5 Jun 2015


Tunahitaji Rais mpinga ufisadi si wa kujitetea eti yeye si fisadi

HATIMAYE baada ya taarifa za muda mrefu zisizo rasmi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alitangaza mwishoni mwa wiki iliyopita dhamira yake kukiomba Cchama Cha Mapinduzi (CCM) kimpitishe kuwa mgombea wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Taarifa za Lowassa kutaka urais zimekuwa zikivuma kwa muda mrefu mno, na kwa hakika haikuwa jambo la kushangaza alipoamua majuzi kuzibadili taarifa au tetesi hizo kuwa jambo kamili.

Binafsi, baada ya kuisikia hotuba yake aliyoitoa jijini Arusha mbele ya halaiki ya wananchi nimebaki na swali moja la msingi: Lowassa ana kipi hasa cha kuwafanya Watanzania waamini kaulimbiu yake ya ‘safari ya matumaini.’
Sijui kwenu wasomaji wapendwa, lakini kwangu kubwa linalonifanya nimkumbuke Lowassa ni kashfa ya Richmond ambayo hatimaye ilisababisha ajiuzulu wadhifa wake wa Uwaziri Mkuu.

Na kwa sababu anazojua yeye mwenyewe, hotuba yake ya Arusha haikugusia suala hilo ambalo awali alipozungumza na waandishi wa habari alidai angeliongelea kwa kirefu. Tayari kuna baadhi yetu tunaoanza kuhoji uwezo wa mwanasiasa huyo kushika nafasi nyeti ya urais, na swali ni hili: kama ndani ya wiki moja anaweza kuahidi kuzungumzia kashfa ya Richmond na kisha asizungumzie, je mustakabali wa taifa letu utakuwaje mikononi mwa mtu anayeweza kuvunja ahadi anazojiwekea mwenyewe?

Pengine katika hatua hii ni muhimu nitanabaishe kuwa sina tatizo na Lowassa kutumia haki yake ya kikatiba na kidemokrasia kuwania urais. Hiyo ni haki ya kila Mtanzania mwenye sifa stahili. Lakini kwa hakika natatizwa sana na uadilifu wake.

Licha ya suala la Richmond, ambalo amedai yeye hahusiki, kuna hoja ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ‘kumwekea vikwazo’ huko nyuma katika nia yake ya urais, ambapo inaelezwa kuwa Nyerere alitatizwa na utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo usio na maelezo ya kuridhisha.

Na majuzi Lowassa katamka bayana kuwa anauchukia umasikini. Na amekiri kuwa yeye ni ‘tajiri kiasi.’ Lakini pengine Watanzania wengi wangependa sana kufahamu chanzo cha utajiri wake kwa sababu sote tunajua mtu haamki tu na kujikuta tajiri. Sawa, amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu, lakini kwa jinsi anavyomudu ‘kumwaga pesa’ katika shughuli mbalimbali, ni vigumu kuamini kuwa chanzo cha fedha hizo ni utumishi wake wa muda mrefu serikalini pekee.

Nyakati kadhaa amekuwa akitueleza kuwa kuna marafiki zake wanaomchangia fedha ‘anazomwaga’ katika hafla mbalimbali. Je, ni marafiki gani hao? Lakini kubwa zaidi, vyanzo vya utajiri wao ni vipi hasa?

Kadhalika, mwanasiasa huyo ameonekana kuzungukwa na wanasiasa wenzake kadhaa ambapo miongoni mwao ni majeruhi wa skandali mbalimbali za ufisadi. Waingereza wana msemo, nionyeshe marafiki zako, nami nitakueleza wewe ni nani’ (show me your friends and I will tell who you are). Hivi Lowassa anaweza kutueleza lolote kuhusu ukaribu alionao na watu hao?

Kwa upande mwingine, mie nilipoisikiliza kwa makini hotuba yake ya majuzi huko Arusha niliona kama ninamsikiliza mtu ambaye tayari ameshapitishwa na chama chake kugombea urais na kilichobaki ni taratibu tu za kumkabidhi wadhifa huo. Sina tatizo na kujiamini kwake lakini kuna wanaojiuliza, hivi huyu mtu asipopitishwa na chama chake itakuwaje?

Kuhusu kaulimbiu yake ya ‘safari ya matumaini,’ bahati nzuri siku moja tu baada ya kuitangaza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, akawafumbua macho Watanzania kwa kuwaeleza kuwa kinachohitajika sio safari ya matumaini bali ya uhakika. Watanzania wamekuwa wakiishi kwa matumaini kwa muda mrefu sana; matumaini kwamba siku moja nchi yao itaondokana na umasikini ilionao na kuishi kulingana na utajiri lukuki iliyojaliwa nao; matumaini ya kuondokana na janga la ufisadi linalozidi kuota mizizi; matumaini ya kuona sarafu yao ikiacha kuporomoka kwa kasi; matumaini ya mgawo wa umeme wa kudumu kufikia kikomo; matumaini ya maisha bora kwa kila Mtanzania waliyoahidiwa miaka 10 iliyopita na timu ya uchaguzi ya Rais Jakaya Kikwete ambayo ilikuwa ikiongozwa na Lowassa, na matumaini mengine kadha wa kadha

Hapana, Watanzania wanaotaka safari ya uhakika, kama alivyosema Dk. Slaa, na sio ya matumaini hewa kama yaliyoahidiwa miaka kumi iliyopita na yamebaki kuwa historia tu.

Awali, Lowassa alidai kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu ni elimu, na kuleta kaulimbiu nyingine ya elimu kwanza. Labda kabla ya yeye kuiponda kaulimbiu ya kilimo kwanza angewaambia Watanzania kwa nini imebaki kuwa porojo tu lakini hiyo yake itatekelezwa kwa vitendo.

Pengine atazungumzia uanzishwaji wa shule za kata. Tukiweka kando matatizo kadhaa yanayozikabili shule hizo, maarufu kama ‘Santa Kayumba,’ ni muhimu Watanzania wenzangu kutambua kuwa hazikujengwa kutoka hela za mfukoni mwa Lowassa. Ninaelewa kwa nini mwanasiasa huyo anaweza kutaka kujichukulia pointi kwenye suala hilo; kasumba iliyojengeka miongoni mwetu kwamba mtu akiajiriwa kutimiza wajibu fulani na analipwa kutimiza wajibu huo anaonekana mchapakazi. Yaani tumefika mahala kuwa inatarajiwa mtu akipewa majukumu atafanya ubabaishaji, Kwa hiyo yule atakayefanya kinyume cha kuwajibika, basi inakuwa kama miujiza.

Sidhani kama Lowassa ana moja la kuwaeleza wananchi kuwa hili nililifanya kwa jitihada zangu kama Edward na sio Waziri Mkuu niliyekuwa ninalipwa mshahara kutimiza wajibu huo.

Tukirejea kwenye hotuba yake, binafsi sikusikia jambo lolote geni ambalo hatulifahamu. Sote tunajua kuhusu umasikini wetu, sote tunafahamu kuhusu matatizo yote aliyoyataja katika hotuba yake. Na kwenye tatizo la foleni za magari jijini Dar es Salaam amnbazo amedai atazimaliza ndani ya miezi 12, niseme tu kuwa hiyo ni porojo.

Kwanza, kwani alipokuwa Waziri Mkuu huko nyuma tatizo hilo halikuwepo hadi hakuona haja ya kulitatua? Pili, foleni sio tatizo jijini Dar es Salaam tu bali hata kwenye majiji makubwa ya Ulaya na katika mabara mengine. Kwetu linakuwa tatizo sugu zaidi kutokana na miundombinu mibovu na idadi kubwa ya uhamiaji mijini isiyoendana na wahamiaji, sambamba na wingi wa magari yakiwemo yasiyostahili kuwepo barabarani.

Amejitahidi kutueleza matatizo ambayo kila mmoja wetu anayafahamu. Hata hivyo kama ilivyo kwa maradhi, suala sio tu tabibu kuelezea mgonjwa anakabiliwa na tatizo gani la kiafya bali kumwelekeza tiba na hatimaye kumpatia tiba husika. Wanasiasa wetu hawaishiwi umahiri wa kuyajua matatizo ya wananchi, hata kama wanasiasa hao hawajawahi kukumbana na matatizo hayo ‘ana kwa ana.’ Sawa, ili kuweza kulitatua tatizo ni lazima kujua chanzo chake, lakini haina manufaa kutaja tu matatizo tuliyonayo pasi kuyaeleza yametokana na nini au jinsi gani tunaweza kuyakabili.

Nikiri kwamba nilipata hasira kumsikia Lowassa akiwaimbia wananchi kuhusu ‘mchakamchaka wa maendeleo’ bila kuwaambia maendeleo hayo yataletwa vipi, na kwa nini miaka zaidi ya 50 tangu tupate Uhuru (na Lowassa akiwa mtendaji wa serikali katika miaka kadhaa katika hiyo) bado tunasuasua kimaendeleo.

Nimalizie makala hii kwa kurejea nilichoandika hapo awali kuwa Lowassa ana haki kikatiba kuwania urais. Hata hivyo, name kama Mtanzania pia nina haki ya kuelezea bayana kuwa mwanasiasa huyu hafai kuwa rais wetu ajaye, sababu kubwa zaidi ikiwa ni suala la ufisadi wa Richmond.

Hatuhitaji mgombea wa urais ambaye badala ya kutueleza jinsi ya kukabiliana na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili Tanzania, yaani ufisadi, anatumia muda mwingine kujitetea kuwa yeye sio fisadi.


Wito wangu kwa Watanzania wenzangu ni huu: tunastahili kilicho bora. Haiingii akilini kabisa kuamini kuwa mtu aliyelazimika kujiuzulu kwa kashfa ya ufisadi akiwa Waziri Mkuu, atakuwa kiongozi bora akishika urais. Ni muhimu kufumbua macho na masikio na kuacha kuamini hizo porojo ambazo tumekuwa tukizisikia miaka nenda rudi lakini Tanzania yetu inazidi kudidimia.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.