KWA miaka kadhaa, makala zangu za wiki
ya mwanzo wa mwaka huzungumzia matukio mbalimbali yanayotarajiwa kutawala
habari katika mwaka husika. Makala hii ni mwendelezo wa utamaduni huo.
Inajaribu kufanya ubashiri wa baadhi ya matukio yanayotarajiwa kujiri katika
mwaka huu, ndani na nje ya nchi yetu.
Nianze na ubashiri wa matukio ya
kimataifa. Mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu nchini Marekani. Kwa kuzingatia
mwelekeo wa kampeni zinazoendelea nchini humo, ninabashiri kuwa Hillary Clinton
atafanikiwa kushinda kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Democrats,
ilhali kuna uwezekano mkubwa wa Donald Trump kuibuka mgombea kwa tiketi ya
Chama cha Republicans.
Hata hivyo, uwezekano huo unategemea
mambo matatu muhimu. Kwanza, kwa wote wawili, nafasi zao kushinda au kushindwa
zitategemea mwenendo wa uchumi wa taifa hilo kubwa duniani. Iwapo uchumi wa
Marekani utaimarika zaidi, basi Hillary na chama chake watakuwa na fursa nzuri
zaidi hasa kwa kutegemea uungwaji mkono wa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Barack
Obama, kujivunia rekodi ya uchumi chini ya chama chao. Uchumi ukiyumba, Trump,
ambaye ni mfanyabiashara tajiri anaweza kuonekana kama chaguo sahihi kuwa rais
ajaye wa nchi hiyo.
Jambo la pili, ambalo pia linawahusu
wote wawili, ni hali ya usalama nchini humo. Iwapo hali itaendelea kuwa salama
kama ilivyokuwa katika miaka minane ya Rais Obama, mgombea wa Democrats, ambaye
ninabashiri atakuwa Hillary, atakuwa na nafasi nyingine nzuri ya kujivunia
umahiri wa Rais kutoka Democrats kama Obama kulihakikishia usalama taifa hilo linalowindwa
kwa udi na uvumba na vikundi mbalimbali vya ugaidi wa kimataifa. Iwapo kwa
bahati mbaya kutatokea tukio lolote kubwa la ugaidi, basi hali hiyo yaweza
kumnufaisha mgombea wa Republicans, ambaye ninabashiri atakuwa Trump, kwa
kigezo chepesi tu kuwa Democrats wameshindwa kuiweka Marekani kuwa salama.
Jambo la tatu ni mwenendo binafsi wa
wanasiasa hao wawili. Kwa upande wa Hillary, uwezekano wa yeye kuibuka mgombea
wa Democrats utategemea uchunguzi unaoendelea kuhusu matumizi ya barua-pepe
binafsi akiwa Waziri wa Mambo ya Nje. Japo Wamarekani wengi hawaonekani kuguswa
na yaliyokwishafahamika kuwemo katika maelfu ya barua-pepe hizo, iwapo
uchunguzi utabaini makosa makubwa zaidi, basi nafasi ya mwanamama huyo
anayewania kuwa rais wa kwanza mwanamke wa taifa hilo itakuwa finyu, na huenda
akalazimika kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Kikwazo kingine kwa Hillary ni tuhuma
zilizoibuka hivi karibuni zinazoashiria uhusika wake katika tenda inayoihusisha
Kampuni ya Symbion ambayo inahusu mradi wa uzalishaji umeme nchini Tanzania.
Japo alichofanya mwanasiasa huyo sio kitu cha ajabu katika siasa za Marekani na
hata katika nchi nyingine, ikigundulika kuwa taratibu zilikiukwa ili kupendelea
marafiki zake, anaweza kuathirika vibaya na pengine kulazimika kujiondoa katika
harakati zake za urais.
Wasiwasi mkubwa kuhusu Trump ni ile
tabia yake ya kuwa kama bomu lililotegeshwa kwa muda (time bomb). Pamoja na
kuendelea kung’ara katika kura za maoni miongoni mwa ‘wagombea’ wa Republicans,
mwanasiasa huyo hana upungufu wa vioja, na fursa yake ya ushindi itategemea
sana jinsi atakavyodhibiti mdomo wake kati ya sasa na wakati wa mchakato rasmi
wa chama chake kuteua mgombea. Na hata akiruka kikwazo hicho, bado kuna
wasiwasi iwapo Wamarekani watakuwa tayari kumchagua mwanasiasa asiyetabirika.
Na endapo watamchagua, basi taifa hilo linaweza kutengwa na nchi nyingi
duniani.
Iwapo Hillary hataibuka mshindi kwa
tiketi ya Democrats, ninabashiri kuwa nafasi hiyo itakwenda kwa Bernie Sanders,
ambaye hata hivyo ana nafasi finyu kumshinda mgombea yeyote atakayepitishwa na
Republicans. Na iwapo Trump hatopitishwa, ninabashiri mbadala wake kuwa aidha
Ted Cruz au Marco Rubio.
Katika anga hizo za kimataifa,
ninabashiri kuwa hali nchini Burundi itakuwa mbaya zaidi ya ilivyokuwa mwaka
jana. Kadhalika, ninabashiri hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo kuzorota, hasa baada ya jitihada za Rais Joseph Kabila kutaka kuendelea
kubaki madarakani.
Kadhalika, ninabashiri kuwa kundi la
kigaidi la Boko Haram litaendelea kuisumbua Nigeria, huku kundi jingine la
kigaidi la Al-Shabaab likiendelea kuzisumbua Somalia na Kenya. Pia kuna
uwezekano wa kuwepo matatizo ya kisiasa huko Afrika Kusini na Zimbabwe
yanayoweza kusababisha kung’oka madarakani kwa viongozi wa nchi hizo.
Habari za ugaidi wa kimataifa
zinatarajiwa kuendelea kutawala anga za kimataifa huku makundi mawili hatari ya
ISIS na Al-Qaeda yakiendelea kuwa tishio duniani, hususan nchi za Magharibi.
Kadhalika, ninabashiri kuwa eneo la
Ghuba na Mashariki ya Kati kuingia katika mgogoro mkubwa utakaoligawa eneo hilo
kati ya Waislam wa madhehebu ya Sunni wakiongozwa na Saudi Arabia, na wale wa
Shia wakiongozwa na Iran.
Kwa huko nyumbani, ninabashiri kuwa Rais
Dk John Magufuli ataendelea na utumbuaji majipu, japo habari ninayobaishiri
kuwa itatawala zaidi ni kuibuka kwa skandali mbalimbali zilizojitokeza wakati
wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na ambazo umma haukuwahi kuzifahamu.
Kimsingi, harakati za Dk. Magufuli kutumbua majipu zina kila ishara ya kukutana
na madudu yaliyosheheni wakati wa utawala wa mtangulizi wake.
Kadhalika, ninabashiri uwezekano wa
baadhi ya mawaziri au manaibu wao kufukuzwa kwa kushindwa kuendana na falsafa
ya Hapa Kazi Tu. Kwa vile si vema kumwombea mtu mabaya, ninahifadhi majina ya
mawaziri ninaodhani wanaweza kuwa waathirika wa awali.
Vile vile, ninabashiri uwezekano wa
kuwepo jitihada za chini chini ndani ya CCM kukwamisha dhamira ya Dk. Magufuli
kukabiliana na ufisadi, rushwa, ujangili, biashara ya dawa za kulevya, na maovu
mengine. Hata hivyo, jitihada hizo hazitafanikiwa.
Kwa upande mwingine, ninabashiri kuwa
Dk. Magufuli ataendelea kunga’ra ndani na nje ya nchi, na dunia itaelekeza
macho yake nchini Tanzania kutokana na mafanikio makubwa ya kiuongozi na
jitihada za kufufua na kuboresha uchumi.
Kingine ninachoweza kubashiri ni ujio wa
sura mpya nyingi katika uongozi ngazi za mikoa na wilaya, huku ikitarajiwa kuwa
kama ilivyokuwa kwa Baraza la Mawaziri na Makatibu wakuu, wasomi mbalimbali
wakiteuliwa kushika nyadhifa za u-RC na u-DC.
Kwa upande wa vyama vya upinzani,
ninabashiri uwezekano wa jitihada za kumng’oa Mwenyekiti wa taifa wa Chadema,
Freeman Mbowe, japo haitakuwa jambo la kushangaza iwapo atanusurika. Kwa kiasi
kikubwa, uhai wa kisiasa wa Mbowe utategemea uhusiano wake na aliyekuwa mgombea
urais kwa tiketi ya Ukawa, Edward Lowassa.
Eneo ambalo ninashindwa kubashiri kwa
uhakika ni hali ya kisiasa huko Zanzibar. Hata hivyo, ninaweza kubashiri bila
uhakika kuwa CCM itafanikiwa kulazimisha marudio ya uchaguzi, na kuna uwezekano
CUF wakasusia. Uwezekano mwingine ni kurejewa kwa kilichofanyika baada ya
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, yaani kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Ubashiri sio sayansi timilifu (exact science) kwa hiyo nitahadharishe kuwa
baadhi ya niliyobashiri yanaweza kuwa kinyume.
Ubashiri huu umetokana na kufuatilia kwa
karibu siasa za kimataifa na za huko nyumbani.
Nimalizie makala hii kwa kuwatakia tena
heri na baraka za mwaka mpya 2016. Kwa huko nyumbani (Tanzania), kuna kila
sababu ya mwaka huu kuwa mzuri kutokana na dalili za awali za utawala wa Dk.
Magufuli kuiondoa Tanzania yetu katika lindi la ufisadi na rushwa, vitu
vilivyochangia mno kudumisha umasikini wa nchi yetu. Lakini ili afanikiwe, ni
wajibu wa kila Mtanzania kutimiza ‘Hapa ni Kazi Tu’ kwa vitendo.
9