Makala hii imechapishwa katika toleo la wiki hii la gazeti la RAIA MWEMA lakini tovuti ya gazeti hilo haijaweka habari mpya, kwahiyo nimeonelea ni vema nikiitundika hapa (na sina hakika lini Raia Mwema wata-update tovuti yao). Kichwa cha habari cha makala hii gazetini kinaweza kuwa tofauti na hiki nilichotumia kwenye blogu.
Ijumaa iliyopita itabaki kuwa siku ya
kumbukumbu kwa muda mrefu katika siasa za nchi yetu na medani nzima ya uongozi
wa taifa letu. Siku hiyo, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi mno, Rais wa
nchi yetu alimtimua waziri wake mwandamizi ‘bila kuuma maneno’
Tukiweka kando zama za utawala wa Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, tangu tupate uhuru hadi alipong’atuka mwaka
1985, kipindi ambacho kutokana na urefu wake kilishuhudia majeruhi kadhaa wa
kisiasa, kwa zaidi ya miaka 30 Tanzania yetu haijashuhudia kulichofanywa na
Rais Dkt John Magufuli mwishoni mwa wiki iliyopita ‘alipomtumbua’ aliyekuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga kwa kosa la kuingia bungeni
akiwa amelewa.
Uzito wa hatua hiyo unatokana zaidi na
mambo makuu matatu. Kwanza, Kitwanga ni rafiki wa muda mrefu wa Rais Magufuli,
na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, alimtambulisha kama mtu
anayemfahamu vizuri, waliyesoma pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Bila
kujali uzito wa kosa la Kitwanga, ilihitaji ujasiri mkubwa kwa Magufuli
kumtimua ‘hadharani’ rafiki yake huyo.
Pili, uzito wa hatua hiyo unatokana na
hicho nilichokiandika katika paragrafu iliyotangulia; katika miaka 10 ya
utawala wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, miaka 10 ya utawala
wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa wa Awamu ya Tatu, na miaka 10 iliyomalizika
mwaka jana ya utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete wa Awamu ya Nne,
hakujawahi kutokea hatua kama hiyo aliyochukua Rais Magufuli.
Kila ilipojitokeza kasoro ya kiutendaji,
marais waliotangulia waliishia aidha kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri
pasipo maelezo ya kutosha kuwa “uwaziri wa flani umetenguliwa kwa sababu flani”
au pengine waziri kutolewa wizara moja na kupelekwa wizara nyingine. Na hali
hiyo ya ‘boronga hapa uhamishiwe kule’ ilikuwepo pia katika zama za Awamu ya
Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Kwa kifupi, Dokta Magufuli amevunja
mwiko wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu mno, na kwa hilo tu anastahili kila
aina ya pongezi, sio tu kwa sababu ya kuandika upya historia ya taifa letu bali
ukweli kwamba hatua hiyo inamtambulisha Rais wetu kama mtu anayeweka mbele
zaidi maslahi ya taifa letu kuliko maslahi binafsi.
Tatu, miaka nenda miaka rudi, baada ya
kuingia kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi, marais wetu kama wenyeviti wa
chama tawala CCM, wamekuwa wakijitahidi kadri wawezavyo kujifanya ‘viziwi’ kila
zinapojitokeza ‘kelele’ kutoka vyama vya upinzani. Kabla ya ‘kutumbuliwa,’
baadhi ya vyama vya upinzani vilikuwa vikimlalamikia Rais Magufuli kuwa
‘anamlinda Kitwanga’ kuhusiana na kashfa ya ufisadi ya Lugumi, na vilikuwa
vikipiga kelele kumtaka ‘amtumbue’ Kitwanga.
Sasa, katika mazingira ya kawaida tu,
ingeweza kuwa vigumu kwa Dkt Magufuli kumtimua Kitwanga kwa kuhofia “kuwapa
wapinzani ushindi wa bure” katika suala hilo. Kwamba, wapinzani wangeweza
kujigamba kuwa shinikizo lao ndio limepelekea Rais ‘kumtumbua’ rafiki yake.
Na katika hilo, ni muhimu kutambua kuwa
Dkt Magufuli “ana wabaya wake ndani ya CCM,” na angeweza kuchelewa kumtimua
Kitwanga kwa vile “wabaya wake hao” wangeweza kutafsiri kitendo hicho kama
udhaifu, kwa maana ya “kuendeshwa na kelele za Wapinzani.”
Kwa kiwango kikubwa, hatua hiyo ya Dkt
Maguguli imepokelewa vizuri na Watanzania wengi, hasa ikizingatiwa kuwa licha
ya ‘kumtumbua Kitwanga,’ suala zima la kuchukua hatua stahili pale
inapohitajika ni kama kitu kigeni kwa wananchi wengi, ikizingatiwa kuwa kwa
muda mrefu nchi yetu imekuwa ikiongozwa kwa siasa za kulindana. Kwahiyo, ahadi
za Dkt Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na baada ya kuapishwa kuwa
rais, kwamba hatomwonea aibu mtu yeyote zimethibitika zaidi katika suala hilo
la ‘kumtumbua’ Kitwanga.
Hata hivyo, Tanzania yetu imegawanyika
kuliko wengi tunavyoiona. Na mgawanyiko mkubwa wa nchi yetu ni athari ya moja
kwa moja ya uchaguzi mkuu uliopita. Kuna kundi kubwa tu la wenzetu ambao hadi
dakika hii hawataki kuamini kuwa “mgombea wao alishindwa.” Hapa namzungumzia
mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Edward Lowassa. Sasa kwa wenzetu hao, Dkt
Magufuli sio tu “hakushinda kihalali” bali pia ni “dikteta anayetumbua watu
bila kuzingatia sheria, mwenye jazba, nguvu ya soda” na kila baya unaloweza
kumuongelea kiongozi.
Waungwana hawa walikuwa wakipiga kelele
mno kumtaka Rais amwajibishe ‘swahiba wake’ Kitwanga ili kuwezesha uchunguzi wa
kashfa ya Lugumi ufanyike kwa ufanisi zaidi hasa kwa vile nafasi ya Kitwanga
kama Waziri mwenye mamlaka juu ya Jeshi la Polisi ingeweza kuathiri uchunguzi
huo.
Akina sie pia tulimshauri
Rais afikiri kutengua uwaziri wa Kitwanga, lakini tunapopishana na wenzetu hao
ni kwamba hata baada ya Rais “kusikiliza kilio cha kumtaka amtumbue Kitwanga”
bado wanamlaumu. Baadhi wanadai kuwa “kumtumbua Kitwanga ili kuuwa suala la
Lugumi.” Wengine wanakwenda mbali zaidi na kudai “suala hilo ni mchezo wa
kuigiza usioingia akilini.” Wanasema eti “Kitwanga ametolewa kafara ili
kuwanusuru vigogo flani.”
Lawama kwa Dkt Magufuli hata baada ya
kuweka kando urafiki na kuchukua hatua stahili dhidi ya swahiba yake, zinaweza
kumvunja moyo. Tukumbuke, yeye ni binadamu kama sie. Na ni wazi, unapokubali
lawama kutoka kwa mtu wako wa karibu ili tu kukidhi matakwa ya jamii, kisha
ukaishia kulaumiwa na baadhi ya wanajamii, inavunja moyo. Hata hivyo,
ninatumaini kuwa Dkt Magufuli hatoyumbishwa na lawama hizo. Kimsingi,
zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo kwa sababu tatizo sio anachofanya bali
imani fyongo ya “wenzetu” kuwa aliyepaswa kuwa rais ni yule “mtu wao.”
Kama kuna lawama au kasoro inayoweza
kujadiliwa basi ni kuhusu utaratibu wa kiusalama uanaofahamika kama “vetting.”
Kabla ya kuteuliwa, jina la Kitwanga lilipelekwa Idara ya Usalama wa Taifa kwa
ajili ya kufanyiwa vetting. Swali, je Idara hiyo ilishindwa kubaini kuwa
“Kitwanga ana kasoro ya ulevi ambayo sio tu ingeweza kuathiri utendaji kazi
wake bali pia ingeweza kuhatarisha usalama wa taifa”? Je inawezekana kuwa Idara
hiyo ilitekeleza jukumu lake ipasavyo lakini ‘mfanya uteuzi’ akapuuzi ushauri
wa mashushushu hao?
Huu sio muda wa kunyoosheana vidole.
Kama Idara yetu ya Usalama wa Taifa ilizembea kwenye vetting basi na
ijirekebishe haraka. Kama ‘mfanya uteuzi’ alipuuzia ushauri wa mashushushu hao
basi ameshapata funzo muhimu.
Ikumbukwe kuwa hadi muda huu hatufahamu
kuwa ‘tatizo la ulevi wa Kitwanga’ limeathiri vipi utendaji wake wa kazi kama
Waziri wa wizara nyeti ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kiusalama, hakuna kitu
majasusi kutoka nchi za nje wanaombea kama kukutana na mtendaji wa serikali
katika eneo nyeti ambaye ana udhaifu kama huo wa ulevi. Na ninaamini kuwa ndugu
zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa wanafahamu fika jinsi majirani zetu
walivyojaza majasusi ndani ya Tanzania yetu, hususan baada ya ujio wa Dkt Magufuli
unaoanza kuifanya nchi yetu kuwa tishio kiuchumi kwa majirani zetu.
Ni matumaini yangu makubwa kuwa
kutafanyika uchunguzi wa kina kuhakikisha kuwa mapungufu ya Kitwanga
hayakuathiri usalama wa taifa letu kwa maana ya kwamba hakuna aliyetumia ‘ulevi
wake’ kum- “blackmail” ili atoe siri za serikali.
Kiu kubwa kwa Watanzania kwa muda huu ni
kuona Bunge litachukua hatua gani dhidi ya ‘mwenzao.’ Hata hivyo, ishara mbaya
zimeanza kuonekana baada ya Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, kunukuliwa akidai
kuwa “hakuna kifungu chochote cha kanuni za Bunge kinachomzuwia mtu kuingia
Bungeni akiwa amelewa.” Yaani hawa waheshimiwa wana kinga dhidi ya Kanuni za
Utumishi wa Umma zinazokataza “tabia inayovunja heshima ya utumishi kwa umma
hata nje ya mahali pa kazi” kwa mfano ulevi.
Lakini kubwa zaidi ni kuona kuwa
‘kutumbuliwa’ kwa Kitwanga haukuathiri uchunguzi wa suala tete la Lugumi.
Kimsingi, kwa kutolewa uwaziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kamati Teule ya Bunge
inayochunguza suala hilo sasa haina kisingizio chochote cha kutowapatia Watanzania
kile wanachostahili: ukweli kamili kuhusu suala hilo.
Nimalizie makala hii kwa kumpongeza Rais
Dkt Magufuli kwa kuwakumbusha watendaji wote wa serikali kuwa “zama za nchi
kujiendesha yenyewe (autopilot) zimekwisha, na sasa ‘Hapa Ni Kazi Tu’.” Kwamba
kiongozi atakayezembea atatumbuliwa bila kuonewa haya. Kadhalika, hongera
nyingi kwa Rais wetu kwa kuweka mbele zaidi maslahi ya taifa kuliko maslahi
binafsi, umekubali lawama kuliko fedheha. Mwenyezi Mungu akulinde katika utendaji
kazi wako, wenye hila mbaya washindwe na uendelee kuwatumikia Watanzania kwa
uwezo wako wote.
Mungu Mbariki Rais wetu Dkt John
Magufuli.
Mungu Wabariki Watanzania wote wenye
kuitakia mema nchi yetu.
Mungu Ibariki Tanzania.