Taasisi za usalama nchini Kenya zitaendelea kusuasua kuepusha umwagaji damu kama uliotokea mwezi uliopita kwenye shambulizi kwenye eneo la maduka ya Westgate, iwapo watendaji wa kada za chini wa vyombo hivyo wataendelea kuwa wanahongeka kirahisi na endapo uhasama baina ya vyombo hivyo utaendelea kuathiri ushirikiano wa kupashana habari za kiusalama.
Shambulio la kigaidi lililofanywa Septemba 21 mwaka huu na kupelekea zaidi ya vifo 67, na kudumu kwa siku kadhaa, limeishtua nchi hiyo inayojivunia wanausalama wenye uzoefu mkubwa katika kupambana na ugaidi.
Lakini wakati uchunguzi unaendelea katika eneo la tukio ili kuwatambua wahusika na mbinu walizotumia, changamoto mbalimbali kwa taifa hilo lililo mshirika muhimu wa nchi za Magharibi katika kupambana na magaidi wa Kiislam zinaanza kujitokeza.
Maafisa Usalama wa zamani na wa sasa, wanadiplomasia na wataalam wanaelezea vyombo vya usalama vinavyotumia isivyo ujuzi uliopatikana kwa msaada wa Marekani na Uingereza na wakufunzi wengine kwa vile watuhumiwa wanaweza kuhonga na kuepuka kukaguliwa na polisi, huku ushirikiano duni kati ya vymbo vya usalama ukimaanisha ni vigumu kukamilisha taarifa za kiusalama.
Pia wanaharakati wanasema kuwa vyombo vya dola vimeingizwa mno kwenye siasa za ndani ya nchi hiyo badala ya kuweka mkazo kwenye majukumu yao ya kiusalama.
Hakuna anayetarajia kuwa Kenya itaweza kuzwia kila shambulio la kigaidi, na kwa hakika wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wanazipongeza taasisi za usalama za nchi hiyo kwa kufanikiwa kuzuwia mashambulizi kadhaa kabla ya hilo la Westgate.
Lakini, kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab,ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo, kimedhirisha kuwa Somalia itaendelea kuwa kiota cha kuanzishia mashambulizi ya kigaidi kama hayo.Kenya kama jirani wa Somalia haiwezi kumudu kupuuza mapengo yanayosababishwa na mapungufu ya kitaasisi na utumishi.
"Hata kama utawekeza nguvu kiasi gani katika taasisi za usalama, ruhswa bado itaathiri malengo yako," anasema Meja Jenerali Mstaafu Charles Mwanzia, ambaye alikuwa mkuu wa idara ya usalama jeshini hadi mwaka 2005.
"Ni fundisho chungu na wito wa kuamka ili kuboresha usalama wa nchi hii katika maeneo ya kukusanya na usimamizi wa taarifa za usalama" anasema Jenerali huyo kuhusiana na shambuliz la Westgate.
Dalili za uhasama miongoni mwa vyombo vya dola vya nchi hiyo zilionekana wakati wa mapambano kati ya wanasualama na magaidi katika eneo hilo la maduka jijini Nairobi.
Afisa upelelezi mmoja, ambaye kama wengine, aliongea na Shirika la Habari la Reuters kwa masharti ya kutotajwa jina, alieleza jinsi kikosi maalum cha jeshi na polisi (General Service Unit) kilichokuwa cha kwanza kufika eneo la tukio kilivyosukumwa kando baada ya askari wa Jeshi la Ulinzi (KDF) kuwasili.
MAADUI DHIDI YA URAFIKI
Kutokuwepo ushirikiano wakati wanajeshi hao wa KDF wanaingilia kati mapambano hayo kulitoa fursa kwa magaidi kujipanga upya, na pengine hiyo ilichangia kurefusha harakati za kuwadhibiti magaidi hao (zilzodumu kwa angalau siku 4). "Maafisa wa ngazi za juu wa GSU na KDF hawakuwa na ushirikiano wa kutoa mwongozo," anaeleza afisa upelelezi huyo.
Serikali ya Kenya ilidai kuwa operesheni ya kukabiliana na magaidi hao iliendeshwa kwa ushirikiano wa vymbo mbalimbali vya dola vikifanya kazi kwa ushirikiano. KDF imejitetea kuwa jeshi la polisi ndilo lililoongoza operesheni hiyo.KDF pia imesema itachunguza tuhuma kuwa baadhi ya askari wake walishiriki kupora mali katika maduka mbalimbali ya Westgate wakati wa operesheni hiyo.
Pamoja na kukoselewa huko, wataalam wa usalama na wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walieleza kuwa chombo chochote cha usalama kingekuwa na wakati mgumu kupambana na magaidi hao wenye mafunzo na uwezo wa hali ya juu, katika eneo kubwa kama maduka ya Westgate.
Hata hivyo, wanaona mapungufu katika hatua za kujiandaa na operesheni hiyo dhidi ya magaidi. Wanasema kuwa taasisi za usalama za Kenya hufanya kazi kama maadui baina yao badala ya kushirikiana, hukataa kujumuisha taarifa za kiusalama pamoja, kiasi kwamba tetesi za matishio ya kiusalama zinaweza kutoonekana na pia dondoo zinazopatikana kwenye ufuatiliaji wa washukiwa (surveillance) zinakuwa vigumu kuunda picha ya kuwezesha kfanya maamuzi stahili.
"Ni wazuri katika wanachofanya, hususan katika ukusanyaji wa taarifa za kiusalama...lakini hawajui nini cha kufanya na wanachokipata, na jinsi ya kutengeneza picha kubwa (putting together the big picture)," alisema mtaalam mmoja wa usalama ambaye amefanya kazi na majeshi na idara za usalama za Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa.
"Nina hakika hawana mawasiliano kati yao,"alisema kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa, kitengo cha usalama wa taifa jeshini na idara za upelelezi na ushushushu za jeshi la polisi.
Wanasiasa wa Kenya na wanahabari wameeleza viokezo mbalimbali ambavyo havikuonwa mapema.Taarifa moja ya kiusalama iliyochapishwa kwenye magazeti, ambayo hata hivyo haikuweza kuthibitishwa rasmi, iliorodhesha nyendo za waliodhaniwa kuwa memba wa Al-Shabaab nchi humo, sambamba na dalili kwamba kuna uwezekano wa shambulizi la kigaidi katika maduka ya Westgate au kanisa.
Wakongwe wa usalama na wanadiplomasia wanaeleza pia kuwa taasisi za kishushushu za nchi za Magharibi nazo zilitetereka katika kuzuia shambulio hilo, kutokana na mawasiliano hafifu miongoni mwao, lakini tatizo hilo ni la dharura zaidi nchini Kenya.
Uratibu hafifu unaweza kuathiri utajiri mkubwa wa Kenya katika uwezo wake kuwafuatilia magaidi, kutoka kwenye mashushushu, majeshi yake nchini Somalia hadi vikosi vya kupambana na ugaidi, ambao hupokea misaada ya vifaa na mafunzo kutoka Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Magharibi.
Israeli pia ilitoa msaada wa mafunzo ya kiintelijensia na ilipeleka 'washauri wa usalama' wakati wa tukio la Westgate.
Lakini hata kama intelijensia ingekuwa imara, bado rushwa ingeathiri ufuatiliaji wa watuhumiwa.Kwa fedha zenye thamani ya dola mia kadhaa tu, mtuhumiwa anaweza kununua passport, kupita vikwazo vya upekuzi wa polisi (police checkpoints) pasi kupekuliwa, na kununua silaha, wanaeleza maafisa na wataalam wa usalama.
Hiyo inamaanisha hata kama kuna nyenzo za kisasa kabisa za ufuatiliaji, bado washukiwa wanaweza 'kupotea kwenye rada' na kulazimisha ufuatiliaji usiwe na faida.
KUFIKIA ENEO KUSUDIWA (TARGET)
"Kenya inakabiliwa na tatizo kubwa katika safu ya kati,kwa sababu rushwa imetawala mno kwa polisi wa nchi hiyo" anaeleza mwanadiplomasia mmoja wa nchi ya Magharibi.
"Wamekuwa na mafanikio sana kuwazuwia Al-Shabaab...lakini kitu kisichoweza kukubalika ni jinsi magaidi walivyoweza kuingia nchini na kufikia eneo kusudiwa (target)" anasema mwanadiplomasia huyo.
Hiyo inafanya vigumu kujipenyeza ndani ya vikundi vya kigaidi, jambo ambalo ni muhimu katika kuvidhibiti.
"Inahitaji polisi mmoja tu mlarushwa kuwezesha ukiukwaji mkubwa wa kiusalama, kupita mpakani isivyostahili, kwa shilingi kutumbukizwa mfukoni na mtu kufanikiwa kuvuka mpaka," anaeleza mtaalam mwingine.
Jeshi la polisi linadai linauhamasisha umma kuripoti rushwa na kuchukua hatua stahili za kinidhamu.
"Hatuwezi kusema hakuna rushwa," alikiri Msemaji wa Polisi, Gatiria Mboroki, lakini akaongeza kuwa "Ukisharipoti, tukio hilo huchunguzwa."
Afisa mmoja wa zamani wa usalama wa taifa anaeleza kuwa wakati flani alijaribu kuwathibitishia wenzake jinsi rushwa ilivyo sugu, ambapo aliweza kuwaingiza nchini humo watoa habari wake kutoka Somalia baada ya kununua passport kwa dola 300 kila moja.
"Nikwenda mbali kuthibitisha kuwa udhibiti katika mipaka yetu ni dhaifu," alisema.
Mageuzi kwa jeshi la polisi yalikuwa moja ya vipaumbele vya Katiba mpya ya Kenya ya mwaka 2010. Lakini ukiweka kando uteuzi wa maafisa waandamizi, mageuzi kwa polisi hayajaleta chochote cha maana.
"Wanasema lakini hawafanyi lolote kuhusu hicho wanachosema. Haihitaji fedha.Inahitaji mabadiliko ya mtazamo," anasema mpigania haki Maina Kiai. "Mashushushu wanapaswa kufahamu kuwa kazi yao sio ya kisiasa, ni ya kiusalama."
Kauli hiyo iliungwa mkono na afisa wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa ambaye alieleza kuwa wanausalama walivurugwa na Uchaguzi Mkuu uliopita. "Usalama wote umeelekezwa kwenye usalama wa kisiasa badala ya usalama wa taifa," alisema.
Ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliopita ulionyesha kuwa ukabila bado ulikuwa na nafasi muhimu kwa wapiga kura, suala ambalo pia linaathiri teuzi za watendaji mbalimbali katika taasisi za usalama.
Serikali imedai kuwa teuzi hufanywa kwa kuzingatia uwezo, sio asili ya mteuliwa. Msemaji wa Polisi Mboroki kuwa jeshi la polisi haliyumbishwi na wanasiasa kwani ni taasisi ya umma.
Hata hivyo, wanaharakati na wataalam wanasema hatua zaidi zinahitajika.
"Pasipo mfumo wa kuwawajibisha kwa matendo yao na kuondoa rushwa," anasema mataalam wa usalama, "hakuna chochote kitakachobadilika."
Imetafsiriwa kutoka wavuti ya Reuters