Pili, nitajitahidi kadri nitakavyoweza kuepuka 'mtazamo wangu' na badala yake niongozwe na kanuni za uchambuzi wa kiintelijensia. Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa moja ya nyenzo muhimu kwenye intelijensia ni mwanadamu, iwe kwenye kukusanya taarifa za kiintelijensia, kuchambua au kushauri. Kwahiyo, japo nitajitahidi kuepuka 'mtazamo wangu,' siwezi kuepuka ubinadamu wangu kama mchambuzi wa kiintelijensia wa somo husika.
Kwa kifupi, tuanze na tunachofahamu hadi muda huu. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo mauaji yanayojumuisha eneo la Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU) yalianza Januari 2015 na hadi sasa yamegharimu uhai wa watu 40 wakiwemo askari polisi 13.
Tukisema tuorodheshe mlolongo wa kauli za viongozi mbalimbali, wa serikali na wa jeshi la polisi, basi huenda itabidi kukesha hapa, au kuandika kitabu kizima. Hata hivyo, kwa kifupi, miongoni mwa kauli hizo ni kama ifuatavyo
Rais John Magufuli:
Kwa ujumla, Rais Magufuli ametoa matamko makubwa matatu kuhusu mauaji yanayoendelea katika eneo la MKIRU. Tamko la kwanza ni salamu za rambirambi alizotoa kufuatia mauaji ya askari polisi wanane, ambapo alilaani mauaji hayo. Hiyo ilikuwa April 14 mwaka huu.
Tamko la pili la Rais lilikuwa majuzi alipofanya ziara mkoani Pwani ambapo Juni 20 aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa serikali na vyombo vya dola ili kukomesha mauaji hayo. Rais alieleza kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya mauaji "tunakaa nao, tunawaficha, ni watoto wetu." Kadhalika, Rais Magufuli alieleza kuwa "serikali ya Awamu ya Tano sio ya kuchezewa" na kudai kuwa "(wauaji hao) wameshaanza kunyooka."
Hata hivyo, siku moja baada ya Rais kutoa kauli hiyo ya kutia matumaini, askari polisi wawili waliuawa na gari lao kuchomwa moto, pengine ikiwa ni jibu la wauaji hao kwa Rais aliyedai kuwa "wameshaanza kunyooka."
Tamko la tatu la Rais, na pengine kali kuliko hayo mawili, lilitolewa jana jijini Dar wakati wa uzinduzi wa upanuzi wa Bandari ya Dar, ambapo katika kilichoonekana bayana kuwa majibu kwa rai ya Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kwa Rais Magufuli kumtaka atafakari kuhusu 'mashehe wa Uamsho' wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.
Katika tamko hilo Rais aliwaomba wanasiasa wanaosema kuwa hawa (mashehe wa Uamsho) wameshikiliwa kwa muda mrefu "wajizuwie midomo yao," na kudai kuwa "hata kuna watu kule Marekani walikaa Guantanamo muda mrefu," na kudai kuwa (wanaoongea kama Lowassa kuwa kesi yao ishughulikiwe) inaweza kuwafanya watu kuhisi (anayesema hivyo) ni "mmoja wao."
Rais Magufuli alihoji "kwanini hata siku moja mtu asijitokeze kualaani wanaouawa bila hatia kule (MKIRU), lakini kwa kutafuta sifa za kisiasa, mtu anatoka anasema watu wako ndani muda mrefu." Rais aliwataka polisi kufanya kazi yao, na kuwaagiza kuwakamata "hao wanaoropoka waisaidie polisi," na "msiogopee sura, awe na mwendo wa haraka, polepole au kukimbia, mkamateni kusudi akaisaidie polisi kule ndani."
Rais alidai pia mtu aliyekamatwa na sare 500 za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni "inaonekana anahusiana na walioko ndani (mashehe wa Uamsho)."
Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba na Naibu Waziri wake Yusuph Masauni
Kwa nyakati mbalimbali, viongozi hawa wawili wametoa kauli kadhaa kuhusiana na mauaji yanayoendelea huko MKURU. Kuorodhesha kauli zote kwahitaji makala nyingine pekee, lakini kwa kifupi, Waziri Mwigulu ameshanukuliwa akidai kuwa "mauaji hayo yana harufu ya kisiasa," na kuhoji "Ujambazi gani huo wa Wana
CCM tu? Hako kamchezo tumeshakagundua. Dhahiri, huo ni ushamba wa vyama vingi.”
Waziri Mwigulu alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa chanzo cha mauaji hayo ni chuki za vyama vya upinzani dhidi ya CCM.
Awali Waziri Mwigulu alieleza Bungeni kuwa serikali imeshabaini kuwa wanaohusika na mauaji hayo wanatoka maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji, na kwamba changamoto ya mauaji hayo ipo mbioni kutatuliwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Masauni amenukuliwa akieleza kuwa serikali inalipa kipaumbele suala hilo na lazima mauaji hayo yadhibitiwe. "Tuweze
kuharakisha zoezi hili ambalo kwa hakika kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa sisi
tunaosimamia haki na uhai wa raia wasio kuwa na hatia hii vita lazima tushinde
inshaallah,” alinukuliwa Masauni hivi karibuni.
IGP Sirro na mtangulizi wake IGP Mangu:
Wakati IGP Simon Sirro ameanza jukumu hilo la ukuu wa jeshi la polisi wakati jeshi hilo likikabiliwa na changamoto za mauaji ya MKURU, mtangulizi wake IGP Mangu huenda akakumbukwa zaidi kwa onyo lake la kuwasaka "watu waliofurahia mauaji ya askari wanane," kauli ambayo ilionekana kama 'kusaka adui wa kufikirika.' Hata hivyo, suala hilo aliloongelea IGP Mangu lilipaswa kuibua tafakuri pana na endelevu kuhusu uhusiano mbovu kati ya jeshi la polisi na wananchi.
Kadhalika IGP Mangu alieleza kuwa jeshi lake lingeanza kutumia nguvu ilizonazo kulazimisha upatikanaji wa taarifa kuhusu mauaji hayo.
Kwa upande wa IGP Sirro, masaa machache tu baada ya kukutana na wazee wa Kibiti na Rufiji kujadiliana nao kuhusu mauaji hayo, mkazi mwingine aliuawa na watu wasiojulikana. Awali, IGP Sirro aliwaeleza waandishi wa habari kuwa "wauaji hao hawatachukuwa muda mrefu kukamatwa" na kwamba "siku zao zinahesabika." Kadhalika, mkuu huyo mpya wa jeshi la polisi alidai kuwa maongezi yake na wazee wa Kibiti na Rufiji yatafanikisha kukamatwa kwa wauaji hao.
Baada ya kuteuliwa wadhifa huo, IGP Sirro alitangaza dau la shilingi milioni 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.
Juni 25 mwaka huu, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa jeshi lake halifahamu wahusika wa mauaji hayo, kauli iliyokinzana na ya bosi wake, Waziri Mwigulu kwamba chanzo cha mauaji hayo ni chuki ya vyama vya upinzani kwa CCM.
Julai 5 mwaka huu, IGP Sirro alieleza kuwa mauaji hayo ya MKIRO 'yana mkono kutoka nje ya nchi' bila kufafanua nchi gani inayohusika. Kadhalika, taarifa hiyo iliyaeleza mauaji hayo kama yaliyokuwa yakiendelea kwa takriban miaka mwili sasa.
Edward Lowassa:
Rai ya Lowassa kwa Rais Magufuli kuhusu hatma ya 'mashehe wa Uamsho' nimeitaja hapo juu, lakini kwa urefu, habari hiyo ipo HAPA.
Zitto Kabwe
Kufuatia kilichotafsiriwa kama majibu ya Rais Magufuli kwa Lowassa, kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha ACT- Wazalendo Zitto Kabwe alitoa maoni yake katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook.
Rais anakosea Sana kuhusisha suala la Masheikh waliopo ndani na mauaji ya MKIRU. Amewapa maadui silaha. Acha... https://t.co/wKq2QY6SN2— Zitto Kabwe Ruyagwa (@zittokabwe) July 2, 2017
Uchambuzi wa kiintelijensia
Hadi muda huu, hakuna kikundi kilichojitokeza hadharani kudai kuhusika na mauji hayo. Hata hivyo, bila hata kuhitaji uzoefu wa kishushushu, sio vigumu kuhisi kuwa
1. Mauaji hayo yanafanywa na kikundi maalum
2. Wahusika ni watu wenye uelewa/uzoefu wa mbinu za mauaji
Hata hivyo, licha ya kutojitokeza kikundi chochote kudai kuhusika na mauaji hayo, taarifa zilizopatikana siku chache zilizopita zilieleza kwamba kuna ujumbe uliotumwa na 'wahusika wa mauaji hayo,' unaosomeka kama ifuatavyo
Tunawatangazia wananchi tumewaua hawa kwa sababu wanadhulumu watu kwa kutumia kazi zao na yeyote atakayefanya kazi hapa au nje ya hapa tutamtafuta hadi nyumbani kwake.
Sisi tumejitolea kufa kuliko kuishi, kwa hiyo dereva au raia popote uwaonapo toa taarifa iwe nyumbani au kazini.
Hakuna njia ya kumaliza dhuluma isipokuwa chuma tu, hapa chuma tuuu!
Kwa mujibu wa taarifa, ujumbe huo uliandikwa kwa kalamu na kisha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Turudi nyuma kidogo hadi mwaka 2013 ambapo kulitokea uhasama mkubwa kati ya Polisi na baadhi ya wakazi wa Kibiti kufuatia kifo cha mkazi mmoja wa eneo hilo, Athuman Hamis aliyefariki kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo cha polisi (kwa mujibu wa maelezo ya wakazi hao).
Habari kamili ipo HAPA
Katika kufanya uchambuzi wa kiintelijensia wa suala kama hilo la mauaji hayo ya MKIRU, yahitajika vitu viwili. Kwanza, kuwa na maelezo sahihi kuhusu tatizo husika, na pili, matokeo tarajiwa zaidi ni yapi.
Katika uchambuzi wa mauaji hayo ya MKIRU, ninatumia moja ya njia za uchambuzi wa kiintelijensia, inayojulikana kama ACH - Analysis of Competing Hypotheses - yaani Uchambuzi wa Dhana Zinazoshindana.
Hatua ya kwanza ni kutambua dhana husika. Ili kupata dhana hizo, niliendesha kura ya maoni isiyo ya kisayansi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Vipengele vinne vilivuounda swali husika vilitokana na maelezo mbalimbali yaliyokwishatolewa kuhusu zinazoweza kuwa sababu za mauaji huko MKIRU
Jumla ya kura zilizopigwa ni 496, na matokeo ndio hayo pichani. #TanzaPoll inawashukuru nyote mlioshiriki. Ripoti ya #MKIRU yaja hivi punde. pic.twitter.com/qugsa09SYZ— Evarist Chahali (@Chahali) July 5, 2017
Kama inavyoonekana katika 'tweet' hiyo yenye matokeo ya kura ya maoni, dhana kuu nne ni
- Ugaidi
- Chuki za kisiasa
- Chuki za wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi
- Uhalifu kama mwingine
Kuorodhesha dhana hizo (kama ilivyo hapo juu) na kuzipitia kwa kina zaidi na kujumuisha 'ushahidi uliopo' kwa kila moja (kama inavyofuata hapa chini) ni hatua ya pili ya ACH.
Tuanze na dhana kuwa mauaji hayo yanatokana na chuki za wananchi. 'Ushahidi' kuhusu dhana hii ni wa aina mbili. Kwanza, Januari 23, 2013, kulijitokeza vurugu kubwa huko Kibiti zilizolazimu jeshi la polisi kutumia helikopta kuzidhibiti. Vurugu hizo zilitokana na kifo cha mkazi mmoja wa Kibiti aliyefariki Hospitali ya Taifa Muhimbili alikopelekwa kutibiwa majeraha ambayo ilidaiwa aliyapata kutokana na kupigwa na polisi.
Vurugu hizo zilipelekea Barabara ya Kilwa kufungwa kwa zaidi ya amsaa matatu, na hivyo kuathiri usafiri kwenda mikoa ya Mtwara na Lindi; sambamba na wananchi kuvamia kituo kimoja cha polisi na kuchoma moto nyumba moja ya polisi.
'Ushahidi' wa pili wa dhana kuwa chanzo cha mauaji ya MKIRU ni chuki za wananchi dhidi ya jeshi la Polisi ni ripoti maalum ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi iliyochapishwa Mei 26 mwaka huu.
Kwa kifupi, ripoti hiyo inaeleza kwamba wengi wa wakazi wa MKIRU ni masikini wenye elimu duni, na tegemeo lao kubwa la kipato ni kuvuna raslimali nyingi zilizopo eneo hilo na kuzuza. Biashara kubwa ambayo vijana wanajihusisha nayo ni uchomaji na uuzaji wa mkaa, uvunaji magogo kwa ajili ya mbao, uuzaji wa kuni na mazao mengine ya mashambani kama vile mpunga na mihogo, imeajiri vijana wengi katika maeneo hayo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofnywa na mamlaka za mitaa, maofisa wa Idara ya Maliasili, jeshi la mgambo na polisi.
Licha ya mamlaka husika kuweka lundo la vizuizi, pia wananchi hao walilalamikia 'kodi za kukomoana.' Kwa miaka mingi sasa, wananchi wamekuwa wakilalamikia vizuizi hiyo kuwa kitovu cha dhuluma na uonevu mkubwa wanaofanyiwa wananchi na wasimamizi wa vizuizi ambao wamekuwa wakikadiria kodi za kukomoa, kutaifisha magunia ya mkaa na mbao na mali nyingine za wananchi.
Wananchi hao wanadai kuwa uonevu na dhuluma vimechokoza hasira za vijana wengi, ambao "kazi zao ndio mkaa, kuni na mbao au mihogo." Kuhusu matumizi ya silaha, ilielezwa kuwa vijana wengi katika maeoeneo hayo wana mafunzo ya mgambo na JKT huku wakiwa hawana ajira nyingine zaidi ya kutegemea biashara hizo.
“Si suala la kidini. Ni manyanyaso tu. Leo unadhulumu watano, kesho kumi, hawa wakiji-organise unatarajia nini?” aliuliza mkazi mmoja wa eneo hilo, na kuongeza kuwa ingawa dhehebu moja la kidini lina vijana wengi lakini halina uhusiano na mauaji.
Kuhusu dhana nyingine kwamba mauaji ya MKIRU yantokana na ugaidi, kuna 'ushahidi' wa matukio mbalimbali kwa takriban miaka mitano sasa ambayo japo serikali imekuwa ikiyaita kuwa ni ujambazi, yana viashiria vya ugaidi.
Moja ya vitu vinavyoleta ugumu katika kutanabaisha ugaidi au lani kasumba iliyoshamiri kitambo ambapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wepesi kuwatuhumu wapinzani wao wa kisiasa kuwa wanapanga au wanajihusisha na vitendo vya kigaidi kwa minajili tu ya uhasama wa kisiasa.
Baadhi ya wanasiasa wa chama tawala CCM, kwa nyakati tofauti wamewahi kuvituhumu vyama vya upinzani vya CUF na Chadema, na baadhi ya viongozi na wanachama wake, kuwa wahusika wa ugaidi, tuhuma ambazo mara zote hazikuweza kuthibitishwa.
Japo magaidi hupendelea wafahamike kuwa ndio wahusika wa tukio la kigaidi, kunapojitokeza watu wasio na hatia kutuhumiwa kuwa ndio magaidi, hiyo inaweza kurahisisha kazi ya magaidi halisi.
Katika mlolongo wa matukio mbalimbali yenye viashiria vya ugaidi, Julai 2 mwaka huu, Rais Magufuli aligusia kuhusu 'mashehe wa UAMSHO' ambao wapo gerezani kwa zaidi ya miaka minne sasa wakisubiri hatma ya mashtaka ya ugaidi yanayowakabili. Katika hotuba yake jijini Dar, Rais Magufuli aliashiria kuwa kuna uhusiano katika ya mauaji ya MKIRU na mashehe hao wa UAMSHO, huku akiibua taarifa mpya kuwa hata sare 500 za jeshi zilizokamatwa jijini Dar zilikuwa na uhusiano na mashehe hao/ 'ugaidi' huko MKIRU.
Kadhalika, Julai 5 mwaka huu, IGP Sirro alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa mauaji ya MKIRU yana 'mkono wa nchi za nje.' Kingine cha muhimu katika maelezo ya IGP Sirro ni kubainisha kuwa mauaji ya MKIRU yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miaka miwili.
Tukio jingine ni pamoja na lile la Mei mwaka jana huko Mwanza ambapo kulitokea mapambano makali kati ya askari wa jeshi la polisi wakisaidiwa na wenzao wa Jeshi la Wananchi dhidi ya kilichoelezwa na serikali kuwa ni genge la majambazi. Mapambano hayo yalielezwa kuwa na uhusiano na uvamizi kwenye msikiti wa Rahman jijini humo, ambapo kulitokea mauaji ya kutisha baada ya watu wasiofahamika kuvamia msikiti huo na kuwauwa kwa kuwachinja Imamu aliyekuwa
akiswalisha swala ya Isha, Ferouz Elias (27) na waumini wawili, Mbwana Rajab na Khamis Mponda.
Tukio jingine lilitokea Novemba 22 mwaka jana ambapo Jeshi la Polisi lilikamatwa wanawake wanne na watoto wannewaliodaiwa kuwa katika mafunzo ya kigaidi, huko Vikindu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam
Tukio jingine ni lile la Machi 2 mwaka juzi ambalo lililozua taharuki miongoni mwa Watanzania wengi kufuatia kuibuka kwa video yenye ujumbe ulioashiria uwepo wa kundi linalopambana na jeshi la polisi kwa sababu za kidini
Kadhalika, Juni mwaka 2015, taasisi ya ACLED ilitoa taarifa iliyoonyesha kulikuwa na ongezeko la matukio yenye viashiria vya ugaidi. Ripoti hiyo iliyoambatana na majedwali yanayoonyeshwa mwenendo wa matukio hayo ilitokana na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari vya Tanzania.
Taarifa hiyo ambayo unaweza kuisoma HAPA ilibainisha kwamba Tanzania ina vikundi vidogo vya kigaidi vyenye uhusiano na kundi la Al-Shabaab la Somalia au Al-Hijra la Kenya. Vikundi hivyo ni pamoja na Ansar Muslim Youth Centre cha mjini Tanga.
Pia, Novemba mwaka 2013, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watu 69 waliokuwa kwenye kilichoelezwa kuwa ni mafunzo ya kigaidi kuhusu kundi la Al-Shabaab.
Vilevile, takriban mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, watu wengine 11 walikamatwa na Polisi mjini Mtwara wakituhumiwa kujihusisha na kundi la Al-Shabaab.
Kadhalika, mwezi huohuo, mfanyabishara Juma Abdallah Heri alikamatwa na polisi kwa tuhuma za kufadhili vikundi vya kigaidi nchini Tanzania.
Mwendelezo wa matukio hayo ni pamoja na lile la April mwaka jana ambapo zilipatikana taarifa kuwa Mtanzania Issa James Mwesiga aliuawa na kundi la Al-Shabaab nchini Somalia kwa tuhuma za ujasusi. Inaelezwa kuwa Mtanzania huyo alijiunga na kundi hilo la kigaidi mwaka 2013.
Agosti 2015, Watanzania sita walikamatwa huko Garissa, nchini Kenya wakiwa njiani kuelekea Somalia kujiunga na kundi la Al-Shabaab. Walikutwa na mabomu saba na bastola saba.
Awali, Machi mwaka huohuo, mwanamke mmoja, Ummur Kayr Sadir, alikamatwa na wenzie wawili wakiwa safarini kwenda Somalia kujiunga na kundi hilo la kigaidi.
Septemba mwaka jana, taasisi ya Intergovernmental Authority on Development (IGAD) ilitoa ripoti iliyoeleza kuwa kundi la Al-Shabaab lilikuwa ikifanya jitihada kubwa kupata wafuasi wa kiume na kike wa kujiunga na kundi hilo, hata nje ya Somalia (lilipo kundi hilo) na Tanzania, Uganda, Ethiopia na Djibouti zilikuwa zilikilengwa katika jithada hizo.
Februari 28 mwaka jana, watu watatu waliuawa na polisi jijini Arusha, huku taarifa zikieleza kuwa watu hao walikuwa wanakikundi wa Al-Shabaab.
Juni mwaka jana, watu wanane waliuawa kinyama huko Tanga, ikiwa ni wiki mbili tu baada ya tukio jingine la kinyama jijini Mwanza ambapo Imamu wa msikiti wa Rahman na waumini wawili walichinjwa.
Oktoba mwaka jana, polisi walimkamata mwalimu mmoja wa madrasa huko Bagamoyo kufuatia taarifa za wananchi kwa polisi. Mwalimu huyo alikamatwa akiwa na watoto 22 ambapo polisi pia walikuta maandiko mbalimbali ya kuhusu ugaidi na walikuta bomu la gesi nyumbani kwa mwalimu huyo.
Mei mwaka jana, kikundi kilichojitambulisha kama Ahl Kalf Mujahidina kilitoa wito kwa Waislam kuwa wajiunge nacho, ambapo kilieleza kuwa kimeweka makazi yake kwenye mapango ya Amboni huko Tanga.
A poorly visible video claims to show a group of ISIS (armed) supporters in a cave in Tanzania. #ISIL #IS pic.twitter.com/CbsStWtFrA— Harun Maruf (@HarunMaruf) May 18, 2016
April mwaka jana zilipatikana taarifa za kuundwa kwa kundi jipya la kigaidi linalofahamika kama Jahba East Africa ambalo lilijitangaza kuwa wafuasi wa kundi hatari la kigaidi la ISIS. Kadhalika kundi hilo lilidai kuwa miongoni mwa wafuasi wa filisofia yake wapo nchini Tanzania.
Kwahiyo hadi hapa, tumeshaona dhana mbili na 'ushahidi' wake, na sasa tumalizie na dhana mbili zilizosalia. Dhana nyingine ni kwamba mauaji hayo ya MKIRU yanayokana na chuki za kisiasa. 'Ushahidi' pakee katika dhana hii ni kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, kwamba mauaji hayo 'yananuka siasa.'
Na dhana ya nne na ya mwisho ni kwamba mauaji hayo ni matukio ya uhalifu kama matukio mengine. 'Ushahidi' kuhusu dhana hiyo ni ukweli kwamba takwimu za uhalifu nchini Tanzania kwa mwaka 2013 na 2014 na 2015 zinaonyesha mauaji kama kosa kubwa la pili kwa ukubwa (wingi) nyuma ya ubakaji katika kundi la makosa dhidi ya binadamu.
Hatua ya tatu ya ACH inahusisha kuandaa 'matrix' yenye dhana husika, kwa minajili ya kupima 'consistency' au inconsistency.' Pia kuna fursa ya kupima kuaminika na kulandana kwa kila dhana.
Hatua ya nne ya ACH inahusisha kuangalia 'diagnosticity' - uwezekano wa dhana kuwa sahihi. Kadhalika katika hatua hii, dhana yenye/zenye mapungufu - kwa maana ya kwamba hazijitshelezi kueleza somo linalochunguzwa - yaweza/zaweza kuondolewa. Na katika somo hili la mauaji ya MKIRU, nimefikia hitimisho la kuondoa dhana mbili za 'mwisho' (nitaeleza maana ya 'mwisho' mbeleni) yaani "chuki za kisiasa" na "mauaji hayo ni uhalifu kama mwingine." Kwahiyo ninabakiwa na dhana mbili, yaani "ugaidi" na "hasira za wananchi."
Hatua ya tano ya ACH inatokana na hatua ya nne na imenipelekea kuwa na matrix yenye dhana mbili, ya ugaidi na hasira za wananchi.
Mkiru Matrix Drawn Down by Evarist Chahali on Scribd
Hatu ya saba ya ACH ni kuripoti matokeo ya uchambuzi. Najua hayo majedwali ya matrix yanaweza kumchanganya msomaji lakini nyenzo muhimu kufikia hitimisho la karibu zaidi na ukweli. Ikumbukwe kuwa intelijensia sio sayansi timilifu kwa asilimia 100 - kwa kimombo wanasema "intelligence is not exact science." Kwahiyo, dhana, ushahidi wake, na msaada mkubwa wa ACH unanipeleka kufikia hitimisho lifuatalo.
1. Kumekuwa na harakati za muda mrefu za kusambaza na hatimaye kuimarisha ugaidi nchini Tanzania. Katika uchambuzi huu, ushahidi uliotumika umeanzia mwaka 2013, miaka minne iliyopita. Hata hivyo, jitihada hizo za kusambaza/kuimarisha ugaidi zimekuwa kama za kulipuka na kufifia (sporadic), japo kama tukiamini kuwa mauaji ya MKURU ni sehemu ya harakati hizo, basi hitimisho linakuwa kwamba harakati hizo zimefanikiwa kujikita.
2. Chuki ya wakazi wa maeneo husika zinasaidia kufanikisha harakati hizo za magaidi hao. Katika matrix ya pili iliyobakiwa na dhana mbili badala ya nne za awali, kuna 'consistency' katika 'uhusiano' wa dhana ya ugaidi na chuki ya wananchi. Pengine hili limechangiwa na mamlaka husika kutofanyia kazi vilio vya wakazi wa eneo hilo (rejea taarifa ya kiuchunguzi ya Gazeti la Mwananchi kuhusu maujai ya MKIRU).
3. Kauli ya IGP kuwa mauaji hayo yana mkono wa kutoka nje inapewa uzito na matukio mbalimbali yaliyotumika katika uchambuzi huu. Na katika hitimisho langu, natafsiri kuwa mauaji yanayoendelea katika maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji ni ugaidi unaofanywa na kundi lenye asili ya nje ya Tanzania lakini lenye ufuasi wa kutosha nchini humo, na linapatiwa msaada na wakazi wa eneo hilo.
4. Kuhusu 'mashehe wa UAMHO,' hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha kauli ya Rais Magufuli hivi karibuni iliyoashiria kuwa kuna uhusiano kati sare za jeshi zilizokamatwa hivi karibuni, mashehe wa UAMSHO na mauaji ya MKIRU. Kinachowezekana ni wahusika (magaidi) wanaweza kutumia suala la mashehe hao kama sababu ya kufanya ugaidi wao.
5. Tukiafikiana kuwa mauaji ya MKIRU yanafanywa na magaidi, na tukiafikiana pia kuwa magaidi hao wanaweza kutumia suala la 'mashehe wa UAMSHO' kama moja ya sababu zao, bado ni muhimu kuepuka kulifanya suala hilo kuwa linatokana na masuala ya kidini. Kama ambavyo kuna wanasiasa wanaotumia mauaji hayo kuendeleza chuki za kisiasa na hatusemi siasa ndio chanzo cha mauaji hayo, ndivyo ilivyo kwa wanaoweza kutumia dini kama kisingizio cha kufanya ugaidi. Hili ni muhimu sana kuzingatiwa kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa MKIRU ni Waislamu, na kuhusisha ugaidi huo na Uislamu/Waislamu sio tu itaathiri uwezekano wowote wa ushirikiano baina ya wakazi wa eneo hilo na vyombo vya dola/serikali bali pia inaweza kuzua balaa la machafuko ya kidini.
6. Tukiafikiana kuwa kinachoendelea huko MKIRU ni ugaidi basi itabidi pia tuafikiane kuwa mapambano dhidi ya ugaidi yanahitaji uwekezaji mkubwa kweli intelijensia kuliko matumizi ya nguvu. Taarifa kwamba baadhi ya wakazi wa maeneo ya MKIRU wamelazimika kuhama makazi yao kwa "kuhofia vipigo kutoka kwa Polisi" zinafanya uwezekano wa kupata ufumbuzi kuwa mgumu.
7. Kwa wanaofahamu vema pwani ya mkoa wa Pwani sambamba na jiografia yake na mikoa ya jirani watatambua kuwa wingi wa "vipenyo" (ambavyo hadi hivi karibuni vilikuwa vikitumika kama 'njia za panya' kuingiza na kutoa bidhaa mbalimbali) na mtawanyiko wa makazi yaliyochanganyika na mashamba, mapori na misitu, vinaweza kuwa mazingira mwafaka kwa watu hao wenye nia mbaya.
Nihitimishe uchambuzi huu kwa kusisitiza kuwa intelijensia sio exact science. Nimejitahidi kadri nilivyoweza kuongozwa na ACH kufikia hitimisho husika. Lengo la kufanya uchambuzi huu sio kuonyesha mapungufu ya mtu au taasisi fulani. Nimekuwa nikitumia ACH kwa majukumu yangu binafsi, na nimeona sio vibaya kuitumia kwenye suala hili la MKIRU. Hakuna anayelazimishwa kuafikiana na uchambuzi huu.