Showing posts with label SHAMSI VUAI NAHODHA. Show all posts
Showing posts with label SHAMSI VUAI NAHODHA. Show all posts

29 Jun 2011


Serikali yafanya kufuru
• Yatumia milioni 50/- kumlipia Waziri Hoteli

na Martin Malera Dar na Dauson Kaijage, Dodoma

SERIKALI inatumia zaidi ya sh milioni 50 kwa mwezi kwa ajili ya kugharimia malazi na chakula kwa ajili ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, anayeishi katika Hoteli ya New Afrika tangu alipoteuliwa, Tanzania Daima Jumatano, limebaini.

Taarifa ya Waziri Nahodha kuishi hotelini, ziliibuliwa bungeni wiki iliyopita wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Ingawa taarifa ya bungeni hazikuwa za kina, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini Nahodha ambaye amepata kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amekuwa akiishi hotelini hapo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Novemba mwaka jana.

Habari kutoka ndani ya hoteli hiyo yenye hadhi ya Nyota Nne zilisema waziri huyo amepangishiwa vyumba vitatu ndani ya hoteli hiyo.

Inaelezwa kwamba amepanga kwenye moja ya vyumba maalumu kwa vigogo, (Executive); chumba ambacho kina sehemu mbili, ikiwemo ya kulala na ya kumpumzikia.

Kwa mujibu wa habari hizo, chumba hicho kinalipiwa dola 300 kwa siku, sawa na sh 480,000.

Vyanzo vyetu vya habari vilitonya kuwa chumba cha pili kinatumika kwa ajili ya walinzi na wasaidizi wake na cha tatu ni kwa ajili ya wageni muhimu wanaomtembelea hotoleni hapo hasa familia yake ambayo iko Zanzibar.

Habari hizo zinasema vyumba hivyo vinagharimu dola 220 kila kimoja kwa siku.

“Kwa maana hiyo, serikali kwa siku inalipa dola 740, sawa na sh 1,124,800 kwa ajili malazi tu ya Waziri Nahodha.

“Kwa hiyo ukifanya hesabu kwa mwezi serikali inalipa sh milioni 33.7 kwa ajili ya malazi tu ya Waziri mmoja na hadi sasa ana miezi saba hotelini,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Kwa mujibu wa habari hizo, gharama hizo ni mbali ya chakula na huduma zingine hotelini ambazo kwa mwezi ni zaidi ya sh milioni 20, hivyo kufikia kiasi cha sh milioni 50 kwa mwezi.

Sababu kubwa ambayo inadaiwa na serikali kumfanya waziri huyo aishi hotelini ni uhaba wa nyumba za mawaziri.

Inadaiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani aliyepita, Laurence Masha, alikuwa akiishi nyumbani kwake katika kipindi chote alichoshika nafasi hiyo na wala siyo kwenye nyumba ya serikali.

“Kwa hiyo Nahodha alipoteuliwa kushika wadhifa huo, serikali ikajikuta haina nyumba kwa ajili ya Waziri wa Mambo ya Ndani na hicho ndicho chanzo cha Waziri Nahodha kulala hotelini,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Mbali ya Nahodha, kuna mawaziri wengine wanne wanaoishi hotelini kutokana na uhaba wa nyumba za serikali.

Uchunguzi zaidi unasema kuwa sababu kubwa ya Waziri Nahodha na wenzake kukosa nyumba, ni serikali kuwaacha baadhi ya mawaziri waliotemwa kuendelea kuishi kwenye nyumba za serikali.

“Kuna waziri alifariki; mjane wake bado anaishi kwenye nyumba za serikali, wapo mawaziri waliotemwa, wameomba wabaki kwa muda kwenye nyumba za serikali, ili wajipange. Hawa wote wameziba nafasi za mawaziri wa sasa,” alisema mmoja wa maofisa wa Wizara ya Ujenzi.

Habari zaidi kutoka ndani ya Wizara ya Ujenzi zimedokeza kuwa Nahodha ilishapata nyumba ya kuishi, lakini alikataa kwa madai kuwa haina ulinzi na samani za ndani.

Mtoa habari huyo alisema mvutano uliopo sasa ni kuwa kiongozi huyo anataka apewe stahiki hizo kama Waziri Kiongozi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wakati Wizara ya Ujenzi ikipinga jambo hilo kwamba anapaswa kugharimiwa sawa na mawaziri wengine.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa kilimtaarifa Waziri Shamsi kuwa kama anataka samani za nyumba awasiliane na Wizara ya Mambo ya Ndani anayoiongoza ili kuangalia uwezekano wa kupata vitu anavyovitaka.

Chanzo kingine cha Tanzania Daima Jumatano, kimedokeza kuwa Shamsi, anaweza kupewa huduma hizo kama angeendelea kuwapo Zanzibar na si bara ambako hivi sasa ameteuliwa kuwa waziri.

Kilibainisha kuwa SMZ, haina utaratibu wa kuwapangia nyumba na kuwapa huduma mbalimbali ikiwemo ulinzi na wahudumu wa ndani viongozi wake wanaoishi nje ya Zanzibar.

Kiliongeza kuwa Shamsi, anapata huduma za hadhi ya Waziri Kiongozi kila anapokuwapo visiwani humo lakini anapotoka nje ya mipaka hiyo kwa maana ya kuwa Tanzania Bara, anagharimiwa sawa na mawaziri wengine.

Alipoulizwa na gazeti hili sababu za Waziri Nahodha kuendelea kuishi hotelini na gharama ambazo serikali inazipata, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ol- Medeye, alisema wizara yake haihusiki na utoaji wa makazi ya viongozi na watendaji wa serikali, bali inahusika kwa Watanzania wote.

“Suala hili sio la wizara yetu, hatuhusiki kabisa na makazi ya mawaziri wala viongozi wengine wa serikali, tunahusika na makazi ya Watanzania wote,” alisema Naibu Waziri huyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipoulizwa kuhusiana na suala la makazi la Waziri Nahodha na wengine, alisema hajui chochote kwani yuko mjini Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge la Bajeti.

“Mimi sijui chochote, muulizeni Katibu Mkuu ambaye yuko jijini Dar es Salaam, atawapa ufafanuzi,” alisema kwa kifupi Dk. Mwakyembe.

Sakata la Waziri Nahodha kuishi hotelini, liliibuliwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Chambani, Salim Hemed Khamis (CUF).

Mbubge huyo alitoa taarifa zilizomshtua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na wabunge wengine kuwa Waziri Nahodha, anaishi hotelini.

Kabla ya kutoa kauli hiyo, mbunge huyo alihoji dhamira ya serikali katika kupunguza matumizi.

Alisema serikali inakusudia kusitisha ununuzi na matumizi ya mashangingi, kuacha kuagiza fenicha kutoka nje na kupunguza posho kama moja ya njia ya kupunguza gharama za matumizi kwa serikali.

Alisema pamoja na dhamira hiyo ya kubana matumizi, serikali imewaacha baadhi ya mawaziri wake waishi hotelini na hivyo kuongeza gharama za matumizi.

“Kuna mawaziri wanaishi hotelini tangu walipoteuliwa hadi sasa, serikali haioni kama hali hiyo ni kikwazo kwa mafanikio ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano tulioupitisha hivi karibuni bungenin?” alihoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Pinda kwanza alionekana kushangazwa na taarifa hiyo na baadaye alimtaka ataje majina ya mawaziri anaowajua wanaishi hotelini hadi sasa tangu walipoteuliwa.

“Naomba Mheshimiwa Mbunge nitajie majina ya mawaziri unaowajua kwamba wanaishi hotelini,” alisema Pinda.

Mbunge huyo ambaye alikuwa akisubiri majibu ya Waziri Mkuu kwa hamu, akataja jina la Waziri Nahodha kwamba ni mmoja wa mawaziri wanaoishi hotelini.

Huku akiwa haamini na kumwangalia Waziri Nahodha, Pinda alijibu kwa kifupi tu: “Basi nimesikia.”


11 May 2010

Shamsi Vuai Nahodha.Huyu ni Waziri Kiongozi huko Zanzibar.Naomba kukiri hadharani kuwa kwa muda mrefu nimekuwa nikimuona mwanasiasa huyu kama 'yupo yupo' tu.Unajua kuwa mwanasiasa au kiongozi kunapaswa kuendana na mchango wa namna flani kifikra au kimatendo.Nyerere hakumbukwi kwa vile tu alikuwa mwanasiasa au kiongozi bali jitihada na mchango wake kwa umma,hata kama baadhi ya maeneo alikosea (hiyo ni makala nyingine: ALIPOKOSEA NYERERE).
Pasipo kutarajia,Nahodha kanipa 'surprise ya nguvu'.Ameongea maneno ya busara sana kuhusu fikra potofu zilizotawala akilini mwa viongozi wengi wa CCM kuwa chama hicho kitatawala milele.Japo si dhambi kwa chama kutawala milele (kama inawezekana na kama kinakidhi matakwa ya kinaowaongoza),ni uzembe wa tafakuri kuamini kuwa CCM itatawala daima hasa kutokana na uswahiba wake na ufisadi,kauli za kibabe hata kwenye mwaka wa uchaguzi na kupuuza watu waliokiweka chama hicho madarakani.Sasa,Waziri Kiongozi Nahodha amewatahadharisha wana-CCM wenzake kwamba KUNA SIKU CCM ITANG'OLEWA.Hebu msome hapa chini
Nahodha: Iko siku CCM itang'olewa


• AKUMBUSHA WAJIBU WA VIONGOZI KWA WANANCHI
na Mwandishi Maalum, Mererani
WAZIRI KIONGOZI wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha amewataka wana CCM kuacha kujidanganya kwamba chama chao kitaendelea kutawala milele.
Nahodha, mmoja wa viongozi wa juu wa CCM na serikali alitoa kauli hiyo jana wakati akiwahutubia wananchi katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Rafiki Child Care kilichoko Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Kiongozi huyo ambaye kimamlaka ni wa pili baada ya Rais Amani Karume katika SMZ aliwataka wana CCM kuachana na dhana kwamba chama chao hakiwezi kuondolewa madarakani na vyama vya upinzani.

“Ninatofautiana kimtazamo na watu wanaosema kwamba CCM itaendelea kutawala milele na milele, hapa kama hatutajipanga vizuri ipo siku chama chetu kitang’olewa madarakani…tusibweteke,” alisema Nahodha.

Waziri Kiongozi alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro, aliyetajwa kwa jina moja la Mujungu kuhutubia na kutamka kuwa, CCM haiwezi kuondolewa madarakani na vyama vya upinzani.

“Wapo wana CCM ambao kimtazamo wanaona sisi ndiyo wenyewe, kumbe wenye chama ni wananchi wanaowatawala. Tuna kila sababu ya kuwa makini katika utelezaji wa majukumu yetu… jambo hili nawaambia si kweli,” alisema Nahodha.

Akitoa mfano, Nahodha aliwataka wana CCM kujifunza kutoka katika nchi jirani ambako baadhi ya vyama vilivyopigania uhuru kama ilivyo CCM vimeng’olewa madarakani.

Alikitaja chama cha Kenya African National Union (KANU) ambacho kilipigania uhuru wa Kenya kuwa mmoja wa vyama vilivyopata kung’olewa madarakani.

“Kumbukeni namna ambavyo KANU ilisambaratika kule Kenya… leo hii imesahaulika kabisa. Lakini si huko tu, kule Zambia (UNIP) na Malawi (MCP) vyama tawala vilibwagwa vibaya na sasa vimesahaulika masikioni mwa wananchi,” alionya Nahodha.

Akiendelea, alisema ni wazi ipo siku wananchi wanaweza kukichoka CCM na kukibwaga iwapo viongozi watashindwa kutimiza ndoto za wananchi za kuwaletea maendeleo.

“Kuna mwanafalsafa mmoja mmoja anasema, msitafute uzuri wetu kwa kuangalia jinsi tulivyo, bali kwa kuangalia yale mema tuliofanya,” alisisitiza Nahodha.

Alisema uwajibikaji wa baadhi ya viongozi wanatokana na CCM ndani ya CCM unatia shaka inayoweza kuwafanya wananchi kukichukia chama hicho.

Alisema jukumu kubwa la viongozi wanaotokana na CCM ni kutekeleza majukumu yao kwa Watanzania kwa kuyafanya maisha yao yawe bora zaidi.

“Yuko mwanafalsafa mmoja wa zamani, aliwahi kusema maneno haya: ‘Tutakapokufa msitutafute katika makaburi yetu yaliyotengenezwa vizuri kwa chokaa bali mtutafute katika nyoyo za watu tuliowasaidia’. Ninawashauri viongozi wenzangu wa serikali na chama tuitumie sana busara ya mwana falsafa huyo,” alionya Vuai.

Katika hatua nyingine, Nahodha alieleza kusikitishwa na kuibuka kwa malumbano ya kisiasa miongoni mwa viongozi katika mkoa wa Manyara akisema hali hiyo haina faida kwa wananchi wanaowaongoza.

Kauli hiyo ya Nahodha iliyoonekana kuzungumzia na kukerwa na malumbano yaliyoibuka wiki iliyopita kati ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.