Showing posts with label EDWARD HOSEA. Show all posts
Showing posts with label EDWARD HOSEA. Show all posts

19 Jan 2013


IMG-20130119-00371 a18f1
Yuko nje ya nchi kwa matibabu

*Waziri Mkuchika akataa kusema lolote
* Manumba aendelea kupumulia mashine

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Dk. Joseph Hosea, anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matitabu.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya TAKUKURU, Dk. Hosea, alianza kuugua tangu mwanzoni mwa Desemba mwaka jana na ilipofika Desemba 15 hali ilibadilika.



Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU kilisema hadi sasa haijafahamika ugonjwa unaomsumbua.



“Ni kweli Mkurugenzi anaumwa na kuna taarifa yuko ya nje ya nchi kwa matibabu kati ya Ujerumani au Uingereza.



“Kwa mara ya mwisho nilimuona Mkurugenzi akiwa hayupo sawa kiafya na hata alipokuwa anakuja kazini alikuwa katika muonekano ambao ni wazi anaumwa. Lakini katika wiki hizi sijamuona hapa ofisini,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU.



MTANZANIA pia ilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) George Mkuchika kwa njia ya simu kupata taarifa za kina kuhusu tukio hili lakini alisema hana taarifa yoyote.



“Mhhhh katika hili la ugonjwa wa Dk. Hosea sina taarifa na kama ujuavyo nilikuwa katika msiba wa baba yake Naibu Waziri wa Mifugo, kule Kiteto. Tangu jana nilikuwa n rejea na nimefika Morogoro nimelala hapa na sasa nimeanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.



“Kama kuna taarifa yoyote kuhusu hilo kwa sasa siwezi kusema lolote hadi nitakapofika ndugu yangu,” alisema Waziri Mkuchika.



Hata hivyo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Dk. Hoseah yupo nje ya nchi kwa mapumziko ya likizo.



“Ni kweli ofisa uhusiano yupo likizo na pia mkubwa (Dk. Hoseah) naye yupo Marekani ameenda kwa ajili ya mapumziko ya likizo hakuna mtu anayeumwa,” alisema.



MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa TAKUKURU Dorine Kapwani ambaye muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa hata alipopigiwa kwa simu ya mezani.



Mbali na hatua hiyo hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa simu ya kiganjani ambao ulisomeka; “Dada habari, kuna taarifa Dk. Hosea anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu je kuna ukweli gani” hakujibu chochote hadi tunakwenda mitamboni jana usiku.



DCI Manumba apumulia mashine



Naye Elizabeth Mjatta anaripoti kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba sasa anapumua kwa msaada wa mashine baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.



DCI Manumba jana alitumia takribani siku nzima kuwa katika chumba cha uchunguzi kwa ajili ya vipimo zaidi, baada ya kutolewa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.



MTANZANIA ilishuhudia DCI akitolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi saa 11:25 akipelekwa katika chumba cha uchunguzi huku akiwa amezungukwa na madaktari na wauguzi huku baadhi yao wakiwa wameshikilia vifaa maalumu ambavyo vilikuwa vikimsaidia kupumua. 



Hata hivyo, baadhi ya madaktari waliokuwa wamemzunguka hawakuweza kuthibitisha iwapo vifaa alivyokuwa amewekewa DCI Manumba vilikuwa ni sehemu ya mashine iliyokuwa ikimsaidia kupumua.



Hali hiyo iliwafanya ndugu na watoto wa kamanda huyo kuwa katika hali ya taharuki ambako baadhi yao walionyesha kushikwa na huzuni huku mmoja wa watoto wake ambaye jina lake halikupatikana akiwa katika hali ya majonzi makubwa.



Hadi MTANZANIA inaondoka katika Hospitali ya Aga khan saa 5:45 jioni mgonjwa huyo bado alikuwa hajatolewa katika chumba cha uchunguzi hali iliyowafanya ndugu kuendelea kusubiri katika eneo la mapokezi ya wagonjwa mahututi.



Alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu hali ya mgonjwa, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk. Jaffer Dharsee alisema kwa sasa hawezi kusema lolote hadi vipimo vya uchunguzi vitakapokamilika, huku akiwaahidi waandishi wa habari kuwa atatoa taarifa hiyo leo asubuhi.



“Siwezi kusema kitu kwa sasa kwani bado hali ya DCI inahitaji uchunguzi wa karibu wa madaktari na hadi sasa bado yupo katika chumba cha uchunguzi zaidi hivyo sina cha kusema nasubiri nikamilishe ripoti yote labda kesho ndiyo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema kitu,” alisema Dk Dharsee.



Hata hivyo katika kipindi chote hicho, hali ya ulinzi ilikuwa imeimarika ambako polisi na askari kanzu walikuwa wamezunguka katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha.



Viongozi



Jana viongozi mbalimbali waliendelea kufika hospitalini hapo kumjulia hali Manumba. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima ambaye aliwasili hospitali hapo mchana pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick.



Viongozi wote hao walipokewa na daktari mkuu wa polisi aliyefahamika kwa jina moja la Dk Makata ambaye aliwapeleka moja kwa moja katika jengo la tatu kilipo chumba cha uchunguzi kwa ajili ya kumjulia hali DCI Manumba.



Dk. Nchimbi baada ya kutoka katika chumba cha mgonjwa hakutaka kuzungumza chochote licha ya kutakiwa kufanya hivyo na waandishi wa habari. “Mnataka niseme nini kwamba mgonjwa hali yake nzuri au mbaya? Mimi si daktari lakini kwa namna nilivyomuona nasema anaendelea vizuri,” alisema Dk. Nchimbi.



DCI Manumba aliugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili na Januari 14 alihamishiwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).



Manumba ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mwaka 2006 akichukua nafasi ya Adadi Rajabu, haijaelezwa wazi kuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani, ingawa taarifa za awali zinasema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo.

CHANZO: Mtanzania

23 Jul 2011


Hili sio ombwe tena bali mkusanyiko wa wababaishaji walioteuliwa na mtu asiyejua kwanini aliwateua,na ndio maana wanaendesha mambo kama kwenye mchezo maarufu wa watoto ujulikanao kama kombolela.Watu wazima ovyoo!Lakini ni wazi wanapata jeuri ya kufanya ubabaishaji huo kwa vile wanafahamu fika kuwa aliyewateua hana jeuri ya japo kuwawajibisha,let alone kuwakemea.

Anyway,hebu soma madudu yao hapa chini:

DPP amkana Hoseah  
Friday, 22 July 2011 20:27

ASEMA HAJAPATA JALADA LA CHENGE, AAMBIWA AKAANGALIE MASJAJA
Nora Damian
SIKU moja baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, kusema kwamba ofisi yake imekamilisha uchunguzi wa madai ya kumiliki Dola za Marekani 1.2 milioni katika Kisiwa cha Jersey, Uingereza yanayomkabili Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge na kwamba imekabidhi faili lake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kumfungulia mashtaka, kiongozi wake, Eliezer Feleshi amejitokeza na kusema kwamba hawahi kuliona jalada hilo.

"Niko safarini subiri hadi wiki ijayo… kwanza ashtakiwe kwa kosa gani? Acheni siasa nyie,” alisema DPP alipotakiwa kuthibitisha kama jalada hilo limefika mezani kwake na lini Mwanasheria huyo Mkuu wa zamani wa Serikali atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili... “Aseme ni tarehe gani alileta jalada hilo kwangu?”

Kutokana na majibu hayo ya DPP, Mwananchi lilimtafuta Dk Hoseah kupata ukweli juu ya kauli yake hiyo aliyoitoa juzi huko Arusha na kusisitiza kuwa jalada hilo limepelekwa katika Ofisi ya DPP na kumtaka mkuu huyo wa Mashitaka nchini asiharakishe kusema hajaliona, kwani siyo lazima kila kitu akabidhiwe mikononi... “Kwani kila kitu kinachopelekwa kwake lazima akione? Ameangalia registry (masjala)?. Suala hili nimeshaliongea nanyi vya kutosha hivyo muulizeni zaidi DPP.”

Juzi, Dk Hoseah alisema taasisi yake imekamilisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Chenge na kwamba jalada lake limepelekwa kwa DPP kwa hatua zaidi. Alisema Chenge atashtakiwa chini ya Kifungu cha 27 cha Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007. Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu akiwa na mali ambazo hazilingani na kipato chake alichokipata akiwa madarakani au baada ya kuondoka ni kosa kisheria.

Chenge anadaiwa kukutwa na kiasi hicho cha fedha mwaka 2008 baada ya uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa rada uliofanywa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO). Tuhuma hizo ndizo zilizomfanya alazimike kujiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu mwaka huo.

Malumbano kati ya Dk Hoseah na Feleshi siyo ya kwanza. Mwaka jana waliwahi kulumbana baada ya mkuu huyo wa Takukuru kusema kuna majalada takriban 50 ya kesi za rushwa ambayo yamekaliwa na DPP.

Pia Dk Hoseah aliwahi kumshutumu DPP mbele ya wabunge wakati wa semina elekezi mapema mwaka huu akidai kwamba amekuwa kikwazo cha kesi kubwa za ufisadi kupelekwa mahakamani kwa kukwamisha majalada.

CHANZO: Mwananchi 

26 Feb 2010



Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa TAKUKURU Dr. Edward Hosea akimkaribisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete kufungua mkutano mkuu wa Mwaka wa taasisi hiyo.Picha kwa hisani ya MJENGWA

Hivi karibuni,uongozi wa kampuni ya magari ya Toyota ya Japan ulifanya jambo moja la kiungwana kwa kuwaomba radhi wateja wake kutokana na hitilafu za kiufundi katika modeli moja ya magari yake.Japo sakata hilo bado ni bichi hasa kwa vile inaelekea hitilafu hiyo bado haijapatiwa ufumbuzi,na tayari kuna habari za kushuka kwa hisa za kampuni hiyo katika masoko mbalimbali ya mitaji duniani,ni dhahiri hatua ya kuomba radhi imeonyesha kwamba kwa namna flani kampuni hiyo inatambua wajibu wake na inawajali wateja wake.

Majuzi,Rais Jakaya Kikwete alimwaga sifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) huku akijigamba kwamba serikali ya awamu ya nne imekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa.Binafsi sidhani kama kauli hiyo ya JK inaendana na hali halisi ya utendaji na ufanisi wa TAKUKURU.

Kimsingi,tatizo haliko kwenye taasisi hiyo pekee bali kwenye medani nzima ya utawala bora.Angalia,kwa mfano,kauli za Waziri mwenye dhamana ya Utawala Bora,Mheshimiwa Sophia Simba,wakati wa sakata lililowahusisha wafanyabiashara wawili mashuhuri Bwana Reginald Mengi na Bwana Rostam Aziz.Badala ya kuhamasisha wananchi wanaojitokeza kuwaumbua hadharani mafisadi,Waziri Simba aliamua kuelemea upande mmoja ambapo bila aibu alimkemea Bwana Mengi huku akimlinda Bwana Rostam.

TAKUKURU hiyohiyo inayopongezwa na JK haijafanikiwa kujisafisha na tuhuma za namna ilivyouhadaa umma kuhusu suala la utapeli wa kampuni ya Richmond.Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata hilo ilipendekeza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Dr Edward Hosea,uamuzi ambao uko mikononi wa aliyemteua Hosea,yaani JK mwenyewe.Kwa hali ilivyo,na ukitilia maanani pongezi alozotoa JK kuhusu ufanisi katika mapambano dhidi ya ufisadi,ni dhahiri kuwa Rais hana mpango wa kumwajibisha Dr Hosea.

Nimesema tatizo liko kwenye utawala bora kwa vile hata chama tulichokipa dhamana ya kutuongoza-CCM-kimeendelea kufanya dhihaka linapokuja suala la utawala bora.Hivi inaingia akilini kweli kusikia kuwa Mbunge wa Bariadi,Bwana Andrea Chenge,bado ni mwenyekiti wa kamati ya maadili ya chama hicho tawala licha ya kuhusishwa kwake na tuhuma za ufisadi wa ununuzi wa rada!?Tusisahau kuwa pamoja na mageuzi ya kisiasa ya miaka ya tisini,bado chama tawala kimeendelea kuwa na nguvu pengine zaidi ya serikali,hoja kubwa ikiwa serikali hiyo imeundwa kutokana na ushindi wa chama husika.Kinachopuuzwa ni ukweli kuwa chama hicho hakikuomba ridhaa ya wanachama wake pekee bali Watanzania kwa ujumla.

Ni dhahiri kwamba kunakosekana utashi na udhati wa kupambana na ufisadi.Na kikwazo kikubwa kimeendelea kuwa kuweka mbele maslahi binafsi na ya chama badala ya maslahi ya umma/taifa.Pengine,na kwa hakika,badala ya kutetea mapungufu,ni muhimu kwa CCM na serikali yake kuiga mfano wa kampuni ya Toyota.Imetuangusha sana sio tu kwa kulegea katika mapambano dhidi ya ufisadi bali pia kwa ushiriki wake kwa kuwalinda watuhumiwa wa ufisadi.Laiti chama hicho kingekuwa na dhamira na utashi wa kukabiliana na ufisadi basi ni dhahiri Kamati ya Mwinyi inayoshughulikia mpasuko ndani ya chama hicho (wengine wanadai hakuna mpasuko) ingekuwa na kazi nyepesi tu ya kupendekeza wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili wasafishwe au waadhibiwe huko.Ikumbukwe kuwa tuhuma zinazowakabili watuhumiwa hao hazijaiathiri CCM pekee bali Watanzania wote kwa ujumla.

Nimalizie kwa kukumbushia usemi wa Kiingereza kwamba To err is human but to rectify is greatness,yaani (kwa tafsiri isiyo rasmi) kukosea ni ubinadamu lakini kujirekebisha ni uungwana.

13 Dec 2009


Mara Sophia Simba dhidi ya Anne Kilango,mara Rostam Aziz dhidi ya Mwakyembe,mara tunaambiwa Kamati ya Mwinyi nako "hakieleweki",na sasa watendaji wakuu na wateuliwa muhimu wa Rais,Mkurugenzi wa TAKUKURU Dr Edward Hosea na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Eliezer Feleshi nao wameingia kwenye malumbano,kama linavyoripoti jarida la Mwananchi

DPP amvaa Dk Hoseah, ataka mdahalo majalada kesi za kifisadi

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah ambaye jana alidai kuwa DPP amekalia kesi 60 tuhuma za rushwa

James Magai

KWANZA ilikuwa ni ndani ya chama tawala CCM, lakini malumbano baina ya vigogo sasa yamehamia serikalini baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi kujibu mashambulizi ya mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, akitaka uitishwe mdahalo baina ya wawili hao ili ajibu tuhuma dhidi yake.

Pendekezo hilo la Feleshi limekuja wakati malumbano baina ya viongozi wa CCM hayajapoa baada ya kutuhumiana kwa ufisadi na wivu wa nafasi mbalimbali zilizotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Dk Hoseah, ambaye amekuwa akirusha makombora kwa taasisi tofauti, juzi alitoa tuhuma nzito alipokaririwa na gazeti moja akisema kuwa ameshawasilisha kesi zaidi ya 60 za tuhuma za rushwa kwa DPP na akashangaa sababu za mteule huyo mwenzake wa rais kukalia mafaili hayo badala ya kufungua kesi dhidi ya watuhumiwa.

Lakini jana Feleshi alikuwa mbogo na akasema kuwa ili ukweli uwekwe bayana kuna haja ya kuandaa mdahalo baina yake na Hoseah.

DPP Feleshi, akizungumza na gazeti dada la Mwananchi la The Citizen baada ya hafla ya mafunzo ya kamati ya kitaalamu ya mawakili wa serikali iliyofanyika Kunduchi jijini Dar es Salaam, alisema njia pekee ya kuweka sawa rekodi ni kuwepo kwa mdahalo huo wa wazi.

"Ninataka mdahalo na Hoseah katika masuala haya yanayoendelea hata kama utakuwa wa simu tena iwekwe ‘loud speaker (kipaza sauti)’ ili tujadili masuala haya na kumaliza kiu ya wananchi," aliweka msimamo DD Feleshi.

"Kama mtu anasema kuna majalada 60 ofisini kwangu, then (kisha) tunamuuliza yamefika lini? Yeye pia atajibu, kwa kufanya hivyo tutatoa mwanga mzuri kwa wananchi ambao ofisi hizi zipo kwa ajili yao tu."

DPP Feleshi alisema anataka mdahalo huo ufanyike mbele ya waandishi wa habari ili jamii ijue masuala mbalimbali yanayoelekezwa ofisini kwake.

Hoseah pia aliwahi kuirushia kombora mahakama akisema inaendesha taratibu kesi za ufisadi, hivyo kupunguza kasi ya taasisi hiyo kushughulikia watuhumiwa wa rushwa.

Miongoni mwa kesi ambazo zilifunguliwa kwa wingi hivi karibuni na Takukuru ni pamoja na kesi zaidi ya 20 zinazohusu wizi kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), matumizi mabaya ya madaraka na uzembe na tuhuma za kula njama na kuisababishia hasara serikali.

Hata hivyo, mwenendo wa kesi nyingi umekuwa wa kasi ndogo kutokana na upande wa mashtaka kutokamilisha ushahidi.

Akizungumzia madai hayo ya Hoseah, Feleshi aliweka bayana kwamba hayajui majalada hayo na anachojua ni kwamba ofisini kwake kuna majalada ya kesi ambayo yanaingia na kutoka kila siku na anayashughulikia kwa mujibu wa sheria.

Feleshi, ambaye aliwahi kurejesha Takukuru baadhi ya majalada kutokana na kuonekana udhaifu katika ushahidi, alimtaka Dk Hoseah kutoa ufafanuzi kwa kueleza ni majalada gani yanayokaliwa na ofisi yake na yamefika lini.

Alifafanua kwamba ofisi yake haiwezi kukalia majalada kwa kuwa inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwa maslahi ya umma na kusisitiza hayajui majalada hayo 60 anayodai Dk Hoseah kwamba yamekaliwa ofisini hapo.

"Hayo mafaili (majalada) ya vigogo mimi siyajui. Ninachojua ni kwamba tuna majalada yanaingia kila siku ya Watanzania wanaotuhumiwa. Tunapokea na kuyafanyia kazi... na hatubagui kuwa haya ni ya PCCB (Takukuru) , TRA( Mamlaka ya Mapato) au ya Polisi. Katiba ya nchi inatoa haki sawa kwa wote kufikishwa mbele ya sheria ili kupata haki," aliongeza DPP.

"Tunafanya kazi kwa maslahi ya umma na tunaendesha shughuli zetu kisheria wala si kwa kuzingatia jambo lolote kwa kuwa hatuna maslahi yoyote kumshtaki mtu bila kuwa na ushahidi wala hatuna maslahi yoyote kumwachia mtu kama kuna ushahidi. Ndiyo maana nasema hakuna kukalia majalada."

Feleshi, ambaye ana mamlaka ya kufunga au kufungua mashtaka kwa watuhumiwa, alisema katika hali hiyo ni vigumu kusema kuna majalada yana muda mrefu kwani hajui hayo yanayosemwa yaliingia lini ofisini kwake.

"Labda kama angekuwepo mwenyewe (Dk. Hoseah) angeeleza zaidi hayo majalada anayodai tumeyakalia. Ni vema mkamuuliza hilo," alisema.

Hizi ni dalili za wazi kwamba kuna ombwe la uongozi wa kitaifa.Yaani kila mtu anaropoka anavyopenda hasa kwa vile mwenye jukumu la kukemea yuko usingizini fofofo.Nidhamu imekuwa zero kwa vile anayepaswa kuwaadabisha watovu wa nidhamu yuko bize na mambo mengine yasiyo na umuhimu kwa taifa.

Tunaelekea pabaya japo Watanzania wengi hawaonekani kuguswa na hali hii.

Ni vema tukaamua kuchukua maamuzi mazito kabla hali haijafikia mahala tusipoweza kurekebisha.Tusipoziba ufa tujajenga ukuta.Unfortunately,baada ya ukuta kuanguka kutokana na nyufa zilizopo tunaweza kushindwa kujenga ukuta huo baada ya matofali yote na tanuru zima kuuzwa na mafisadi.

2010 INAKUJA.IT'S THEN OR NEVER!

12 Nov 2008

MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, amesema kuwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi kwa pamoja kunaweza kusababisha nchi kuyumba.

Hoseah alisema hayo katika siku ambayo hakukuwa na mtuhumiwa yeyote katika sakata la wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) aliyefikishwa mahakamani baada ya wafanyabiashara 20 kupandishwa mfululizo kizimbani kuanzia Jumatano iliyopita hadi juzi.

Akitoa mada kwenye semina iliyohusisha vyuo vikuu tisa nchini iliyofanyika kwenye Hoteli ya Blue Pearl jijini, mkurugenzi huyo wa Takukuru alisema: "Tukiwapeleka wote mara moja mahakamani, nchi inaweza 'ikaparalyse' (ikapooza) ni lazima kuwe na 'stability' (kutoyumba), tufanye kwa kuwa ni sahihi," alisema Hoseah.

Akitoa mada katika semina hiyo iliyowahusisha wajumbe wa kamati za maadili kutoka vyuo hivyo, Hoseah alieleza kuwa, mapambano dhidi ya rushwa kubwa yanapaswa kufanyika kukiwa na utashi wenye nguvu wa kisiasa, mikakati sahihi ya kiuchumi pamoja na kuzuia rushwa.

Alisema kuwa watuhumiwa wa rushwa kubwa wana nguvu kutokana na fedha nyingi wanazomiliki, kiasi cha kuweza kuhatarisha usalama wa watu wengine kwa kutumia vibaya fedha zao.

Dk Hoseah ni kigogo wa tatu kuzungumzia uwezo wa mafisadi na hatari ya kuwashughulikia bila ya umakini baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kulieleza bunge kuwa, kushughulikia watu wenye uwezo wa kifedha ni kazi ngumu, kama ilivyoelezwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan Mwinyi kuwa mafisadi ni hatari.

Watuhumiwa katika kashfa hiyo ya EPA wanadaiwa kuchota fedha hizo katika kipindi cha mwaka 2005/06 wakisingizia kupewa au kulipa madeni na makampuni ya nje yaliyokuwa yakiidai serikali. Watuhumiwa hao wanadaiwa kuchota Sh133 bilioni.

Pamoja na kilio cha wananchi kuwa wote waliochota fedha hizo wapandishwe kizimbani, Rais Jakaya Kikwete alitoa maagizo kuwa wale ambao wangeshindwa kurejesha fedha walizochota kabla ya Oktoba 31, ndio waliotakiwa kufikishwa mahakamani.

Na watuhumiwa hao 20 waliofikishwa mahakamani hadi sasa wamekuwa wakipandishwa kizimbani kwa nyakati tofauti na wengi wameshtakiwa kwa makosa tofauti, wakipandishwa mmoja mmoja na wakati mwingine kuunganishwa na wenzao na kwa mahakimu tofauti.

Akitoa mada yake jana, Dk Hosea alisema Takukuru peke yake haiwezi kumaliza tatizo la rushwa nchini bila kuwepo ushirikiano kutoka kwa taasisi za elimu, mashirika mbalimbali na wananchi.

Aliongeza kuwa, mapambano dhidi ya rushwa, kubwa na ndogo yanapaswa kuwashirikisha wananchi wote, huku akielezea Watanzania kuwa ni waoga kutokana na kukosa ufahamu wa masuala mbalimbali yanayowahusu.

Hoseah alisema kuwa katika mapambano ya rushwa ni vema kuzuia rushwa na kwamba uadilifu ndiyo njia bora ya kulitokomeza tatizo hilo.

Alisema moja ya kasoro za Tanzania ni kuwa na taasisi nyingi dhaifu, zisizo na uwezo zinazofanya kazi zake bila ya uwazi, hali aliyoielezea kuwa inakaribisha rushwa.

"Moja ya kasoro za Tanzania ni kuwa na taasisi dhaifu, zisizo na uwazi... lazima tufanye kazi kuzipa nguvu kwa kurejesha maadili," alisema Hoseah.

Aliongeza kuwa, ndani ya serikali pia uadilifu upo chini na kueleza kuwa kuwa kutokana na hali hiyo ni vema wananchi wakaacha kulalamika badala yake kutafuta ufumbuzi wa tatizo kwa kushiriki kurejesha maadili na kupambana na rushwa.

Alisema kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakilalamikia tatizo la rushwa huku wakishinikiza Takukuru ichukue hatua bila wao kushiriki katika mapambano hayo ambayo alisema kuwa ni ya kila mmoja.

Mkurugenzi huyo wa Takukuru alisema kuwa katika kutilia maanani umuhimu wa kuongeza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa nchini, wameanzisha mkakati maalumu wenye lengo la kurejesha uadilifu nchini.

"Tunataka kurejesha maadili, lengo ni kuzuia rushwa, jukumu letu ni kuwawezesha watu wafahamu na kushiriki katika mapambano hayo," alisema.

Kwenye Mahakama ya Kisutu, hali jana ilikuwa shwari baada ya siku nne za purukushani za kupandisha kizimbani watuhumiwa hao 20, ambao kati yao ni wawili tu waliopata dhamana kutokana na mahakama kuweka masharti magumu, anaripoti James Magai na Paulina Richard.

Hadi majira ya alasiri jana, hakuna mtuhumiwa hata mmoja mpya kwenye kesi hiyo ambaye alikuwa amefikishwa mahakamani hapo.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Charles Kenyela, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi mchana huo hakuwa na taarifa za kuwepo kwa watuhumiwa wengine ambao wangepandishwa kizimbani.

Mpaka sasa ni wamiliki wa kampuni 10 tu kati ya 22 zinazodaiwa kuchota fedha hizo ambao walikuwa wameshafikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akiwemo mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya Kiasia, Jayatkumar Chantubhai Patel, ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Jeetu Patel.

Tofauti na siku nyingine jana hali ilionekana kuwa tulivu mahakamani hapo huku kukiwa na pilikapilika chache za baadhi ya ndugu wa watuhumiwa katika kashfa hiyo ya EPA ambao walikuwa wakishughulikia dhamana za watuhumiwa hao.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Elieza Feleshi, hakutaka kuwaambia waandishi kama kuna watuhumiwa zaidi ambao wangefikishwa mahakamani jana na badala yake alisema aulizwe msemaji wa Wizara ya Sheria na Katiba.

Hata hivyo, msemaji huyo, Omega Ngole alijibu kwa ufupi kuwa hawawezi kusema ni lini watuhumiwa wanapelekwa mahakamani na badala yake taratibu zinapokamilika na DPP kujiridhisha, wahusika hufikishwa mahakamani.

“Hivyo ninachoweza kukuambia ni kwamba, tumwache DPP afanye kazi, kama kuna watu wa kuwapeleka mahakamani akishajiridhisha atawapeleka,” alisema Ngoe.

Wamiliki wa makampuni waliofikishwa mahakamani mpaka sasa ni Johnson na Mwesiga wanaomiliki kampuni ya Kernel, Ketan Chohan, Jeetu Patel na Amit Nandy (Bina Resort na Itoh), Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Edah Nkoma Mwakale (Changanyike Residential Compelex Ltd)

Wengine ni Rajabu Farijala, Japhet Lema na Rajabu Malanda (Mibale Farm), Rajabu Farijala na Rajabu Malanda (Money Planner), Japhet Lema (Njake Enterprises) na Ajay Somani na Jay Somani (Liquidity Services).

Wengine ni Jeetu Patel na ndugu zake wanaomiliki kampuni za Bencon International Ltd, Maltan Mining Ltd na Navy Cut Tobacco (T) Ltd.

CHANZO: Mwananchi

HAYO NDIO MATUNDA YA PhD YA HOSEA KATIKA KUPAMBANA NA RUSHWA AU NDIO APPLICATION YA THEORY FLANI YA KULINDA UHALIFU INAYODAI KWAMBA UKIFUTA KABISA UHALIFU KWENYE JAMII BASI VYOMBO VYA KUPAMBANA NA UHALIFU VITAKUWA HAVINA KAZI YA KUFANYA?MBONA VITA YA SOKOINE DHIDI YA WAHUJUMU UCHUMI HAIKUYUMBISHA NCHI?

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.