Makala yangu hii ilichapishwa katika jarifa la RAIA MWEMA Toleo la wiki iliyopita lakini 'nilizembea' kui-post hapa bloguni. Endelea kuisoma:
NIANZE kwa kuelezea matukio mawili, moja linaihusu Marekani na jingine laihusu Israel.
Tukio la kwanza linahusu kujiuzulu kwa aliyekuwa mkuu wa moja ya idara za usalama za Marekani (zipo nyingi) ambayo ina dhamana ya ulinzi na usalama wa viongozi wakuu wa taifa hilo na familia zao, US Secret Service.
Mkuu huyo, mwanamama Julia Piersons, alilazimika kujiuzulu baada ya tukio la hivi karibuni la kuhatarisha usalama wa Rais Barack Obama, kutokana na mtu mmoja, Omar Gonzalez, kuruka uzio wa Ikulu ya nchi hiyo akiwa na kisu, kabla hajadhibitiwa na maafisa wa Secret Service.
Hatimaye tukio hilo lililotawala sana katika vyombo vya habari vya Marekani lilimfanya mwanamama huyo, shushushu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 30, kuitwa na kuhojiwa na kamati moja ya Bunge la Congress, na mwishowe alitangaza kujiuzulu.
Licha ya ukweli kwamba mkuu huyo wa mashushushu hakuwa eneo la tukio, dhamira ilimtuma kuwa kama kiongozi wa taasisi yenye dhamana ya ulinzi wa viongozi wakuu wa nchi hiyo, anawajibika kwa uzembe au makosa ya watendaji wake.
Piersons alikuwa kwenye wadhifa huo kwa takriban miezi 18 tu baada ya mtangulizi wake, Mark Sullivan, kulazimika kujiuzulu baada ya kashfa iliyohusisha baadhi ya maafisa wa Secret Service ‘kufumwa’ wakiwa na makahaba katika ‘msafara wa utangulizi’ (advance party) kabla ya ziara ya Rais Obama nchini Colombia, mwaka juzi.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya ushushushu wanamuona Piersons kama mhanga tu wa mapungufu ya kimfumo na kiutendaji yanayoikabili taasisi aliyokuwa akiongoza.
Wanadai kuwa alikuwa akikabiliwa na jukumu gumu la kuleta mabadiliko ndani ya taasisi hiyo, na wadhifa wake ulikuwa sawa na ‘jukumu lisilowezekana.’ Hata hivyo wanampongeza kwa ‘kubeba mzigo wa lawama’ kwa niaba ya watendaji wake.
Tukio la pili linahusu filamu ya maelezo (documentary) iitwayo The Gatekeepers, iliyoonyeshwa kwenye kituo cha runinga cha BBC2 mwishoni mwa wiki.
Filamu hiyo ni ya mahojiano na wakuu sita wa zamani wa Idara ya Usalama wa Ndani wa Israeli, Shin Bet (au 'Shabak' kama inavyojulikana kwa Kiyahudi).
Filamu hiyo iliyotengenezwa mwaka juzi na kuteuliwa kuwania tuzo za Oscars, imeendelea kuwa na mvuto mkubwa kutokana na ukweli kuwa ni vigumu mno, hasa kwa ‘nchi ya kiusalama’ kama Israeli, kupata fursa ya kufanya mahojiano na wakuu wa taasisi za usalama.
Katika filamu hiyo inayoelezea kwa undani utendaji kazi wa Shin Bet, idara ya ushushushu yenye ufanisi mkubwa duniani, ikiwa ni pamoja na operesheni mbalimbali za Shin Bet dhidi ya ‘magaidi’ wa Palestina, wakuu hao – Avraham Shalom (1980-1986), Yaakov Peri (1988-1994), Carmi Gillon (1994-1996), Avi Dichter (2000-2005) na Yuval Diskin (2005-2011)- wanatanabahisha jinsi wanasiasa na Wayahudi wenye msimamo mkali walivyo vikwazo kwa jitihada za kutafuta amani ya kudumu katika mgogoro wa muda mrefu wa Israeli na Palestina.
Kwa ujumla, wote wanahitimisha kuwa licha ya umuhimu kwa serikali ya Israeli na taasisi zake za ulinzi na usalama kutumia nguvu dhidi ya ‘ugaidi wa Wapalestina,’ ukweli mchungu ni kuwa matumizi hayo ya nguvu si tu yanachochea ‘ugaidi’ zaidi bali pia yanakwaza uwezekano wa kupatikana amani ya kudumu.
Filamu hiyo ilisababisha wakuu hao kushutumiwa na Waisraeli wengi, wakilaumiwa kwa msimamo wao uliotafsiriwa kama kuhalalisha ‘ugaidi’ wa Wapalestina, huku wengine wakiwashutumu kuwa ‘waliongea walichoongea baada ya kustaafu badala ya kubainisha mitizamo yao wakiwa madarakani.’
Kwa hakika filamu hiyo (unayoweza kuiangalia hapa http://goo.gl/gY4K6O) si tu inaeleza kwa undani operesheni hatari na za ‘ufanisi wa hali ya juu’ zilizofanywa na Shin Bet chini ya uongozi wa mashushushu hao lakini pia inamsaidia anayeiangalia kufahamu kwa undani mchanganyiko wa siasa na dini na mwingiliano wake katika utendaji kazi wa taasisi za kiusalama za Israeli, na kubwa zaidi ni maelezo ya kina kuhusu mgogoro kati ya nchi hiyo na Palestina.
Lengo la makala hii si kujadili matukio hayo mawili bali kuyatumia kama ‘darasa la bure’ kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa. Binafsi, nimekuwa moja ya sauti chache kuhusu haja ya mageuzi ya kimfumo na kiutendaji kwa taasisi hiyo muhimu.
Kwa bahati mbaya – au makusudi- utendaji kazi na ufanisi wa Idara hiyo haukuguswa kwa kiwango kinachohitajika katika kikao cha Bunge la Katiba na hatimaye Katiba pendekezwa.
Idara hiyo inakabiliwa na matatizo makubwa japo aidha hayafahamiki sana au yanapuuzwa, na huo ndio msingi wa ushauri wangu kuwa kuna haja ya mageuzi ya haraka.
Tukijifunza katika kujiuzulu kwa mkuu wa Secret Service, twaweza kujiuliza, hivi kwanini hakuna anayewajibishwa licha ya Idara yetu ya Usalama wa Taifa kuboronga mara kwa mara?
Pengine kuna watakaojiuliza 'imeboronga lini na katika nini?’ Jibu rahisi ni kwamba, kwa mujibu wa ‘kanuni za taaluma ya usalama wa taifa,’ kushamiri kwa vitendo vinavyotishia usalama wa nchi ni dalili ya wazi ya udhaifu wa idara ya usalama wa taifa ya nchi husika.
Kwa maana hiyo, kushamiri kwa ufisadi, kwa mfano mmoja tu, ni dalili kwamba taasisi hiyo imeshindwa kazi yake. Kadhalika, Idara hiyo kufanya kazi zake kama ‘kitengo cha usalama cha CCM’ si tu kunaipunguzia kuaminika kwake kwa umma bali pia kunaathiri uwezo wake katika kukabiliana na matishio kwa usalama wa Taifa.
Majuzi, aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo, Jack Zoka, ‘alizawadiwa’ ubalozi wa nchi yetu huko Canada. Sihitaji kuingia kwa undani kuhusu utendaji kazi wa shushushu huyo lakini atakumbukwa sana na vyama vya upinzani, hasa CHADEMA, sambamba na wengi wa waliojitoa mhanga kuwa sauti ya wanyonge, kwa jinsi alivyowadhibiti. Pengine kabla ya kupewa ubalozi baada ya kustaafu utumishi wa umma, ahojiwe kuhusu mchango wake katika ‘ufanisi’ au udhaifu wa Idara hiyo.
Ni mwendelezo wa kasumba inayolikwaza Taifa katika nyanja mbalimbali: mtu anaboronga pale, anahamishiwa kule. Kwanini watendaji wengine wahofie kuboronga katika majukumu yao ilhali wenzao ‘wanazawadiwa’ badala ya kuwajibishwa?
Somo kutoka kwa wakuu sita wa zamani wa Shin Bet katika filamu ya The Gatekeeper ni kubwa zaidi. Ukiondoa ‘sauti ndogo’ ya Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, Hans Kitine, takriban viongozi wote wastaafu wa Idara hiyo wamekuwa hawana mchango wa maana katika kuiboresha na hata kuisadia isimame katika upande stahili.
Ni kweli Tanzania si Israeli, lakini wengi wa wastaafu wa taasisi hiyo, kama ilivyo kwenye taasisi nyingine, ni watu wenye ushawishi mkubwa na wanaheshimika vya kutosha, lakini ukimya wao wakati mambo yanakwenda kombo ni doa.
Mashushushu hao sita wa Israeli walipokubali kushiriki kwenye filamu hiyo walikuwa wanatambua bayana athari zake, kubwa ikiwa ni uwezekano wa kuonekana wasaliti. Lakini ujasiri ni pamoja na kusema yasiyosemeka.
Na kwa vile, kimsingi, ukiwa shushushu unabaki kuwa shushushu milele, na kwa sababu ni watu wachache katika jamii wenye uelewa kuhusu utendaji kazi wa taasisi za kiusalama, wastaafu au watumishi wa zamani ndio watu pekee wenye fursa ya ‘kuokoa jahazi.’
Nihitimishe makala hii kwa kutaja kwa kifupi maeneo yanayohitaji mageuzi (reforms) kuhusiana na Idara yetu ya Usalama wa Taifa. La kwanza ni umuhimu wa uwazi zaidi katika teuzi za viongozi wakuu wa Idara hiyo, hususan Mkurugenzi Mkuu.
Ni muhimu kutengeneza mazingira yatakayoepusha uwezekano wa Rais ‘kumteua mtu wake au rafiki yake’ kuongoza taasisi hiyo. Madhara ya uswahiba katika uteuzi kuongoza taasisi nyeti kama hiyo ni pamoja na mteuliwa kujiona ana ‘deni la fadhila’ kwa aliyemteua.
Kuna haja ya, kwa mfano, uteuzi wa viongozi wa juu wa taasisi hiyo kuidhinishwa na Bunge.
Pili, ni ulazima wa taasisi hiyo kuwajibika kwa umma kupitia taasisi kama Bunge. Hapa ninamaanisha haja ya viongozi wa taasisi hiyo kuitwa katika kamati husika za Bunge, kwa mfano, kuwaeleza Watanzania ‘kwanini ufisadi unazidi kushamiri ilhali taasisi hiyo haipo likizo?’
Tatu ni mabadiliko ya kiutendaji ambapo Idara hiyo iwezeshwe kuufanya ushauri wake utekelezwe, badala ya mazingira yaliyopo ambapo kwa kiasi kikubwa suala hilo linabaki kuwa ridhaa ya Rais ambaye ndiye ‘consumer’ wa taarifa za kiusalama anazopatiwa na Idara.
Hivi inakuwaje pale Idara hiyo inaposhauri kuhusu suala linalohatarisha usalama wa taifa lakini Rais akalipuuza?
Mwisho, lengo la makala hii ni jema: kuiboresha Idara yetu ya Usalama wa Taifa (ambayo licha ya mapungufu yake lukuki, binafsi nina imani kuwa inaweza ‘kujikwamua’ kama si kukwamuliwa) kwa maslahi na mustakabali wa Taifa.
Tanzania ni yetu sote na si kwa ajili ya kikundi kidogo kinachojiendeshea mambo kitakavyo.Penye nia pana njia.