13 Aug 2015

MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika gazeti hili katika toleo la wiki iliyopita. Katika makala hiyo nilijadili kwa kirefu kuhusu kile nilichokiyumkinisha kuwa usaliti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), si tu kumpokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa (aliyelazimika kujiuzulu Uwaziri Mkuu kufuatia skandali ya ufisadi wa Richmond), bali pia kumteua kuwa mgombea wake urais kupitia UKAWA.
Kadhalika, pamoja na mambo mengine, nilieleza kusikitishwa kwangu na kile nilichokitafsiri kama mwelekeo wa siasa za Tanzania yetu kutoka mfumo wa awali wa chama kimoja hatimaye vyama vingi na hiki tunachoshuhudia baada ya Lowassa kujiunga na Chadema, ninachokiita ‘chama cha mtu mmoja.’
Katika makala hii nitajadili nafasi za kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao kwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt John Magufuli, na huyo wa Chadema/UKAWA, yaani Lowassa, sambamba na vikwazo vinavyowakabili kila mmoja wao.
Nianze na Magufuli. Kwa kada huyo, binafsi ninaona kuwa ana nafasi nzuri ya kushinda hasa kwa sababu, kama alivyotamka Rais Jakaya Kikwete hivi majuzi, CCM ina uwezo na nyenzo kumwezesha mgombea wao kufanya vizuri. Vyote viwili – uwezo na nyenzo – vimeshathibitika kuwa na ufanisi mkubwa katika chaguzi zilizopita.
Na vyote viwili vipo katika pande mbili; halali na isivyo halali. Uwezo halali wa CCM unatokana zaidi na mitandao wake mpana hasa vijijini. Kwa bahati mbaya au makusudi, licha ya maeneo mengi ya vijijini katika nchi yetu kukabiliwa na umasikini mkubwa, pia yana uhaba wa ‘wasomi,’ huku wachache waliopo wakiwa aidha wamekumbatiwa na ‘mfumo unaoilinda CCM’ au wameukumbatia kwa minajili ya kulinda nafasi zao.
Ninaposema ‘wasomi’ simaanishi maprofesa au watu wenye elimu ya juu bali hata wale wenye elimu ya wastani tu ambao ni muhimu sana katika kuhamasisha na kuleta mabadiliko katika nyanja mbalimbali.
Katika mazingira ya kawaida, mtumishi wa umma kijijini anaweza kuwa na chaguo rahisi ‘kuitumikia CCM’ badala ya chama cha upinzani kwa vile hasa kwa vile katika maeneo mengi ya vijijini, ni vigumu kuitofautisha CCM na serikali.
Kuna tatizo la ziada kuhusu ‘wasomi’ wetu. Wakati katika stadi za matabaka, wasomi wanatarajiwa kuwa sio tu kiungo katika ya tabaka la walalahoi na tabaka tawala, wasomi wetu wengi sio tu hawamtaki kujihusisha na tabaka la walahoi bali pia wanajibidiisha – hata kwa kuiga tu – kuwa sehemu ya tabaka tawala. Na Wasomi wachache tulionao vijijini wanaotaka waonekane kama ‘vigogo’ au ‘vingunge’ badala ya wananchi wa kawaida au walalahoi. CCM inatambua udhaifu huu na kutumia ipasavyo.
Ikumbukwe pia kuwa wengi wa ‘wasomi’ hao ndio watumishi muhimu katika shughuli nzima ya uchaguzi, na yayumkinika kuamini kuwa wamekuwa na ‘msaada’ mkubwa kwa CCM katika chaguzi zilizopita, na wanaweza kuendelea kuwa nyenzo muhimu kwa chama hicho tawala.
Lakini pengine kubwa zaidi ni turufu ya CCM hasa katika maeneo ya vijijini kuwa ‘inaweza kuonyesha jinsi ilivyowatumikia wananchi’ tofauti na ‘vyama vya upinzani vinavyokuja kufanya majaribio ya kuongoza nchi.’ Ni hoja isiyo na msingi kwa wenye uelewa wa kuchanganua mambo, lakini kwa huko vijijini, kuipinga kwahitaji kazi kubwa na sio takriban miezi mawili iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu.

CCM inabaki kuwa ‘zimwi likujualo’ ilhali kwa vyama vya upinzani, tegemeo lao kubwa ni kuonyesha mapungufu ya chama hicho tawala, na kutegemea wananchi watawaelewa na kuwaamini, na ‘kucheza bahati nasibu’ ya kuwakabidhi madaraka.
Ukichanganya na ukweli usio rasmi kuwa CCM ni mnufaika mkubwa wa uhusiano wake na taasisi za serikali – Tume ya Uchaguzi, vyombo vya dola, nk – chama hicho tawala kitaingia katika uchaguzi kikiwa na nyenzo na uwezo wa kushindwa hata kama ni kwa tabu.
Kwa kifupi, mazingira yaliyoiwezesha CCM kushindwa chaguzi kuu zilizopita bado yapo na mfumo wa uchaguzi bado unakitengenezea chama hicho tawala nafasi ya kufanya vizuri.
Hata hivyo, ili Magufuli ashinde, inategemea zaidi mshikamano ndani ya CCM. Na nikiongelea mshikamano simaanishi matukio yanayoanza kujitokeza ya makundi ya wana-CCM kadhaa kuhama chama hicho na kujiunga na vyama vya upinzani. Ninamaanisha wanasiasa wenye nguvu na ushawishi katika chama hicho kumuunga mkono mgombea wa chama chao au kumsaliti.

Lakini tangu Lowassa ajiunga na Chadema/UKAWA, sijaona kile kilichotarajiwa kuwa ‘mafuriko’ ya viongozi muhimu wa CCM na maelfu ya wanachama kukiasi chama hicho tawala na kujiunga na wapinzani. Kwahiyo, yayumkinika kuhisi kuwa hadi muda huu Magufuli bado ana sapoti ya kutosha ndani ya chama chake.
Kanuni isiyo rasmi ya siasa za uchaguzi Barani Afrika ni kwamba ‘chama tawala hakishindwi uchaguzi, na kikishindwa basi si kwa sababu wapinzani wana nguvu kubwa bali migongano ndani ya chama tawala inayotoa fursa kwa wapinzani.’ Sawa, labda CCM kumkata jina la Lowassa wakati wa mchujo wa wagombea wake kumesababisha mpasuko wa aina flani, lakini kama nilivyobainisha hapo juu, mpasuko huo sio mkubwa kama ilivyotarajiwa, na sidhani kama unaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM.
Kwahiyo, kwa upande wa Magufuli, takriban mazingira yote yaliyowawezewezesha wagombea wenzake wa nafasi ya urais huko nyuma kufanya vizuri bado yapo ilhali vikwazo dhidi ya yeye kufanya vizuri ni hafifu, na pengine vya kufikirika zaidi kuliko uhalisia.
Twende kwa Lowassa. Mtaji mkubwa wa mwanasiasa huyo ni umaarufu wake. Iwapo umaarufu huo unachangiwa na kinachoelezwa kuwa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha au ‘uchapakazi’ wake, hilo ni suala linalohitaji mjadala katika makala tofauti. Lakini kilicho bayana ni ukweli kwamba umaarufu ni turufu muhimu kwa mgombea yeyote yule katika uchaguzi.

Turufu nyingine kwa Lowassa ni hali halisi ilivyo katika mahusiano kati ya CCM na Watanzania wengi. Kwa muda mrefu chama hicho tawala kimekuwa kikichukulia chaguzi mbalimbali, kuu na ndogo, kama utaratibu tu wa kukipatia nafasi za uongozi. Hakijawahi kupigania ‘kufa na kupona’ kubaki madarakani. Kwa sababu nilizozitoa hapo juu, ukichanganya na udhaifu wa wapinzani wake, bila kusahau hujuma mbalimbali dhidi yao, tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, chama hicho tawala kimekuwa kikiingia kwenye chaguzi kikiwa na uhakika mkubwa wa kushindwa.
Hata hivyo, safari hii kinaweza kukumbana na ushindani mkubwa (japo hadi muda huu ni suala la kufikirika zaidi) baada ya kada wake maarufu kabisa, Lowassa, kujiunga na wapinzani. Sasa kwa vile CCM haijawahi na haijazowea kuwa katika mazingira yaliyopo sasa, yayumkinika kuhisi kuwa inaweza ‘kupaniki’ na hivyo kutoa mwanya kwa Lowassa na Chadema/UKAWA yake kufanya vizuri.
Lowassa na Chadema/UKAWA wanatambua bayana kuwa kuna mamilioni ya Watanzania waliokwishaichoka CCM na pengine wangependa kuoina iking’oka madarakani. Ni rahisi kwa wapinzani hao kubainisha ‘maovu’ ya chama hicho tawala kwa sababu mengi yanaonekana waziwazi. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa kuna ‘mazuri’ kadhaa ya utawala wa CCM, na uzoefuwaonyesha kuwa chama hicho tawala ni mahiri katika kuyanadi ‘mazuri’ hayo, ambayo pia si vigumu kuyaona.
Kikwazo kwa Chadema/UKAWA ni jinsi ya kubadili maelezo waliyoyasimamia kwa muda mrefu kuwa ‘Lowassa ni fisadi.’ Kwa mitizamo wangu, muda uliosalia haitoshi kwa vyama hivyo vinavyounda UKAWA kuwashawishi Watanzania kuwa ‘Lowassa sasa si fisadi kwa vile amejiunga nasi tuliokuwa tunapambana na ufisadi.’ Na kwa bahati mbaya, hasa kwa Chadema ambayo ilikuwa mahiri kukemea ufisadi, Watanzania wengi tu wanaonekana kutafsiri Lowassa kukubaliwa kujiunga na chama hicho ni usaliti kwa wengi waliokiamini.
Hoja kwamba ili ukiondoa CCM kuna haja ya kushirikiana na watu kama Lowassa inakabiliwa na hoja mbadala kuwa ‘kwanini tuwaamini watu msio na uwezo wa kuleta mabadiliko wenyewe hadi mtegemee makapi ya CCM?’ Hoja hiyo mbadala inapewa nguvu na ukweli kuwa UKAWA ‘walisuasua’ kwa muda mrefu kutangaza mgombea wao, na sasa twajua kuwa walikuwa wanamsubiri mwana-CCM kama Lowassa awasaidie.
Lakini mtihani mwingine kwa UKAWA na Lowassa ni huu: Magufuli anagombea urais kwa tiketi ya CCM, ambayo sio tu ni chama tawala na ambacho kipo madarakani hata kabla ya ujio wa mfumo wa vyama vingi, lakini pia kinafahamika kwa wengi. Kwa UKAWA, na hili ni kosa lao kwa kuchelewa kupata mgombea wao wa kiti cha urais, inaonekana kama ni chama ‘kipya’ cha siasa. Laiti muungano huo wa vyama vinne vya siasa (Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD) ungepata mgombea wake mapema, na kumnadi kwa nguvu wakati CCM inahangaika kupata mgombea wake, basi muda huu wangekuwa na kazi moja tu ya kupambana na Magufuli na CCM kwani wao tayari wangeshakuwa wanajulikana kwa wengi.
Vilevile, kuna suala nililozungumzia katika makala iliyopita ambapo, dalili zilizopo zinaashiria uchaguzi wa rais ni katika ya CCM na Magufuli wake dhidi ya Lowassa. Hapa ninamaanisha kwamba ni rahisi kumwona mgombea huyo wa CCM kama anayewakilisha chama chake ilhali kwa Lowassa ni kama ‘mgombea binafsi.’ Utafiti kidogo tu katika vyombo vya habari waweza kukuonyesha msomaji kuwa wakati ‘kampeni’ za CCM zimeelemea zaidi katika kumnadi Magufuli na CCM, kwa Chadema/UKAWA ni suala la kumnadi Lowassa pekee kana kwamba ni mgombea binafsi.
Na hilo linachangiwa na ukweli kuwa UKAWA si chama bali ushirikiano wa vyma ambavyo awali lengo lao lilikuwa suala la mabadiliko ya Katiba. Vyama hivyo vina sera tofauti, na japo vyawezxa kutengeneza ilani moja ya uchaguzi, muda hauko upande wao. Kwa CCM, ni mwendelezo tu wa walichokifanya mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010.
Kadhalika, wakati nimetaja kuwa umaarufu wa Lowassa ni mtaji wake mkubwa huko Chadema/UKAWA, pengine ni mapema mno kuhitimisha kuwa umaarufu huo alioupata akiwa CCM, utaendelea kuwa juu wakati huu amejiunga na Chadema/UKAWA. Ikumbukwe kuwa wapinzani wakubwa wa Lowassa alipokuwa CCM hawakuwa ndani ya CCM bali katika vyama hivyohivyo ambavyo leo vimemfanya mgombea wao wa urais. Hilo laweza kuirahisishia CCM jukumu la kumbomoa kwani ‘wanamjua vilivyo.’
Kikwazo kikubwa lakini kisicho wazi ni nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika uchaguzi huo, kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita. Hata tukiweka kando kile kwenye Baiolojia wanakiita ‘symbiotic relationship’ (uhusiano wa kutegemeana kati ya kiumbe kimoja na kingine) ambapo ustawi wa taasisi hiyo na wa CCM na serikali zake ni wa kutegemeana, Idara hiyo yaweza kutumia ‘kisingizio’ kama ‘Lowassa ni tishio kwa usalama wa taifa letu,’ ambapo kwa taratibu zisizo rasmi za Usalama wa taifa sehemu nyingi duniani, anaweza ‘kudhibitiwa.’ Hili ni gumu kulieleza kwa undani kutokana na sababu za kimaadili.
Nihitimishe makala hii ndefu kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi zaidi kuhusu uchaguzi mkuu kwa ujumla, hususan katika nafasi ya urais, hasa ikitarajiwa kuwa tunaweza kushuhudia mengi zaidi ya tukio lililogusa hisia za wengi la aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba kujiuzulu ghafla, sambamba na ‘sintofahamu’ kuhusu hatma ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dkt Willibrord Slaa.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.