27 May 2016


Makala hii imechapishwa katika toleo la wiki hii la gazeti la RAIA MWEMA lakini tovuti ya gazeti hilo haijaweka habari mpya, kwahiyo nimeonelea ni vema nikiitundika hapa (na sina hakika lini Raia Mwema wata-update tovuti yao). Kichwa cha habari cha makala hii gazetini kinaweza kuwa tofauti na hiki nilichotumia kwenye blogu. 

Ijumaa iliyopita itabaki kuwa siku ya kumbukumbu kwa muda mrefu katika siasa za nchi yetu na medani nzima ya uongozi wa taifa letu. Siku hiyo, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi mno, Rais wa nchi yetu alimtimua waziri wake mwandamizi ‘bila kuuma maneno’

Tukiweka kando zama za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, tangu tupate uhuru hadi alipong’atuka mwaka 1985, kipindi ambacho kutokana na urefu wake kilishuhudia majeruhi kadhaa wa kisiasa, kwa zaidi ya miaka 30 Tanzania yetu haijashuhudia kulichofanywa na Rais Dkt John Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita ‘alipomtumbua’ aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kwa kosa la kuingia bungeni akiwa amelewa.

Uzito wa hatua hiyo unatokana zaidi na mambo makuu matatu. Kwanza, Kitwanga ni rafiki wa muda mrefu wa Rais Magufuli, na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alimtambulisha kama mtu anayemfahamu vizuri, waliyesoma pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Bila kujali uzito wa kosa la Kitwanga, ilihitaji ujasiri mkubwa kwa Magufuli kumtimua ‘hadharani’ rafiki yake huyo.

Pili, uzito wa hatua hiyo unatokana na hicho nilichokiandika katika paragrafu iliyotangulia; katika miaka 10 ya utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, miaka 10 ya utawala wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, na miaka 10 iliyomalizika mwaka jana ya utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne, hakujawahi kutokea hatua kama hiyo aliyochukua Rais Magufuli.

Kila ilipojitokeza kasoro ya kiutendaji, marais waliotangulia waliishia aidha kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri pasipo maelezo ya kutosha kuwa “uwaziri wa flani umetenguliwa kwa sababu flani” au pengine waziri kutolewa wizara moja na kupelekwa wizara nyingine. Na hali hiyo ya ‘boronga hapa uhamishiwe kule’ ilikuwepo pia katika zama za Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Kwa kifupi, Dokta Magufuli amevunja mwiko wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu mno, na kwa hilo tu anastahili kila aina ya pongezi, sio tu kwa sababu ya kuandika upya historia ya taifa letu bali ukweli kwamba hatua hiyo inamtambulisha Rais wetu kama mtu anayeweka mbele zaidi maslahi ya taifa letu kuliko maslahi binafsi.

Tatu, miaka nenda miaka rudi, baada ya kuingia kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, marais wetu kama wenyeviti wa chama tawala CCM, wamekuwa wakijitahidi kadri wawezavyo kujifanya ‘viziwi’ kila zinapojitokeza ‘kelele’ kutoka vyama vya upinzani. Kabla ya ‘kutumbuliwa,’ baadhi ya vyama vya upinzani vilikuwa vikimlalamikia Rais Magufuli kuwa ‘anamlinda Kitwanga’ kuhusiana na kashfa ya ufisadi ya Lugumi, na vilikuwa vikipiga kelele kumtaka ‘amtumbue’ Kitwanga.

Sasa, katika mazingira ya kawaida tu, ingeweza kuwa vigumu kwa Dkt Magufuli kumtimua Kitwanga kwa kuhofia “kuwapa wapinzani ushindi wa bure” katika suala hilo. Kwamba, wapinzani wangeweza kujigamba kuwa shinikizo lao ndio limepelekea Rais ‘kumtumbua’ rafiki yake.

Na katika hilo, ni muhimu kutambua kuwa Dkt Magufuli “ana wabaya wake ndani ya CCM,” na angeweza kuchelewa kumtimua Kitwanga kwa vile “wabaya wake hao” wangeweza kutafsiri kitendo hicho kama udhaifu, kwa maana ya “kuendeshwa na kelele za Wapinzani.”

Kwa kiwango kikubwa, hatua hiyo ya Dkt Maguguli imepokelewa vizuri na Watanzania wengi, hasa ikizingatiwa kuwa licha ya ‘kumtumbua Kitwanga,’ suala zima la kuchukua hatua stahili pale inapohitajika ni kama kitu kigeni kwa wananchi wengi, ikizingatiwa kuwa kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa ikiongozwa kwa siasa za kulindana. Kwahiyo, ahadi za Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na baada ya kuapishwa kuwa rais, kwamba hatomwonea aibu mtu yeyote zimethibitika zaidi katika suala hilo la ‘kumtumbua’ Kitwanga.

Hata hivyo, Tanzania yetu imegawanyika kuliko wengi tunavyoiona. Na mgawanyiko mkubwa wa nchi yetu ni athari ya moja kwa moja ya uchaguzi mkuu uliopita. Kuna kundi kubwa tu la wenzetu ambao hadi dakika hii hawataki kuamini kuwa “mgombea wao alishindwa.” Hapa namzungumzia mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa. Sasa kwa wenzetu hao, Dkt Magufuli sio tu “hakushinda kihalali” bali pia ni “dikteta anayetumbua watu bila kuzingatia sheria, mwenye jazba, nguvu ya soda” na kila baya unaloweza kumuongelea kiongozi.

Waungwana hawa walikuwa wakipiga kelele mno kumtaka Rais amwajibishe ‘swahiba wake’ Kitwanga ili kuwezesha uchunguzi wa kashfa ya Lugumi ufanyike kwa ufanisi zaidi hasa kwa vile nafasi ya Kitwanga kama Waziri mwenye mamlaka juu ya Jeshi la Polisi ingeweza kuathiri uchunguzi huo.

Akina sie pia tulimshauri Rais afikiri kutengua uwaziri wa Kitwanga, lakini tunapopishana na wenzetu hao ni kwamba hata baada ya Rais “kusikiliza kilio cha kumtaka amtumbue Kitwanga” bado wanamlaumu. Baadhi wanadai kuwa “kumtumbua Kitwanga ili kuuwa suala la Lugumi.” Wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai “suala hilo ni mchezo wa kuigiza usioingia akilini.” Wanasema eti “Kitwanga ametolewa kafara ili kuwanusuru vigogo flani.”

Lawama kwa Dkt Magufuli hata baada ya kuweka kando urafiki na kuchukua hatua stahili dhidi ya swahiba yake, zinaweza kumvunja moyo. Tukumbuke, yeye ni binadamu kama sie. Na ni wazi, unapokubali lawama kutoka kwa mtu wako wa karibu ili tu kukidhi matakwa ya jamii, kisha ukaishia kulaumiwa na baadhi ya wanajamii, inavunja moyo. Hata hivyo, ninatumaini kuwa Dkt Magufuli hatoyumbishwa na lawama hizo. Kimsingi, zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo kwa sababu tatizo sio anachofanya bali imani fyongo ya “wenzetu” kuwa aliyepaswa kuwa rais ni yule “mtu wao.”

Kama kuna lawama au kasoro inayoweza kujadiliwa basi ni kuhusu utaratibu wa kiusalama uanaofahamika kama “vetting.” Kabla ya kuteuliwa, jina la Kitwanga lilipelekwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa ajili ya kufanyiwa vetting. Swali, je Idara hiyo ilishindwa kubaini kuwa “Kitwanga ana kasoro ya ulevi ambayo sio tu ingeweza kuathiri utendaji kazi wake bali pia ingeweza kuhatarisha usalama wa taifa”? Je inawezekana kuwa Idara hiyo ilitekeleza jukumu lake ipasavyo lakini ‘mfanya uteuzi’ akapuuzi ushauri wa mashushushu hao?

Huu sio muda wa kunyoosheana vidole. Kama Idara yetu ya Usalama wa Taifa ilizembea kwenye vetting basi na ijirekebishe haraka. Kama ‘mfanya uteuzi’ alipuuzia ushauri wa mashushushu hao basi ameshapata funzo muhimu.

Ikumbukwe kuwa hadi muda huu hatufahamu kuwa ‘tatizo la ulevi wa Kitwanga’ limeathiri vipi utendaji wake wa kazi kama Waziri wa wizara nyeti ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kiusalama, hakuna kitu majasusi kutoka nchi za nje wanaombea kama kukutana na mtendaji wa serikali katika eneo nyeti ambaye ana udhaifu kama huo wa ulevi. Na ninaamini kuwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa wanafahamu fika jinsi majirani zetu walivyojaza majasusi ndani ya Tanzania yetu, hususan baada ya ujio wa Dkt Magufuli unaoanza kuifanya nchi yetu kuwa tishio kiuchumi kwa majirani zetu.

Ni matumaini yangu makubwa kuwa kutafanyika uchunguzi wa kina kuhakikisha kuwa mapungufu ya Kitwanga hayakuathiri usalama wa taifa letu kwa maana ya kwamba hakuna aliyetumia ‘ulevi wake’ kum- “blackmail” ili atoe siri za serikali.

Kiu kubwa kwa Watanzania kwa muda huu ni kuona Bunge litachukua hatua gani dhidi ya ‘mwenzao.’ Hata hivyo, ishara mbaya zimeanza kuonekana baada ya Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, kunukuliwa akidai kuwa “hakuna kifungu chochote cha kanuni za Bunge kinachomzuwia mtu kuingia Bungeni akiwa amelewa.” Yaani hawa waheshimiwa wana kinga dhidi ya Kanuni za Utumishi wa Umma zinazokataza “tabia inayovunja heshima ya utumishi kwa umma hata nje ya mahali pa kazi” kwa mfano ulevi.

Lakini kubwa zaidi ni kuona kuwa ‘kutumbuliwa’ kwa Kitwanga haukuathiri uchunguzi wa suala tete la Lugumi. Kimsingi, kwa kutolewa uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamati Teule ya Bunge inayochunguza suala hilo sasa haina kisingizio chochote cha kutowapatia Watanzania kile wanachostahili: ukweli kamili kuhusu suala hilo.
Nimalizie makala hii kwa kumpongeza Rais Dkt Magufuli kwa kuwakumbusha watendaji wote wa serikali kuwa “zama za nchi kujiendesha yenyewe (autopilot) zimekwisha, na sasa ‘Hapa Ni Kazi Tu’.” Kwamba kiongozi atakayezembea atatumbuliwa bila kuonewa haya. Kadhalika, hongera nyingi kwa Rais wetu kwa kuweka mbele zaidi maslahi ya taifa kuliko maslahi binafsi, umekubali lawama kuliko fedheha. Mwenyezi Mungu akulinde katika utendaji kazi wako, wenye hila mbaya washindwe na uendelee kuwatumikia Watanzania kwa uwezo wako wote.

Mungu Mbariki Rais wetu Dkt John Magufuli.
Mungu Wabariki Watanzania wote wenye kuitakia mema nchi yetu.

Mungu Ibariki Tanzania.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.