12 Nov 2008

MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, amesema kuwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wa ufisadi kwa pamoja kunaweza kusababisha nchi kuyumba.

Hoseah alisema hayo katika siku ambayo hakukuwa na mtuhumiwa yeyote katika sakata la wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) aliyefikishwa mahakamani baada ya wafanyabiashara 20 kupandishwa mfululizo kizimbani kuanzia Jumatano iliyopita hadi juzi.

Akitoa mada kwenye semina iliyohusisha vyuo vikuu tisa nchini iliyofanyika kwenye Hoteli ya Blue Pearl jijini, mkurugenzi huyo wa Takukuru alisema: "Tukiwapeleka wote mara moja mahakamani, nchi inaweza 'ikaparalyse' (ikapooza) ni lazima kuwe na 'stability' (kutoyumba), tufanye kwa kuwa ni sahihi," alisema Hoseah.

Akitoa mada katika semina hiyo iliyowahusisha wajumbe wa kamati za maadili kutoka vyuo hivyo, Hoseah alieleza kuwa, mapambano dhidi ya rushwa kubwa yanapaswa kufanyika kukiwa na utashi wenye nguvu wa kisiasa, mikakati sahihi ya kiuchumi pamoja na kuzuia rushwa.

Alisema kuwa watuhumiwa wa rushwa kubwa wana nguvu kutokana na fedha nyingi wanazomiliki, kiasi cha kuweza kuhatarisha usalama wa watu wengine kwa kutumia vibaya fedha zao.

Dk Hoseah ni kigogo wa tatu kuzungumzia uwezo wa mafisadi na hatari ya kuwashughulikia bila ya umakini baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kulieleza bunge kuwa, kushughulikia watu wenye uwezo wa kifedha ni kazi ngumu, kama ilivyoelezwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Ali Hassan Mwinyi kuwa mafisadi ni hatari.

Watuhumiwa katika kashfa hiyo ya EPA wanadaiwa kuchota fedha hizo katika kipindi cha mwaka 2005/06 wakisingizia kupewa au kulipa madeni na makampuni ya nje yaliyokuwa yakiidai serikali. Watuhumiwa hao wanadaiwa kuchota Sh133 bilioni.

Pamoja na kilio cha wananchi kuwa wote waliochota fedha hizo wapandishwe kizimbani, Rais Jakaya Kikwete alitoa maagizo kuwa wale ambao wangeshindwa kurejesha fedha walizochota kabla ya Oktoba 31, ndio waliotakiwa kufikishwa mahakamani.

Na watuhumiwa hao 20 waliofikishwa mahakamani hadi sasa wamekuwa wakipandishwa kizimbani kwa nyakati tofauti na wengi wameshtakiwa kwa makosa tofauti, wakipandishwa mmoja mmoja na wakati mwingine kuunganishwa na wenzao na kwa mahakimu tofauti.

Akitoa mada yake jana, Dk Hosea alisema Takukuru peke yake haiwezi kumaliza tatizo la rushwa nchini bila kuwepo ushirikiano kutoka kwa taasisi za elimu, mashirika mbalimbali na wananchi.

Aliongeza kuwa, mapambano dhidi ya rushwa, kubwa na ndogo yanapaswa kuwashirikisha wananchi wote, huku akielezea Watanzania kuwa ni waoga kutokana na kukosa ufahamu wa masuala mbalimbali yanayowahusu.

Hoseah alisema kuwa katika mapambano ya rushwa ni vema kuzuia rushwa na kwamba uadilifu ndiyo njia bora ya kulitokomeza tatizo hilo.

Alisema moja ya kasoro za Tanzania ni kuwa na taasisi nyingi dhaifu, zisizo na uwezo zinazofanya kazi zake bila ya uwazi, hali aliyoielezea kuwa inakaribisha rushwa.

"Moja ya kasoro za Tanzania ni kuwa na taasisi dhaifu, zisizo na uwazi... lazima tufanye kazi kuzipa nguvu kwa kurejesha maadili," alisema Hoseah.

Aliongeza kuwa, ndani ya serikali pia uadilifu upo chini na kueleza kuwa kuwa kutokana na hali hiyo ni vema wananchi wakaacha kulalamika badala yake kutafuta ufumbuzi wa tatizo kwa kushiriki kurejesha maadili na kupambana na rushwa.

Alisema kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakilalamikia tatizo la rushwa huku wakishinikiza Takukuru ichukue hatua bila wao kushiriki katika mapambano hayo ambayo alisema kuwa ni ya kila mmoja.

Mkurugenzi huyo wa Takukuru alisema kuwa katika kutilia maanani umuhimu wa kuongeza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa nchini, wameanzisha mkakati maalumu wenye lengo la kurejesha uadilifu nchini.

"Tunataka kurejesha maadili, lengo ni kuzuia rushwa, jukumu letu ni kuwawezesha watu wafahamu na kushiriki katika mapambano hayo," alisema.

Kwenye Mahakama ya Kisutu, hali jana ilikuwa shwari baada ya siku nne za purukushani za kupandisha kizimbani watuhumiwa hao 20, ambao kati yao ni wawili tu waliopata dhamana kutokana na mahakama kuweka masharti magumu, anaripoti James Magai na Paulina Richard.

Hadi majira ya alasiri jana, hakuna mtuhumiwa hata mmoja mpya kwenye kesi hiyo ambaye alikuwa amefikishwa mahakamani hapo.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Charles Kenyela, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi mchana huo hakuwa na taarifa za kuwepo kwa watuhumiwa wengine ambao wangepandishwa kizimbani.

Mpaka sasa ni wamiliki wa kampuni 10 tu kati ya 22 zinazodaiwa kuchota fedha hizo ambao walikuwa wameshafikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, akiwemo mfanyabiashara maarufu mwenye asili ya Kiasia, Jayatkumar Chantubhai Patel, ambaye anajulikana zaidi kwa jina la Jeetu Patel.

Tofauti na siku nyingine jana hali ilionekana kuwa tulivu mahakamani hapo huku kukiwa na pilikapilika chache za baadhi ya ndugu wa watuhumiwa katika kashfa hiyo ya EPA ambao walikuwa wakishughulikia dhamana za watuhumiwa hao.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Elieza Feleshi, hakutaka kuwaambia waandishi kama kuna watuhumiwa zaidi ambao wangefikishwa mahakamani jana na badala yake alisema aulizwe msemaji wa Wizara ya Sheria na Katiba.

Hata hivyo, msemaji huyo, Omega Ngole alijibu kwa ufupi kuwa hawawezi kusema ni lini watuhumiwa wanapelekwa mahakamani na badala yake taratibu zinapokamilika na DPP kujiridhisha, wahusika hufikishwa mahakamani.

“Hivyo ninachoweza kukuambia ni kwamba, tumwache DPP afanye kazi, kama kuna watu wa kuwapeleka mahakamani akishajiridhisha atawapeleka,” alisema Ngoe.

Wamiliki wa makampuni waliofikishwa mahakamani mpaka sasa ni Johnson na Mwesiga wanaomiliki kampuni ya Kernel, Ketan Chohan, Jeetu Patel na Amit Nandy (Bina Resort na Itoh), Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Edah Nkoma Mwakale (Changanyike Residential Compelex Ltd)

Wengine ni Rajabu Farijala, Japhet Lema na Rajabu Malanda (Mibale Farm), Rajabu Farijala na Rajabu Malanda (Money Planner), Japhet Lema (Njake Enterprises) na Ajay Somani na Jay Somani (Liquidity Services).

Wengine ni Jeetu Patel na ndugu zake wanaomiliki kampuni za Bencon International Ltd, Maltan Mining Ltd na Navy Cut Tobacco (T) Ltd.

CHANZO: Mwananchi

HAYO NDIO MATUNDA YA PhD YA HOSEA KATIKA KUPAMBANA NA RUSHWA AU NDIO APPLICATION YA THEORY FLANI YA KULINDA UHALIFU INAYODAI KWAMBA UKIFUTA KABISA UHALIFU KWENYE JAMII BASI VYOMBO VYA KUPAMBANA NA UHALIFU VITAKUWA HAVINA KAZI YA KUFANYA?MBONA VITA YA SOKOINE DHIDI YA WAHUJUMU UCHUMI HAIKUYUMBISHA NCHI?

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.