Hapana,leo sio April 1-Siku ya Wajinga- bali habari ifuatayo ni ya kweli na wala si kanyaboya flani.Baada ya usanii uliodumu kwa takriban mwezi mzima,hatimaye CCM imerejea kwenye asili yake.Wengine tulishashtukia mapema usanii uliobeba jina la "kujivua magamba".Tangu lini nyoka akageuka mjusi baada ya kujivua magamba?Na tangu lini mchawi akageuka mtu mwema kwa vile tu kavua tunguri?
Enewei,habari kamili ni hii:
CCM yatoa msimamo
*Mukama asema maazimio ya NEC yamepotoshwa*Ataka chama kiheshimu taratibu, aisulubu ChademaNa Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, amesema Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, haijawahi kutoa maazimio ya kuwataka watuhumiwa wa ufisadi kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya siku 90, ila wenye kutoa kauli hizo wanapotosha.
Mukama alikuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari vyote nchini, walipokutana jijini Dar es Salaam jana. Alitoa kauli hiyo baada ya kuhojiwa ataje majina ya mafisadi ni akina nani, na kwamba barua wanazosema watapewa zitakabidhiwa lini kwa wanachama hao wa CCM.
Akizungumza kwa tahadhari kubwa, Mukama alisema NEC ilitoa maazimio 26, na kati ya hayo, azimio namba 15 lilikuwa likiwataka watuhumiwa wa ufisadi, “kupima, kutafakari na kuchukua hatua wenyewe,” ila akaongeza kuwa wakati Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete anafunga kikao cha NEC, alisema watuhumiwa wasipochukua hatua wenyewe chama kitawachukulia hatua.
“Kwa maana hiyo, kuna watu wame-hype information (wamepotosha taarifa kwa propaganda)… sijui hizi siku 90 zimetoka wapi? Kwanza NEC haikutani kila baada ya siku 90. NEC inakutana kila baada ya siku 120, yaani miezi minne au mara tatu kwa mwaka… Mimi nasema maamuzi ya NEC hayakutaja majina ya watu. Kitu hiki hakipo. Mtuache kama Chama tuna taratibu zetu, wala hatuhitaji mashinikizo kutoka popote,” alisema Mukama.
Mukama alisema yeye anaamini katika utaratibu wa kuendesha chama kama taasisi, hivyo kauli za watu zinazotoa siku 90 si za chama, bali chama kinasimamia maamuzi yanayotokana na kumbukumbu rasmi ambazo ni maazimio 26 ya NEC na hotuba rasmi ya Mwenyekiti wao wakati anafunga kikao cha NEC.
Msimamo huu wa Katibu Mkuu Mukama, umekuwa tofauti na kauli zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Chiligati na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambao wamekuwa wakitamba kuwa baada ya siku 90 chama kitawafukuza kwenye chama watuhumiwa wa ufisadi ikiwa wao watashindwa kujiondoa sasa.
Hata hivyo, Mukama alisema watu wanaotuhumiwa wanapaswa kufikiri na kuchukua hatua wenyewe wanazoona zinafaa kwa nia ya kujenga chama chao upya. Alisema falsafa ya kujivua gamba imefanyiwa kazi kwa Kamati Kuu na sekretarieti ya chama kujiuzulu, hivyo hakuna sababu ya watu kupotosha falsafa hiyo na kukilazimisha chama kufanya maamuzi ya kujiua.
Wakati huo huo, Mukama alikishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa kitakufa kabla ya CCM, kwani chama hicho kimeanzishwa kwa shinikizo la Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF). “You can quote me on this (nikariri katika hili) Chadema kilianzishwa kwa shinikizo la IMF. Yule aliyetofautiana na Nyerere ndiye aliyekwenda kukianzisha,” alisema Mukama bila kufafanua.
Katika mkutano huo, Mukama aliambatana na Katibu wa Idara ya Siasa na Mambo ya Nje, January Makamba, Katibu wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Mchemba na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Mukama alisema CCM haijapoteza mwelekeo, na itaendelea kujijenga upya kwa nia ya kutumikia vyema wananchi, huku akisisitiza kuwa mabadiliko yaliyofanywa yalikuwa ya lazima kukipa uhai mpya chama hicho.
CHANZO: New Habari