31 Oct 2014

Makala hii ilipaswa kuchapishwa katika jarida la Raia Mwema toleo la Oktoba 22, 2014 lakini kwa sababu wanazozijua wahusika pekee haikuchapishwa. Nomba kukupa fursa ya kuisoma katika uhalisi wake.

Duru za siasa za Uingereza zimevamiwa na mwanasiasa hatari lakini mahiri kwa ushawishi, ndivyo wanavyoeleza baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini hapa kufuatia kuibuka kwa kasi kwa Nigel Farage na chama chake ‘cha kibaguzi’ cha United Kingdom Independence Party (UKIP).

Pamoja na kauli zake za kukera na pengine za ubaguzi wa waziwazi, Farage ana kipaji muhimu kwa mwanasiasa: kutumia mapungufu  ya vyama vikuu – Conservatives, Labour na Liberal Democrats – kuwavuta wananchi wakiunge mkono chama chake. Na anafanikiwa kwa kiasi kikubwa, hasa baada ya chama hicho kushinda kiti cha ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la uchaguzi la Clacton huko England.

Matokeo hayo yamekipatia chama hicho mbunge wa kwanza, Douglas Carswell, ambaye alihama kutoka Conservatives hivi karibuni. Taratibu duru za kisiasa nchini hapa zinaanza kuiona UKIP kama chama makini licha ya sera zake zenye mwelekeo wa ubaguzi.

Ajenda kuu ya UKIP ni kuitaka Uingereza ijiondoe kwenye Umoja wa nchi za Ulaya (European Union). Kadhalika, chama hicho kinapinga vikali ujio wa wageni nchini hapa, huku kikidai kuwa serikali ya chama tawala (Conservatives) inayoshirikiana na Liberal Democrats, imeshindwa kama ilivyokuwa kwa serikali iliyotangulia ya Labour kutatua tatizo hilo.

Suala la uhamiaji ni moja ya turufu muhimu kila unapojiri uchaguzi katika nchi hii, na UKIP wanaitumia ajenda hiyo kwa ufanisi mkubwa. Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanatahadharisha kuwa Farage ni mtu hatari kwa sababu ya mrengo wake mkali wa kulia ambao unakaribiana na ule wa chama cha wazi cha kibaguzi cha British National Party. Baadhi ya wachambuzi wanaiona UKIP kama mchanganyiko wa Conservatives na BNP, lakini wanatambua kuwa mvuto wake unachangiwa na kuongea yale yanayowagusa wapiga kura wengi.

Laiti UKIP ikiendelea kufanya vema, na dalili zipo za kutosha, kuna uwezekano wa chama hicho kuweza kuunda serikali ya umoja na Conservatives baada ya uchaguzi mkuu ujao. Laiti hilo likitokea, ni wazi kuwa Uingereza itakuwa taifa tofauti kwa kiasi kikubwa na hilo tulilonalo hivi sasa.

Lengo la makala hii sio kumzungumzia Farage au chama chake cha UKIP bali kuangalia haja ya kuwa na ‘akina Nigel Farage wa siasa za Tanzania.’ Hapo simaanishi kuwa na wanasiasa wenye sera za kibaguzi bali wenye kutambua matatizo yanayoikabili Tanzania yetu na sio tu kuyatumia kupata sapoti bali kuyatafutia ufumbuzi. Kwa sasa hatuna mwanasiasa wa aina hiyo.

Sijui hadi muda huu ni Watanzania wangapi wanatambua kuwa tuna chini ya mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu hapo mwakani. Sintofahamu ya Bunge la Katiba na hatimaye kupatikana kwa Katiba pendekezwa kumewachanganya wananchi vya kutosha. Na katika kukoroga mambo zaidi, yayumkinika kuhitimisha kuwa ni Watanzania wachache tu wanaofahamu iwapo kutakuwa na kura ya maoni ya kupitisha au kukataa Katiba pendekezwa. Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshatamka kuwa haiwezi kuharakisha kura hiyo, japo Rais Jakaya Kikwete ameendelea kuwahakikishia Watanzania kuwa Katiba mpya itapatikana hivi karibuni.

Tupate Katiba mpya au la, mwaka mmoja kutoka sasa tutamchagua mrithi wa Rais Kikwete, awe ni kutoka CCM au chama kingine. Mazingira yalivyo hadi sasa hayatoi mwelekeo wa nani anayeweza kushika wadhifa huo muhimu kwa Tanzania yetu. Binafsi, ninaamini kuwa mrithi wa Kikwete atakuwa ‘mtu wake wa karibu,’ chaguo lake ambalo kwa mbinu za wazi na zisizo wazi atapigiwa upatu hadi kushika wadhifa huo.

Sababu ya Kikwete kuuhitaji ‘mtu wake’ ipo wazi. Vipindi vyake viwili vya utawala vimetawaliwa na mlolongo wa kashfa mbalimbali za ufisadi. Pasipo kuwa na mtu ‘wa kuaminika,’ si ajabu tukashuhudia yaliyomkumba Rais wa zamani za Zambia Frederick Chiluba. Na hata kama haistahili kwa Rais aliye madarakani kumwandama mrithi wake, mantiki ya kawaida tu inatosha kueleza kuwa hakuna mtu anayetaka kustaafu huku hajui hatma yake itakuwa vipi. Moja ya kanuni isiyo rasmi ya siasa ni hii: “kamwe usimkabidhi madaraka adui yako. Atakuangamiza hata kabla hajaizowea ofisi uliyomkabidhi.” Ni wazi Kikwete analitambua hilo.

Mengi yanaongelewa kuhusu ‘watu wa karibu na Kikwete’ lakini ni vigumu kujua ukweli. Kama kuna mwanasiasa ambaye amefanikiwa sana kuonekana kama mrithi asiye rasmi wa Kikwete ni Edward Lowassa. Lakini taarifa zinakanganya kuhusu mahusiano ya wanasiasa hao ambao walikuwa marafiki wakubwa. Kuna wanaodai urafiki wao umevurugika, lakini uzoefu wa kisiasa waonyeshe kuwa hakuna maadui (au marafiki) wa kudumu katika siasa. Kwa vile Lowassa (Akishirikiana na mwanasiasa mwingine Rostam Aziz) alimsaidia sana Kikwete kuingia madarakani, yawezekana ‘deni’ hilo likapelekea Kikwete kumsaidia Lowassa kuwa mrithi wake, hasa endapo (Lowassa) atamhakikishia Kikwete ‘usalama wake’ baada ya kustaafu.

Kuna wanaosema Bernard Membe, mwanasiasa mwingine aliye karibu na Kikwete ni miongoni mwa wanaoweza kupewa nafasi hiyo. Nilishawahi kuongelea vikwazo dhidi ya Membe lakini kwa vile ni vigumu kwa nchi ya Kiafrika kupata Rais kinyume na matakwa ya Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika, na kwa vile Membe ni shushushu mstaafu, basi hakuna lisilowezekana iwapo atapata sapoti ya kutosha kutoka kwa ‘mashushushu wenzake.’

Lipo suala la Zanzibar ambalo kwa akina sie tunaochimbachimba mambo tunaona ni kama bomu la wakati (time bomb) linalosubiri kulipuka kuhusiana na hatma ya Muungano. Sahau kuhusu Katiba pendekezwa, hatma ya Muungano itategemea uwezo wa aliyepo madarakani kulazimisha matakwa ya watawala. Na kwa minajili hiyo, naona uwezekano wa Dkt Ali Shein kupigiwa chapuo amrithi Kikwete. Na kwa vile Shein amekuwa Makamu wa Rais wa Kikwete kwa miaka 10, si vigumu kumpatia ‘bosi wake wa zamani’ uhakika wa ustaafu wake.

Kuhusu Waziri Mkuu Mizengo Pinda, binafsi ninashindwa kuelewa malengo yake kuhusu kuwania urais. Labda yawezekana ni kile kinachoitwa ‘Plan B’ yaani iwapo kila ‘mrithi mtarajiwa wa Kikwete’ akishindikana, basi Pinda anakuwa ‘mchezaji wa akiba’ wa kuokoa jahazi. Katika mazingira ya kawaida, ni miujiza tu ndiyo inayoweza kumwingiza Pinda Ikulu. Sababu ni nyingi, nitaziongelea katika makala zijazo. Hata hivyo, kama alivyo Membe, Pinda ni shushushu mstaafu, na hilo laweza kuwa turufu kwake.

Wakati takriban yote niliyoyaongelea hapo juu ni ya kufikirika zaidi kwa maana hayajiri waziwazi, mwanasiasa pekee ambaye tangu aitangaze nia yake ya kutaka urais hapo mwakani ameendelea kuwaaminisha Watanzania kuwa yupo ‘serious’ ni January Makamba. Ninaomba kukiri kwamba awali nilipomsikia January akitangaza nia hiyo nilidhani anatania. Siku kadhaa baadaye, kwa kutumia mitandao ya kijamii hasa Twitter, mwanasiasa huyo kijana amejitanabaisha kama mtu anayetaka kwa dhati kuliongoza taifa hili.

Hivi ninavyoandika makala hii, January ameanzisha utaratibu wa maswali na majibu (question and answer session) huko Twitter kwa kutumia ‘hashtag’ #askJanuary yaani ‘Muulize January.’ Japo ninatambua kuwa ni vigumu kuhitimisha ‘mafanikio’ ya mwanasiasa kwa kuangalia ‘anavyojichanganya na watu’ katika mtandao wa kijamii, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba bado Watanzania wengi si watumiaji wa mitandao ya jamii, January amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga sio tu kuaminika kuwa yupo ‘serious’ katika dhamira yake ya kutaka urais mwakani lakini pia amejiweka karibu na watu wengi wanaotumia mitandao hiyo ya kijamii.

Sasa kama Rais ajaye atatokana na kutambulika kwake kwa angalau baadhi ya wapiga kura, basi hadi muda huu January anaongoza katika hilo- pasi haja ya kufanya opinion poll. Alitangaza anataka urais, ameendelea kuwaaminisha wananchi kuwa anataka urais, anaendelea kueleza atafanya nini akiwa Rais, na kwa sie tunaoamini kuwa mitandao ya kijamii ni moja ya nyenzo muhimu kufikisha ujumbe kwa wananchi (angalau huku nchi za Magharibi), basi lolote linawezekana kwa mwanasiasa huyo kijana.

Nihitimishe makala hii kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu wa wagombea urais ambapo katika moja ya makala zijazo nitazungumzia ‘muungano wa UKAWA kumsimamisha mgombea mmoja’ nikielemea zaidi kwenye vikwazo kutoka kwa ‘nguvu za giza’, sambamba na kuwachambua wanasiasa wengine wanaotajwatajwa. Kwa mfano, kuna anayedhani Ridhiwani Kikwete anaweza kuingia katika mbio za kurithi nafasi inayoshikiliwa na baba yake hivi sasa?

Mwisho kabisa, kama tahadhari, uchambuzi wangu unaelemea zaidi katika kile tunachoita’ hali halisi mtaani,’ kufuatilia matokeo kadri yanavyojiri, upepo wa kisiasa unavyovuma, na ninajitahidi kuepuka kutumia uelewa wangu wa stadi za siasa au taaluma nyinginezo kuniongoza katika uchambuzi huu.  Kwa kifupi, ninaongozwa na hali halisi.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com  


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.