
Tunahitaji
Rais mpinga ufisadi si wa kujitetea eti yeye si fisadi
HATIMAYE
baada ya taarifa za muda mrefu zisizo rasmi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, alitangaza mwishoni mwa wiki iliyopita dhamira yake kukiomba Cchama
Cha Mapinduzi (CCM) kimpitishe kuwa mgombea wa kiti cha urais katika Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Taarifa
za Lowassa kutaka urais zimekuwa zikivuma kwa muda mrefu mno, na kwa hakika
haikuwa jambo la kushangaza alipoamua majuzi kuzibadili taarifa au tetesi hizo
kuwa jambo kamili.
Binafsi,
baada ya kuisikia hotuba yake aliyoitoa jijini Arusha mbele ya halaiki ya
wananchi nimebaki na swali moja la msingi: Lowassa ana kipi hasa cha kuwafanya
Watanzania waamini kaulimbiu yake ya ‘safari ya matumaini.’
Sijui
kwenu wasomaji wapendwa, lakini kwangu kubwa linalonifanya nimkumbuke Lowassa
ni kashfa ya Richmond ambayo hatimaye ilisababisha ajiuzulu wadhifa wake wa
Uwaziri Mkuu.
Na
kwa sababu anazojua yeye mwenyewe, hotuba yake ya Arusha haikugusia suala hilo ambalo
awali alipozungumza na waandishi wa habari alidai angeliongelea kwa kirefu.
Tayari kuna baadhi yetu tunaoanza kuhoji uwezo wa mwanasiasa huyo kushika
nafasi nyeti ya urais, na swali ni hili: kama ndani ya wiki moja anaweza
kuahidi kuzungumzia kashfa ya Richmond na kisha asizungumzie, je mustakabali wa
taifa letu utakuwaje mikononi mwa mtu anayeweza kuvunja ahadi anazojiwekea
mwenyewe?
Pengine
katika hatua hii ni muhimu nitanabaishe kuwa sina tatizo na Lowassa kutumia
haki yake ya kikatiba na kidemokrasia kuwania urais. Hiyo ni haki ya kila
Mtanzania mwenye sifa stahili. Lakini kwa hakika natatizwa sana na uadilifu
wake.
Licha
ya suala la Richmond, ambalo amedai yeye hahusiki, kuna hoja ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere, ‘kumwekea vikwazo’ huko nyuma katika nia yake ya urais,
ambapo inaelezwa kuwa Nyerere alitatizwa na utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo
usio na maelezo ya kuridhisha.
Na
majuzi Lowassa katamka bayana kuwa anauchukia umasikini. Na amekiri kuwa yeye
ni ‘tajiri kiasi.’ Lakini pengine Watanzania wengi wangependa sana kufahamu
chanzo cha utajiri wake kwa sababu sote tunajua mtu haamki tu na kujikuta
tajiri. Sawa, amekuwa mtumishi wa umma kwa muda mrefu, lakini kwa jinsi
anavyomudu ‘kumwaga pesa’ katika shughuli mbalimbali, ni vigumu kuamini kuwa
chanzo cha fedha hizo ni utumishi wake wa muda mrefu serikalini pekee.
Nyakati
kadhaa amekuwa akitueleza kuwa kuna marafiki zake wanaomchangia fedha
‘anazomwaga’ katika hafla mbalimbali. Je, ni marafiki gani hao? Lakini kubwa
zaidi, vyanzo vya utajiri wao ni vipi hasa?
Kadhalika,
mwanasiasa huyo ameonekana kuzungukwa na wanasiasa wenzake kadhaa ambapo
miongoni mwao ni majeruhi wa skandali mbalimbali za ufisadi. Waingereza wana
msemo, nionyeshe marafiki zako, nami nitakueleza wewe ni nani’ (show me your
friends and I will tell who you are). Hivi Lowassa anaweza kutueleza lolote
kuhusu ukaribu alionao na watu hao?
Kwa
upande mwingine, mie nilipoisikiliza kwa makini hotuba yake ya majuzi huko
Arusha niliona kama ninamsikiliza mtu ambaye tayari ameshapitishwa na chama
chake kugombea urais na kilichobaki ni taratibu tu za kumkabidhi wadhifa huo.
Sina tatizo na kujiamini kwake lakini kuna wanaojiuliza, hivi huyu mtu
asipopitishwa na chama chake itakuwaje?
Kuhusu
kaulimbiu yake ya ‘safari ya matumaini,’ bahati nzuri siku moja tu baada ya
kuitangaza, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willbroad Slaa, akawafumbua macho Watanzania kwa kuwaeleza kuwa kinachohitajika
sio safari ya matumaini bali ya uhakika. Watanzania wamekuwa wakiishi kwa
matumaini kwa muda mrefu sana; matumaini kwamba siku moja nchi yao itaondokana
na umasikini ilionao na kuishi kulingana na utajiri lukuki iliyojaliwa nao;
matumaini ya kuondokana na janga la ufisadi linalozidi kuota mizizi; matumaini
ya kuona sarafu yao ikiacha kuporomoka kwa kasi; matumaini ya mgawo wa umeme wa
kudumu kufikia kikomo; matumaini ya maisha bora kwa kila Mtanzania
waliyoahidiwa miaka 10 iliyopita na timu ya uchaguzi ya Rais Jakaya Kikwete
ambayo ilikuwa ikiongozwa na Lowassa, na matumaini mengine kadha wa kadha
Hapana,
Watanzania wanaotaka safari ya uhakika, kama alivyosema Dk. Slaa, na sio ya
matumaini hewa kama yaliyoahidiwa miaka kumi iliyopita na yamebaki kuwa
historia tu.
Awali,
Lowassa alidai kuwa moja ya vipaumbele vyake vikuu ni elimu, na kuleta
kaulimbiu nyingine ya elimu kwanza. Labda kabla ya yeye kuiponda kaulimbiu ya
kilimo kwanza angewaambia Watanzania kwa nini imebaki kuwa porojo tu lakini
hiyo yake itatekelezwa kwa vitendo.
Pengine
atazungumzia uanzishwaji wa shule za kata. Tukiweka kando matatizo kadhaa
yanayozikabili shule hizo, maarufu kama ‘Santa Kayumba,’ ni muhimu Watanzania
wenzangu kutambua kuwa hazikujengwa kutoka hela za mfukoni mwa Lowassa.
Ninaelewa kwa nini mwanasiasa huyo anaweza kutaka kujichukulia pointi kwenye
suala hilo; kasumba iliyojengeka miongoni mwetu kwamba mtu akiajiriwa kutimiza
wajibu fulani na analipwa kutimiza wajibu huo anaonekana mchapakazi. Yaani
tumefika mahala kuwa inatarajiwa mtu akipewa majukumu atafanya ubabaishaji, Kwa
hiyo yule atakayefanya kinyume cha kuwajibika, basi inakuwa kama miujiza.
Sidhani
kama Lowassa ana moja la kuwaeleza wananchi kuwa hili nililifanya kwa jitihada
zangu kama Edward na sio Waziri Mkuu niliyekuwa ninalipwa mshahara kutimiza
wajibu huo.
Tukirejea
kwenye hotuba yake, binafsi sikusikia jambo lolote geni ambalo hatulifahamu.
Sote tunajua kuhusu umasikini wetu, sote tunafahamu kuhusu matatizo yote
aliyoyataja katika hotuba yake. Na kwenye tatizo la foleni za magari jijini Dar
es Salaam amnbazo amedai atazimaliza ndani ya miezi 12, niseme tu kuwa hiyo ni
porojo.
Kwanza,
kwani alipokuwa Waziri Mkuu huko nyuma tatizo hilo halikuwepo hadi hakuona haja
ya kulitatua? Pili, foleni sio tatizo jijini Dar es Salaam tu bali hata kwenye
majiji makubwa ya Ulaya na katika mabara mengine. Kwetu linakuwa tatizo sugu
zaidi kutokana na miundombinu mibovu na idadi kubwa ya uhamiaji mijini
isiyoendana na wahamiaji, sambamba na wingi wa magari yakiwemo yasiyostahili
kuwepo barabarani.
Amejitahidi
kutueleza matatizo ambayo kila mmoja wetu anayafahamu. Hata hivyo kama ilivyo
kwa maradhi, suala sio tu tabibu kuelezea mgonjwa anakabiliwa na tatizo gani la
kiafya bali kumwelekeza tiba na hatimaye kumpatia tiba husika. Wanasiasa wetu
hawaishiwi umahiri wa kuyajua matatizo ya wananchi, hata kama wanasiasa hao
hawajawahi kukumbana na matatizo hayo ‘ana kwa ana.’ Sawa, ili kuweza kulitatua
tatizo ni lazima kujua chanzo chake, lakini haina manufaa kutaja tu matatizo
tuliyonayo pasi kuyaeleza yametokana na nini au jinsi gani tunaweza kuyakabili.
Nikiri
kwamba nilipata hasira kumsikia Lowassa akiwaimbia wananchi kuhusu
‘mchakamchaka wa maendeleo’ bila kuwaambia maendeleo hayo yataletwa vipi, na
kwa nini miaka zaidi ya 50 tangu tupate Uhuru (na Lowassa akiwa mtendaji wa
serikali katika miaka kadhaa katika hiyo) bado tunasuasua kimaendeleo.
Nimalizie
makala hii kwa kurejea nilichoandika hapo awali kuwa Lowassa ana haki kikatiba
kuwania urais. Hata hivyo, name kama Mtanzania pia nina haki ya kuelezea bayana
kuwa mwanasiasa huyu hafai kuwa rais wetu ajaye, sababu kubwa zaidi ikiwa ni
suala la ufisadi wa Richmond.
Hatuhitaji
mgombea wa urais ambaye badala ya kutueleza jinsi ya kukabiliana na moja ya
matatizo makubwa kabisa yanayoikabili Tanzania, yaani ufisadi, anatumia muda
mwingine kujitetea kuwa yeye sio fisadi.
Wito
wangu kwa Watanzania wenzangu ni huu: tunastahili kilicho bora. Haiingii
akilini kabisa kuamini kuwa mtu aliyelazimika kujiuzulu kwa kashfa ya ufisadi
akiwa Waziri Mkuu, atakuwa kiongozi bora akishika urais. Ni muhimu kufumbua
macho na masikio na kuacha kuamini hizo porojo ambazo tumekuwa tukizisikia
miaka nenda rudi lakini Tanzania yetu inazidi kudidimia.
0 comments:
Post a Comment