Showing posts with label USHOGA. Show all posts
Showing posts with label USHOGA. Show all posts

10 Jul 2016


Check this out on Chirbit

22 May 2016Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa kuna ongezeko kubwa la Watanzania wanaojihusisha na ushoga na usagaji japokuwa vitendo hivyo ni kinyume na sheria za nchi na haviendani na mila na desturi zetu.

Hata hivyo, yawezekana kushamiri kwa vitendo hivyo kunaendana na taarifa za kitafiti kuwa sie Watanzania twaongoza kwa unafiki. Wiki chache zilizopita niliweka bandiko hapa bloguni lililohusu ripoti ya utafiti wa kundi la wasomi katika chuo kikuu cha Nottingham, hapa Uingereza, ulivyobainisha kuwa Tanzania yaongoza duniani kwa unafiki.

Binafsi sikushangazwa na ripoti hiyo hasa kwa vile kuna maeneo mawili yanayothibitisha bayana unafiki wetu. La kwanza ni uhusiano kati ya ucha-Mungu wetu na maovu.

Asilimia kubwa ya Watanzania ni wacha-Mungu. Takwimu zaashiria kuwa takriban asilimia 70 ya Watanzania ni aidha Wakristo au Waislam. Wengi kati ya hao ni watu wasiokosekana kanisani au misikitini. Swali: kama wengi wetu ni waumini kiasi hicho, ni akina nani basi wanaojihusisha na ufisadi, rushwa, biashara ya madawa ya kulevya, ushirikina, na maovu mengine katika jamii?

Tofauti na huko nyumbani, ucha-Mungu hapa Uingereza ni wa kusuasua mno. Watu wengi hapa hawamtambui Mungu na wanajitambulisha kuwa hawana dini. Makanisa mengi yanageuzwa kuwa baa au kumbi za starehe kutokana na uhaba wa waumini.Lakini licha ya udhaifu katika mahusiano kati yao na Mungu, wenzetu hawa kwa kiasi kikubwa sio wanafiki. Asilimia kubwa kabisa ya watu hawa wanaishi kwa kipato halali, wanaamini katika ukweli, kwa maana ya kusema ukweli na sio wadanganyifu, wanafuata sheria na taratibu mbalimbali, kwa mfano moja ya dhambi kuu hapa ni ukwepaji kodi, kitu ambacho ni kama hobby ya wengi wa wafanyabiashara huko nyumbani.

Eneo la pili ni suala la ushoga na usagaji. Kwa huko nyumbani, suala hili ni mwiko mkubwa, ni laana, ni kinyume na maadili yetu. Lakini kuthibitisha unafiki wetu, sio tu ushoga na usagaji upo bali pia unakua kwa kasi kubwa.

Nenda katika kitchen parties za watu maarufu na 'wakata viuno' ni mashoga huku wengi wa 'makungwi' wakituhumiwa kuwa wasagaji. Inaelezwa kuwa njia moja maarufu ya kusambaa kwa usagaji huko nyumbani ni 'makungwi' wanaofundisha mabinti (kwa malipo) jinsi ya kufanya tendo la ndoa. Hawa wametapakaa jijini Dar na baadhi wanahamia mikoani. Kimsingi, 'darasa la tendo la ndoa' wanalofundisha ni kwa kusagana na 'wanafunzi' wao.

Shughuli za 'madada wa mujini' hazijakamilika kama hakuna akina 'anti naniliu au anti nanihino.' Lakini watu haohao ndio wanaohubiri kwa sauti kubwa kuwa "habari za ushoga na usagaji huko huko kwao (wazungu)."

Kuna kitu kingine 'kichafu' ambacho Watanzania twasifika mno, nacho ni umahiri katika tendo la ndoa kinyume cha maumbile. Kwa kifupi, hii ndio sababu ya kushamiri kwa biashara ya "dawa za makalio feki ya Mchina." Tendo la ndoa kinyume cha maumbile limekuwa kama 'fasheni' kwa wengi wetu huko nyumbani na huku ugenini tunakoishi. 

Sasa, japo tendo la ndoa kinyume cha maumbile sio ushoga per se, kuna hisia kuwa wazoefu wa tabia hiyo "wakikosa nyama wanaweza kula majani." Yaani wanaume wanaopenda tabia hiyo wakikosa mwanamke wanaweza kufanya hivyo na mwanaume shoga.

UTHIBITISHO wa unafiki wetu: Well, sehemu mwafaka zaidi ya kutambua unafiki wetu kuhusu ushoga na usagaji ni INSTAGRAM. Huko, kuna mashoga wanaojinadi waziwazi. Lakini tatizo sio wao kujinadi tu bali ni idadi ya 'followers' wao. Ni wazi kuwa laiti ingekuwa watu wanachukia ushoga 'kihivyo' basi mashoga huko Insta wasingekuwa maarufu kiasi cha kupata followers hadi laki na zaidi.

Profiles hizi pichani chini ni za baadhi tu ya mashoga wa Kitanzania huko Instagram.  Je kama sie sio wanafiki na laiti tungekuwa tunauchukia ushoga 'kihivyo' hao maelfu kwa malaki ya followers kwa hao mashoga wangetaka wapi?


Ukitaka kuchimba zaidi kuhusu 'unafiki' wetu, geukia suala jingine maarufu huko nyumbani: USHIRIKINA. Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni wa taasisi moja ya kimataifa inayoheshimika kwa utafiti ya PEW ya Marekani, Tanzania ipo 'matawi ya juu' katika masuala ya juju, ndumba na ngai, tunguri, kamati ya ufundi, wanga...USHIRIKINA... kama inavyoonyeshwa kwenye chati na ramani hapo chini.
Kwa vile lawama pekee hazijengi, ni muhimu kujaribu kuangalia njia zinazoweza kutuondoa katika lindi hilo la unafiki. Binafsi, ninashauri tuwekeze zaidi katika dua na sala za dhati na sio za kinafiki. Au wewe msomaji mpendwa una maoni gani?11 Jun 2012


Pichani ni shoga maarufu Bilali Mashauzi ambaye ni nadra kukosekana kwenye sherehe za akinadada maarufu Tanzania


SUNDAY, JUNE 10, 2012


MSIMAMO WANGU KUHUSU USHOGA

umeibuka mjadala mkubwa leo twitter kuhusiana na group la facebook la kudai haki za mashoga tanzania. i saw this coming, Mashoga wapo, walikuwepo na wataendelea kuwepo regardless tumewakubali au tumewakataa.

kwanza niseme Imani yangu ya dini, mwenendo wangu wa maisha na jamii ninayoishi nayo hainiruhusu kukubali ushoga. Natamka kuwa siukubali ushoga kwa kuwa kiimani ya dini yangu ni dhambi, lakini pia katika mfumo wa maumbile ya mwanadamu ni kinyume.

Lakini pia Sikubali uzinzi, uasherati, ushirikina, wizi pamoja na dhambi nyengine ambazo kwa utamaduni wa mtanzania ni makosa na dini zote tunazoamini Tanzania ni makosa hali kadhalika.

jambo linalonifanya niandike makala hii ni kuweka wazi kama hata Leo mashoga wakiandamana barabarani kudai Haki zao au nikisikia serikali imeruhusu ndoa za jinsia moja, nitaumia moyoni kwa kuwa kwa imani yangu si sahihi lakini sitatoka kuungana na WANAFIKI kupinga haki za mashoga

Nimetumia neno wa WANAFIKI kwa kuwa watanzania wengi ni WANAFIKI. kati yenu, nani dini yake inaamini uasherati na uzinzi ni sahihi? kipo kitabu cha dini kinaruhusu Uzinzi? je utamaduni wa Mtanzania unaruhusu Uzinzi? na je wewe mwenyewe unaamini Uasherati na Uzinzi ni sahihi?

kama dini yako hairuhusu uzinzi, wewe mwenyewe unaamini uzinzi na uasherati si sahihi, na utamaduni wako unakataa uzinzi na uasherati, UMEFANYA NINI KUHUSU SHERIA YA TANZANIA KAMA UKIKAA NA MWANAMKE/MWANAUME ZAIDI YA MIAKA MIWILI INAITWA NDOA? nguruwe huli ila mchuzi wake unakunywa?

Sisi wenyewe, ndugu zetu, jamaa na marafiki tunasifiana uzinzi, tunafanya uzinzi, tuna facebook groups za uzinzi, kitu ambacho kitamaduni na kidini si sahihi, lakini tukisikia shoga tunapiga kelele.. huo ni unafiki

Wapo waislamu wenzangu ambao ni walevi wa pombe lakini Nguruwe hawali kwa kuwa ni Haramu, pombe ni halali? mlevi ataingia peponi kwa imani yako? Baba Yangu ana msemo "ukiamua kula nguruwe, chagua aliyenona" meaning ukiamua fanya dhambi wewe fanya tu kwa kuwa kwa mungu hakuna dhambi ndogo

Niwakumbushe kwa mungu kuna njia mbili, Ama PEPONI au MOTONI. naamini kutokana na Mafundisho yangu kwamba Shoga, Mzinzi, Mwizi, Muasherati, Muuaji pamoja na dhambi nyengine wataingia moto mmoja hivyo basi ukiamua kataza maovu, acha kwanza wewe na kemea maovu yote bila kubagua kwa kuwa hata usipofanya ushoga ukafanya wizi, utakuwa hujajinasua na moto

sikatazi watu kupinga USHOGA na hata nikikataza mimi sio Mtume wala Rais na wala neno langu sio Sheria ila nasema Siungani na nyie Kwenye kupinga haki ya Mashoga kuoana wakati mmekalia kimya uzinzi, uasherati, na ushirikina ambavyo vyote havikubaliki kwa utamaduni wa mtanzania wala kwa dini tuanzoamini watanzania

*********HAYO NI MAONI YANGU NA NDIO MSIMAMO WANGU*****24 May 2012
Uamuzi mgumu na ujasiri wa kisiasa

Evarist Chahali
Toleo la 240
23 May 2012
WIKI iliyopita, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliingia kwenye vitabu vya historia ya taifa hilo kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja. Kwa muda mrefu Obama alikuwa aidha akipinga suala hilo nyeti au kuchelea kuweka wazi msimamo wake.
Tayari suala hilo la ndoa za jinsia moja limezua mgawanyiko mkubwa wa kimtizamo ingawa kura mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa msimamo huo ‘mpya’ wa Obama hautoathiri kwa kiasi kikubwa maamuzi ya wapigakura katika uchaguzi mkuu wa Marekani unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa kura za maoni za hivi karibuni, takriban asilimia 60 ya Wamarekani wanasema kitendo cha Obama kuunga mkono ndoa za mashoga hakitowashawishi kumpigia au kutompigia kura.
Lakini moja ya makundi ambayo yanaonyesha kuguswa na suala hilo ni Wamarekani Weusi. Kama ilivyo kwetu Waafrika, Wamarekani Weusi wamekuwa wapinzani wakubwa si tu wa ndoa, bali hata uhusiano wa kawaida wa watu wa jinsia moja. Mara kadhaa wasanii wengi wa muziki wa kufokafoka (hip-hop/rap), ambao ni maarufu kwa Wamarekani Weusi, wamekuwa wakilaumiwa kwa tungo zao zenye kuonyesha bayana upinzani dhidi ya ushoga.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, baadhi ya viongozi wa makanisa ya Wamarekani Weusi wameeleza bayana kuwa hawamuuingi mkono Obama katika suala hilo, huku wengine wakitishia kutompigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Japo Obama anaendelea kuungwa mkono na kundi hilo (la Wamarekani Weusi) huku akionekana kuwa ni ‘mwenzao’, kura za maoni zinaonyesha kuwa asilimia 49 inampinga katika msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga kulinganisha na asilimia 43 ya Wamarekani Weupe.
Obama mwenyewe amekiri kuwa anafahamu bayana msimamo wake huo utawaudhi baadhi ya wanaomuunga mkono. Lakini akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha luninga cha ABC cha Marekani, Rais huyo alieleza kuwa inamwia vigumu kuendelea na ‘sintofahaumu’ katika ‘ubaguzi’ dhidi ya mashoga ilhali Wamarekani kadhaa anaowaongoza wamo kwenye kundi hilo.
Alifafanua kuwa kama mzazi, alikuwa anapata wakati mgumu kutokuunga mkono ndoa za mashoga ilhali wanae Sasha na Malia wana  baadhi ya marafiki zao ambao wazazi wao ni mashoga.
Kadhalika, alieleza kuwa ilikuwa inamsumbua pia kuendelea kutokuunga mkono ndoa za mashoga huku baadhi ya makundi muhimu katika nchi hiyo, kwa mfano, wanajeshi wanaolitumikia taifa hilo kwa uadilifu mkubwa, yakijumuisha mashoga.
Lengo la makala hii si kumuunga mkono au kumpinga Obama katika msimamo wake huo kwa ndoa za mashoga bali kupigia mstari nafasi ya ujasiri katika uongozi.
Kama alivyokiri mwenyewe kuwa anafahamu bayana uamuzi wake wa kutangaza hadharani msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga utawakera wengi, na pengine kumgharimu katika uchaguzi mkuu ujao, lakini Obama ameweza kufanya ujasiri wa kusimamia kile anachokiamini.
Japokuwa kuna baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaotafsiri hatua hiyo ya Obama kama kigeugeu-kwa maana alishawahi kuwa mpinzani wa ushoga- huku wengine wakidai hatua hiyo ni ‘janja yake’ tu kusaka kura za mashoga, jambo la msingi hapa ni ukweli kwamba amediriki kuweka kando uoga (huku akijua madhara) na kuweka wazi wapi anasimamia katika suala hilo.
Kwa upande fulani, uamuzi huo unaweza kumnufaisha dhidi ya mpinzani wake mtarajiwa kutoka chama cha Republicans, Mitt Romney, ambaye kama ilivyo kwa wahafidhina wengi, suala la ushoga ni kama laana.
Sasa, kwa vile moja ya misingi muhimu ya taifa la Marekani ni uhuru wa mtu kufanya apendacho alimradi havunji sheria, sambamba na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Obama na wanaomuunga mkono wanaweza kuutumia upinzani wa Romney dhidi ya ndoa za mashoga kama mfano hai wa jinsi mgombea huyo (mtarajiwa) na chama chake cha Republicans walivyobobea kwenye ‘ubaguzi na kuminya uhuru’  wa Wamarekani.
Kwa mtizamo wangu, ujasiri alionyesha Obama (bila kujali kama naafikiana au ninapingana naye katika suala la ndoa za mashoga) ninaulinganisha na kauli za hivi karibuni za aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa sasa wa Monduli (CCM), Edward Lowassa. Naomba niweke wazi kuwa ninaamini wasomaji wengi wa makala hizi wanafahamu fika msimamo wangu dhidi ya Lowassa, hususan kuhusiana na tuhuma za ufisadi. Lakini msimamo huo haumaanishi nichelee kumuunga mkono pale anapoonyesha ujasiri wa kisiasa.
Kwa muda mrefu sasa, Lowassa amejitokeza kuwa mmoja wa wanasiasa wachache ndani ya CCM wanaoeleza waziwazi mapungufu ya chama hicho na jinsi yanavyoliathiri taifa kwa ujumla. Lakini kama ilivyozoeleka, msimamo huo (ambao hapa ninauita ujasiri) umemfanya mwanasiasa huyo aonekane kama kiumbe hatari kabisa kwa ustawi na uhai wa chama hicho tawala.
Majuzi, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alinukuliwa akimpinga Lowassa kutokana na kauli yake katika mkutano wa hadhara huko Mto wa Mbu, Arusha, kuwa tatizo la CCM ni uongozi kuacha kusimamia misingi. Katika majibu yake kwa Lowassa, Mukama alimtaka mbunge huyo wa Monduli kushughulikia matatizo jimboni kwake kwanza.
Kuna wanaotafsiri kuwa msimamo wa Lowassa kukikosoa chama chake ni sehemu tu ya mikakati yake ya kuwania urais mwaka 2015. Lakini wanaofikiria hivyo wanapaswa kumtendea haki mwanasiasa huyo hasa kwa vile hajatangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Kadhalika, ni muhimu kutanua upeo wetu na kuzichambua kauli za Lowassa pasipo kuzihusisha zaidi na malengo yake ya baadaye ya kisiasa.
Kimsingi, tukiweka kando hisia za ‘unafiki wa kisiasa’, anayoongea Lowassa kuhusu CCM ni ya kawaida sana kwa maana kwamba kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufikiri anaelewa ‘mchango wa CCM katika kukwaza maendeleo ya nchi yetu.’
Kama chama tawala, CCM haiwezi kujinusuru dhidi ya shutuma kwamba inachangia sana kukwaza jitihada za kulikwamua taifa kutoka kwenye lindi la umasikini unaochangiwa zaidi na vitendo vya ufisadi.
Kwamba Lowassa ni mmoja wa wana-CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi si sababu ya kumfanya mwanasiasa huyo kutozungumzia suala hilo. Na hata hizo tuhuma dhidi yake zinaweza kukosa nguvu kwa vile CCM yenyewe imeshindwa kuchukua hatua zozote dhidi yake.
Makala hii haina maneno ya kuitia moyo CCM katika msimamo wa baadhi ya viongozi wake wanaokerwa na kauli za Lowassa, hasa ikizingatiwa kuwa anachofanya mwanasiasa huyo ni kuwakilisha tu mtizamo wa Watanzania wengi (ikiwa ni pamoja na wana-CCM) dhidi ya chama hicho tawala. CCM inaweza hata kumtimua Lowassa lakini isipojirekebisha, kuna kila dalili kuwa itang’olewa madarakani huko mbeleni.
Japo ninaelewa msimamo wa Mukama kwamba kama kiongozi wa CCM Lowassa anapaswa kuongelea matatizo ya chama hicho kwenye vikao vya ndani, kimsingi hilo ni moja ya vyanzo vya matatizo yanayosababisha watu kama Lowassa kuamua kuweka hadharani matatizo hayo.
Ni hivi, kama chama hicho kina matatizo, kisha yanazungumzwa kwenye vikao vya ndani na hayapatiwi ufumbuzi, kwa nini basi kiongozi asishawishike kuyaongelea matatizo hayo hadharani?
Halafu kuna suala la maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya chama. Kwa vile CCM ni chama tawala, kila inachofanya au kuzembea kufanya kinaligusa taifa moja kwa moja. Kwa mantiki hiyo, wakati Mukama anaweza kuyaona matatizo ya CCM kuwa ni suala la kichama, kiuhalisi matatizo hayo si tu yanaligusa taifa bali pia ni suala la kitaifa. Na kwa vile Tanzania ni yetu sote, basi ni sahihi na halali kwa kila Mtanzania, ikiwa ni pamoja na Lowassa, kuyaongelea matatizo yanayolisumbua taifa letu pasi uoga wa kumuudhi mtu flani.
Naomba kuhitimisha makala hii kwa kurejea kuweka bayana msimamo wangu kuwa lengo halikuwa kuunga mkono msimamo wa Obama kuhusu ndoa za mashoga wala kugeuka muungaji mkono wa Lowassa (japo vyote si dhambi).
Makala hii imelenga kuwapongeza wanasiasa hao kwa ujasiri wa kuweka wazi misimamo yao hata pale kufanya hivyo kunapoweza kuwaingiza matatizoni. Kinyume cha ujasiri ni uoga na unafiki, na sote tunafahamu kuwa kiongozi mwoga na/au mnafiki si tu hawezi kusimamia yale anayoamini lakini pia ni kikwazo katika jitihada za kuleta mabadiliko muhimu kwa anaowaongoza.


11 Nov 2011

Tatizo ni unafiki wetu, si ushoga

Uskochi
MOJA ya mambo yaliyonishitua sana nilipofika hapa Uingereza kwa mara ya kwanza ni jinsi Ukristo ulivyopoteza nguvu yake (hususan mahudhurio kanisani na watu wanaofuata Ukristo). Kilichonishitua ni ukweli kwamba Ukristo uliletwa huko nyumbani na “wazungu” hawa na nilitarajia wangekuwa wacha Mungu wakubwa.
Dalili za Ukristo kupoteza nguvu yake zinaonekana katika namna makanisa yanavyoishia kugeuzwa kumbi za starehe baada ya kukosa waumini. Kadhalika, asilimia kubwa ya waumini makanisani ni wageni kutoka nje ya nchi hii. Na japo Malkia wa Uingereza ni Mkuu wa Kanisa la Anglikana na Askofu Mkuu wa Canterbury ni mithili ya Baba Mtakatifu (Papa) kwa Kanisa hilo, idadi kubwa ya Waingereza inajitambulisha kama watu wasiofuata dini. Na kuna kundi kubwa tu la wanaojitambulisha kama Wakristo lakini wasiotia mguu kanisani.
Hakuna jibu jepesi kuhusu kwa nini Ukristo unazidi kupoteza nguvu nchini hapa lakini baadhi ya watu niliowahoji wanadai huenda maendeleo katika nyanja mbalimbali ni chanzo kwa baadhi ya watu “kupuuza” umuhimu wa imani katika maisha ya mwanadamu.
Lakini pamoja na Ukristo kupoteza nguvu yake miongoni mwa Waingereza, kwa kiasi kikubwa uadilifu katika nyanja mbalimbali za maisha umeendelea kuwa wa kiwango cha juu. Na hapa ndipo unaweza kubaini tofauti kubwa kati ya Waingereza “wanaopuuza dini” na akina sie huko nyumbani ambao dini inaonekana kuwa sehemu muhimu kwa maisha yetu.
Neno mwafaka linaloweza kuelezea tofauti hiyo ni UNAFIKI. Ni hivi, ni bora kuwa na watu wasio na dini au wasioabudu uwepo wa Mungu lakini wakaishi na kutenda mambo kiadilifu kuliko kuwa na ‘washika’ dini wasiokosekana makanisani au misikitini lakini uadilifu wao ni haba kama sio sifuri kabisa.
Na suala la unafiki linaweza kuchukua nafasi muhimu katika mjadala mkali uliosababishwa na kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza kuwa nchi yake itasitisha misaada kwa nchi zinazokiuka haki za mashoga. Tayari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameweka bayana msimamo wa Serikali kwamba Tanzania ipo tayari kukosa misaada ya Uingereza kuliko kubadilisha sheria za nchi zinazopiga marufuku ushoga.
Lakini kabla sijaingia kwa undani katika kujadili suala hili ni vema nikaweka wazi msimamo wangu. Imani yangu kama Mkristo wa madhehebu ya Katoliki (ambaye almanusura ningekuwa padre iwapo nisingeghairi kujiunga na seminari mwaka 1986) sio tu inapinga ushoga bali pia inauona kama dhambi. Kwa hiyo, naomba ifahamike kuwa lengo la makala hii si kuunga mkono ushoga.
Kwa upande mmoja, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alikuwa na haki ya kuweka masharti katika misaada wanayotoa. Ifahamike kuwa misaada hiyo inatokana na fedha za walipa kodi wa Uingereza na inatarajiwa ielekezwe kwa nchi zinazoonekana machoni mwa Waingereza kama zinazoendana na maadili yao. Na moja ya masuala yanayopewa kipaumbele na nchi hii ni haki za binadamu (ikiwa ni pamoja na haki za mashoga).
Kwa hiyo basi si kwamba Cameron alikurupuka tu na tamko hilo ambalo baadhi ya wenzetu wamelitafsiri kama ajenda ya kueneza ushoga, bali anawakilisha hisia za wananchi wake ambao kimsingi ndio chanzo za fedha tunazopatiwa kama misaada.
Ni wazi kuwa kiongozi yeyote yule anayejua anachofanya atahakikisha anasimama upande wa wananchi wake. Kwa mantiki hiyo wananchi wake wanapotaka fedha yao wanayotupatia kama msaada ielekezwe tu kwa nchi zinazojali haki za binadamu (ikiwa ni pamoja na haki za mashoga) tu basi hana budi kufanya hivyo.
Japo siungi mkono ushoga lakini ninaelewa mantiki ya Cameron kutoa tamko hilo linaloakisi matakwa ya wananchi wake. Lakini kwa vile matakwa ya Waingereza kuhusu haki za binadamu hayaishii kwa mashoga pekee, ingeleta maana zaidi iwapo tishio la kukata misaada lingeelekezwa pia kwenye tatizo sugu la rushwa (na ufisadi kwa ujumla) ambalo si tu linakwaza haki za binadamu za masikini (ambao ni wengi kuliko mashoga) bali pia linaweza kusababisha wanyonge kupoteza maisha (kwa mfano rushwa inayowezesha  vyombo vya usafiri vyenye hitilafu kuendelea na kazi na hatimaye kusababisha ajali).
Sasa nigeukie unafiki unaoandamana na jinsi tamko la Cameron lilivyopokelewa. Haihitaji utafiti wa kina kubaini kwamba si tu Tanzania (na nchi nyingine zinazolengwa na tishio hilo la kukatiwa misaada) ina mashoga lakini pia ushoga unazidi kuongezeka. Hivi nani anayesoma magazeti ya burudani au blogu hajamwona shoga mmoja aliyejipachika jina Seduction ambaye ni kama yupo kwenye kila shughuli za mabinti maarufu jijini Dar?
Nilipokuwa huko nyumbani mwaka 2005 na niliporejea tena mwaka 2008 nilishuhudia idadi kubwa tu ya mashoga katika maeneo mbalimbali ya burudani jijini Dar es Salaam. Na uchunguzi usio rasmi ulionesha kuwapo kwa mashoga kwenyekitchen parties ni kama suala la kawaida tu. Nilibaini kwamba kumbi za muziki wa mwambao zilikuwa ni chaguo kubwa la mashoga.
Lakini jambo moja la wazi ni kwamba hakukuwa na upinzani, chuki au hasira dhidi ya mashoga hao. Na sijawahi kusikia kuna shoga amekamatwa na polisi, kupelekwa mahakamani na hatimaye kufungwa kwa “kosa” la kuwa shoga. Na ukidhani hilo la kutokamatwa kwa mashoga ni la kushangaza sana, basi kubwa zaidi ni uteuzi wa kigogo mmoja (mstaafu sasa) wa shirika la umma ambaye kila aliyemjua alikuwa anafahamu  tabia yake ya ushoga (kwa maana ya tendo la ndoa na watu wa jinsia yake).
Nina hakika aliyemteua alikuwa anafahamu hilo lakini haikuzuia kigogo huyo kupewa nafasi ya kufisadi shirika hilo hadi alipoondoka huku akijimwagia sifa za vichekesho.
Tuache unafiki, hivi maadili tunayodai ni haya ya wengi wa vigogo wetu kutumainia waganga wa kienyeji katika kila wanalofanya? Maadili haya ya “wachunga kondoo wa Bwana” kuishi maisha ya kifahari kama matajiri wakubwa ilihali waumini wao hohehahe wakihimizwa kuongeza kiwango cha sadaka? Au maadili haya ya Wakristo na Waislamu wasiokosekana kwenye nyumba za ibada lakini ndio wahusika wakuu wa ufisadi? Au haya ya ushirikina kuwa muhimu kuliko kumtumainia Mungu?
Au maadili tunayodai kuwa nayo ni haya ya majambazi wanaotupora utajiri wetu kisha kuibukia makanisani au misikitini na kutoa sadaka au zaka kubwa (iliyotokana na fedha ileile waliyotuibia)? Au maadili tunayodai Waziri Mkuu Cameron anayapuuza ni haya ya wengi wa wasanii wetu wa kike kwenye fani ya filamu ambao licha ya kupendelea kuvaa nusu uchi, hawana mishipa ya aibu kutangazia umma uchafu wanaofanya katika maisha yao? Maadili haya ya wasanii wa Khanga Moja na Kitu Tigo wanaoigiza u-Sodoma na Gomora hadharani kwa kisingizio cha burudani lakini hakuna wa kuwachukulia hatua?
Ni maadili gani anayozungumzia Kikwete na Waziri wake Membe ilihali katika hotuba yake iliyogusia mafisadi wa EPA alikumbushia umuhimu wa haki zao za binadamu (na ikambidi aliyekuwa Spika, Samuel Sitta, amkumbushe Rais kuwa haki za wananchi ni muhimu kuliko za mafisadi)?
Mbona hakukuwa na maandamano ya kumlaani Kikwete kwa kutetea haki za binadamu ambao ni mafisadi lakini leo tunawalaani Waingereza kwa kutishia kutunyima fedha zao kama tusipofuata matakwa yao?
Lakini unafiki mkubwa zaidi ni huu: viongozi hawa hawa ambao licha ya kukiri hadharani kuwa hawajui kwa nini nchi yetu ni masikini (labda pia hawajui kwa nini waliamua kutuongoza) pia ni washiriki wakubwa wa ufisadi unaotufanya tuishi kwa kutegemea fadhila za wafadhili kama Uingereza, wanatuhadaa kuwa ni bora tunyimwe misaada kuliko kukiuka maadili yetu. Lakini wababaishaji hawa hawatuambii jinsi watakavyofidia pengo litakalotokana na kukatwa misaada hiyo.
Na hawatuambii kwa sababu hajui watafidia vipi na hawajali kwa vile wao hawataathiriwa na kukatwa misaada hiyo. Na kama ambavyo tatizo la umeme linavyodumishwa na mafisadi ili kujaza akaunti za vijisenti huku nje, si ajabu tukikatiwa misaada mafisadi watapata kisingizio kipya cha “imebidi mabilioni haya ya shilingi yatumike kufidia pengo lililotokana na uamuzi wa Uingereza kutukatia misaada.”
Nimalizie makala hii kwa kutamka bayana kuwa kama ambavyo sipingi uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa vile hainihusu mie Mkristo, sina tatizo na kurekebisha sheria za ushoga kwa vile si tu mashoga wapo na wanazidi kuongezeka (na hakuna anayewachukulia hatua kwa kuvunja sheria) lakini pia sheria hizo hazinihusu mimi au yeyote yule asiye shoga.

4 Nov 2011Waziri Membe asema kama ni misaada yao basi
Raymond Kaminyoge 
TANZANIA imesema ipo tayari kukosa  misaada yote kutoka Serikali ya Uingereza  na kamwe haiwezi kuruhusu sheria inayotambua mashoga na kuhalalisha ndoa za jinsia moja.Msimamo huo mzito wa serikali umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kutamka kwamba nchi yake ina mpango wa kusitisha misaada yake kwa nchi ambazo sheria na katiba zao, hazitambui mashoga na ndoa za jinsia moja.

Cameron alikaririwa akithibitisha kuwa tayari amewajulisha juu ya suala hilo Wakuu  wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola waliokuwa wakihudhuria mkutano wa Jumuiya hiyo uliomalizika siku nne zilizopita,  mjini Perth , Austaralia ambao pia ulihudhuriwa na Rais Jakaya Kikwete.

Waziri Mkuu huyo kutoka chama cha Conservative ambacho kilishinda uchaguzi Mei mwaka jana, alisema  suala hilo la mashoga na ndoa za jinsi moja ni moja ya mambo yanayoongoza sera ya serikali yake kuhusu misaada kwa mataifa mbalimbali na kwamba tayari imeanza kutekelezwa katika maeneo kadhaa duniani.

Kauli ya Cameron imechukuliwa kama kielelezo cha ukoloni mamboleo ambao Uingereza inajaribu kuupandisha daraja  kwa mataifa yanayoendelea kwa kigezo cha misaada  

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe,  alisema pamoja na umasikini wake, Tanzania kamwe haitaruhusu upuuzi huo kwa kigezo cha misaada.

“ Tanzania ni nchi maskini lakini hatutakubali kuruhusu upuuzi huo eti kwa sababu ya misaada yake na fedha zao, lakini ushoga si utamaduni wetu, hata sheria zetu zinakataa,” alisema Membe.

Alifafanua kuwa katika kuonesha msimamo wa kutokukubaliana na masharti hayo, Tanzania imeshikilia msimamo thabiti kupinga  upuuzi huo ambapo  Januari mwaka huu,  ilimkataa balozi shoga ambaye aliteuliwa na nchi yake kuja kuiwakilisha hapa  nchini. Hata hivyo Waziri Membe hakutaja jina la balozi huyo wala nchi  anayotoka.
“Niwape siri moja ambayo tuliificha lakini leo ngoja niwaambie, mwanzoni mwa mwaka jana nililetewa barua  kunijulisha ujio wa balozi mmoja anayekuja kuiwakilisha nchi yake, mwanamume mwenye ndoa ya jinsia moja. Nilikwenda kumweleza Rais Jakaya Kikwete kuhusu wasifu wa balozi huyo mtarajiwa naye akajibu kwa maneno matatu, yarabi toba! Mkatae!” 
Waziri Membe alifafanua kuwa serikali ilimkataa balozi huyo kwa kuwa ni kinyume cha utamaduni wetu na sheria za nchi kuwa na watu wenye tabia hizo.

Alisema alimjulisha waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kwamba balozi huyo haruhusiwi kuja kufanya kazi nchini kwa kuwa ni kinyume na utamaduni wetu.  “ Waliendelea kuniomba kwamba balozi huyo akija hatatoka kwenye makazi yake akiwa na mwenza wake hivyo watu hawatamuona lakini tulimkataa kabisa, wakatuelewa,” alisema Membe.

 Alieleza kuwa  tamko hilo la Waziri Mkuu Cameron linaweza kusababisha hatari ya kuvunjika kwa uhusiano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola na koloni mama  Uingereza na waziri huyo atabeba lawama hizo

 Akisisitiza msimamo huo wa serikali, Membe,  alisema  Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha tisa, kinatambua ndoa ya jinsia mbili tofauti,  yaani mume na mke.  “ Sheria hizi tunazozitumia hivi sasa tumezirithi kutoka Uingereza ambako leo wanatukuza ndoa za jinsia moja na ushoga,” alisema Membe.
Suala la kile kinachoitwa haki za binadamu kuhusu ushoga ilikuwa moja ya ajenda ambazo viongozi kadhaa walishindwa kuafikiana katika mkutano  Perth .
Hoja ya  kukomesha vizuizi dhidi ya ushoga na ndoa za jinsi moja lilikuwa moja ya mapendekezo yaliyokuwamo katika ripoti ya ndani kuhusu matarajio ya baadaye ya Jumuiya hiyo ya Madola.
  
Itakumbukwa kwamba, Malawi tayari imeathirika na mpango huo wa Uingereza kwa sehemu ya misaada yake kusitishwa kutokana na msimamo wa nchi hiyo kuhusu kile Uingereza na nchi za Magharibi zinazokiita haki za mashoga. Ikumbukwe pia kuwa, mjadala mzito ulioibuka katika Bunge la Uganda mwaka 2009 kuhusu ndoa za jinsi moja ilikuwa sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo ya Uingereza na washirika wake.
CHANZO: Mwananchi

31 Mar 2010

Picha kwa Hisani ya Blogu ya Dina Marios
Mie kama Mkatoliki,siafikiani na ushoga au usagaji.Lakini kutoafikiana na kitu ni jambo moja na kukizuia ni jambo jingine.Ni ukweli usiofichika kuwa vitendo vya ushoga na usagaji vinaanza kuonekana kuwa vya kawaida katika jamii ya Kitanzania,hususan jijini Dar es Salaam.Je wakati umefika sasa kuhalalisha ushoga na usagaji?Na je kwa sheria za nchi ku-criminalise homosexuality inakiuka haki za binadamu?Na pengine swali la ziada,kuufanya ushoga na usagaji kuwa mithili ya laana kumesaidia chochote kuukomesha? Ni mjadala wa miaka nenda miaka rudi,karne baada ya karne.Je ushoga na usagaji ni tabia tu ya mwanadamu au ni asili?Ukitafuta jibu la mkato,unaweza kutotenda haki kwa upande mwingine wa mjadala.Kwa ufahamu wangu mdogo,kuna maelezo ya takriban aina mbili.Hoja ya kwanza,ushoga na usagaji ni suala la kimaumbile/kibaiolojia zaidi kuliko ridhaa ya mwanadamu.Maelezo haya yanazingatia wingi wa homini za jinsia tofauti kwatika mwili.Kwa maana kwamba mwanamke mwenye homoni nyingi za kiume ana uwezekano wa kuwa msagaji,na mwanaume mwenye homoni nyingi za kike anaweza kuwa shoga.Ni ishu complicated lakini nimejaribu kuieleza kwa kifupi.

Hoja ya Pili,ushoga na usagaji ni tabia tu ya mwanadamu kama zilivyo tabia nyingine.Yaani ni kama mtu anapoamua kuwa mvuta sigara au mtumia kilevi.Namna mhusika anavyoangukia kwenye tabia ya ushoga au usagaji nayo inaweza kuangalia kwa namna kadhaa.Kwa mfano,mwanadamu anaweza kuangukia kwenye ushoga au usagaji kwa tamaa.Au anaweza kuingia kwenye vitu hivyo kutokana na kuiga.Au pia anaweza kuwa 'majeruhi wa mchezo mchafu' i.e. alilawitiwa jela akaishia kupenda,alijaribu akanogewa,nk.La muhimu hapa ni kwamba uamuzi wa kuwa shoga au msagaji ni katika kile wanasosholojia wanakiita rational choice.Mtu anapima faida na hasara (cost and benefit analysis) kisha anachukua uamuzi anaoona unafaa.Pia hapa kuna suala la makuzi (socialisation) ambapo zawadi na adhabu (rewards and punishment),au tuseme sanctions,zinachangia kukua au kusinyaa kwa tabia husika.Kama familia,kwa mfano,haikemei tabia flani basi kuna uwezekano wa tabia hiyo kuonekana inakubalika.Lakini pia kuna vitu kama fedha ambapo mtoto analawitiwa kisha anapewa fedha inayoweza kumwaminisha kuwa alichofanya ni sahihi.Again,ni maelezo complicated sana na ni ya kitaaluma zaidi kuliko kimtaani.

Yote katika yote,ushoga na usagaji unazidi kushamiri katika jamii yetu licha ya 'jicho kali' la jamii.Je hiyo inamaanisha kuwa ukali huo dhidi ya tabia hiyo umeshindwa kuleta ufanisi?Tukiangalia suala hilo kwa mtazamo wa kisosholojia,inawezekana jibu lisiwe kuwa jamii imeshindwa bali ni ukweli kwamba katika jamii yoyote kuna uwezekano wa kuwepo tabia zisizokubalika.Hiyo ni katika kile wanasosholojia wanakiita deviance.Kila jamii ina walevi,wazinzi,vibaka,mafisadi,nk.Ni makundi yanayokwenda kinyume na kanuni na taratibu zinazoiongoza jamii husika.

Kwa huku nchi za Magharibi,ushoga na usagaji unazidi kuwa jambo la kawaida katika jamii.Lakini sio kirahisi hivyo kwani bado mashoga na wasagaji wanaangaliwa kwa 'jicho la shaka'.Na wao ni miongoni mwa makundi yanayolalamikia kubaguliwa.Hata hivyo,sheria zinawalinda na katika baadhi ya nchi hata ndoa zao zinatambulika kuwa ni ndoa halali.Lakini tena,kuwa na sheria ni kitu kimoja,na jamii kuiheshimu ni kitu kingine.Ni katika minajili hiyo,mashambulizi au uonevu dhidi ya mashoga na wasagaji si jambo geni katika nchi hizo.

Hawa wenzetu wanaamini kuwa mashoga na wasagaji hawastahili kubaguliwa,pasipo kujali kwanini mtu amekuwa shoga au msagaji.Na kinachoangaliwa hapo ni haki za binadamu.Wanasema ushoga au usagaji haumuondolei mtu haki zake kama mwanadamu.Je,kwa mtizamo huo wa Kimagharibi,ina maana jamii yetu huko nyumbani inawanyima haki wanajamii wenzao wanaojihusisha na ushoga na usagaji?Well,kuna wanaosema mila na desturi zetu zinapinga vitendo kama hivyo.Je mila hizo ziendelee kudumu hata kama zinawabagua baadhi ya wanajamii?Binafsi sina jibu sahihi bali nadhani swali hilo linabaki mikononi mwa jamii yetu.

Sijui wewe msomaji unaonaje lakini mie binafsi,nikiweka kando imani yangu ya Kikatoliki,sijali sana namna gani mtu anatumia uhuru wake wa kijinsia alimradi hanikwazi kwa namna yoyote.Naweza kutamka bayana kuwa namchukia zaidi fisadi anayekwaza maendeleo ya nchi yangu kuliko shoga au msagaji anayefanya anachoamini ni sahihi kwake.Lakini hiyo sio kusema naunga mkono vitendo hivyo hasa kwa vile imani yangu kiroho haiafiki.

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.