21 Jan 2016


 
MOJA ya mada zinazotawala vyombo vya habari huko nyumbani ni zoezi linaloendelea la bomoabomoa. Zoezi hilo limepokelewa kwa hisia tofauti huku baadhi ya wananchi wakiliunga mkono (hususan wasioguswa nalo) huku wengine wakiilaumu (hususan waathirika wa zoezi hilo)

Kwa upande mmoja serikali na mamlaka husika zipo sahihi kutekeleza zoezi hilo kwa vile suala hilo licha ya kuwa la muda mrefu lakini pia limekuwa na gharama kubwa, kwa serikali na mamlaka husika, kwa maana ya kuwakwamua wakazi wa mabondeni kila yanapojiri mafuriko, na kwa wakazi hao kukumbwa na hasira kubwa kila msimu wa masika.

Kwa maana hiyo, ilikuwa lazima kwa serikali kufika mahala kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo. Na kwa kiasi kikubwa, hakukuwa na njia ya mkato au ufumbuzi rahisi. Na vyovyote ambavyo ingeamuliwa, ilikuwa lazima wakazi hao wa mabondeni waondoke, aidha kwa hiari yao wenyewe au kwa serikali na mamlaka husika kuwaondosha.

Tayari baadhi ya watu wameanza kuhusisha zoezi la bomoa bomoa na upungufu wa Rais Dk. John Magufuli. Sidhani kama wanamtendea haki. Sawa, tunatambua kuwa kubomolewa makazi na kukosa makazi mbadala si kitu kizuri. Lakini hata hivyo, si Dk. Magufuli au serikali yake iliyowashauri wakazi wa mabondeni kuendelea kuishi katika mazingira hatarishi.

Na kama nilivyoeleza awali, mara nyingi wakazi hao wanapokumbwa na mafuriko, serikali hulazimika kuingia gharama ili kunusuru maisha yao. Kwa hiyo, katika mazingira ya kawaida tu, kwa minajili ya kuepusha gharama hizo, ilikuwa lazima kwa serikali kuchukua hatua stahili.

Lakini pia serikali ina jukumu la kuhakikisha usalama wa raia wake. Kuendelea kuwaachia wakazi wa mabondeni kuishi katika mazingira hatarishi kungekuwa ni sawa na serikali hiyo kuzembea kutekeleza jukumu hilo la msingi, yaani jukumu la kuhakikisha usalama wa raia.
Hata hivyo, pamoja na dhamira nzuri ya serikali katika utekelezaji wa zoezi hilo, pengine ni muhimu kuupa nafasi ubinadamu. Kimsingi, makosa yaliyosababisha uwepo wa makazi hatarishi mabondeni ni ya pande zote mbili: serikali na mamlaka husika, kwa upande mmoja, na wakazi hao, kwa upande mwingine.

Si kwamba siku moja tuliamka na kukuta nyumba zimejengwa mabondeni au kwenye hifadhi za barabara. Misingi ya nyumba ilichimbwa, matofali na vifaa vingine vya ujenzi vililetwa, na ujenzi ukafanyika, na hatimaye wakazi hao kuhamia maeneo hayo, na muda wote huo, serikali na mamlaka husika walikuwepo na hawakuchukua hatua stahili. Japo sio kisingizio mwafaka kwa wakazi hao, lakini kwa serikali na mamlaka husika kutozuia ujenzi huo wakati huo inaweza kuwa ilichangia sio tu kuwafanya waliokwishajenga hapo kudhani wana ruhusa isiyo rasmi bali pia kuliwavuta wengine wasio na mahala pa kujenga.

Sasa, kama wasemavyo waswahili yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo, la muhimu kwa sasa ni kupata ufumbuzi utakaozinufisha pande zote mbili.

Kwa vile ujumbe umekwishafika, kwa maana ya wakazi waliosalia mabondeni wamekwishaona yaliyowakuta wenzao, basi sidhani kama kuna ubaya wa kutoa muda wa kutosha na wa kiuhalisia wa kuwaagiza wakazi hao kuhama kwa hiari yao. Kumpa mtu wiki moja ahame sehemu aliyoishi kwa miaka kadhaa sio kuzingatia uhalisia.

Kama iliwezekana kuwapa wakwepa kodi matajiri siku kadhaa walipe madeni, licha ya ukweli kuwa kukwepa kodi ni kosa la jinai, na matokeo yake (tunaambiwa) wengi walitekeleza agizo hilo, basi kwa nini tusijaribu njia hiyo hiyo kwa wakazi wa mabondeni?

Kwa upande mwingine, japo ujenzi wa mabondeni sio tu ni kinyume cha sheria lakini pia unahatarisha maisha ya wakazi husika, madhara yake kwa jamii sio makubwa kama matatizo mengine ya dharura yanayohitaji kushughulikiwa haraka, hususan biashara ya dawa ya kulevya.

Ndio, makazi mabondeni yanahatarisha usalama wa wakazi wa maeneo hayo, lakini angalau hayahatarishi uhai wa wasiokaa mabondeni. Vipi kuhusu dawa za kulevya? Yanapoteza uhai wa vijana wetu kila kukicha huku yakichangia uhalifu kwa kiwango kikubwa. Naam, mtumia dawa za kulevya akikosa fedha ya kununulia dawa hizo, njia ya mkato ni kufanya uhalifu.

Kwa maana hiyo biashara ya dawa ya kulevya ina madhara makubwa kwa jamii kuliko makazi ya mabondeni. Lakini kinachoanza kuvunja moyo ni ukimya wa serikali katika kushughulikia suala hilo ambalo lilipewa kipaumbele cha hali ya juu na Rais Dk. Magufuli alipotangaza dira ya serikali yake wakati anazindua Bunge jipya.

Sambamba na suala la dawa za kulevya ni suala la ufisadi. Ndio, ziara za kushtukiza zimezaa matunda lakini kumekuwa na ukimya kidogo hapa katikati, na sio wa ziara hizo tu bali pia hata utekelezaji wa uanzishwaji wa mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za ufisadi.

Siku chache zilizopita nilikutana na habari kuhusu Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa amebaini kuna rushwa katika Mahakama. Hilo sio suala geni, na binafsi nilishangaa kusikia Waziri Mwakyembe amebaini sasa ilhali ripoti mfululizo za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikiitaja Mahakama kama miongoni mwa taasisi zinazoongoza kwa rushwa. Je, Waziri Mwakyembe hakuwa akizisoma au kuzisikia habari hizo?

Lakini kilichonikera zaidi ni ukweli kwamba wakati wa mjadala wa ufisadi wa Tegeta-Escrow, zilipatikana taarifa zilizoonyesha majina ya baadhi ya majaji waliopokea mgao uliotokana na ufisadi huo. Hadi leo, majaji hao hawajachukuliwa hatua. Kadhalika, ziliwahi kupatikana taarifa zilizowataja majaji waliotuhumiwa kuwasaidia watuhumiwa wa kesi za dawa za kulevya. Hata hao wanasubiri kuundwa kwa mahakama za ufisadi?

Na tuwe wakweli, hivi kuunda mahakama za ufisadi kunahitaji muda gani hasa ilhali tayari tuna mfumo wa mahakama unaoshughulikia kesi za jinai?

Rais Dk. Magufuli alituasa tumsaidie katika vita dhidi ya maovu mbalimbali yanayoikabili nchi yetu. Kumsaidia si kwa kupiga vigelegele pekee zinapofanyika ziara za kushtukiza au fulani anapofukuzwa kazi bali pia kukosoa pale inapobidi. Matarajio ya wananchi bado yapo juu, na hii ni muhimu sana kwa mafanikio ya mapambano dhidi ya uozo mwingi unaohitaji kushughulikiwa. Kasi hafifu ya kushughulikia matatizo ya ufisadi na uhalifu – kama biashara ya dawa za kulevya – sio tu yaweza kupunguza ari ya wananchi lakini pia yaweza kutoa mwanya kwa wahusika kubuni mbinu mpya, sambamba na kuvutia wahalifu wapya (hususan wale wanaobaini kuwa Shamba la Bibi limefungwa).

Nimalizie makala hii kwa kukumbushia haja ya kuitumia vizuri fursa hii kuikwamua Tanzania yetu kutoka kwenye lindi la umasikini, unaochangiwa na ufisadi na uhalifu mwingine, sambamba na kuweka vipaumbele vyetu sawia kwa kushughulikia matatizo ya haraka badala ya yale yanayoweza kushughulikiwa taratibu. Ndio, Waingereza wanasema “two wrongs don’t make a right,” yaani kufanya kosa la pili hakulifanyi kosa la kwanza kuwa jambo sahihi, na kwa maana hiyo sina maana kuwa kutochukuliwa hatua dhidi ya ‘wauza unga’ kunahalalisha kutofanya bomoa bomoa. Hata hivyo, haja ya kuwashughulikia wahalifu ni ya dharura mno kuliko ya wakazi wa mabondeni.



1 comment:

  1. ni kweli mr Chahali mh anahitaji maombi na msaada ktk kutekeleza majukumu yake maake nchi hii ilielekea pabaya na wananchi kukosa imani

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.