Sijui ni ulevi wa madaraka,au ulevi wa kilevi,lakini kauli za baadhi ya watendaji ni za kihuni,usizorarajia kabisa kuzisikia kutoka kwa watu wenye nyadhifa muhimu kwa Taifa.
Nadhani wengi wetu bado tunakumbuka taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa,Jack Zoka (pichani chini),ambapo ilikuwa na "kauli za mtaani" kinyume na wadhifa wake nyeti katika taasisi hiyo na Taifa kwa ujumla.
Baadaye tukapewa dozi ya kauli zilizojaa ngebe na kichwa ngumu kutoka kwa Frederick Werema,mtu aliyewahi kushika wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu,na kwa sasa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.Mtu huyu ni kama ana "bifu" na jamii anayopaswa kuitumikia.Ukisikia kauli zake kuhusu suala la Katiba na ishu ya Dowans,utabaki mdomo wazi kama sio kufura kwa hasira.
Kana kwamba kuna mashindano ya kauli za ovyo ovyo,Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu,Salva Rweyemamu,nae hajataka kuachwa nyuma.Japo ana rekodi nzuri ya kusema ovyo,safari hii nadhani amevuka mpaka.Anyway,hebu soma taarifa yake ifuatayo:
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Wilboard Slaa, leo, Jumapili, Januari 2, 2011, amekaririwa na Gazeti la Tanzania Daima, linalomikiwa na chama chake hicho, akidai kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ni mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans.
Huu ni uongo wa mchana, ni uzushi wa karne na propaganda ya hatari. Kwa hakika na kwa namna isiyoweza kuelezeka kwa ufasaha, tumeshtushwa sana na kauli hii ya Dkt. Slaa na hatutaki kuamini kabisa wala kukubali kuwa ni kweli kauli hii imetolewa na mtu ambaye majuzi tu alikuwa akiwania kuwa kiongozi wa juu wa taifa letu, yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na kama kweli Dkt. Slaa ametoa kauli hii na kusema maneno ya namna hii basi sasa Watanzania wanayo kila sababu na haki ya kuamini kuliko wakati mwingine wowote kuwa mzee huyu sasa amechanganyikiwa na ni mtu wa hatari sana kwa utulivu wa nchi hii. Kwa nini?
Sababu ni rahisi sana. Mheshimiwa Rais Kikwete siyo mmiliki wa Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Dowans. Hakupata kuwa mmiliki, siyo mmiliki na wala hatakuwa, hata siku moja, mmiliki wa Kampuni hii.
Kama Dkt. Slaa anataka kweli kujua wamiliki wa Kampuni ya Dowans, basi atafute ukweli huo na aachae tabia ya kutapatapa na udhabinadhabina yenye lengo la kuwapaka watu watope. Tabia ya kuwasingizia na kusema uongo kuhusu viongozi wa taifa letu ni tabia ya hatari.
Mheshimiwa Rais Kikwete hahusiki na Kampuni ya Dowans wala na kampuni nyingine yoyote ya kibiashara. Yeye ni kiongozi wa juu kabisa wa siasa wa nchi yetu na siyo heshima wala haki kumhusisha na jambo la kutunga na kuzua na lisilokuwa la ukweli wowote.
Kiongozi huyo wa upinzani ametoa shutuma zake dhidi ya Rais Kikwete kufuatia Kampuni ya Dowans kulishitaki Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) na Mahakama hiyo ikaamua kuwa Dowans ilipwe kiasi cha sh bilioni 185.
Dkt. Slaa amezomoko na kumshutumu Rais Kikwete eti kwa sababu Mheshimiwa Rais hakuzungumzia suala hilo katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Ijumaa iliyopita.
Mwaka huu, Dkt Slaa aliwania urais wa Tanzania kupitia CHADEMA na akashindwa vibaya sana. Tokea wakati huo amekuwa mtu wa kutunga na kuzua stori za kila aina ya uongo na umbea kuwachanganya Watanzania kwa sababu ya kinyongo chake cha kushindwa.
Tunapenda kuwataka na kuwaomba Watanzania, kama ambavyo wamekuwa wanapuuza uongo na uzushi mwingine wa mara kwa mara wa Dkt. Slaa, waupuuze uzushi na uongo wa sasa kuhusu miliki ya Dowans. Ni sehemu ya tabia iliyoanza kuzoeleka sasa ya Mzee huyo kutapatapa kisiasa.
Imetolewa na Salva Rweyemamu – Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais - Ikulu
Unajua watu hawa wanapata wapi jeuri ya kusema ovyo?Well,ni huyo aliyewateua.Heshima ni mithili ya barabara ya kwenda na kurudi (two-way).Ukijiheshimu utaheshimiwa.Na pia,heshima kwa aliyekuteua inaweza kuonekana kwa namna unavyomwakilisha katika jamii.Wateuliwa wa Rais ni sawa na taswira ya Rais kwa jamii.Kauli za kihuni za wateuliwa hao zinaweza kutoa picha kuwa Rais kateua wahuni au wababaishaji.
KWA KIFUPI,NA PASIPO KUUMAUMA MANENO,KAULI ZA WATENDAJI HAO MUHIMU WA RAIS KIKWETE NI TASWIRA YA KIKWETE MWENYEWE NA UONGOZI WAKE.