14 Feb 2009

HEBU KWANZA MSIKILIZE KIONGOZI HUYU WA UMMA HUKO ZENJI ANAVYOJITETEA DHIDI YA WITO WA KUMTAKA AJIUZULU KISHA TUJADILI KIDOGO:



WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Haroun Ali
Suleiman, amesema haoni sababu ya kujiuzulu wadhifa huo kwa madai ya wanafunzi
wengi Zanzibar kufanya vibaya katika mitihani yao ya kidato cha nne.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema utamaduni kama huo haupo Zanzibar na
wangejiuzulu mawaziri wengi wa elimu waliopita akiwamo Katibu Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad.

Waziri Suleiman ametoa kauli hiyo huku kukiwa
na malalamiko kutokana na matokeo mabaya ya mitihani, huku baadhi ya wanasaisa
wakimtaka awaombe radhi Wazanzibari na kutangaza kuwajibika kutokana na
kusimamia vibaya sekta hiyo.

Alisema
kimsingi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inapaswa kupongezwa kutokana na
mafanikio inayopata katika sekta ya elimu, ikiwamo kuongezeka kwa shule za
serikali kutoka sita kabla ya Mapinduzi hadi 134 hivi sasa
.

Inashangaza kuona watu wamekuwa wepesi wa
kulaumu pale matokeo yanapokuwa mabaya, lakini yanapokuwa mazuri hushindwa kumpa
sifa anazostahili.
Tangu kushika wadhifa huo mwaka 2001, kuna
mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa vile kiwango cha kufaulu kimeongezeka
kutoka asimilia 77.3 mwaka 2000 hadi asilimia 84.6 mwaka 2007.

Matokeo mabaya yaliyojitokeza mwaka huu si jambo
geni
kwa vile wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri katika baadhi
ya wakati na mara nyingine kufanya vibaya. Akiwa ameshikilia takwimu za kufaulu
wanafunzi tangu mwaka 1971, alisema hata yeye hakufurahishwa na kiwango cha
kufaulu kuanguka mwaka huu kutoka asilimia 84. 6 hadi 77.3.

Mwaka 1982
wakati Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa Waziri wa Elimu
Zanzibar, kiwango cha kufaulu kilishuka zaidi hadi asilimia 64.4.

Haroun
alisema hivi sasa kuna sababu mbalimbali zinazochangia wanafunzi kutofanya
vizuri ikiwamo upungufu wa vitendea kazi, uhaba wa vifaa vya sayansi pamoja na
walimu wa masomo hayo.

Hata hivyo, alisema Serikali ya Zanzibar kwa
kushirikiana na Serikali ya Marekani imeanza kuchukua hatua za kuondoa uhaba wa
vifaa, ikiwamo vitabu vya sayansi na kujenga shule za sekondari 19 ambazo kila
wilaya itanufaika hapa Zanzibar.

Hadi ifikapo mwaka 2010 tatizo kwa
baadhi ya wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha pamoja na kuwapo uwiano kati
ya idadi ya wanafunzi na walimu katika darasa. Hivi sasa serikali inaendelea na
programu ya kusomesha walimu katika ngazi mbalimbali ambao watatumika kufundisha
katika shule za sekondari.

Hata hivyo, ni kweli Zanzibar inakabiliwa na
wimbi la walimu wanaomaliza katika viwango vya shahada kukimbilia ajira binafsi
zenye maslahi zaidi. Ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali imeamua kupitia
utaratibu wa malipo kwa walimu kuyaboresha zaidi.

Juzi Chama cha
Wananchi (CUF) kilisambaza taarifa kwa vyombo vya habari kikimtaka waziri huyo
kuwaomba radhi wazee na vijana wa Zanzibar kwa kushindwa kwake kuinua na kukuza
elimu Zanzibar.



JAPO SIAFIKIANI NA HOJA ZILIZOTOLEWA NA MHESHIMIWA HUYU KUTETEA UNGA WAKE,NASHAWISHIKA KUKUBALIANA NAE KWENYE KAULI YAKE KUWA UTAMADUNI WA KUJIUZULU HAUPO (SI ZANZIBAR TU BALI TANZANIA KWA UJUMLA).HEBU TUANGALIE MFANO WA CHAPCHAP HUKO ATCL,UNADHANI KWANINI HADI MUDA HUU HAKUNA ALIYEJIUZULU?MAJUZI MMOJA WA MANAIBU GAVANA BOT AMETAJWA MAHAKAMANI KUWA ANAHUSIKA KWA NAMNA FLANI KWENYE SKANDALI LA EPA,KWANINI HAJAJIUZULU KUPISHA UCHUNGUZI?BAADHI YA WATENDAJI WALIOTAJWA KWENYE TUME YA MWAKYEMBE HAWAJAJIUZULU HADI LEO,KWANINI?JIBU LISILOHITAJI TAFAKURI NI HILO ALOTOA MUUNGWANA HUYO WA ZENJE:HAKUNA UTAMADUNI WA KUJIUZULU.JE CHANZO NI NINI?KWA MTIZAMO WANGU TATIZO LIKO KWA WALIOWATEUA WA HAO WANAOPASWA KUJIUZULU.UTAMADUNI HUU UMELELEWA NA UKWELI MCHUNGU KWAMBA MTU ANAWEZA KUAMUA KUJIUZULU PINDI ANAPOBORONGA JUKUMU FLANI LAKINI ALIYEMTUA HAONI UMUHIMU WA KUFANYA HIVYO.FRANKLY SPEAKING,UKOSEFU WA UWAJIBIKAJI KATIKA MAONEO MBALIMBALI UNACHNGIWA ZAIDI NA TABIA YA KULEANA NA KUBEMBELEZANA KATI YA MABOSI NA WALIO CHINI YAO.LAITI KUNGEKUWA NA KANUNI KWAMBA "UKIBORONGA ,UNAWAJIBIKA.USIPOWAJIBIKA UNATIMULIWA" BASI SI AJABU TUNGESHUHUDIA WABABISHAJI WENGI WAKIACHIA NGAZI KUEPUKA FEDHEHA YA KUTIMULIWA AMBAYO MARA NYINGI HUAMBATANA NA KUNYIMWA MARUPURUPU YA KUMALIZA AJIRA.



INACHEKESHA (JAPO INAUDHI BAADA YA KICHEKESHO HICHO) KUMSIKIA MUUNGWANA HUYU WA KIZANZIBARI AKIDAI PONGEZI ZA "kuongezeka kwa shule za serikali kutoka sita kabla ya Mapinduzi hadi 134 hivi sasa".HUU NI UGONJWA MWINGINE UNAOSHAMIRI KILA KUKICHA;KUTUMIA TAKWIMU NZURI ZA IDADI NA KUFUMBIA MACHO TAKWIMU MBAYA ZA VIWANGO (QUANTINTY vs QUALITY).HIVI KUONGEZEKA KWA IDADI YA SHULE NI MUHIMU ZAIDI YA UBORA WA ELIMU INAYOTOLEWA KWENYE SHULE HUSIKA HATA KAMA NI CHACHE?




ANASEMA "watu wamekuwa wepesi wa kulaumu pale matokeo yanapokuwa mabaya, lakini yanapokuwa mazuri hushindwa kumpa sifa anazostahili" KANA KWAMBA PAMOJA NA MATOKEO YA MWAKA HUU KUWA MABAYA BADO WIZARA ILISTAHILI PONGEZI KWA VILE ILIFANYA VIZURI MWAKA JANA.UGONJWA ULEULE WA TAKWIMU ZA MAZURI ZINAZOTUMIKA KUFICHA TAKWIMU ZA MABAYA.




SAFARI YA MAENDELEO YA KWELI BADO NI NDEFU SANA HASA KUTOKANA NA MENTALITY YA BAADHI YA WALIOPEWA JUKUMU LA KUTONGOZA KWENYE SAFARI HIYO,KAMA HUYU MUUNGWANA WA ZENJI.

13 Feb 2009



12 Feb 2009

Ni kweli nimewachapa, mara hii nimewachapwa wakiwa wamefungiwa, wakati mwingine watachapwa hadharani.” Ni kauli ya MKUU wa Wilaya ya Bukoba, Albert Mnali kuthibitisha habari kwamba aliamuru polisi mmoja kuwachapa viboko walimu katika shule tatu za msingi zilizo Bukoba, kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba. Huu sio udikteta bali DC huyo yaelekea haelewi aliteuliwa kufanya nini wilayani humo.Kwa habari kamili,BONYEZA HAPA

Soma zaidi HAPA.

Madaktari wamefanikiwa kuondoa virusi vya ukimwi katika mwili wa mgonjwa kwa kutumia bone marrow transplant,hatua inayoonekana kuwa ya mafanikio zaidi kuelekea kupatikana kwa tiba ya kudumu ya ugonjwa huo.Kwa habari kamili,BONYEZA HAPA.

11 Feb 2009


10 Feb 2009

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, jana aliishambulia Mahakama kwa kutoa baadhi ya maamuzi yanayowakwaza wananchi, na kueleza kuwa vitendo hivyo haviwezi kunyamaziwa.

Spika Sitta alitoa mashambulizi hayo wakati akitoa matangazo ya kawaida bungeni, baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu.

Alisema, watumishi wa Mahakama lazima watambue kuwa wanaishi miongoni mwa jamii ambayo maamuzi yake mengine yanaikwaza na inapaswa kutambua kuwa jamii inaiangalia Mahakama pale inapokosea.

“Maamuzi mengine ya Mahakama yanakwaza sana wananchi, watumishi wa Mahakama wanapaswa kutambua kuwa wanaishi miongoni mwa jamii hii na wanajamii wanaiangalia Mahakama.

“Hapa pia wanaweza kusema naingilia uhuru wa Mahakama, potelea mbali bwana, liwalo na liwe,” alisema Spika Sitta na kufanya wabunge waangue kicheko.

Spika alitoa kauli hiyo baada ya kueleza kutoridhishwa kwake na kauli ya Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa hafla ya Siku ya Sheria nchini, alililaumu Bunge na waandishi wa habari kwa kuingilia baadhi ya maamuzi ya Mahakama.

Katika kile kilichoonyesha kuwa ni kujibu kauli hiyo, Spika Sitta alisema kauli hiyo ya Jaji Mkuu Ramadhani, haiwezi kupita bila kujadiliwa, kwa sababu suala hilo ni la kikatiba na Bunge kama taasisi haliwezi kukaa kimya.

Aliitaka Mahakama isilalamike kuwa inaingiliwa na mihimili mingine ya dola wakati baadhi ya maamuzi inayoyatoa hayaiingii akilini, na aliahidi kutoa tamko rasmi la Bunge kuhusu malalamiko hayo ya Jaji Mkuu dhidi ya Bunge leo.

Alitoa mfano kuwa, aliwahi kulalamikia kitendo cha hakimu mmoja ambaye hakumtaja jina, aliyetengua amri ya Mamlaka ya Udhitibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ya kumfungia kufanya biashara mmoja wa wafanyabiashara aliyekamatwa akiuza mafuta yaliyochanganywa na maji.

Alisema mfanyabiashara huyo alikimbilia mahakamani na katika hali ya kushangaza, hakimu huyo alitengua amri ya EWURA na kuruhusu mafuta yaliyochanganywa na maji yaendelee kuuzwa.

“EWURA walifanya ukaguzi wakagundua baadhi ya vituo vinavyouza mafuta yaliyochanganywa na maji wakavifunga. Matajiri wakakimbilia mahakamani, hakimu akatengua amri ya EWURA, akaruhusu mafuta yaliyochanganywa na maji yaendelee kuuzwa.

“Sasa hapo kwa maana nyingine ni kwamba serikali inaruhusu wafanyabiashara kuuza bidhaa chafu, halafu unataka sisi tunyamaze, haiwezekani,” alisema kwa mshangao Spika Sitta.

Alisisitiza kuwa hata kama Mahakama itaona inaingiliwa, msimamo wake ni kutetea walio wengi, hivyo hatakaa kimya iwapo ataona haki inapindishwa kwa namna yoyote ile.

Wiki iliyopita, Jaji Mkuu, alisema dhana ya mgawanyo wa madaraka lazima izingatiwe, kwani kuna wakati Bunge limekuwa likiingilia madaraka ya Mahakama.

Alitoa kauli hiyo mbele ya Rais Jakaya Kikwete na Sitta mwenyewe, katika sherehe za Siku ya Sheria Tanzania, zilizofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu, Dar es Salaam, kuashiria mwanzo rasmi wa kazi za Mahakama kwa mwaka huu.

Akitolea mfano wa kesi ya mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, Jaji Ramadhani alisema Bunge lilichukua kazi ya Mahakama na kusikiliza tatizo kati ya wawili hao wakati mmoja hakuwa mbunge.

“Kwa upande mwingine, Bunge liliwahi kutaka liwe na madaraka ya kimahakama dhidi ya watu wanaozozana na waheshimiwa wabunge. Kwa bahati nzuri wazo hilo halikufanikiwa, lakini bado Bunge lilichukua kazi ya Mahakama na kusikiliza tatizo hilo kati ya Malima na Mengi, ambaye si mbunge,” alisema.

Jaji huyo pia alisema hivi sasa limezuka tishio jingine dhidi ya uhuru wa Mahakama kutoka mhimili wa nne wa dola kama vyombo vya habari vinavyojiita.

Alisema baadhi ya vyombo hivyo huandika maoni kana kwamba ndio ukweli wenyewe, na kwa hali hiyo hupotosha wananchi na athari iletwayo haitibiki hata kwa shubiri .
SWALI MUHIMU:
JE SHERIA NI NZURI PALE TU INAPOTOA MAAMUZI YANAYONUFAISHA UPANDE MMOJA?


Pengine mie mshamba.Huenda ndio matokeo ya kutozaliwa Ocean Road hospital i.e. "kuja mjini ukubwani".Au labda huu ndio "ukale",au tuseme "kutokwenda na wakati."Lakini nabaki kuwa mmoja wa watu wanaoiona tarehe 14 ya mwezi Februari,Valentine's Day-Siku ya Wapendanao-kuwa siku ya kawaida kama siku nyingine katika mwaka.Na nisemapo "siku ya kawaida" simaanishi tu kwamba ina masaa 24 kama siku nyingine bali pia napigilia msmari kwenye umuhimu wa siku yenyewe.

Kwangu,na kwa misingi yangu ya Uafrika,kumpenda mwandani wangu ni suala la kila siku.Napojimudu kumnunulia zawadi,basi hilo ni suala la kila wakati pasipo kutegemea mwezi au majira.Kwangu,siku ya wapendanao ni kila siku niliyo kwenye mapenzi ya dhati.

Sina takwimu sahihi kuhusu Siku ya Wapendano huko nyumbani lakini nachokumbuka ni kwamba ilianza kuchukua kasi sambamba na zama za mageuzi katikati ya miaka ya 80 (mid-1980s),mageuzi yaliyopelekea mabadiliko kwenye nyanja za siasa,uchumi,jamii na utamaduni.

Sina ugomvi na wanaoienzi siku hiyo,hususan wale walio kwenye mapenzi ya dhati,lakini nina walakini na wale wanaoigeuza siku hiyo kama fursa ya utapeli wa mapenzi (ntafafanua) na commercialization ya siku yenyewe.Naam,siku hiyo hutumiwa na baadhi ya matapeli wa mapenzi "kuthibitisha" mapenzi yao kwa watapeliwa.Iko hivi:unaye-spend nae Siku ya Wapendanao ndio mpenzi wako wa dhati (unaweza kubisha lakini ndio kanuni zisizo rasmi za siku hiyo huko mtaani).Matapeli wanaweza kuzungukia nyumba ndogo zote na kuishia kulala na aidha mama watoto au nyumba ndogo kuu.Uzoefu unaonyesha kuwa wake/mama watoto ni victims wakuu wa Valentine's Day,ambapo waume kudanganya kuhusu semina za dharura nje ya mji au udhuru wowote utakaomwezesha mume tapeli kulala nje,ni mambo ya kawaida.Ndio maana katika siku hiyo baadhi ya akinamama huwawakia waume zao wanaozuga kuleta rundo la maua na kuwauliza "badala ya kuleta vichanja vya mchicha,wewe unatuletea hiyo mimaua...je tutakula ugali na maua?"Sio kwamba wana hasira na maua,bali umuhimu wake unakuwa umepotezwa na matendo kati ya tarehe 15 ya mwaka uliopita hadi mkesha wa Siku ya Wapendanao.
Takwimu zisizo rasmi (au ziite za kimbeya) zinadai kwamba ni rahisi zaidi kwa kabwela kupata chumba cha kupanga mwaka mzima huko Masaki,Oysterbay,Mikocheni na sehemu nyingine za "kishua" kuliko kupata chumba cha usiku mmoja tu kwenye guest houses katika Valentine's Day (labda booking iwe imefanyika mapema zaidi).





6 Feb 2009

MBUNGE wa Karatu kwa tiketi ya Chadema, Dk. Willbroad Slaa amedai kuwa amegundua vifaa maalum vya kunasa sauti vilivyotegwa kwenye chumba chake, ambavyo anahisi viliwekwa ili kupata taarifa ya mazungumzo yake.

Katika hali isiyo ya kawaida, mbunge huyo, ambaye amekuwa akipasua mabomu mbalimbali dhidi ya serikali na viongozi wake, aliitisha mkutano na waandishi wa habari majira ya saa 6:00 usiku kueleza mkasa huo.

Dk. Slaa alidai kuwa vifaa hivyo alivikuta vikiwa vimetegeshwa kwenye chaga za vitanda katika chumba chake kilicho Hotel Fifty Six mjini hapa ambako anahudhuria Mkutano wa 14 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Nilikuwa nimeambatana na watoto wangu wawili na nilipoingia chumbani niliwaeleza kuhusu suala hilo la bugging (uchunguzi wa kikachero)... naona hawakunielewa lakini kwa kuwa nilishasoma novel (vitabu vya hadithi) nyingi zinazohusiana na mambo hayo, nilijua nini cha kufanya,” alisema Dk Slaa alipokuwa akieleza waandishi kuhusu tukio hilo.

“Tulipofika tu chumbani kwanza tulichunguza kwenye sehemu za umeme za kuchomeka charger za simu, sikuona kitu. Tukajaribu kufunua makochi nako hatukuona kitu. Tukaanza kuchunguza sehemu zote zenye matobo hadi bafuni sikuona kitu. Tulipofunua godoro ndipo tukashuhudia lidude hilo kwenye chaga za kitanda.”

Alisema baada ya kuona hivyo, aliwaita baadhi ya wabunge wenzake na katika kujihami wakaanza tena kuchunguza kwenye vyumba vya wabunge wengine watatu ambao wote ni wa kambi ya upinzani, wanaolala kwenye hoteli hiyo.

Katika kupekua kwenye vitanda ndipo wakagundua pia kwa Dk. Ali Tarab Ali, mbunge wa Konde ambaye anaishi chumba kinachofuatia, pia kulikuwa na kifaa cha namna hiyo lakini kwenye vyumba vya wabunge wengine- Charles Mwera (Tarime-Chadema) na Mwajuma Hassan Khamis (Magogoni-CUF)- hakuona kitu kama hicho.

Alisema baadaye walipiga simu polisi mkoani hapa pamoja na katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah. Inadaiwa kuwa vinasa sauti hivyo viligundulika juzi saa 4:00 usiku wakati wabunge hao waliporejea kulala kwenye hoteli hiyo ambayo ipo katika jengo la ghorofa mbili na ambalo bado ujenzi wake haujakamilika.

Taarifa za tukio hilo zilisambaa kwenye vyombo vya habari kupitia vyanzo tofauti na Mwananchi ilipowasili kwenye hoteli hiyo saa 5:00 usiku huo, tayari kulikuwa na umati wa watu waliofika kushuhudia mkasa huo, wakiwemo wabunge wa Chadema na CUF waliopo mjini hapa, wafanyakazi wa hoteli hiyo na ofisa mmoja wa polisi.

Kifaa hicho ni kidogo sawa na kidole gumba cha mkono ama kifaa cha kuwekea mafaili ya kompyuta maarufu kama ‘USB Flash’ ambacho kila baada ya sekunde 10, kilikuwa kinatoa mwanga mwekundu kama ilivyo baadhi ya simu za mikononi ambazo hutoa mwanga kuashiria kuwa ipo kwenye eneo ambalo mfumo wa mawasiliano ya kampuni husika unapatikana. Kifaa hicho kilikuwa na tobo kwa juu katika sehemu ya chaga ambayo kilikuwa kimebandikwa kimshazari kwa kutumia gundi maalum.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika mtandao wa internet kifaa hicho ambacho hutumiwa na wataalam wa ukachero, kina uwezo mkubwa wa kunasa sauti kwa muda mrefu kulingana na aina ya kifaa hicho. Muda wa kunasa sauti huweza kuanzia saa 18 hadi 300 huku kikitumia kiasi kidogo sana cha umeme au betri. Kina kalenda ambayo mtumiaji huweza kuiseti kwa jinsi anavyotaka.

Kwa mujibu wa mtandao wa kampuni ya Ts- Market ya Russia inayotengeneza vifaa vya kunasia sauti katika mfumo wa video na sauti, kifaa hicho kina uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira ya kila aina ikiwa ni pamoja na vumbi na joto kali.

Pamoja na hayo, mtumiaji anaweza kuweka neno la siri kuhakikisha hakuna mtu mwingine anayeweza kutumia ikiwa ni njia salama ya kuhakikisha alichorekodi kinabaki salama. Pia kina chaguzi mbalimbali za lugha ambazo zinaweza kutumika.

Kwenye chaga la kitanda cha Dk. Slaa ilionekana alama nyeupe ambayo iliwafanya baadhi ya wabunge waliofika kwenye tukio hilo kueleza kuwa inaashiria sehemu hiyo ilibandikwa kifaa kingine na pengine baada ya taarifa kujaa, kikachukuliwa na kuwekwa kingine.

Akihadithia jinsi alivyogundua kuwepo kwa kifaa hicho chumbani mwaka, Dk. Slaa alisema kuwa juzi saa 5:00 wakati akiwa anahudhuria vikao bungeni, aliarifiwa na mmoja wa marafiki zake ambaye hakumtaja kwamba kwenye chumba chake kuna kinasa sauti cha kikachero. “Mimi sikushtuka sana, nikawa naendelea na vikao bungeni. Kama unavyojua jana jioni nilikuwa nahudhuria kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,” alisema Dk Slaa.

Kwenye kikao hicho, ilikuwa inajadiliwa hoja binafsi ambayo alitarajia kuiwasilisha bungeni akimtuhumu Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa kwa kutaka kampuni ambao iliondolewa hatua za wali, irejeshwe.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema bungeni wiki iliyopita kuwa hoja ya Dk. Slaa inatokana na taarifa iliyonyofolewa kutoka kwenye faili Wizara ya Mambo ya Ndani na mtu ambaye hajulikani. Uchunguzi wa aliyeiba nyaraka hizo bado unafanyika.

Dk. Slaa aliendelea kusema kuwa baada ya kutoka kwenye kikao hicho saa 11:00 jioni alienda kula chakula cha jioni na saa 4:00 usiku alirejea kwenye hoteli aliyokuwa anaishi na alipokuwa akipanda ngazi, ndipo akakumbuka juu ya onyo alilopewa na msiri wake kuhusu kinasa sauti kilicho chumbani kwake.

Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), Salum Msangi alifika eneo hilo kabla ya hali kutulia akiwa na maofisa kadhaa wa polisi ambao walianza kwa kupata maelezo ya Dk. Slaa na baadaye Dk. Ali na walichomoa vifaa hivyo na kuondoka navyo kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Msangi aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa eneo hilo kuwa ni mapema kueleza chochote kuhusu kifaa hicho, lakini akaahidi kuwa baada ya uchunguzi kukamilika, ataweka hadharani mambo yote. Wabunge wote wawili walisema kuwa wapo tayari kuendelea kulala kwenye hoteli hiyo usiku ule lakini taarifa zilizopatikana mjini hapa jana zilieleza kuwa tayari wamehama na haijulikani wanakoishi kwa sasa.

“Kwa vile nimesoma hadithi kwenye vitabu vingi kuhusu mambo haya ya ‘Bugging’ siogopi nitaendelea kulala,” alisema Dk. Slaa baada ya polisi kuondoka na kifaa hicho, lakini awali alikuwa akisema kuwa hajui kama kifaa hicho kinatoa miale ya kumdhuru.

Dk. Slaa alisema kutokana na tabia yake ya kuwa mkweli na hata kuthubutu kufumua madhambi wanayoyafanya vigogo serikalini kwa maslahi ya wananchi wote wa Tanzania, amekuwa akiishi kwa tahadhari akitambua kuwa anaweza kuwekewa kudhuriwa kwa namna yoyote ile kama vile kuwekea sumu kwenye vyakula.

Kwa sababu hiyo alisema kuwa amekuwa akichukua tahadhari kubwa katika vyakula anavyokula kwa kuhakikisha wale wanaompatia chakula anawafahamu. “Hata hapa hotelini wanajua, chakula changu huletwa kwa utaratibu maalumu,” alisema Dk. Slaa bila kutaka kufafanua.

Alitoa mfano kuwa katika siku za karibuni alipewa zawadi ya mvinyo kwenye chupa yenye ujazo wa lita moja na mtu ambaye hakumfahamu, lakini alitaka maelezo juu ya mtu aliyempatia.
“Niliirudisha kule reception (mapokezi) nikitaka maelezo juu ya mtu aliyeileta lakini baadaye walisema ni mwalimu wa CBE (Chuo cha Biashara) hapa Dodoma. Kwa kuwa sikumfahamu, sikuitumia,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa baada ya kuichunguza kwa juu aliona matobo matatu kuashiria kuwa kuna kitu chenye ncha kama sindano kilitoboa, hivyo akaitilia shaka hasa ikizingatia kuwa mtoa zawadi hakuwa anamfahamu. Divai hiyo ambayo Mwananchi ililishuhudia inaitwa Altar Wine.

Hata hivyo, Dk. Slaa alisema kuwa ni mapema kuhitimisha kuwa aliyemzawadia mvinyo hiyo alikuwa na lengo baya la kumdhuru kwa sababu haijafanyiwa uchunguzi wowote wa kitaalamu.
Baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo walithibitisha kuwa mwalimu wa CBE aliyempelekea Dk. Slaa divai hiyo wanamfahamu kwa sura kwa kuwa amekuwa akifika mara kwa mara hotelini hapo.

Katibu wa bunge alisema kuwa si rahisi kuweza kuelezea kifaa hicho kilikuwa ni kinasa sauti cha kikachero kwa sababu uchunguzi wa kina unahitajika.
CHANZO: Mwananchi

Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.