Showing posts with label ALOYCE KIMARO. Show all posts
Showing posts with label ALOYCE KIMARO. Show all posts

30 May 2009


MHH,AJALI ZINAZOWAANDAMA WABUNGE "WA AINA MOJA" ZINAWEZA KUZUA MASWALI YA NAMNA FLANI JAPO YAWEZEKANA KABISA KUWA NI AJALI KAMA NYINGINEZO.HEBU SOMA KWANZA HABARI IFUATAYO,KISHA TUJIULIZE MASWALI MAWILI MATATU:

Ally Sonda na Rehema Matowo, Mwanga

MBUNGE wa Jimbo la Vunjo, Aloyce Kimaro amenusurika kufa baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kuparamia mawe yaliyopangwa barabarani na kupata ajali usiku wa kuamkia jana. Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Kimaro na polisi zinasema kuwa, ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Mikongeni kata ya Lembeni wilayani Mwanga, Kilimanjaro kwenye barabara kuu ya Moshi-Tanga, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kwenda jimboni kwake.

Kwa mujibu wa habari hizo, wakati ajali hiyo inatokea, Kimaro alikuwa na rafiki yake Joseph Temu ambaye ndiye aliyekuwa anaendesha gari hilo aina ya Mercedes Benz akiwa na mkewe na watoto wake watatu. Katika ajali hiyo hakuna aliyejeruhiwa.

Kimaro alisema baada ya ajali hiyo mfanyabiashara wa Mwanga, Shafii Hasanal alitoa msaada wa kulivuta gari hilo hadi kwenye kituo cha mafuta Kisangara.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 2:30 usiku, chanzo kikiwa ni mawe makubwa na matofali yaliyokuwa yamepangwa barabarani katika eneo lenye kona na mlima.

Kamanda Ng’hoboko alisema kuwa watu wanaosadikiwa kuwa ni wezi, walipanga mawe hayo barabarani kwa lengo la kusababisha ajali ili kuwaibia abiria.

“Gari ya mbunge huyo ilipofika katika eneo hilo likiwa katika mwendo wa kawaida na mbele yao kukiwa na lori ambalo liliweza kuyapita mawe hayo bila tatizo, wao walipojaribu kuyapita tairi la mbele upande wa kulia na ‘sampo’ ya gari hilo vilipasuka wakashindwa kuendelea na safari,” alisema Ng’hoboko.

Kamanda huyo alisema kuwa miaka ya nyuma eneo hilo lilikuwa na matukio mengi ya aina hiyo ambayo yameanza kujitokeza upya, kwa kuwa awali wananchi wa eneo hilo kwa kushirikiana na polisi walikuwa wameyamaliza. Alibainisha kuwa polisi wanafanya operesheni ili kuwadhibiti wezi hao na kuwasaka waliohusika na tukio hilo ili wafikishwe mbele ya sheria.


Kimaro ni miongoni mwa wabunge waliojitokeza hadharani kupambana na vitendo vya ufisadi. Mwaka jana aliibua hoja bungeni kutaka, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ashitakiwe kwa kutumia madaraka vibaya ya kufanya biashara akiwa ikulu.

Hii ni ajali ya pili inayohusisha wabunge kutokea ndani ya wiki mbili baada ya ajali iliyomhusisha mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe iliyotokea eneo la Ihemi, Ifunda mkoani Iringa. Dk Mwakyembe, alinusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Kyela kwenda Dar es Salaam kuacha njia na kupinduka.

Ripoti ya polisi iliyotolewa wiki hii ilieleza kwamba ajali hiyo ilitokana na uzembe wa dereva, lakini mbunge huyo ameiponda na kuifananisha na ripoti ya mpiga ramli kwa vile haikuzingatia vigezo na utaalamu katika uchunguzi.


CHANZO: Mwananchi
NAAMINI WENGI WETU TUNAKUMBUKA AJALI ILIYOMHUSISHA MHESHIMIWA CHEYO a.k.a "Mzee wa Vijisenti" AMBAYO ILIPELEKEA VIFO VYA WATU WAWILI.TOFAUTI KATI YA AJALI YA CHENGE NA HIZI ZA MWAKYEMBE NA KIMARO NI REACTION YA POLISI.BAADA YA GARI LA CHENGE KUUA,SIKUWAHI KUSIKIA RPC AU RTC AKIKURUPUKA KUELEZA CHANZO CHA AJALI HUSIKA (JAPO KATIKA MAZINGIRA YA KAWAIDA,NI RAHISI KUIHUSISHA AJALI YA SAA 10 ALFAJIRI NA STIMU ZA KILEVI).BADALA YAKE ILIUNDWA TUME AMBAYO HADI LEO HAIJATUELEZA MATOKEO YA UCHUNGUZI WAKE (IF AT ALL ILIFANYA UCHUNGUZI).WORSE STILL,INAELEZWA KUWA WAKATI AJALI HIYO INATOKEA GARI LA CHENGE LILIKUWA NA BIMA ILIYOISHA MUDA WAKE.


ALIPOPATA AJALI MWAKYEMBE,RPC AKAKURUPUKA NA KUDAI KWAMBA CHANZO CHA AJALI NI MWENDO MKALI NA SHIMO LILILOKUWA BARABARANAI.BAADAYE TUME YA KAMANDA KOMBE IKAZIDI KUCHANGANYA MADAWA KWA KUTOA FINDINGS AMBAZO SI TU ZIMEINGILIA KAZI YA MAHAKAMA KWA KUWAHUKUMU MWAKYEMBE (kuwa alikuwa amelala wakati wa ajali) NA DEREVA WAKE (kwa uzembe) LAKINI PIA HAZIKUHUSISHA MAELEZO YA MWAKYEMBE KWA VILE HAKUHOJIWA NA TUME HIYO!


KINGINE CHA KUSHANGAZA NI KWAMBA WHILE KWENYE AJALI YA CHENGE,DEREVA WA BAJAJI NA MMILIKI WAKE WALIAMRIWA KUJISALIMISHA POLISI MARA MOJA,HATUJASIKIA KAULI YOYOTE KUTOKA KWA POLISI KUHUSU DEREVA WA LORI LILIOHUSIKA KWENYE AJALI YA MWAKYEMBE!


NA SASA KATIKA AJALI YA KIMARO TUNAELEZWA KUWA MAWE HAYO YALIPANGWA NA WEZI.HOW DID THE POLICE KNOW KUWA WALIOFANYA HIVYO NI WEZI NA SIO WATU WALIOKUWA WANAWINDA UHAI WA MHESHIMIWA KIMARO?KWANINI(ANGALAU KWA KUTUZUGA) ISIUNDWE TUME KAMA ILE YA AJALI YA CHENGE AMBAPO HAKUKUWA HATA HAJA YA KUFANYA SPECULATION LET ALONE KUUNDA TUME?


CALL ME A CONSPIRACY THEORIST,LAKINI NADHANI AJALI HIZI ZINA TAFSIRI KUBWA ZAIDI YA TUNACHOSIKIA AU KUONA KWA MACHO YETU.LET'S WAIT AND SEE!13 Apr 2009


Ally Sonda, Moshi

MBUNGE wa Jimbo la Vunjo(CCM) Aloyce Kimaro,amewataka mafisadi wanaojiandaa kumng'oa madarakani Rais Jakaya Kikwete na kundi la wabunge waliojitoa kafara kupinga ufisadi kuvunja mtandao wao mara moja kwa kuwa hautafanikiwa.

Akizungumza kwa kujiamini na huku akishangiliwa na umati wa watu,Kimaro alisema mwaka ujao wa uchaguzi, Rais Kikwete atashinda kwa kura nyingi sanjari na wabunge mahiri wanaomsaidia kupambana na ufisadi wakiwa ndani na nje ya Bunge.

Kimaro ambaye alikuwa akiwahutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kata ya Kahe Mashariki,alisema mafisadi wote wasiotaka Kikwete aendelee kuiongoza nchi kutokana na chuki za kuumbuliwa wataaibika zaidi mwaka ujao.

"Hivi sasa tunajua kuwa wapo mafisadi wanajipanga kuhakikisha kuwa Rais na wabunge waliojitoa mhanga kufa kwa kupinga ufisadi nikiwemo mimi tunang'oka mwaka 2010. Nasema hivi, hang'oki mtu hapa,Kikwete ni Rais hadi 2015 na sisi wabunge tutashinda vilevile, Mungu yupo mbele yetu,"alisema Kimaro.

Alisema bomu alilolilipua bungeni kuhusu uuzwaji wa nyumba za serikali ambalo limeanza kuleta mafanikio baada ya nyumba hizo kuanza kurejeshwa ni sehemu ndogo sana ya mikakati yake ya kupambana na mafisadi 'wanaoitafuna' nchi bila kunawa.Kimaro alisema ufisadi ndani ya Tanzania ni mkubwa na ndiyo sababu nchi inaendelea kuwa maskini na hivyo kujiendesha kwa kuombaomba misaada kutokana na watu wachache kuiba raslimali za taifa na kuzitorosha nje ya nchi.

Akizungumzia watu wanaolimezea mate jimbo lake na hivyo kujipanga kuwania ubunge mwakani, Kimaro alisema hana tatizo na vyama vya upinzani ambavyo vimeanza kutangaza kusimamisha wagombea, bali ugomvi wake ni kwa wanaCCM walioanza kujitangazia ubunge wa jimbo hilo hivi sasa. Aliiomba CCM wilaya ya Moshi Vijijini, kuwaonya wanachama hao kwa madai kuwa wanaleta mgawanyiko ndani ya CCM, kitendo ambacho kinaweza kutumika vibaya na kambi ya upinzani kuwasambaratisha wanaCCM.

"Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM, nakiomba Chama kiwaonye wanaCCM hawa wanaojitangazia ubunge wa Vunjo wakati wanajua kuwa mimi ndiye Mbunge halali wa Vunjo,nakuomba sana waonye la sivyo wataona cha mtema kuni,"alisema Kimaro bila kufafanua.

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Moshi,ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya wilaya hiyo,Alhaji Musa Samizi,Mwenyekiti wa CCM,Gabriel Masenga aliwataka wanaCCM wote wanaotaka ubunge wa Moshi Vijijini na Vunjo wasubiri muda muafaka ufike.

"Napenda kuwaomba wanaCCM wote wanaotaka Ubunge kwenye majimbo yetu mawili (Moshi Vijijini na Vunjo) wawe watulivu muda muafaka ufike,tutawapa fomu,tutawachuja kwa kura kama wanafaa,kujipitishapitisha hivi sasa ni kuleta vurugu ndani ya Chama na Jumuiya zake"alisema Masenga.

Masenga alitumia mkutano huo kuwataka baadhi ya wanachama wanaokikashifu Chama na viongozi wake baada ya kuadhibiwa kwa mujibu wa Katiba na hivyo kutishia kukihama CCM , waondoke mara moja na kujiunga upinzani kwa madai kuwa kuendelea kwao kuwa CCM ni sawa na kukumbatia Bomu.

"Wapo baadhi ya wanaCCM wameadhibiwa kwa kukiuka katiba ya Chama,sasa wana hasira wamekuwa wakikashifu Chama na baadhi ya viongozi,sasa kwa niaba ya Chama nawaomba waondoke CCM,huenda wakijiunga na vyama vya upinzani watafanya kazi yao vizuri ya kupambana na CCM,"alisema Masenga kwa kujiamini.
CHANZO: Mwananchi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.