Zaidi ya shilingi bilioni 150 zimefisadiwa kutoka katika Mfuko wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi,na hiyo ni kwa mwaka juzi (2008) pekee. Kiasi hicho kinajumuisha shilingi bilioni 71.2 zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2007/8 lakini hazifika mahala zilipokusudiwa.Utafiti unachofuatilia mwenendo wa matumizi ya fedha za umma-PETS (Public Expenditure Tracking Survey)kinaonyesha kuwa takriban shilingi bilioni 47 zinatafunwa kila mwaka kwa udanganyifu wa malipo hewa katika sekta ya elimu.
Ripoti inayoonyesha ufisadi huo,ambayo ni ya kina zaidi kuliko zilizotangulia,ilikabidhiwa kwa serikali tangu mwezi April mwaka jana.
Gazeti la Citizen limepata nakala ya ripoti hiyo ambayo inaonyesha kwa kiasi gani udhibiti hafifu wa mifumo ya fedha za umma unavyochangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.
Serikali iliamua kuagiza utafiti huo kwa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara ili kubaini kama kutanuka kwa miundombinu ya elimu na kiwango cha wanafunzi wanaojiunga na shule kunaendana na kuongezeka kwa raslimali zinazotengwa.
Kadhalika,ilitaka kufahamu kama raslimali zinafika kwa watoa huduma,hususan shule, na kwa kiwango gani mipango ya utanuzi imetekelezwa pasipo kuathiri kiwango cha ubora wa elimu kwa kuzingatia kipimo cha matokeo ya wanafunzi.
Taasisi zilizoshirikishwa katika kipimo hicho ni pamoja na Wizara za Elimu na Mafunzo,Fedha na Mipango ya Uchumi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa),Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto,na Shirika la Taifa la Takwimu (TBS).Kadhalika,wawakilishi wa vikundi vya kiraia na wahisani walihusishwa.
Kwa majibu wa matokeo ya utafiti huo,wakati kwa miaka kadhaa sasa serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya elimu kutoka shilingi bilioni 701.1 mwaka 2005/6 hadi kufikia shilingi trilioni 1.43 mwaka 2008/9 na shilingi trilioni 2.045 kwa mwaka 2010/11,raslimali kwa elimu ya msingi zimekuwa zikishuka kutoka asilimia 55.8 zilizotengwa miaka mitano iliyopita hadi asilimia 46.6 mwaka juzi.
Fedha kwa ajili ya ujezi wa madarasa,nyumba za walimu,vyoo na miundombinu mingine pia zimekuwa zikishuka kwa kasi.Wakati wastani wa fedha zilizotengwa zilikuwa wastani wa shilingi bilioni 109 katika awamu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (PEPD)kutoka mwaka 2002 hadi 2006,kiwango hicho katika mwaka wa fedha 2010/11 kimeshuka hadi kufikia shilingi bilioni 14 tu katika awamu ya pili ya PEPD kuanzia mwaka 2007 hadi 2011.
Na athari ni za hapo kwa hapo na za kina.Kwa mujibu wa takwimu,wakati madarasa 10,771 yalijengwa miaka saba iliyopita,idadi hiyo imepungua hadi kufikia 1,263 katika mwaka 2008.Hiyo ni mbali ya ukweli kwamba uwiano kati ya wanafunzi na uwezo wa darasa ulikuwa 1:78 kwa mwaka huo ni takrban maradufu ya uwiano stahili wa darasa moja kwa wanafunzi 40 (1:40)
Pia Utafiti huo ulibaini kuwa wakati shilingi bilioni 544.2 zilitolewa kwa manispaa kama mtaji na misaada ya kawaida kwa sekta ya elimu katika mwaka wa fedha 2008,kiwango halisi kilichopokelewa kilikuwa shilingi bilioni 473 na kuacha pengo la shilingi bilioni 71.2
Kadhalika,utafiti huo unaonyesha kuwa mamlaka 66 kati ya 131 zilizohusishwa katika utafiti huo zilielekeza shilingi bilioni 28.9 kwenye matumizi mengineyo badala ya minajili ya elimu kama ilivyokusudiwa.
Mwaka 2008,serikali iliwapangia vituo walimu wapya 1271 katika maeneo ya vijijini lakini ni asilimia 35 tu (walimu 444) walioripoti maeneo hayo.Lakini,wakati jiji la Dar es Salaam lilipangiwa walimu 182 tu,mamlaka husika ziliajiri walimu 441.
Habari hii imetafsiriwa kutoka gazeti la The Citizen