Yuko nje ya nchi kwa matibabu
*Waziri Mkuchika akataa kusema lolote
* Manumba aendelea kupumulia mashine
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Dk. Joseph Hosea, anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matitabu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya TAKUKURU, Dk. Hosea, alianza kuugua tangu mwanzoni mwa Desemba mwaka jana na ilipofika Desemba 15 hali ilibadilika.
Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU kilisema hadi sasa haijafahamika ugonjwa unaomsumbua.
“Ni kweli Mkurugenzi anaumwa na kuna taarifa yuko ya nje ya nchi kwa matibabu kati ya Ujerumani au Uingereza.
“Kwa mara ya mwisho nilimuona Mkurugenzi akiwa hayupo sawa kiafya na hata alipokuwa anakuja kazini alikuwa katika muonekano ambao ni wazi anaumwa. Lakini katika wiki hizi sijamuona hapa ofisini,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU.
MTANZANIA pia ilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) George Mkuchika kwa njia ya simu kupata taarifa za kina kuhusu tukio hili lakini alisema hana taarifa yoyote.
“Mhhhh katika hili la ugonjwa wa Dk. Hosea sina taarifa na kama ujuavyo nilikuwa katika msiba wa baba yake Naibu Waziri wa Mifugo, kule Kiteto. Tangu jana nilikuwa n rejea na nimefika Morogoro nimelala hapa na sasa nimeanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.
“Kama kuna taarifa yoyote kuhusu hilo kwa sasa siwezi kusema lolote hadi nitakapofika ndugu yangu,” alisema Waziri Mkuchika.
Hata hivyo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Dk. Hoseah yupo nje ya nchi kwa mapumziko ya likizo.
“Ni kweli ofisa uhusiano yupo likizo na pia mkubwa (Dk. Hoseah) naye yupo Marekani ameenda kwa ajili ya mapumziko ya likizo hakuna mtu anayeumwa,” alisema.
MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa TAKUKURU Dorine Kapwani ambaye muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa hata alipopigiwa kwa simu ya mezani.
Mbali na hatua hiyo hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa simu ya kiganjani ambao ulisomeka; “Dada habari, kuna taarifa Dk. Hosea anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu je kuna ukweli gani” hakujibu chochote hadi tunakwenda mitamboni jana usiku.
DCI Manumba apumulia mashine
Naye Elizabeth Mjatta anaripoti kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba sasa anapumua kwa msaada wa mashine baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
DCI Manumba jana alitumia takribani siku nzima kuwa katika chumba cha uchunguzi kwa ajili ya vipimo zaidi, baada ya kutolewa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.
MTANZANIA ilishuhudia DCI akitolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi saa 11:25 akipelekwa katika chumba cha uchunguzi huku akiwa amezungukwa na madaktari na wauguzi huku baadhi yao wakiwa wameshikilia vifaa maalumu ambavyo vilikuwa vikimsaidia kupumua.
Hata hivyo, baadhi ya madaktari waliokuwa wamemzunguka hawakuweza kuthibitisha iwapo vifaa alivyokuwa amewekewa DCI Manumba vilikuwa ni sehemu ya mashine iliyokuwa ikimsaidia kupumua.
Hali hiyo iliwafanya ndugu na watoto wa kamanda huyo kuwa katika hali ya taharuki ambako baadhi yao walionyesha kushikwa na huzuni huku mmoja wa watoto wake ambaye jina lake halikupatikana akiwa katika hali ya majonzi makubwa.
Hadi MTANZANIA inaondoka katika Hospitali ya Aga khan saa 5:45 jioni mgonjwa huyo bado alikuwa hajatolewa katika chumba cha uchunguzi hali iliyowafanya ndugu kuendelea kusubiri katika eneo la mapokezi ya wagonjwa mahututi.
Alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu hali ya mgonjwa, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk. Jaffer Dharsee alisema kwa sasa hawezi kusema lolote hadi vipimo vya uchunguzi vitakapokamilika, huku akiwaahidi waandishi wa habari kuwa atatoa taarifa hiyo leo asubuhi.
“Siwezi kusema kitu kwa sasa kwani bado hali ya DCI inahitaji uchunguzi wa karibu wa madaktari na hadi sasa bado yupo katika chumba cha uchunguzi zaidi hivyo sina cha kusema nasubiri nikamilishe ripoti yote labda kesho ndiyo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema kitu,” alisema Dk Dharsee.
Hata hivyo katika kipindi chote hicho, hali ya ulinzi ilikuwa imeimarika ambako polisi na askari kanzu walikuwa wamezunguka katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha.
Viongozi
Jana viongozi mbalimbali waliendelea kufika hospitalini hapo kumjulia hali Manumba. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima ambaye aliwasili hospitali hapo mchana pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick.
Viongozi wote hao walipokewa na daktari mkuu wa polisi aliyefahamika kwa jina moja la Dk Makata ambaye aliwapeleka moja kwa moja katika jengo la tatu kilipo chumba cha uchunguzi kwa ajili ya kumjulia hali DCI Manumba.
Dk. Nchimbi baada ya kutoka katika chumba cha mgonjwa hakutaka kuzungumza chochote licha ya kutakiwa kufanya hivyo na waandishi wa habari. “Mnataka niseme nini kwamba mgonjwa hali yake nzuri au mbaya? Mimi si daktari lakini kwa namna nilivyomuona nasema anaendelea vizuri,” alisema Dk. Nchimbi.
DCI Manumba aliugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili na Januari 14 alihamishiwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Manumba ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mwaka 2006 akichukua nafasi ya Adadi Rajabu, haijaelezwa wazi kuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani, ingawa taarifa za awali zinasema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo.
CHANZO: Mtanzania