6 Jul 2011

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalam wa Taifa Rashid Othman (wa tatu kushoto,mwenye shati la kitenge)
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TISS, Jack Zoka

Wabunge walipua Usalama wa Taifa  
Tuesday, 05 July 2011 21:00

Ramadhan Semtawa, Dar
WABUNGE watatu jana waliishambulia Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), bungeni baada ya kueleza kuwa imeshindwa kuzuia uhujumu uchumi na badala yake imejikita kwenye siasa za kukipendelea chama tawala, CCM na kuukandamiza upinzani.

Tuhuma hizo zinakuja wakati tayari nchi imetikiswa na matukio kadhaa ya ufisadi ikiwamo wizi wa zaidi ya Sh133 bilioni katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ununuzi wa rada ya kijeshi na ufisadi unaodaiwa kufanywa katika kampuni za Meremeta, Tangold na Deep Green Finance.

Kwa nyakati tofauti wakichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (Utumishi, Utawala Bora na Uratibu na Mahusiano ya Jamii), wabunge hao waliirushia makombora idara hiyo na kupendekeza ikajifunze nje jinsi ya kufanya kazi zake.

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ndiye alikuwa mwiba zaidi baada ya kuweka bayana kwamba idara hiyo imeshindwa kusaidiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuzuia rushwa kubwa zinazohujumu uchumi wa nchi.

Mchungaji Msigwa ambaye alizungumza kwa hisia kali, alisema idara hiyo imegeuka chombo cha kulinda maslahi ya kisiasa hasa ya CCM na kukandamiza upinzani huku ikiacha uchumi wa nchi ukiendelea kuhujumiwa.

Kwa mujibu wa Msigwa, endapo Idara ya Usalama wa Taifa, ingetumia nguvu nyingi kuzuia uhujumu uchumi kama inavyotumia kukandamiza upinzani kwa kujihusisha kwenye siasa, nchi ingeweza kupiga hatua kubwa.

Alitaka watendaji wake kwenda kujifunza majukumu yao nje ya nchi badala ya kuendelea kujihusisha na siasa kama wanavyofanya sasa.Mchungaji Msigwa alisema nchi inakabiliwa na maadui ndani na nje hivyo ni vema idara ikajikita katika kuwashughulikia hao kuliko kujiingiza zaidi kwenye siasa na kugeuka idara ya usalama ya CCM.


Takukuru na rushwa
Akizungumzia Takukuru na mapambano dhidi ya rushwa kubwa, Mchungaji Msigwa alimtaka Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Edward Hoseah, kuendeleza mapambano na kama wakubwa wakimwekea kiwingu katika utendaji wake, bora aachie ngazi.

Msigwa alifafanua kwamba, hata katika nchi za Kenya na Uganda, wakuu wa taasisi za kupambana na rushwa walipoona mambo ni magumu kutokana na wakubwa kuwadhibiti, waliamua kuachia nyadhifa zao.

Mnyika naye ashambulia usalama
Mbunge wa Ubungo John Mnyika, naye alitumia mjadala huo kuipa somo TISS akiitaka iachane na siasa za kukandamiza upinzani bali ijikite katika kulinda maslahi ya taifa.

Katibu huyo wa wabunge wote wa Chadema bungeni, alisema kazi kubwa za idara hiyo isiwe kujiingiza kwenye siasa kwa kukandamiza upinzani bali kuangalia mustakabali mzuri wa nchi.

Mnyaa: Idara imejikita Bara
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa, alisema awali Usalama wa Taifa ulikuwa ukijitegemea kwa upande wa Zanzibar na iliyokuwa Tanganyika ambayo kwa sasa inaitambulika kwa mwavuli wa Tanzania Bara.

Hata hivyo, alisema baada ya idara hiyo kuunganishwa miaka ya 1980, idara hiyo inaonekana kujikita zaidi Bara huku Zanzibar ikikosa hata ofisi kubwa ya maana kwa ajili ya operesheni.

Maji Marefu aikingia kifua
Hata hivyo, mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Stephen Ngonyani maarufu kama Profesa Majimarefu, alipinga hoja za wabunge wenzake hao, akisema hawaitendei haki kwani imekuwa ikifanya kazi kubwa kulinda usalama wa taifa.

Kwa mujibu wa Ngonyani, wakosoaji hao wa TISS wanapaswa kuwa mashuhuda kwa kwenda nchi jirani na nyingine za Afrika, ambako usalama wa taifa ni mbaya, huku zikikabiliwa na vitisho vikubwa vya mauaji na vurugu.

Akisisitiza alitoa mfano wa nchi moja (hakuitaja) ambako aliwahi kuingizwa ndani kulala wakati wa mchana kutokana na hali mbaya ya usalama katika taifa na kusisisiza, "ninyi mnaoisema Idara ya Usalama wa Taifa hebu acheni kauli zenu hizo."

"Nendeni nchi jirani au kwingine mkaangalie, mimi niliwahi kuingizwa ndani mchana kwenda kulala kutokana na hali mbaya ya usalama. Hapa kwetu Idara inafanya kazi kubwa, nchi imetulia," alizidi kuikingia kifua na kuwararua wakosoaji.

Katika kuonyesha jinsi idara hiyo inavyofanya kazi kwa ufanisi, Ngonyani alitaka Serikali kuongezea mishahara watumishi wa TISS na kuongeza, "hawa vijana tunashinda nao hapa hadi saa 4:00 usiku wanaangalia usalama halafu tunawasema hawafanyi kazi!"

"Tena nasema waongezewe mishara, vijana wanafanya kazi nzuri na kubwa ya kulinda nchi. Tunapaswa kuwapa nguvu siyo kuwalaumu siyo sahihi hata kidogo," alisisitiza Ngonyani.

Katika miaka ya karibuni hasa baada ya kuongezeka vuguvugu la vyama vingi vya siasa, TISS imekuwa ikikokosolewa na baadhi ya watu kutokana na kuacha baadhi ya misingi yake ya kulinda maslahi ya taifa ikiwamo uchumi, kama ilivyokuwa ikifanya wakati wa Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mwaka jana baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu, idara hiyo pia ilijikuta katika tuhuma za kile kilichoelezwa na Chadema kwamba, ilitumikia kuchakachua matokeo ya kura za urais, hali iliyomlazimu Naibu Mkirugenzi Mkuu Jack Zoka, kujitokeza hadharani na kufanya mkutano na waandishi wa habari kuondoa hali tete na giza lililokuwa limegubika nchi. Zoka alikanusha tuhuma hizo kwamba Idara ilihusika katika kuchakachukua matokeo ya urais.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.