13 Apr 2009


Ally Sonda, Moshi

MBUNGE wa Jimbo la Vunjo(CCM) Aloyce Kimaro,amewataka mafisadi wanaojiandaa kumng'oa madarakani Rais Jakaya Kikwete na kundi la wabunge waliojitoa kafara kupinga ufisadi kuvunja mtandao wao mara moja kwa kuwa hautafanikiwa.

Akizungumza kwa kujiamini na huku akishangiliwa na umati wa watu,Kimaro alisema mwaka ujao wa uchaguzi, Rais Kikwete atashinda kwa kura nyingi sanjari na wabunge mahiri wanaomsaidia kupambana na ufisadi wakiwa ndani na nje ya Bunge.

Kimaro ambaye alikuwa akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kata ya Kahe Mashariki,alisema mafisadi wote wasiotaka Kikwete aendelee kuiongoza nchi kutokana na chuki za kuumbuliwa wataaibika zaidi mwaka ujao.

"Hivi sasa tunajua kuwa wapo mafisadi wanajipanga kuhakikisha kuwa Rais na wabunge waliojitoa mhanga kufa kwa kupinga ufisadi nikiwemo mimi tunang'oka mwaka 2010. Nasema hivi, hang'oki mtu hapa,Kikwete ni Rais hadi 2015 na sisi wabunge tutashinda vilevile, Mungu yupo mbele yetu,"alisema Kimaro.

Alisema bomu alilolilipua bungeni kuhusu uuzwaji wa nyumba za serikali ambalo limeanza kuleta mafanikio baada ya nyumba hizo kuanza kurejeshwa ni sehemu ndogo sana ya mikakati yake ya kupambana na mafisadi 'wanaoitafuna' nchi bila kunawa.Kimaro alisema ufisadi ndani ya Tanzania ni mkubwa na ndiyo sababu nchi inaendelea kuwa maskini na hivyo kujiendesha kwa kuombaomba misaada kutokana na watu wachache kuiba raslimali za taifa na kuzitorosha nje ya nchi.

Akizungumzia watu wanaolimezea mate jimbo lake na hivyo kujipanga kuwania ubunge mwakani, Kimaro alisema hana tatizo na vyama vya upinzani ambavyo vimeanza kutangaza kusimamisha wagombea, bali ugomvi wake ni kwa wanaCCM walioanza kujitangazia ubunge wa jimbo hilo hivi sasa. Aliiomba CCM wilaya ya Moshi Vijijini, kuwaonya wanachama hao kwa madai kuwa wanaleta mgawanyiko ndani ya CCM, kitendo ambacho kinaweza kutumika vibaya na kambi ya upinzani kuwasambaratisha wanaCCM.

"Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM, nakiomba Chama kiwaonye wanaCCM hawa wanaojitangazia ubunge wa Vunjo wakati wanajua kuwa mimi ndiye Mbunge halali wa Vunjo,nakuomba sana waonye la sivyo wataona cha mtema kuni,"alisema Kimaro bila kufafanua.

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Moshi,ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya wilaya hiyo,Alhaji Musa Samizi,Mwenyekiti wa CCM,Gabriel Masenga aliwataka wanaCCM wote wanaotaka ubunge wa Moshi Vijijini na Vunjo wasubiri muda muafaka ufike.

"Napenda kuwaomba wanaCCM wote wanaotaka Ubunge kwenye majimbo yetu mawili (Moshi Vijijini na Vunjo) wawe watulivu muda muafaka ufike,tutawapa fomu,tutawachuja kwa kura kama wanafaa,kujipitishapitisha hivi sasa ni kuleta vurugu ndani ya Chama na Jumuiya zake"alisema Masenga.

Masenga alitumia mkutano huo kuwataka baadhi ya wanachama wanaokikashifu Chama na viongozi wake baada ya kuadhibiwa kwa mujibu wa Katiba na hivyo kutishia kukihama CCM , waondoke mara moja na kujiunga upinzani kwa madai kuwa kuendelea kwao kuwa CCM ni sawa na kukumbatia Bomu.

"Wapo baadhi ya wanaCCM wameadhibiwa kwa kukiuka katiba ya Chama,sasa wana hasira wamekuwa wakikashifu Chama na baadhi ya viongozi,sasa kwa niaba ya Chama nawaomba waondoke CCM,huenda wakijiunga na vyama vya upinzani watafanya kazi yao vizuri ya kupambana na CCM,"alisema Masenga kwa kujiamini.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.