6 Aug 2015

NINAANDIKA makala hii nikiwa na masikitiko makubwa mno. Siku zote maishani, twajikuta katika kipindi kigumu sana pale mtu tuliyemwamini kwa dhati anapotugeuka. Wanasema, inachukua muda mwingi na jitihada kubwa kujenga uaminifu japo kosa au tukio moja tu laweza kuondoa kabisa uaminifu huo.
Na hicho ndicho walichofanya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kukubali kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowaasa, sio tu kuwa mwanachama wao bali pia mgombea wao katika nafasi ya urais.
Kama ambavyo tetesi kuwa Lowassa angechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya CCM zilivyozagaa kwa muda mrefu, ndivyo suala la Lowassa kujiunga na Chadema/ UKAWA lilivyokuwa.
Mara baada ya mwanasiasa huyo kukatwa katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake wa Urais, zilisikika tetesi nyingi kuwa kuna uwezekano angejiunga na moja ya vyama vinavyounda UKAWA, na hatimaye kuwa mgombea urais.
Lakini kwa vile Tanzania yetu haina uhaba wa tetesi, baadhi yetu tulidhani kuna ugumu kwa Lowassa kujiunga na UKAWA ni Chadema, kwa vile chama hicho kimejijengea umaarufu mkubwa kwa msimamo wake tuliodhani ni thabiti kupambana na ufisadi na mafisadi.
Na sio msimamo tu dhidi ya ufisadi na mafisadi, Chadema wamelipa gharama kubwa katika harakati zake ambapo baadhi ya wanachama wake walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya, huku wengine wakiishia rumande au magerezani kufuatia maandamano mbalimbali ya kutetea maslahi ya taifa na wanyonge.
Hata nilipoona picha zilizodaiwa kuwa ni za Lowassa akihudhuria moja ya vikao vya UKAWA nilijipa moyo kuwa huenda picha hizo zimefanyiwa ‘ufundi,’ wenyewe wanaita ‘photoshop,’ ambapo picha ya mtu inapandikizwa kwenye picha nyingine.
Faraja iliongezeka baada ya akaunti ya habari za Chadema katika mtandao wa Twitter, Chadema Media, kukanusha uwepo wa Lowassa katika kikao hicho. Hata hivyo muda mfupi baadaye, watu wa karibu na Lowassa walibandika picha zaidi katika mtandao huo kuthibitisha kuwa kweli Lowassa alihudhuria kikao hicho.
Na siku moja baadaye,’bomu lililipuka.’ Kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ambayo sie tulio mbali tuliweza kuyaona mtandaoni, viongozi wakuu wa UKAWA walionekana na Lowassa, na baadaye mwanasiasa huyo kutangaza bayana kuwa amejiunga na umoja huo kupitia Chadema.
Ninachoweza kusema kwa kifupi ni kwamba walichofanya Chadema ni usaliti wa hali ya juu, na hakuna maelezo ya aina yoyote yanayoweza kuhalalisha kitendo hicho. Ndio, ni muhimu kwao kuingia Ikulu, lakini ni muhimu zaidi kwa Chadema kutambua imefikaje ilipo leo.
Jibu la wazi ni kama nilivyotanabaisha hapo juu; msimamo wao imara wa kuuchukia ufisadi na kupambana nao kwa nguvu zote, hatimaye ulifanikiwa kuwafumbua macho Watanzania wengi, sio tu kuhusu kansa ya ufisadi bali pia kujenga hisia kwamba chama hicho ni kwa ajili ya maslahi ya mamilioni ya Watanzania wanyonge na wahanga wakuu wa ufisadi.

Kwahiyo, kwa kumpokea Lowassa, mwanasiasa aliyelazimika kujiuzulu kwa tuhuma za ufisadi wa Richmond, Chadema wametelekeza nguzo muhimu iliyokuwa ikikitambulisha chama hicho. Na kama tunavyoina CCM, chama chochote cha siasa kinachotelekeza nguzo zake, sio tu kinapoteza uaminifu wake kwa jamii bali pia chajichimbia kaburi.
Sawa, labda Lowassa anaweza kushinda urais (hili lahitaji mjadala wa pepe yake) lakini haihitaji kuwa na ujuzi wa uchambuzi wa siasa zetu kubaini kwamba mwanasiasa huyo hakujiunga na Chadema kwa vile anakipenda chama hicho au anaafiki sera zao bali amekitumia kama ngazi ya kuwania urais baada ya kukwamishwa na CCM.
Hilo tu lilipaswa kuifumbua macho Chadema. Lowassa huyohuyo aliyejigamba kwamba jina lake halitakatwa akijivunia ‘uchapakazi’ wake, na utumishi wake wa muda mrefu katika CCM, leo hii kaitelekeza CCM licha ya kudai asiyemtaka ndani ya chama hicho aondoke lakini yeye si wa kuondoka.
Ni wazi kuwa Lowassa ni mwanasiasa mwenye tamaa ya madaraka. Sawa, Katiba yetu yamruhusu kugombea uaongozi kupitia chama chochote kile, lakini moja ya sifa nzuri kwa mwanasiasa ni msimamo na kutokuwa na tamaa ya madaraka.
Leo kaitosa CCM kwa kutaka urais, je ataitendaje Chadema katika kutaka mengineyo?
Lakini pia ni ukweli usiofichika kuwa umaarufu wa Lowassa unatokana na ‘sifa’ kuu mbili: uwezo mkubwa wa kifedha ‘zisizo na maelezo ya kutosha’ na skandali ya Richmond. Katika mazingira ya kawaida, na hasa katika zama hizi za ufisadi, ni vigumu mno kumnadi mwanasiasa wa aina hiyo.

Tayari kuna hisia kuwa ‘fedha zilibadilishana mikono’ hadi akina Freeman Mbowe kukubali kumpokea mwanasiasa huyo ambaye walikuwa wakimwandama kila kukicha kwa kumuita fisadi.
Kama ni fedha kweli au ‘umaarufu,’ tayari Lowassa ndio mnufaika maana kwa muda mfupi tu ndani ya chama hicho, mambo kadhaa yameshabadilika.
Mie nazifuatilia kwa karibu zaidi harakati za Chadema kupitia mitandao ya kijamii au tovuti za vyombo vya habari mbalimbali vya huko nyumbani. Nilichobaini katika siku chache hizi baada ya Lowasaa kujiunga na Chadema, ghafla wanachama na mashabiki wa chama hicho wamegeuka ‘mabubu’ kuhusu masuala ya ufisadi.
Na hilo si la kushangaza kwa sababu watamudu vipi kukemea ufisadi ilhali mgombea wao wa urais ni mtuhumiwa wa ufisadi?
Kwa mujibu wa maelezo ya mmoja wa viongozi wa Chadema, Tundu Lissu, chama hicho na UKAWA kwa ujumla walikuwa wakifuatilia kwa karibu mchakato wa CCM kupata mgombea wake, na wao walitaka kuitumia ‘sintofahamu’ hiyo ndani ya CCM kufanikisha malengo yao ya kuingia Ikulu.
Huu ni udhaifu wa hali ya juu. Lakini angalau hii imesaidia kutufahamisha kwanini chama hicho kilikuwa kinasuasua kumtangaza mgombea wake: kilikuwa kinasubiri ‘makombo’ ya CCM.
Watu hawa wanajifanya kusahau kabisa mafanikio makubwa tu waliyoyapata katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo walisimama wenyewe, wakapata wabunge wa kutosha na madiwani wa kutosha tu, licha ya mgombea wao, Dkt Willbrord Slaa, kushindwa katika mazingira ambayo baadhi yetu tunaamini yalichangiwa na hujuma.
Na ni katika mazingira hayo, baadhi yetu tunaunga mkono Dk. Slaa kujitenga na Chadema. Ni matarajio yangu kuwa hatokubali kuwa sehemu ya usaliti huu hasa kwa kuzingatia gharama kubwa waliyoingia Chadema, kwa maana ya muda na jitihada, sio tu kukitambulisha chama hicho kuwa ni mtetezi wa wanyonge na kiongozi wa mapambano dhidi ya ufisadi bali pia kukiwezesha kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania.
Awali, nilipopata uthibitisho kuwa Lowassa amejiunga na Chadema nilitamka bayana kuwa ‘impact’ ya tukio hilo yapaswa kuonekana angalau ndani ya siku 7. Na siku hizo saba zimeisha juzi. Tuliambiwa tusubiri ‘mafuriko’ ya wana-CCM kumfuata Lowasaa huko Chadema/UKAWA.
Hadi sasa, hakuna dalili yoyote ya mafuriko hayo. Jina kubwa pekee lililojitokeza kumfuata Lowassa ni Naibu wa Kazi na Ajira, Dkt Makongoro Mahanga, ambaye hata hivyo amechukua uamuzi huo baada ya kubwagwa kwenye kura za maoni. Labda kuna wengine watakaomfuata Lowassa lakini sidhani kama watu hao watakuwa na mafuriko yanayotarajiwa.
Kikwazo kikubwa kwa makada wa CCM waliokuwa wakimsapoti mwanasiasa huyo kumfuata kwenye ‘chama chake kipya’ ni ukweli kwamba tayari vyama vinavyounda UKAWA vilishagawana majimbo.
Sasa sidhani kama kuna mwana-CCM mwenye akili zake atakikimbia chama hicho tawala na kujiunga na vyama vinavyounda UKAWA ilhali anatambua kuwa hata akishindwa ubunge au udiwani katika CCM bado ana fursa ya kuteuliwa kwenye nyadhifa nyingine serikalini.
Na ujio wa wafuasi wa Lowassa ndani ya Chadema na UKAWA unaweza kuvibadili vyama hivyo na kuunda makundi ya, kwa mfano, Chadema- asilia na Chadema-Lowassa. Busara za kisiasa zatuonya kuwa chama chenye mgawanyiko hakiwezi kushinda uchaguzi, na hata kikifanikiwa kushinda, hakitoweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wakati kwa kumpokea Lowassa Chadema italazimika kutowekeza nguvu za kutosha katika mtaji wake mkuu katika uchaguzi mkuu uliopita – vita dhidi ya ufisadi (hawawezi kupigia kelele ufisadi huko mgombea wao akiwa mtuhumiwa wa ufisadi) – ni vigumu kubashiri watamnadi Lowassa kwa lipi hasa.
Wao ndio walikuwa vinara wa kumwita Lowassa fisadi, sasa muda haupo upande wao kubadilisha maelezo na kumnadi kama mtu safi.
Na hata maelezo ya Lowassa kuwa ‘alipata maagizo ya juu’ katika suala la Richmond hayana uzito kwa sababu kwanini aongee sasa na si wakati alipobanwa hadi kujiuzulu? Sawa, wengi twafahamu kuwa skandali hiyo iliwahusisha watu wengine pia, lakini ukweli unakuwa na nguvu pale tu unapowekwa hadharani wakati mwafaka.
Ni rahisi kwa CCM kuipangua hoja ya Lowaasa kuwa ‘alitumwa’ kwa kumuuliza ‘ulikuwa wapi siku zote hizi usiyaseme hayo hadi sasa ulipoamua kuingia upinzani kwa tamaa yako ya madaraka?’
Nimalizie makala hii endelevu kwa kurejea kuwakumbusha Chadema kuwa dhambi yao ya usaliti itawaandama milele. Hoja kuwa Lowassa ‘anauzika’ na atawasaidia kuingia Ikulu sio tu haina msingi bali pia yaweza kuwagharimu huko mbeleni hasa kwa vile, kama nilivyoandika hapo juu, mwanasiasa huyo hajajiunga na chama hicho kwa vile anakipenda bali kwa ajili ya maslahi yake binafsi.
Nachungulia kidogo tu ‘marafiki zake’ kisha utaelewa nini kinaisuburi Chadema huko mbeleni. Mie si nabii wa majanga (prophet of doom) lakini ninabashiri kuwa ujio wa Lowassa huko Chadema ni mwanzo wa mwisho wa chama hicho.
Inasikitisha kuona ‘People’s Power’ (nguvu ya watu) iliyowavutia wapenda mabadiliko wengi ikiishia kuwa ‘Money’s Power’ (kwa maana ya nguvu ya Lowassa kifedha).Pia inaumiza kuona demokrasia yetu ikipitia mlolongo huu usiopendeza wa ‘chama kimoja→ vyama vingi → chama cha mtu mmoja’ (one party→multiparty→one man’s party)
ITAENDELEA

1 comment:

  1. Kuna kitu kinachoitwa utawala wa sharia. Kuna kitu kinachoitwa haki za binadamu. Tangazo la kimataifa la haki za binadamu linasema wazi kuwa mtu yeyote anayetuhumiwa kuwa amefanya uhalifu anastahili kuhesabiwa kuwa hana kosa hadi mahakama ithibitishe vinginevyo. Na ndivyo ilivyo kwa Lowassa, kwako mwandishi wa makala hii, kwangu, na kwa kila mtu. Tuna haki ambazo sherti ziheshimiwe.

    Unafanya kosa kubwa na la wazi kwa kumtajataja Lowassa kama fisadi kama vile imethibitishwa mahakamani. Unafuata njia ya majungu ambayo yamezagaa mitaani, badala ya kuonyesha njia ya haki. Unakiuka maadili ya uandishi utakiwao. Nategemea utajirekebisha.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.