22 Mar 2013

Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Othman Rashid

Julai 11, mwaka jana niliandika makala ifuatayo kwenye jarida la Raia Mwema, ikibeba kichwa "Ni Vigumu Kuiamini Serikali kwa Dkt Ulimboka." Ninakusihi uisome kisha nitaeleza kwanini nimeirejea katika post hii
"KWA mara nyingine, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa tuhuma nzito dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), safari hii ikidaiwa kuwa baadhi ya viongozi wa taasisi hiyo nyeti wana mpango wa kuwaua baadhi ya viongozi wa CHADEMA.
Itakumbukwa kuwa wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita, CHADEMA kiliituhumu Idara hiyo kuwa ilikuwa inakihujumu chama hicho, tuhuma ambazo zilifanya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TISS, Jack Zoka (pichani chini), kuzikanusha vikali.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa  Jack Zoka
Tuhuma hizi za CHADEMA zimekuja siku chache baada ya tukio la kusikitisha na la kinyama lililomkuta kiongozi wa jumuiya ya madaktari Dk. Steven Ulimboka ambaye alitekwa na hatimaye kuteswa na watu 'wasiojulikana.'
Katika tukio la Dk. Ulimboka, Serikali imejikuta ikinyooshewa vidole kuwa inahusika, hali iliyomfanya Rais Jakaya Kikwete kulizungumzia suala hilo katika hotuba yake kwa Taifa hivi karibuni.
Lakini takriban kila anayefuatilia kwa ukaribu suala hilo anaweza kuungana nami kutanabahisha ya kuwa japo hotuba ya Rais Kikwete imesaidia kwa namna fulani kuonyesha kuwa Serikali yake imeguswa (kwa maana ya kusikitishwa) na tukio hilo, kwa kiwango kikubwa haijasaidia kuondoa fikra kuwa kuna mkono wa Serikali.
Binafsi, nimelichambua kwa kirefu tukio hilo la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka katika mfululizo wa makala zangu za sauti (podcasts). Makala husika yenye kichwa cha habari “Nani aliyemteka na kumtesa Dk. Ulimboka?”
Kwa kifupi, katika makala hiyo nimezungumzia dhana tatu kuhusiana na tukio la Dk. Ulimboka. Ya kwanza ni hiyo inayogusa hisia za wengi kuwa Serikali inahusika na tukio hilo. Katika makala hiyo, nimeungana kimtizamo na kauli ya Rais Kikwete kuwa “Serikali imteke na kumtesa Dk. Ulimboka ili iweje.”
Kadhalika, nimeeleza kuwa japo kuna nyakati Serikali kwa kutumia vyombo vya dola inaweza kutumia vitisho na hata nguvu ikibidi ili kuzima upinzani dhidi yake, katika mazingira ya kawaida ni vigumu kuamini kuwa Serikali ya Rais Kikwete ingekuwa tayari kujiingiza matatizoni kwa kumteka na kumtesa kiongozi wa madaktari ili tu iwatishe madaktari wanaogoma.
Nimebainisha hivyo kwa vile ninaamini kuwa Serikali inafahamu fika kuwa kumnyamazisha Dk. Ulimboka hakuwezi kuwanyamazisha madaktari wote nchini.
Dhana ya pili ni ile ya hujuma dhidi ya Serikali. Kimsingi dhana hiyo inabashiri kuwa pengine kuna ‘watu wenye nguvu na jeuri ya fedha’ ambao wamefanya unyama huo dhidi ya Dk. Ulimboka kwa minajili ya 'kuikoroga' Serikali. Takriban kila anayefuatilia mwenendo wa siasa ndani ya chama tawala CCM atakuwa anafahamu kuwa kuna mtifuano mkubwa (japo usiosikika sana waziwazi) unaoendelea ndani ya chama hicho, hususan kuhusiana na kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015.
Kwamba kuna mafisadi wanaoweza kumwaga fedha aidha kwa ‘majasusi binafsi’ au ‘majasusi rasmi’ ni jambo linalowezekana. Kinachonifanya niipe uzito mdogo dhana hii ni uchambuzi wa hasara na faida za tendo husika (cost and benefit analysis).
Hivi, kama mafisadi wakimteka na kumtesa Dk. Ulimboka, kisha Serikali ya Kikwete ikaandamwa, mafisadi hao watanufaikaje (zaidi ya kufurahia kuona Serikali inabebeshwa lawama isizostahili)?
Dhana ya tatu, na ambayo binafsi ninaipa uzito mkubwa, ni uwepo wa kile kinachofahamika katika lugha ya Kiingereza kama ‘rogue elements of the state apparatus’ (yaani ‘watendaji katika taasisi za dola ambao wanatenda kazi zao kinyume na taratibu na sheria,’ kwa tafsiri isiyo rasmi).
Dhana hii ya mwisho inaweza kushabihiana na ya pili kwa maana ya hicho nilichoita ‘majasusi rasmi,’ yaani watumishi wa vyombo vya dola ambao wanatumia ujuzi wao kutekeleza matakwa, si ya mwajiri wao, bali ya mafisadi waliowapa fedha kwa ‘kazi maalumu.’
Katika makala hiyo ya sauti nimeeleza kuwa ni wazi vyombo vya dola vilikuwa vikimfuatilia Dk. Ulimboka na waratibu wengine wa mgomo wa madaktari. Hilo si la kuhoji kwani ni utaratibu ‘wa kawaida’ kwa wana usalama. Iwe ni taasisi ya mashushushu wa ndani wa Marekani (FBI), au wenzao wa Uingereza (MI5), au TISShuko nyumbani, kila mtu au kikundi kinachotazamwa kama tishio kiusalama hufuatiliwa kwa karibu.
Sasa basi, kwa kuzingatia dhana hiyo ya ‘rogue elements,’ inawezekana watendaji waliokabidhiwa jukumu hilo waliamua kutumia njia za ‘liwalo na liwe’ (hapana, si kama ile ya tamko la Waziri Mkuu Mizengo Pinda) baada ya ‘njia za kistaarabu’ kumlazimisha Dk. Ulimboka awaeleze ‘nani anayewachochea madaktari kugoma’ kutozaa matunda.
Yaani baada ya diplomasia kushindwa, wakaamua kutumia mateso ya hali ya juu (kwa lugha ya kisheria ‘third degree torture’ na kitaalamu ‘fifth degree torture’).
Kwa nini ninashawishika kuamini kuhusu rogue elements? Tumeshuhudia matukio kadhaa huko nyuma. Naamini wengi wa wasomaji mtakuwa bado mnakumbuka tukio la mwandishi wa habari mahiri na mhariri  wa gazeti la Mwanahalisi, Said Kubenea, kumwagiwa tindikali usoni. Kibaya zaidi katika tukio hilo, mmoja wa wahusika alitajwa kuwa ni mwajiriwa wa TISS.
Sijui kesi hiyo iliishaje lakini la msingi hapa ni kuwa iliacha doa la aina fulani kwa taasisi hiyo hasa kwa vile haikuwahi kumkana afisa huyo (kwa maana ya kusema hakutumwa kiofisi bali alikuwa ‘rogue officer’ tu).
Itakumbukwa pia kuwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe aliwahi kueleza kuwa Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa na mpango wa kumuua. Kama ilivyokuwa kwa tukio la Kubenea lililomhusisha mtu aliyatajwa kuwa ni Afisa Usalama wa Taifa, Idara hiyo haikuwahi kukanusha tuhuma hizo.
Tukirejea kwenye tuhuma za CHADEMA dhidi ya TISS, binafsi nashawishika kuamini kuwa kama kuna ukweli katika tuhuma hizo basi itakuwa ni zilezile ‘rogue elements’ ambazo ninaamini zipo ndani ya taasisi hiyo nyeti.
Najua hili halitowapendeza wahusika, lakini kuna hisia kwamba ukiweka kando taasisi hiyo kuendeshwa kama kitengo cha usalama cha CCM moja ya sababu nyingine kubwa ya matatizo yanayoikabili taasisi hiyo ni ajira zilizotolewa pasipo kuzingatia ‘wito’ na ‘kipaji’ cha kuwa Afisa Usalama.
Popote duniani, maafisa usalama wanapaswa kuwa ‘watu zaidi ya watu wa kawaida’ kwa maana ya kuwa na upeo na uwezo wa hali ya juu katika takriban kila nyanja ya akili zao:  na huo ndio msingi wa neno INTELLIGENCE kwa kimombo.
Sasa tunaporuhusu watoto zetu, ndugu au jamaa zetu kuingizwa kwenye taasisi nyeti kama hiyo kwa vile tu ‘kuna maslahi manono’ tunaiweka rehani nchi yetu.
Naomba niwe mkweli. Madudu mengi yanayoendelea katika Tanzania yetu kwa sasa yanachangiwa na ubabaishaji unaoendelea ndani ya idara hiyo muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa lolote lile duniani. Wao wanafahamu kanuni hii: uimara au kuyumba kwa nchi ni kielelezo cha uimara au udhaifu wa Idara ya Usalama ya nchi husika.
Sasa kama tuna maofisa usalama huko Benki Kuu (BoT) lakini bado ufisadi wa EPA ukafanikiwa, na kama TISS ipo kazini saa 24 lakini bado kuna majambazi wamemudu kutorosha mabilioni ya dola na kuzificha nchini Uswisi basi ni wazi Idara hiyo ni dhaifu.
Na kama tunakubaliana kuwa kuna udhaifu mkubwa katika taasisi hiyo, kwa nini basi CHADEMA wasiamini taarifa kuwa Idara hiyo ina mpango wa kuwadhuru? Sitaki kuamini kuwa, iwapo taarifa hizo ni kweli, basi ni za ki-Idara bali ninaendelea kuhisi kuwa ni matokeo ya kulea ‘rogue elements’ ndani ya chombo hicho muhimu.
Unajua, inapofika mahala Afisa Usalama wa Taifa anaona sifa kutangaza wadhifa wake baa ili vimwana watambue kuwa yeye ni shushushu, au kiongozi mwandamizi wa taasisi hiyo nyeti anapoweza kufanya ‘madudu’ hadi sisi tulio nje ya nchi tukafahamu, basi ni wazi kunahitajika kazi ya ziada kurekebisha mwenendo wa chombo hicho nyeti.
Ninatambua kuwa kuna watakaokerwa (na pengine kushauri hatua ‘mwafaka dhidi ya mtizamo wangu’) lakini ninaamini kuwa kila Afisa Usalama wa Taifa mzalendo na aliyekula kiapo cha utii kwa Taifa anakerwa kuona nchi yetu ikienda kwa mwendo wa bora liende huku rasilimali zetu zikiporwa kwa mtindo wa ‘bandika bandua.’
Pasipo mageuzi ya haraka ndani ya taasisi hiyo si tu itaendelea kutuhumiwa na CHADEMA lakini mwishowe walipa kodi wanaowezesha maslahi manono kwa wanausalama wetu watasema ‘imetosha.’
Watanzania wanaweza kufika mahala wakahoji umuhimu wa kuwa na taasisi ya ‘kufikirika’ ambayo licha ya kuogopwa na wengi (nikiamini bado kuna wanaoiogopa) inashindwa kudhibiti uharamia lukuki unaofanywa dhidi ya nchi yetu na Watanzania wenzetu kwa kutumia madaraka yao.
Nimalizie makala hii kwa kutoa tahadhari kwa Idara hiyo kwamba maswali magumu hayajibiwi kwa majibu mepesi. Mmoja wa viongozi wa ngazi za juu za taasisi hiyo amejibu tuhuma zilizotolewa na CHADEMA kwa namna ileile alivyojibu mwaka 2010 pale Idara hiyo ilipotuhumiwa kuihujumu CHADEMA kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu. Tatizo la kiongozi huyo, na pengine Idara hiyo kwa ujumla ni uzembe wa kusoma alama za nyakati.
Na kila mzalendo-awe ndani ya taasisi hiyo au mwananchi wa kawaida-anapaswa kupinga kwa nguvu zote dalili za kutaka kuigeuza nchi yetu kuwa ‘Mafia State’ (yaani dola ambayo kila TomDick na Harry anaweza kuteka na kutesa au kupanga kuuwa wale  wanaopigania haki za wanyonge kama hao viongozi wa CHADEMA wanaodai kutishiwa kuuawa kwa ‘kosa la kuwakalia kooni wabaka uchumi wetu.’
Biblia inasema mwenye haki ataanguka saba mara sabini lakini atasimama. Na kila mzalendo atakwazwa vya kutosha lakini, inshallah, Tanzania tunayoistahili itafikiwa."
Rais Kikwete (kushoto) akiongea na Othman (katikati) na Mkuu wa  JWTZ  Jenerali Davis Mwamunyange
Juzi, gazeti la Mtanzania limechapisha habari ya kiuchunguzi ambayo kwa kiasi kikubwa imeakisi hicho nilichobashiri katika makala yangu hapo juu.Labda kabla ya kuendelea ninukuu paragrafu zifuatazo kabla hatujaendelea zaidi na mada hii 
"...mgawanyiko kwa wafanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambako uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi yao wameasi na kuamua kufanya kazi kwa karibu na makundi yanayowania urais, badala ya ile ya kusimamia maslahi ya taifa.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya makundi hayo, vinaeleza kuwa matukio ya sasa ya kudhuru watu maarufu yanadaiwa kufanywa na watumishi wenye mafunzo ya kutesa na kuua walio ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa kwa malengo yenye maslahi fulani fulani.

Mmoja wa wanasiasa maarufu hapa nchini ambaye amepata kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, amelieleza MTANZANIA Jumatano kuwa vitendo vya kushambulia na kudhuru raia vinafanywa na watumishi wa Idara ya Usalama walioviasisi kwa madhumuni ya kuwachonganisha wananchi na serikali yao, ili wazidi kujenga chuki na watawala.

Anaeleza zaidi kuwa wanausalama wanaodaiwa kuasi kutokana na kukatishwa tamaa na mwenendo wa uendeshaji serikali sasa wamejipenyeza na kuwa wakala wa moja ya kundi la wanaCCM linalopambana na makundi mengine ya ndani ya chama hicho kushika ukuu wa dola na wapo pia wanaodaiwa kujipenyeza katika vyama vya upinzani, hususani Chadema na kushiriki harakati za kuiondoa CCM madarakani..."
Ukirejea nilichoandika katika makala yangu utabaini kuwa taarifa hiyo ya kiuchunguzi ni kama imekithibitisha.Siandiki post hii kwa minajili ya kupongezwa au kusifiwa bali kupigia mstari umuhimu wa Idara ya Usalama wa Taifa kufanyiwa marekebisho makubwa haraka iwezekanavyo.
Tunapokuwa na chombo nyeti kama hicho kikiwa kimegawanyika mapande mapande, huku baadhi ya maafisa wake wakijichukulia sheria mkononi, basi ni wazi kuwa nchi inaelekea kubaya.
Najua haya ninayoandikwa yatapuuzwa na Serikali ya Rais Kikwete lakini madhara ya kupuuza huko yanaweza kuwa makubwa kuliko inavyofikiriwa sasa. Ni muhimu kwa Rais Kikwete kutambua kuwa usalama wake binafsi na wa viongozi wengine wakuu wa serikali upo mikononi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Hivi katika hali ya kufikirika tu, haiyumkiniki kuhisi kuwa ipo siku baadhi ya maafisa wa Idara hiyo (ambayo ni wazi inaonekana kukosa mwelekeo na mwongozo) wakaishia kumdhuru kiongozi kwa namna moja au nyingine?
Maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakimsaidia Rais Kikwete alipoanguka jukwaani wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Picha hii inaonyesha jinsi wanausalama hao walivyo karibu na viongozi wakuu wa kitaifa
Natambua kuwa Rais Kikwete anaweza kuwa anaelewa kinachoendelea ndani ya Idara hiyo lakini kama ilivyo kwenye maeneo mengine, Rais wetu ni mgumu wa maamuzi.Lakini pengine kitakachomkwaza zaidi kushughulikia tatizo hili ni makosa aliyofanya huko nyuma katika uteuzi wa uongozi wa Idara hiyo ambao ulizngatia zaidi 'ushkaji' badala ya 'uwezo wa kiutendaji kazi.'
Rais Kikwete (katikati) akiomba dua na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Othman Rashid (kushoto) na Makamu wa Rais Dkt Gharib Bilal. Kikwete na Othman ni marafiki wa muda mrefu
I just hoipe hakuna baya litakalojitokeza huko mbeleni lakini hisia yangu ya sita inakinzana na imani hiyo.



NAANDIKA safu hii nikiwa hospitalini nilikolazwa baada ya afya kukongoroka kidogo na pamoja na hali hiyo, inafariji kuona baadhi ya marafiki wakitumia njia mbadala za kumsaidia mgonjwa kupata ahueni, kama ambavyo rafiki mmoja huko Twitter,Slimcony ( almaaruf  ‘Beckham wa Nungwi’) alivyonifanya nisahau maumivu niliyonayo na kunifanya nicheke kwa ‘tweet’ yake aliyohoji kwa utani kama nimeshawekewa sumu ya polonium (kama ‘alivyofanyiziwa’ Alexander Litvinenko).
Moja ya mafanikio makubwa na ya wazi kabisa ya nchi hii ya Uingereza ni kitu kinachofahamika kama National Health Service (NHS), yaani kwa tafsiri isiyo rasmi ‘huduma ya afya ya taifa.’ Kwa kifupi, hii ni mamlaka inayohusika na hospitali na matibabu katika nchi hii.
Kwa bahati mbaya, pengine ili uweze kuelewa umuhimu na ubora wa NHS inakulazimu uwe unahitaji huduma za hospitali, uwe unauguza au uwe umelazwa katika hospitali lukuki zilizo chini ya mamlaka hiyo.
Niseme hivi; kwa kulinganisha na huduma za nyingi ya hospitali zetu huko nyumbani Tanzania, ukilazwa katika moja ya hospitali za NHS unaweza kutamani uendelee kuwa wodini kwa muda mrefu zaidi hata kama ugonjwa uliokupeleka kulazwa umepona.
Hapa kuna mchanganyiko wa teknolojia ya hali ya juu ya matibabu, weledi wa kitaaluma usio na mfano, na watoa huduma (madaktari, manesi, wahudumu, nk) na mazingira ya kumfanya mgonjwa ajisikie kuna wanaomjali. Na yote hayo yanapatikana bure buleshi.
Nilishapata kuandika kuhusu ‘kimbembe’ nilichokumbana nacho huko nyumbani wakati ninamuuguza mama yangu (sasa marehemu) nilipokuja mwaka 2008. Nisingependa kurudia. Lakini kwa kifupi ni kwamba inahitaji moyo na fedha za kutosha kumuuguza mgonjwa katika nyingi ya hospitali zetu huko nyumbani ikiwa pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako mama yangu alilazwa kwa muda.
Licha ya mrundikano wa wagonjwa wodini ambao baadhi yao hulazwa chini kutokana na uhaba wa vitanda, suala la rushwa limekuwa muhimu kama mahitaji ya tiba kwa mgonjwa. Kwa kifupi, ukiwa mgumu wa kutoa rushwa unaweza kuharakisha kifo cha mgonjwa wako hata kama ugonjwa alionao unatibika kirahisi.
Lengo la makala hii leo si kuzungumzia kuyumba kwa afya yangu au ubora wa huduma za afya hapa Uingereza. Nikiwa hapa hospitalini muda unakwenda taratibu kweli, na licha ya kuwa na vitu mbalimbali vya kumburudisha mgonjwa, bado kasi ya muda inaonekana kuwa tofauti na ile tuliyoizowea tukiwa wazima kiafya.
Ni katika kuwa na muda huo ‘wa kupoteza’ ndipo nimepata fursa ya kutosha kufuatilia sakata linaloendelea kuhusu mmoja wa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare.
Nimeweza kupitia kila gazeti la mtandaoni, na zaidi kusoma kila andiko kuhusu sakata hilo katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums, ambako kimsingi ndipo kulipoibuka suala hilo.
Pamoja na kukongoroka kwa afya yangu, nimeweza kulichunguza suala hili katika mtizamo wa kiusalama zaidi kuliko kama msomaji tu wa habari fulani.
Moja ya mambo yanayonitatiza zaidi kuhusu sakata hili ni kauli iliyowahi kutolewa huko nyuma na kiongozi mmoja wa CCM, Mwigulu Nchemba, kuwa chama chao kina mkanda wa video wenye ushahidi kuwa CHADEMA wana mpango wa kufanya ugaidi (kudhuru watu fulani japo hawakutajwa).
Kwa kifupi tu, huhitaji kuwa kiongozi wa CCM au kuwa na uelewa wa mambo ya usalama kutambua kuwa ukikumbana na mkanda wa aina hiyo mahala pa kwanza kukimbilia ni polisi. Je, kwa nini Nchemba hakuwasilisha mkanda huo wa video polisi?
Lakini kwa upande wa jeshi letu la polisi, kwa nini baada ya kupata taarifa hizo hawakumsihi Nchemba awapatie ushahidi huo hadi wasubiri utundikwe huko Jamii Forums, kisha ndipo wamkamate Lwakatare?
Jingine nililobaini katika mkanda huo wa video ni kiwango cha ubora wa picha (nadhani neno sahihi kwa kimombo ni resolution). Kwa tunaofahamu secret recording(kumrekodi mtu kwa siri), ni vigumu sana kupata picha yenye ubora wa kiwango kinachoonekana kwenye mkanda huo wa Lwakatare. Namna pekee ya kuweza kuwa na picha yenye ubora wa namna hiyo ni kwa mhusika kujirekodi mwenyewe, tena si kwa video recorder ya siri bali ya wazi.
Kuna wanaosema huenda video hiyo imefanyiwa uchakachuaji, kwamba labda Lwakatare amepandikizwa maneno. Hilo pia linawezekana japo linahitaji uelewa mkubwa wa teknolojia ya video. Lakini uwezekano wa kupata wataalamu wenye uelewa wa teknolojia ya aina hiyo si mgumu katika zama hizi tunazoshuhudia matukio ya kijahili kana kwamba taifa letu ni ‘Mafia State’ fulani.
Lakini katika mazingira ya kawaida tu, hivi Lwakatare alileweshwa au ‘kurogwa’ hadi kufikia hatua ya kukutana na huyo ‘aliyekuwa akipewa majukumu’ katika eneo la uwazi kama linavyoonekana katika mkanda huo wa video? Sidhani kama hata mwendawazimu anaweza kupanga mipango ya kudhuru watu katika sehemu inayoonekana katika mkanda huo, na sote tunajua Lwakatare si mwendawazimu.
Tukiweka kando suala la Lwakatare, wakati ninafahamu kwa nini polisi wamemkamata kiongozi huyo wa CHADEMA, ninashindwa kabisa kuelewa kwa nini kanda kadhaa za video zilizozagaa huko YouTube zilizorekodiwa hadharani zikimwonyesha Ustaadh Ilunga akihamasisha mauaji ya maaskofu, mapadre na walei wa Kikristo hazijawafanya polisi wamkamate.
Je, alichohamasisha Ilunga ndicho kimetekelezwa kwa kuuawa kwa Padre Evaristus Mushi huko Zanzibar. Sasa kama Lwakatare amekamatwa kwa kuwa tu na mpango wa kufikirika wa kudhuru wanahabari (tukiamini video husika) kwanini basi Ustaadh Ilunga awe huru kana kwamba alichohamasisha ni sera ya chama tawala?
Nimalizie kwa kutahadharisha kuwa tuna tatizo kubwa zaidi ya tunachoshuhudia katika matukio mbalimbali ya hivi karibuni. Kwa upande mmoja kuna uwepo wa rogue elements ndani ya taasisi zetu za usalama, upande mwingine kuna wanasiasa wahuni wanaotumia mbinu chafu kabisa kufanikisha malengo yao mufilisi ya kisiasa/kibinafsi, na cha hatari zaidi ni kile kinachoitwa ‘Deeper State’ yaani ushirikiano rasmi (japo si halali) kati ya magenge ya wahalifu na taasisi za intelijensia.
Pasipo jitihada za makusudi kufanyika kupambana na tatizo hilo basi tujiandae kushuhudia mengi ya kutisha huko mbele (hususan kati ya sasa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015).


Jasusi ChatBot

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.