Kama ni mtumiaji wa mtandao wa kijamii wa Twitter basi nina uhakika ushakutana na neno #mwanaharakati au #wanaharakati. Mara nyingi maneno hayo yamekuwa yakitumika kwa dhihaka, kana kwamba wanajihusisha na harakati wana matatizo flani ya akili. Lakini kama wasemavyo Waswahili, akili ni nywele, kila mtu ana zake. Ukiamua kuwekeza jitihaza zako kwa ajili ya masuala yenye umuhimu kwa jamii, kuna watakaokuona huna kitu cha maana cha kufanya katika maisha yako.
Lakini kwa wengine, 'chuki' yao dhidi ya wanaharakati ni katika kufunika mapungufu yao binafsi. Hawa ni pamoja na wale wasio na la maana katika maisha yao binafsi, na pindi wakimwona mtu anachukua msimamo kuhusu ajenda au suala flani, basi ni kama inawaongezea hasira.
Enewei, tangu majuzi, wanaharakati kadhaa huko Twitter wamekuwa wakiuliza maswali magumu kuhusu klinachoitwa mradi wa treni ya kisasa kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere hadi Mjini Kati. Kiini cha maswali hayo ni kampuni ya mwekezaji ambapo hadi muda huu haijulikani kama ni SHUMAKE RAILS au M/S SHUMOJA. Utata huo nimeuelezea kwa kirefu katika makala niliyoandika hapa jana.
Jana hiyohiyo nilikutana na picha ya toleo la gazeti la ThisDay ikiwa imebeba habari ya utatau unaozunguka mradi huo na mwekezaji husika. Pengine hii yaweza kuonekana ni suala la kawaida tu, lakini kwa sie tunaojihangaisha na suala hili tunafarijika vya kutoka kuona angalau gazeti moja la kitaifa limeipa uzito habari hiyo, na kuifanya habari kuu. Hii ni habari njema sana kwa sie tunaoamini katika umuhimu wa harakati hususan za kijamii (social activism).
Bado safari ni ndefu katika suala hili, hasa kwa vile hatujapata majibu kutoka serikalini. Hata hivyo, kinachotia moyo ni msimamo wa mwanasiasa kijana ambaye ametangaza rasmi nia ya kugombea urais hapo mwakani, Mheshimiwa January Makamba. Mwanasiasa huyo, kutoka chama tawala CCM, na Naibu Waziri wa Mawasiliano, na Mbunge wa Bumbuli, ameonyesha msimamo thabiti na usio na uoga kuhusu suala hilo, na kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Twahitaji kufahamu msimamo wa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wake Harrison Mwakyembe ambao pasi shaka ndio wanaoupigia chapuo mradi huo. Lakini kwa vile mwekezaji huyo pia ni Balozi wa Heshima wa Tanzania huko Marekani, tutafanya jitihada za kumbana Rais Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe watufahamishe ilikuwaje hadi mwekezaji huyo akapewa wadhifa huo.
Binafsi ninaamini kwamba mafanikio ya wanaharakati katika suala hili yanaweza kuhamasisha harakati zaidi kwa vitendo kwenye masuala mengine mbalimbali. Ifike mahala, badala ya kutarajia miujiza kutoka Bungeni, au kwa Idara ya Usalama wa Taifa, au TAKUKURU, au polisi, basi sie wananchi wenyewe tufanye jitihada za kusaka ukweli, na kuuweka wazi hadharani. Ninatambua kuwa yaweza kuwa vigumu kwetu kuchukua hatua dhidi ya wahusika, lakini wakati mwingine, 'mahakama ya umma' yaani hukumu ya jamii ina nguvu zaidi kuliko mahakama asilia.
Ninaomba kutumia fursa hii kuwataka Watanzania wawapuuze wanaobeza unaharakati, na badala yake washiriki katika harakati mbalimbali kwa manufaa yao wenyewe na kwa taifa letu kwa ujumla.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO.