ‘Raha Tupu’ ulipata mafanikio makubwa na kukamata chati za vituo vya radio na runinga,na hatimaye kumtambulisha rasmi AY katika anga za muziki nchi Tanzania.
‘Machoni Kama Watu’, single ya pili (kutoka katika albamu ya ‘Raha Kamili’) iliyomshirikisha Lady Jaydee ilifanya vizuri sana kwenye chati mbalimbali za muziki na ulisaidia sana kupaisha mauzo ya albamu hiyo katika soko.

KUJIIMARISHA KISANII:
Mwaka 2005,AY alitoa albamu yake ya pili aliyoipa jina ‘Hisia Zangu’, na ‘Yule’, single ya kwanza kutoka katika albamu hiyo, ilikamata chati mbalimbali za muziki.Katika albamu hii,AY aliwashirikisha wasanii mbalimbali maarufu katika Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Prezzo,Tattuu na Dexu Vultures (wote kutoka Kenya) na msanii Maurice Kirya kutoka Uganda.Hii ilisaidia sana kumtangaza zaidi AY nje ya mipaka ya Tanzania.Single yake ya pili, ‘Binadamu’,ilifanya vizuri sana ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hatimaye kuteuliwa kugombea Tuzo za Kora,jambo lililoandika historia kwani AY ni msanii wa kwanza wa kiume kutoka Tanzania kuteuliwa kugombea Tuzo hiyo.

KUJIKITA ZAIDI KATIKA MUZIKI
Umaarufu wa AY ulizidi kuongezeka hasa baada ya kutoa albamu hiyo ya pili,na sasa alitambulika kama mmoja wa wasanii mahiri wa Afrika Mashariki.Mwaka 2006 alifanikiwa kupata mkataba wa kutangaza kinywaji (kikali) cha ‘Konyagi’ ambacho ni maarufu ndani na nje ya Tanzania.Mkataba huo ulichangia AY kutambulika zaidi kupitia matangazo ya kinyaji hicho,na ulifungua njia kwa makampuni mengine,kama Coca Cola,Vodacom,Celtel (sasa Tigo) na Kilimanjaro Lager kuingia mikataba na msanii huyo.

STAILI:
Staili ya muziki wa AY ni hip-hop inayozungumzia ishu na maisha ya Mwafrika hivi sasa.Maudhui hayo yanawasilishwa kwa ucheshi lakini pia yanaburudisha.Muziki wa AY unawagusa watu wa rika lote.

TUZO:
Msanii huyo amefanikiwa kuteuliwa katika/kushinda tuzo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.Tuzo hizo ni pamoja na
1 Mwaka 2005 aliteuliwa kugombea Tuzo ya Kora katika kundi (category) ya Msanii Bora wa Kiume kwa Afrika Mashariki na Kati.Wimbo ulioteuliwa ni ‘Binadamu’.
2 Mwaka 2006 aliteuliwa kugombea Tuzo za Kisima (nchini Kenya) katika kundi la Msanii Bora wa Kiume kutoka Tanzania.
3 Mwaka 2007 aliteuliza kugombea Tuzo za Kilimanjaro (Kilimanjaro Music Awards) katika kundi la single bora ya hip-hop.
4 Mwaka huohuo aliteuliwa tena kugombea Tuzo za Kisima (nchini Kenya) katika kundi la video bora ya hip-hop kutoka Tanzania.
5 Mwaka 2007 uliendelea kuwa wa mafanikio kwa AY baada ya kuteuliwa pia kugombea Tuzo za Lulu ya Afrika (Pearl of Afrika) katika kundi la single bora ya hip-hop kutoka Tanzania.
6 Mwaka 2008 AY aliteuliwa kugombea Tuzo za Kilimanjaro katika kundi la collaboration (ushirikiano wa msanii zaidi ya mmoja) bora.
7 Mwaka huohuo,msanii huyo aliteuliwa tena kugombea Tuzo za Lulu ya Afrika katika kundi la msanii bora wa kiume kutoka Tanzania.
8 Katika mwaka huo,Akon-msanii maarufu duniani kutoka Marekani,alikiri hadharani kuwa anavutiwa na staili ya muziki wa AY na akamtabiria kuwa anaweza kabisa kuwa msanii kutoka Afrika atakayefanya vizuri katika anga za muziki kimataifa.
9 Mwaka huu,AY ameteuliwa kugombea tuzo kadhaa ikiwa ni pamoja na Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (kundi la video bora na wimbo bora wa mahadhi ya Reggae),Tuzo za Teen Extra za nchini Kenya (kundi la video bora,msanii bora wa mwaka,collaboration bora ya Afrika,wimbo bora wa mwaka Afrika Mashariki,wimbo bora wa hip-hop, na msanii bora wa kiume).
10 Na hivi karibuni AY alishinda kuwa msanii bora wa Afrika Mashariki katika Tuzo za Teenez nchini Kenya.

MAFANIKIO:
Hadi sasa msanii huyo ameshajikusanyia Tuzo sita.Pia vibao vyake 14 vimefanikiwa kukamata chati mara katika ukanda wa Afrika Mashariki.Kibao chake kinachonyanyasa zaidi ni King and Queens (Wafalme na Malkia),na kimepelekea kumpatia tuzo na umaarufu zaidi kimataifa.Wakati mahojiano haya yanafanyika,wimbo wake ‘Habari Ndio Hiyo’ ulikuwa unakamata nafasi ya 10 katika chati za muziki kwa Afrika (Radio Express-Africa Chart).AY amefanikiwa kuwa msanii pekee wa Kitanzania aliyefanya collaboration nyingi zaidi na wasanii wa nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Chameleone na Ngoni (Uganda),Amani,Nameless na Juacali (Kenya), P Square na J. Martini (Nigeria) na wengineo.

Uzinduzi wa albamu za AY umekuwa wa kihistoria na wenye mafanikio makubwa chini ya udhamini wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) na ulifanyika wakati wa matamasha ya wasanii wa kimataifa kama vile Fat Joe,Eve,Shaggy,nk nchini Tanzania.Kadhalika msanii huyo alikuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki tamasha kubwa la kuhamasisha vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi (Music Against HIV/AIDS) liliodhaminiwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).Pia ameshiriki Coke Side of Life Tour kwa Afrika Mashariki,Tamasha la Vijana la Afro Arab nchini Uganda,Tamasha la Kimataifa la Filamu Zanzibar (Zanzibar International Film Festival),na Tamasha la Sauti za Busara.Kadhalika,AY amewahi kualikwa kutumbuiza wakimbiki kutoka Burundi na Rwanda kwa udhamini wa Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR),alitumbuiza katika sherehe za kuukaribisha mwenge wa Olimpiki nchini Tanzania,na mwaka jana alialikwa kutumbuiza katika Tuzo za Muziki za MTV barani Afrika nchini Kenya.Vilevile,msanii huyo ameshatumbuiza katika nchi mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na eneo la Afrika Mashariki,Rwanda,Burundi,Dubai,Afrika Kusini,Marekani na Uingereza.

NINI KIPYA?
Hivi karibuni AY amezindua tovuti yake inayopatikana katika anuani www.ay.co.tz. Pia single yake ya ‘Binadamu’ itakuwa miongoni mwa nyimbo katika albamu inayoandaliwa na kampuni ya kimaifa ya muziki,Warner Music (Africa).Kadhalika,msanii huyo ameingia mkataba wa kutangaza kinywaji (kikali) cha Waragi nchini Uganda sambamba na mkataba na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.Kwa sasa anandaa ushirikiano na wasanii wa kimataifa kama J. Martin wa Nigeria na wengineo kutoka Afrika Kusini na Marekani.


JE WAJUA?
Kwamba jina halisi la AY ni Ambwene Yesaya?
Staili ya AY ni ‘simple and casual’?
AY alizaliwa Julai 5 na nyota yake ni Kansa?
Rangi aipendayo zaidi ni bluu?
Scent (harufu ya perfume au manukato) aipendayo ni DKNY?

Na msanii anayemvutia zaidi duniani ni Dr Dre?.

MAHOJIANO KAMILI YANAFUATA (BONYEZA) HAPA CHINI .

KULIKONI UGHAIBUNI (K.U): Kwanza blogu hii inatoa shukrani kwa kukubali ombi la kufanya mahojiano haya maalum. Pili, hongera sana kwa kuteuliwa na hatimaye kushinda Tuzo za Teneez Kenya 2010.Wasomaji wangependa kufahamu kwanini unajulikana kama Mzee wa Commercial




A.Y: Producer P.Funk ndio alianza kuniita hiyo baada kuwa kila nikienda Bongo Records alikuwa anaweka beats za aina tofauti na tukawa tunaflow na artists wengine so akaona kila beat naenda nayo na wengine walikuwa wanashindwa katika beats nyingine so akawa ananiita mzee wa commercial ila kwa sasa nimekuwa wa commercial ya muziki wa biashara na biashara kwa ujumla.

K.U: Laiti AY asingekuwa Mzee wa Commercial (yani usingekuwa msanii) unadhani leo angekuwa nani (katika fani gani)?
A.Y: nilikuwa na ndoto sana ya kusomea urubani na naamini ningeendelea nadhani ndoto yangu ingetimia coz nikiamua kufanya kitu naakikisha nimekifanikisha

K.U:Kitu gani kilichokusukuma kuingia kwenye fani ya muziki?
A.Y: kutokana na kusikiliza nyimbo za wasanii wengine wa nje na kuona mbona naweza kujitahidi nikafanya kama wao.

K.U: Kabla hatujagusia mafanikio yako kisanii ,nini hasa kimekuwezesha kubaki kwenye chati kwa kipindi kirefu kiasi hiki?
A.Y: bidii,nidhamu na malengo katika kazi,naipenda kazi yangu na najifunza kila siku na kukubali kuwa kila kitu kinaweza kubadilika

K.U: Tuje kwenye mafanikio yako kisanii.Licha ya kuweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza wa kiume kuteuliwa kugombea tuzo za Kora na baadaye tuzo za Kisima,kuna mafanikio gani mengine unayoyahusisha na fani ya muziki?
A.Y:Ni mengi. (Zaidi angalia wasifu hapo juu)

K.U: Miongoni mwa vilio vya wanamuziki wa Tanzania ni suala la ‘wadosi’.Kama msanii mwenye mafanikio makubwa umewezaje kupambana na suala hilo?
A.Y: hili nimeliongelea sana na sasa sihusiki nao kwa sasa naweza kusema ni tatizo sugu na linaweza kumalizika au kupungua ila naona wengi wenzangu wanaendelea kufanya biashara isiyo kuwa transparent

K.U: Nilidokezwa na Mwana FA kuhusu kampuni yako inayoshughulikia usimamizi na usambazaji wa muziki ijulikanayo kama Unity Entertainment.Wasomaji wangependa kufahamu japo kwa ufupi kuhusu wazo,maendeleo na ufanisi wa mradi huu.





A.Y:(angalia wasifu hapo juu) mpaka sasa kampuni yangu imekuwa na ni wakala wa wasanii wengi ukanda huu wa afrika mashariki kama mwana fa,shaa,nameless,j.martins wa nigeria ambae nimemleta kwenye new campaign ya zain,p.square,amani,chidi benz na wengine wengi wa afrika
K.U:Tuje kwenye ushiriki wako na hatimaye kujitoa kwenye kundi la East Coast Team.Sababu zipi zilipelekea wewe kujiengua?
A.Y: kutofautiana misimamo na malengo 

K.U: Wakati ukiwa na kundi la East Coast kulikuwa na beef na wasanii wa Temeke.Je unadhani beefs zinasaidia au kudumaza maendeleo ya wasanii? (nauliza hivyo kwa sababu wakati mwingine baada ya kufifia kwa beef -kama hiyo yenu-baadhi ya wasanii nao wanafifia)
A.Y: zipo zinazojenga na zipo zinazobomoa

K.U: Je makundi (kama ilivyokuwa East Coast) yanaficha udhaifu wa wasanii dhaifu na kudumaza umahiri wa wasanii bora?(nauliza hivi kwa vile baadhi ya wana-East Coast ‘walipotea’ muda mfupi baada ya wewe na Mwana FA kujitenga):
A.Y: ni kweli kabisa,makundi mengi yakivunjika ndio mnapata ukweli kuwa nani anaweza na nani hawezi kujimanage

K.U: Unatambulika kama mwakilishi bora kabisa wa Tanzania kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa (Kora,Kisima na sasa hii ya hivi karibuni ya Teneez 2010 huko Kenya ambapo umeibuka mshindi).Wasomaji wangependa kufahamu nini siri ya mafanikio yako?
A.Y: ni kama nilivyokwambia ni bidii na nidhamu na malengo bila hivyo huwezi kwenda mbali.na si hizo tu pia nimekuwa nominated kwa mtv awards 2009 (best hip hop artist nikiwa na jay z,kanye west na m.i)kili awards (2 categories),extra teneez awards (1category) na tuzo za Ghana zinaitwa moma (5categories-artist of the year- Africa,best male,collaboration,east African song,hip hop artist) nawaomba watanzania waweze kuvote online na kwa simu kwa walio Tanzania niweze kunyakua tuzo hizo,unaweza kugogle then upate informations

K.U: Kumekuwepo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wasanii kuhusu baadhi ya tuzo za hapo nyumbani hususan suala la upendeleo na mapungufu katika upangaji makundi (categories).Nini mawazo yako katika suala hili?
A.Y:zingine naweza kusema kweli na kuna wakati wasanii wanatakiwa kukubali matokeo maana ukikubaki kuingia katika mashinda jua kuna kushinda na kushindwa

K.U: Ukiwa kama msanii uliyedumu kwenye fani kwa muda mrefu,unaonaje maendeleo ya bongoflava ndani na nje ya Tanzania?
A.Y: inazidi kwenda mbele na kwa sasa wanaoipeleka mbele si wengi so nawaomba wenzangu tuongeze bidii na kutengeneza network zaidi ndani na nje ya nchi

K.U: Baadhi ya kazi zako zimetengenezwa na producers wa nje ya Tanzania.Je kuna tofauti yoyote kati ya kazi zako zinazotengenezwa na producers wa nyumbani na hizo zinazotengenezwa nje?
A.Y: ni ladha hazifanani,napenda sana kuchange plava mara kwa mara kwa audio na hata video






K.U: Swali linaloshabihiana na hilo lililopita.Je kufanya kazi na producers wa nje kunaweza kumsaidia msanii kufanya vyema katika nchi anayotoka producer huyo?
A.Y: sana tu mfano mzuri ni mimi mwenyewe na producer naofanya nao na nafurahi kuona wasanii wengine wa tz wameanza kufuata nyao zangu kwa kuanza kusafiri kurecord sehemu mbali mbali na kushirikiana na wasanii wa nje maana soko limeanza kuwa la afrika na si vile zamani kuwa la kibongo tu,angalia hata charts za redio records nyingi za nje na ndani zinaingia kwa pamoja

K.U: Umewahi kushiriki kwenye fani ya filamu (ambapo ulihusika kwenye filamu ya Girlfriend).Je una mpango wa kuendelea na fani hiyo huko katika siku za usoni?
A.Y:bado sijafikiria kwa kweli kama nitafanya movie 
K.U:Vipi kuhusu umodo hasa ushiriki wako kwenye matangazo mbalimbali ya biashara.Je una mpango wa kuwa full-time model licha ya muziki?
A.Y:hapana ila muda wote huwa wananunua image au sauti yangu kwa ajili ya products zao au campaign zao.

K.U: Unawezaje kumudu majukumu yote hayo (muziki, umodo, biashara) pasipo kuathiri ufanisi wako?
A.Y:na masomo pia,nasomea business administration ktk chuo cha Learn IT,mi ni mtu wajukumu tangu zamani sana so najua kuhandle pressure zote na huwa naishi kwa ratiba maalumu ambazo naziweka kwa simu na calendar yangu.

K.U: Umefanikiwa sana kuteka soko la bongoflava katika eneo la Afrika Mashariki.Nini mipango yako ya baadaye kutanua mafanikio hayo maeneo mengine ya Afrika na nje ya bara hilo?
A.Y:Nimeanza kupata bookings za S.A,DJIBOUTI,NIGERIA na ZAMBIA na pia Ethiopia so nazidi kusogea zaidi.pia natoa wimbo wangu mpya niliomshirikisha J.MARTINS kutoka Nigeria so najua itanijenga zaidi.

K.U:Kwa uzoefu wako,na kwa kuzingatia mafanikio unayopata nje ya mipaka ya Tanzania,unadhani ni jambo gani linalopelekea wasanii wengine wengi wa hapo nyumbani kushindwa kufanya vizuri kwenye anga za kimataifa?
A.Y: wengi ni wagumu kujifunza,kufanya networking.maana vile wengine wengi wa nje ya tz wanavyojituma ndio maana natumia style wazotumia wao.

K.U: Moja ya mambo yanayoisumbua Tanzania kwa sasa ni ufisadi lakini wasanii wengi wa bongoflava wamekuwa wakikwepa kuzungumzia suala hili kwenye tungo zao.Je ni sahihi kuyumkinisha kuwa mnaistarehesha jamii kwa vibao vyenu ‘vikali’ lakini mnawatenga kwa kutolipa kipaumbele suala la ufisadi kwenye tungo zenu?
A.Y: sidhani kama ukiimba ufisadi utaisha, nilichongundua ni kuwa watu hawaipendi nchi yetu ndio maana tunawafumbia macho wanaofanya ufisadi na tuna ile hulka ya kulalamika tu then hakuna hatua tunazochukua ndio maana ktuna matatizo mengi sugu tunayalalamikia tu halafu tunanyamaza

K.U: Nini mipango yako ya baadaye katika fani ya sanaa?
A.Y:kuna surprise kubwa nitawatangazia muda si mrefu naakika nitasogea/tutasogea kisanaa

K.U: Mwisho,una ujumbe gani kwa mashabiki wako na wapenzi wa bongoflava kwa ujumla?
A.Y: tuthamini na kuvipenda vya kwetu kwanza kabla ya vya wengine cz hata wao mnaona jinsiwanavyosupport vya kwao kwanza hata kama ni vibaya ila ni vyao na wanavipush sana mpaka wengine wanavikubali..





Blogu hii inakushukuru sana kwa kutumia muda wako kujibu maswali haya mengi.Pia inakutakia kila la heri na mafanikio katika shughuli zako.Na ni matarajio ya blogu na wasomaji wake kuwa tutapata fursa nyingine ya kuongea huko mbeleni.Asante sana.


ANGALIZO KUTOKA KWA AY: Nyimbo zangu na video zangu zitaanza kupatikana very soon online kupitia moja ya kampuni kubwa duniani,pia May hii nafungua duka la nguo mchanganyiko lipo sinza madukani.karibuni sana na kwa mawasiliano tutaweza kuwasiliana katika email yangu ya [email protected]. Na hapa chini ni wasifu wa kampuni ya Unity Entertainment
Unity Entertainment Profile 2010

15 Apr 2010


Nimefarijika sana kuona mahojiano niliyofanya na msanii mahiri wa Bongoflava,Hamis Mwinjuma a.k.a Mwana FA,yamechapishwa katika tovuti ya kimataifa ya muziki wa hip-hop,
Hip-Hop-Dance.Net.Pamoja na kuwapatia wasomaji wa blogu hii nafasi ya kuwafahamu Watanzania wenzetu wanaotangaza jina la nchi yetu kwa namna moja au nyingine,dhumuni jingine la mahojiano hayo lilikuwa kutangaza vipaji vinavypatikana nchini kwetu. Japo mahojiano hayo yanaelekea kuzua mjadala mwingine ambao binafsi nautafsiri kama uhuru wa mawazo,ninaishukuru sana tovuti ya Hip-Hop-Dance kwa "kutoa shavu" kwa mahojiano hayo hasa kwa vile Mtanzania mwenzetu mmoja aliamua kuyabania licha ya kumpa ombi ayaweke "kiwanjani" kwake.Again,naamini alifanya hivyo kwa kutumia uhuru wake kuchagua nini kinastahili kuwepo hapo kwake.


Kuhusu suala la elimu ya Mwana FA,ninaomba kumtetea,sio kwa vile nilimhoji,bali kwa sababu naamini anastahili zaidi pongezi kuliko criticism.Naomba niweke wazi kuwa Mwana FA hakuomba mahojiano hayo bali ni mimi niliyemwomba (na namshukuru sana kwa kukubali ombi hilo).Pili,kama alivyosema mwenyewe,mtu haihitaji kuwa na Masters ili aweze kufanya vizuri kwenye bongoflava.Alichukua uamuzi wa kujiendeleza kimasomo kwa vile,kwa mujibu wa maeleoz yake nayoafikiana nayo,fani ya muziki (hasa wetu) haitoi mwamana wa mafanikio katika maisha.Kwa amaan nyingine,alimua kuongeza elimu yake kama hatua ya kimaendeleo mbali na mafanikio yake katika Bongoflava.

Na hata kama angekuwa anadanganya kuhusu elimu yake (which he absolutely doesn't) ingemsaidia nini wakati tayari ana jina kubwa ndani na nje ya nchi yetu?Nadhani baadhi ya wasomaji wanaomtaka "aeleze ukweli" wanapaswa kwanza "kueleza uongo wake" kabla ya kumtaka aseme "ukweli".Nasema hivyo kwa maana kama nasema jina langu ni Evarist,halafu mtu anasema hilo sio jina langu ,basi ni muhimu kwake kuthibitisha jina langu halisi ni nani.

Binafsi,kama mwanafunzi,nimekumbana na zahma kama hiyo ya Mwana FA.Nimekuwa napokea barua pepe na hata SMS za watu wanaoulizia lini namaliza shule.By the way,shule huwa haimalizwi bali mtu anahitimu hatua moja na anaweza kuendelea na hatua nyingine.Kadhalika,katika mfumo wa elimu ya juu hapa,mwanafunzi anaweza kuahirisha kozi yake pale atapoona umuhimu wa kufanya hivyo.In my case,majibu yangu kwa watu wanaoniuliza kistaarabu ni kuwa kuchelewa kumaliza kozi yangu kumesababishwa na A,B,C na kadhalika kisha nawafahamisha hatua niliyofikia.Kwa wale wanaouliza kwa minajili ya "kudhani nauhadaa umma kuhusu elimu yangu" jibu langu huwa jepesi: Mind your own damn business.

Kuna wanaojiuliza inakuwaje mtu atoke IFM na kuja kufanya Masters University of Coventry,nawasihi wafanye utafiti kidogo kwenye mfumo wa elimu ya Uingereza,na pengine hata huko nyumbani.Inawezekana kabisa kupata admission kwenye vyuo vya hapa kwa kigezo cha "sifa linganifu" (equivalent qualifications).Ni kama ambavyo baadhi ya wanafunzi wanavyojiunga na MBA pale Mzumbe au kwingineko baada ya kumaliza masomo ya stashahada kutoka IFM,Nyegezi,Ustawi wa Jamii (pale Sayansi),nk.Kwa kifupi,mifumo mingi ya elimu duniani iko so "accommodating" kwa watu wenye nia ya dhati ya kujiendeleza kitaaluma.

Nimalizie kwa kutoa shukrani kwa wote wanaoendelea kutoa mawazo yao kuhusu mahojiano hayo.Sipingani na mawazo yoyote bali huu ni mchango na mtazamo wangu binafsi (ambao pia unaweza kuwa si sahihi kwa mujibu wa mitizamo mingine).Huo ndio uhuru wa mawazo,alimradi tunatumia lugha za kiungwana na "hatutiani vidole machoni".Kwa Mwana FA,hizi ndio changamoto za Tanzania yetu.

Stay tuned for the next interview na Mtanzania mwingine anayetuwakilisha vilivyo.Can you make a wild guess?Au una pendekezo lolote?

12 Apr 2010



Kama nilivyoahidi jana, leo nawaletea mahojiano maalum (exclusive interview) na msanii mahiri wa Bongoflava,Hamis Mwinjuma,almaaruf Mwana F.A.Pamoja na mambo mengine,blogu hii ilionelea umuhimu wa kufanya mahojiano na msanii huyo kwa sababu kuu mbili.Kwanza,yayumkinika kum-describe MwanaFA kama mmoja wa wasanii wenye elimu ya hali ya juu baada ya kuhitimu masomo yake hapa Uingereza.Pili,ilitarajiwa kwamba kwa kuwa kwake nje ya nchi kwa muda mrefu kimasomo atakuwa katika nafasi nzuri ya kutupa mwanga kuhusu nafasi ya bongoflava ndani na nje ya Tanzania.Basi nisimalize ladha bali tiririka na mahojianio hayo hapa chini. 









KULIKONI UGHAIBUNI (K.U.):Kwanza,blogu hii inatoa shukrani kwa kukubali ombi la kufanya mahojiano nawe.Pili ni pongezi kwa kuhitimu masomo yako ya Shahada ya Uzamili nchini Uingereza.


Umekuwa ukifahamika zaidi kwa jina la Mwanafalsafa,na wakati mwingine Binamu.Je nini asili au maana ya majina hayo?


MwanaF.A: Nashukuru ndugu yangu.



Mwanafalsafa nilipewa na producer wangu wa kwanza,Dj Boniluv..nilikuwa na wimbo unaitwa ‘mwanafalsafa’(upo kwenye album yangu ya kwanza) na Boni akadhani itakuwa busara nikilitumia jina hilo sababu ya aina ya uandishi wa mashairi nnaoufanya(kujaribu kuzungumzia vitu kwa uzito)..Binamu lilikuja baadae,na linaelezea mahusiano yangu na hadhira nnayoongea nayo,kwamba nawaambia watu vitu ambavyo kaka na dada zao wangeshindwa kuwaambia,pengine sababu ya heshima za kindugu walizonazo,lakini mimi kwa ukaribu na urafiki wa ki’binamu naweza kuwawasilishia.




K.U:Ukiwa mmoja wa wasanii wakongwe wa bongoflava,je ni kipi kinachokuwezesha kubaki kwenye form kwa muda mrefu kiasi hiki?


MwanaF.A:ah,kitu cha kwanza najua nimekuwa mwenye bahati,na namshukuru Mungu kwa hilo..sababu naamini kuna wengi walikuwa na vipawa vya kuweza kubaki lakini hawapo kwa sababu moja ama nyingine..huwa najaribu kusema vitu watu wanavyotaka kuvisikia,na pengine hawakuvitegemea,natafuta namna ya kuzunguka na ideas na kuzijengea hoja..then kilichobaki ni siasa za mziki.

K.U:Tuje kwenye maisha yako nje ya Tanzania.Kama msanii unaonaje nafasi ya bongoflava kwenye anga za kimataifa?:


MwanaF.A:sio kubwa kwa kweli,ina safari ndefu SANA..kuna mambo ambayo kimsingi tunatakiwa kuanza kwa kuyakubali kwanza,mathalani mipaka ya lugha..hili sio suala dogo,na nasema hivyo sababu ili kufanya vizuri nyumbani itakubidi kufanya kwa Kiswahili,ambapo nje ya nyumbani ni shida kukivusha..ubora wa mziki wetu na kukosa kwake uhalisi(kuna hiphop,r&b,afro pop,zouk,kwaito,lingala nk kwenye bongo flava) vinaiweka kwenye hali ngumu sana wakati wa kuutafutia nafasi.Pengine,tungeanza kwa kufanyia kazi vitu viwili hivi,lugha na uhalisi.







K.U: Je katika kipindi ulichokuwa nje ya Tanzania ulifanya kazi zozote za kisanii kushirikiana na wasanii wa nje au una mpango wa aina hiyo?:


MwanaF.A:sikuweza kwa kweli..nilikaribia kufanya kazi na producer Amit,lakini ratiba zangu na zake zikawa zinapishana mno so sikuweza tena..nna mpango wa kufanya kazi na wasanii wan je ndio lakini bado naifikiria Africa kwanza..so nawaza Nigeria na South Africa kwa kuanzia.




K.U: Umaarufu unaambatana na usumbufu.Je wakati uko masomoni Uingereza,ulimudu vipi kukabiliana na hali hiyo (i.e. muingiliano wa umaarufu wako katika masomo yako)?


MwanaF.A:nimekuwa nikisoma kwa muda sasa wakati najulikana julikana na watu(siuiti umaarufu)..see,nimekuwa nafanya mziki wa kusikika na kuonekana kwa takriban miaka 9 sasa na nimezoea kukabiliana na vikwazo nnapotaka langu liwe..nilisoma IFM kwa miaka kadhaa na bado niliweza kukabana na mazingira ya kujulikana na shule,so nje ilikuwa rahisi zaidi,sababu watu wachache zaidi wananijua kulingana na nyumbani.

K.U: Ni dhahiri kuwa kutokana na kiwango chako cha juu kitaaluma,utakabiliwa na majukumu mengine kama kikazi,nk.Je unataraji kubalansi vipi maisha yako kama msanii na majukumu mengine ya kimaisha (mfano kikazi)?:


MwanaF.A:kwa kuanzia nimempa AY majukumu ya kusimamia sehemu kubwa ya kazi zangu za mziki ili nipate nafasi ya kumudu kufanya mambo mengine kwa kuwa yeye ana kampuni inayojihusisha na masuala ya mziki(Unity Entertainment)..hii inanibakisha na kufanya mziki na shows tu ambapo ni maisha niliyoyazoea..bado naendelea kufikiri namna bora zaidi ya kutogonganisha majukumu..najaribu kutoweka mipaka kwenye idadi ya vitu nnavyoweza kuvifanya,napigana na haya maisha na najaribu kunyoosha mambo kwa kadri nnavyoweza.





K.U:Je unadhani hatua uliyopiga kitaaluma inaweza kuzaa matarajio mapya kwa washabiki wako hususan kwenye ujumbe uliomo kwenye tungo zako?


MwanaF.A:yeah,naishi najifunza..kila hatua ya maisha nnayopitia ni somo kwangu na nadhamiria kuwaambia watu wangu vingi nnavyojifunza..so hata hatua za kitaaluma nnazopiga zinaniongeza uelewa wa vitu na nimepanga kushiriki na hadhira yangu,sio kwa namna ya kishule,bali kwa namna ambayo mitaa itaelewana nayo.








K.U:Swali linaloshabihiana na hilo lililotangulia.Je kwa hatua uliyopiga kitaaluma,jamii itarajie mtazamo mpya kwenye tungo zako?


MwanaF.A:jibu lake ni exactly kama lililopita.


Nnachoweza kuking’arisha hapa ni kuwa sitaki kuchanganya sana shule yangu na huu mziki isipokuwa kwenye namna ya biashara na vitu vichache vitakavyohitaji mawili matatu nnayojifunza kila kukicha...huhitaji masters degree kutengeza mziki mzuri....huu ni wa mtaa na ntaendelea kuufanya kwa ajili ya mitaa,kama unanielewa vizuri..mara nyingi nyumbani unaweza kuhukumiwa kwa kujua.



K.U:Kama msanii msomi kabisa una ushauri gani kwa wasanii wengine kuhusu suala la kujiendeleza kielimu?


MwanaF.A:namna pekee ya kuliangalia hili kwa wasanii ni kuwa,tusiache maisha yetu yakawa sehemu ya mziki tunaoufanya,bali mziki wetu uwe sehemu ya maisha tunayoishi..niliamua kurudi shule sababu nilikuwa nataka kubaki kuwa mtoto wa mama Hamis,na kwa kufanya kile ambacho ningekifanya kama nisingekuwa mwanamuziki...mziki,HASA HUU WETU, una siasa nyingi na hautoi ahadi ya kukupa uwezo wa kuyamudu maisha yako yote yaliyobaki na familia yako,hivyo ni busara kuwa na mipango ya ziada.





K.U: Kwa uzoefu wako baada ya kuwa nje ya Tanzania kwa muda mrefu,una ushauri gani kwa wasanii wenzio kuhusu uwezekano wao kuvusha kazi zao za sanaa nje ya mipaka ya Tanzania?




MwanaF.A:ni kama nilishajibu na hili mkuu..tunapaswa kuondoka kwenye denial state kwanza..tukubali kuufanyia marekebisho ya kimsingi mziki wetu then tukimbizane na chochoro za kuuvusha..vinginevyo tutaendelea kuimbia wa’Tz 200-300 kwenye maonyesho yetu ya nje kila wakati.




K.U: Mwisho,una ujumbe gani kwa mashabiki wako.Je wategemee vitu vipya hivi karibuni?


MwanaF.A:yeah,maskio yakae wazi..nawadondokea punde tu.








Blogu hii inakutakia kila la heri katika shughuli zako.


MwanaFA: Ahsante sana,nashukuru..na pole kwa kuchukua muda mwingi kujibu..mbio za maisha tena..na naamini wewe na watembeleaji wa blogu mtanielewa.


.

11 Apr 2010

Kama nilivyoahidi awali,blogu yako itakuwa ikikuletea mahojiano na Watanzania 'wanaowakilisha' (representing) nchi yetu kwa namna moja au nyingine.Na sasa nafurahi kukujulisha kuwa blogu imekamilisha mahojiano na supastaa big name wa bongoflava.Could you make a guess?Hint: Ni msanii mwenye kipaji cha hali ya juu katika kupangilia verses na lyrics zake,sambamba na uwezo mkubwa wa 'kucheza na maneno' na kwa sasa ni mwana bongofleva mwenye elimu ya kiwango cha juu kabisa. Na hapa chini (video) inakupa hint zkubwa zaidi.
Mahojiano kamili yatawekwa hapa kesho katika versions mbili:Kiingereza na Kiswahili.USIKOSE

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.