22 May 2016



Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la Watanzania wanaojihusisha na ushoga na usagaji japokuwa vitendo hivyo ni kinyume na sheria za nchi na haviendani na mila na desturi zetu.

Hata hivyo, yawezekana kushamiri kwa vitendo hivyo kunaendana na taarifa za kitafiti kuwa sie Watanzania twaongoza kwa unafiki. Wiki chache zilizopita niliweka bandiko hapa bloguni lililohusu ripoti ya utafiti wa kundi la wasomi katika chuo kikuu cha Nottingham, hapa Uingereza, ulivyobainisha kuwa Tanzania yaongoza duniani kwa unafiki.

Binafsi sikushangazwa na ripoti hiyo hasa kwa vile kuna maeneo mawili yanayothibitisha bayana unafiki wetu. La kwanza ni uhusiano kati ya ucha-Mungu wetu na maovu.

Asilimia kubwa ya Watanzania ni wacha-Mungu. Takwimu zaashiria kuwa takriban asilimia 70 ya Watanzania ni aidha Wakristo au Waislam. Wengi kati ya hao ni watu wasiokosekana kanisani au misikitini. Swali: kama wengi wetu ni waumini kiasi hicho, ni akina nani basi wanaojihusisha na ufisadi, rushwa, biashara ya madawa ya kulevya, ushirikina, na maovu mengine katika jamii?

Tofauti na huko nyumbani, ucha-Mungu hapa Uingereza ni wa kusuasua mno. Watu wengi hapa hawamtambui Mungu na wanajitambulisha kuwa hawana dini. Makanisa mengi yanageuzwa kuwa baa au kumbi za starehe kutokana na uhaba wa waumini.



Lakini licha ya udhaifu katika mahusiano kati yao na Mungu, wenzetu hawa kwa kiasi kikubwa sio wanafiki. Asilimia kubwa kabisa ya watu hawa wanaishi kwa kipato halali, wanaamini katika ukweli, kwa maana ya kusema ukweli na sio wadanganyifu, wanafuata sheria na taratibu mbalimbali, kwa mfano moja ya dhambi kuu hapa ni ukwepaji kodi, kitu ambacho ni kama hobby ya wengi wa wafanyabiashara huko nyumbani.

Eneo la pili ni suala la ushoga na usagaji. Kwa huko nyumbani, suala hili ni mwiko mkubwa, ni laana, ni kinyume na maadili yetu. Lakini kuthibitisha unafiki wetu, sio tu ushoga na usagaji upo bali pia unakua kwa kasi kubwa.

Nenda katika kitchen parties za watu maarufu na 'wakata viuno' ni mashoga huku wengi wa 'makungwi' wakituhumiwa kuwa wasagaji. Inaelezwa kuwa njia moja maarufu ya kusambaa kwa usagaji huko nyumbani ni 'makungwi' wanaofundisha mabinti (kwa malipo) jinsi ya kufanya tendo la ndoa. Hawa wametapakaa jijini Dar na baadhi wanahamia mikoani. Kimsingi, 'darasa la tendo la ndoa' wanalofundisha ni kwa kusagana na 'wanafunzi' wao.

Shughuli za 'madada wa mujini' hazijakamilika kama hakuna akina 'anti naniliu au anti nanihino.' Lakini watu haohao ndio wanaohubiri kwa sauti kubwa kuwa "habari za ushoga na usagaji huko huko kwao (wazungu)."

Kuna kitu kingine 'kichafu' ambacho Watanzania twasifika mno, nacho ni umahiri katika tendo la ndoa kinyume cha maumbile. Kwa kifupi, hii ndio sababu ya kushamiri kwa biashara ya "dawa za makalio feki ya Mchina." Tendo la ndoa kinyume cha maumbile limekuwa kama 'fasheni' kwa wengi wetu huko nyumbani na huku ugenini tunakoishi. 

Sasa, japo tendo la ndoa kinyume cha maumbile sio ushoga per se, kuna hisia kuwa wazoefu wa tabia hiyo "wakikosa nyama wanaweza kula majani." Yaani wanaume wanaopenda tabia hiyo wakikosa mwanamke wanaweza kufanya hivyo na mwanaume shoga.

UTHIBITISHO wa unafiki wetu: Well, sehemu mwafaka zaidi ya kutambua unafiki wetu kuhusu ushoga na usagaji ni INSTAGRAM. Huko, kuna mashoga wanaojinadi waziwazi. Lakini tatizo sio wao kujinadi tu bali ni idadi ya 'followers' wao. Ni wazi kuwa laiti ingekuwa watu wanachukia ushoga 'kihivyo' basi mashoga huko Insta wasingekuwa maarufu kiasi cha kupata followers hadi laki na zaidi.

Profiles hizi pichani chini ni za baadhi tu ya mashoga wa Kitanzania huko Instagram.  Je kama sie sio wanafiki na laiti tungekuwa tunauchukia ushoga 'kihivyo' hao maelfu kwa malaki ya followers kwa hao mashoga wangetaka wapi?


Ukitaka kuchimba zaidi kuhusu 'unafiki' wetu, geukia suala jingine maarufu huko nyumbani: USHIRIKINA. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa taasisi moja ya kimataifa inayoheshimika kwa utafiti ya PEW ya Marekani, Tanzania ipo 'matawi ya juu' katika masuala ya juju, ndumba na ngai, tunguri, kamati ya ufundi, wanga...USHIRIKINA... kama inavyoonyeshwa kwenye chati na ramani hapo chini.




Kwa vile lawama pekee hazijengi, ni muhimu kujaribu kuangalia njia zinazoweza kutuondoa katika lindi hilo la unafiki. Binafsi, ninashauri tuwekeze zaidi katika dua na sala za dhati na sio za kinafiki. Au wewe msomaji mpendwa una maoni gani?



0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.