30 Sept 2017

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka juzi nilipata ujumbe kutoka kwa watu kadhaa wakinieleza kuwa kwa namna moja au nyingine niliwasaidia kufanya maamuzi ya kumpigia kura aliyekuwa mgombea wa CCM, John Magufuli.

Unajua, moja ya makosa makubwa waliofanya wana-UKAWA kwenye kampeni za uchaguzi huo ni kutojihangaisha kulifikia kundi muhimu la wapigakura nchini Tanzania: wananchi wasiofungamana na chama chochote.

Ili kulielewa vema kundi hili, inabidi kuangalia idadi ya wanachama wa CCM na UKAWA (kwa kuzingatia uchaguzi wa mwaka 2015). Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa CCM ina wanachama milioni 8. Makadirio ya idadi ya wanachama wa UKAWA ni angalau milioni 5. Kwahiyo makadirio ya jumla ya wapigakura wenye kufungamana na vyama vya siasa ni takriban milioni 13. Tanzania ina watu zaidi ya milioni 50, tukitoa hao milioni 13 tunabakiwa na watu milioni 37. Tukienda kwenye idadi ya waliojiandikisha kupiga kura walikuwa milioni 23 hivi. Kwahiyo, kimahesabu, takriban watu milioni 10 (milioni 23 waliojiandikisha kutoa milioni 13 wenye ufuasi wa vyama vya siasa) walikuwa wapigakura wasiojihusisha na chama chochote.

Tofauti na UKAWA ambayo viongozi na wanachama wake walielemea zaidi kuhamasishana wao kwa wao, wenzao wa CCM waliwalenga hao takriban milioni 10 wasiofungamana na chama chochote.

Na kimsingi, mie japo sikuwa mpigakura, nilikuwa katika kundi la watu wasio na vyama. Mara ya mwisho kuwa mwanachama wa chama cha siasa ilikuwa mwaka 2005, na takriban miaka 15 baadae, sheria ilinizuwia kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Mwaka 2006 nilianza kufuatilia skandali ya Richmond iliyokuwa ikimhusisha aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa. Naweza kwa uhakika kuwa nilikuwa bloga pekee niliyevalia njua suala hilo, sambamba na kuliandikia makala mbalimbali katika magazeti ya ‘Kulikoni’ na baadaye ‘Mtanzania’ na hatimaye Raia Mwema. Ufuatiliaji huo ulinigharimu mno lakini hilo si la muhimu kwa sasa.

Kutokana na bughudha niliyopata kuanzia mwaka 2006 na kuendelea, haikuwa ajabu kwa mie kuunga mkono harakati za Chadema kupambana na ufisadi. Na mwaka 2010 nilishiriki kikamilifu kumnadi mgombea urais wa Chadema, Dkt Wilbrord Slaa. Hata baada ya uchaguzi huo, niliendelea kuunga mkono sera hiyo ya ufisadi ya Chadema. Hata hivyo, sikuwahi kuwa mwanachama wa chama hicho.

Mwanzoni mwa mwaka 2015 nilikuwa miongoni mwa watu waliopiga kelele kwenye mitandao ya kijamii kuwataka UKAWA watangaze mgombea wao wa kiti cha urais mapema hasa ikizingatiwa kuwa CCM walikuwa na safari ndefu ya ‘kung’oana macho’ kugombea kuteuliwa na chama chao kuwania urais. Hata hivyo, kelele hizo hazikuzaa matunda, na utetezi mkubwa ulikuwa “UKAWA inajibidiisha kushughulikia daftari la wapigakura sambamba na kuhamasisha wapigakura watarajiwa kujiandikisha.” Hatimaye tulikuja kufahamu kuwa mbinu hiyo ya “kununua muda” ililenga kumwandalia nafasi Bwana Lowassa endapo asingepitishwa huko CCM. Muungano wa vyama makini vinne vya upinzani unasubiri ‘kapi’ kutoka chama tawala!

Kufupisha stori, mara baada ya UKAWA kumtangaza Lowassa kuwa mgombea wao, kwa sie wengine ilikuwa haiwezekani tena kuunga mkono umoja huo uliojumuisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Kwa vile wagombea wakuu katika uchaguzi huo walikuwa Lowassa na Magufuli, ilikuwa vigumu kumpinga Lowassa bila kumsapoti Magufuli. Kwahiyo japo awali nilijaribu kuepuka kumnadi mgombea wa CCM, Magufuli, mazingira yaliyokuwepo – pamoja na mkataba wa kutoa huduma ya usadi (consultancy) – ilipelekea nami nianze kumnadi Magufuli. Haukuwa uamuzi rahisi hasa kwa kuzingatia serikali ya CCM ilivyonitenda kuanzia mwaka 2006 nilipoanza kufuatilia skandali ya Richmond.

Ushiriki wangu kwenye kampeni haukuwa rahisi. Katika maisha yangu yote sikuwahi kutukanwa kiasi nilichotukanwa katika kampeni za uchaguzi huo. Jitihada zangu za kuwaelewesha watu kwanini nimelazimika kumuunga mkono Magufuli hazikusaidia kitu. Pengine kibaya zaidi ni kwamba wakati wa kuelekea uchaguzi huo nilifiwa na baba yangu, marehemu Mzee Philemon Chahali. Baadhi ya watu bila utu walitumia msiba huo kuingiza uhasama wa kisiasa.

Pamoja na mvua ya matusi ya kila aina, niliendelea na jukumu la kumnadi Bwana Magufuli. Nadhani mchango wangu mkubwa zaidi ulikuwa kwa wapigakura waliokuwa hawajafungama na chama chochote. Na nilifahamu kuhusu hilo baada ya uchaguzi ambapo baadhi yao walinieleza bayana kuwa ushawishi wangu kwao ulipelekea kufanya uamuzi wa kumpigia kura mgombea huyo wa CCM.

Lakini tukiweka kando ‘sababu zangu binafsi,’ Magufuli alionekana kama mgombea bora zaidi ya mpinzani wake Lowassa. Pamoja na sababu nyingine, wakati Magufuli alikuwa ‘mgombea wa CCM kutoka CCM,’ Lowassa alikuwa mgombea wa UKAWA kutoka CCM.

Hatimaye uchaguzi ukafanyika na Magufuli akaibuka mshindi. Kama kuna kitu kilichonipa matumaini sana kuhusu urais wa Magufuli ni hotuba yake aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa bunge la Jamhuri ya Muungano. Katika hotuba hiyo, Magufuli alionyesha kuwa mtu anayezielewa vema shida za Watanzania hususan janga la rushwa na ufisadi, na akaapa kushughulikia kwa nguvu zake zote. Na alipoomba Watanzania wamwombee katika vita hiyo ngumu, naamini hata miongoni mwa wale ambao hawakumpigia kura waliitikia wito huo wa kumfanyia maombi.

Kisha zikaja ziara ya kushtukiza na taratibu tukaanza kuingiwa na matumaini mapya ya “mrithi halisi wa Nyerere/Sokoine.” Na dunia pia ikaungana nasi kusherehekea kiongozi huyo adimu, na ikaibuka alama ya reli #WhatWouldMagufuli Do iliyotamba kila kona ya dunia. Na haikupita wiki bila kushuhudia “tumbua majipu.”

Kwa kufurahishwa na kuridhishwa na utendaji wake, mie ‘nikajipinda’ na kuandika kitabu cha tathmini ya urais wa Magufuli, siku 55 tu baada ya yeye kuapishwa kuwa Rais wa tano wa Tanzania. Watu kadhaa walinikosoa kwamba haikuwa sahihi kwangu kufanya tathmini hiyo mapema kiasi hicho. 


Kwa wakati huo niliona walionikosoa kuhusu suala hilo kama watu wenye chuki binafsi dhidi ya ‘mkombozi’ Magufuli.

Dalili ya kwanza kwamba huenda kuna walakini katika utawala wa Magufuli ni pale alipotangaza baraza lake la mawaziri ambalo ilituchukua wiki kadhaa kulisubiri. Lilipotangazwa, sio tu lilikuwa kubwa kuliko ahadi yake kuwa angeunda serikali ndogo tu ili kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali, bali pia lilijumuisha baadhi ya sura ‘zenye utata.’ Miongoni mwa sura hizo ni Profesa Muhongo, ambaye alilazimika kujiuzulu katika serikali ya Awamu ya Nne kutokana na kuhusishwa na skandali ya Tegeta Escrow.

Kuna tuliouona uteuzi wa mtu kama Nape Nnauye kuwa ni wa kisiasa zaidi, huku sura kama Simbachawene, Lukuvi na Profesa Maghembe zikijenga ishara kuwa huenda mambo hayajabadilika kama tulivyotarajia.

Kisha kukafanyika uteuzi wa mabalozi ambao ulionekana bayana kama kutumia nafasi hizo nyeti kuwaondoa watu flani kwenye nyadhifa zao huko CCM. Baadhi yetu tukaanza kujiuliza, “hivi hatujayashuhudia haya huko nyuma?” Lakini tukaendelea kuwa na matumaini.

Dalili ya kwanza kabisa kuwa pamoja na mazuri yake yaliyowavutia Watanzania wengi na kona mbalimbali duniani, Bwana Magufuli ana mapungufu yake ni pale serikali yake kupitia ‘shujaa wa sasa’ Nape Nnauye ilipozuwia haki ya mamilioni ya Watanzania kusikiliza matangazo ya moja kwa moja ya Bunge. Niwe mkweli, wanaomwona Nape shujaa huwa siwaelewi kabisa. Ningemwona shujaa laiti angetumia ukongwe wake ndani ya CCM kumweleza bosi wake Magufuli kuwa wazo la kuzuwia matangazo ya bunge live ni fyongo, na laiti Magufuli angemomea basi angejiuzulu kishujaa badala ya kusubiri kufukuzwauwaziri kwa kupambana na ‘kimeo kingine cha Magufuli’ yaani Daudi Albert Bashite.

Baadaye likaja zuwio dhidi ya mikutano na maandamano ya vyama ya siasa. Awali baadhi yetu tulijipa matumaini kwamba “ah huu ni muda wa kuchapa kazi. Hayo maandamano na mikutano ni ya nini muda huu?” Kwahiyo kwa wakati huo ili-make sense.

Mara tukakumbwa na janga la tetemeko la ardhi huko Kagera. Ikategemewa Rais angekwenda kuwafariji wahanga hasa ikizingatiwa kuwa anatoka Kanda ya Ziwa. Hakwenda hadi baadaye. Na alipokwenda akatoa hotuba isiyopendeza kuisikiliza. Maneno kama “serikali haikuleta tetemeko la ardhi” sio ya busara hata kidogo. Pia akaongopa kwa kudai hakuna serikali duniani inayotoa misaada kwa wahanga wa majanga ya asili. Sijui muda huu anajisikiaje akiona kwenye runinga jinsi serikali ya Marekani inavyowahudumia wahanga wa vimbunga.

Baadaye kukusikika taarifa mbalimbali za tishio la uhaba wa chakula, lakini badala ya kuwafariji wananchi, Magufuli akawaropokea kwamba serikali yake haitotoa chakula kwa vile serikali haina shamba.
Na wakati mmoja alipita sijui Nzega au Urambo, mwananchi mmoja akamwambia “njaa Mheshimiwa.” Hilo jibu alilotoa utadhani ugomvi. Pamoja na majibu mengine ya ngebe akasema “njaa, kwani mnataka niingie jikoni kuwapikia?” Ovyo kabisa.

Likatokea tukio la maaskari polisi wanane kuuawa huko Kibiti lakini Amiri Jeshi Mkuu akaenda kufungua mabweni chuo kikuu cha Dar es Salaama badala ya kwenda kuaga miili ya askari hao.

Pia kulijitokeza tukio la ‘kupotea’ kwa kada wa Chadema Ben Saanane ambaye hadi ‘kupotea’ kwake alikuwa akihoji kwa nguvu kubwa kuhusu PhD ya Magufuli. Baadhi tulimsihi awe makini (kwa sababu dalili zilishaanza kujionyesha kuwa Magufuli ni mtu wa aina gani) lakini bahati mbaya hakusikia ushauri wetu. Hadi leo haijulikani nini kimemsibu kijana huyo japo Chadema nao hawawezi kukwepa lawama katika poor handling ya suala hilo. Kumekuwa na kauli zinazokinzana kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho kama ile ya mwenyekiti Mbowe kuwa Ben alitekwa huku Mbunge wa chama hicho Saeid Kubenea akidai kuwa kada huyo anaonekana vijiweni. Kwanini chama hicho hakijawabana viongozi hao kufafanua kauli zao, only God knows!

Lakini kama kuna tukio lililompotezea heshima kubwa Bwana Magufuli ni lile la Mkuu wa Mkoa Paul Makonda kuvamia stesheni ya redio na runinga cha Clouds  akiwa na askari wenye silaha. Siku chache baadaye huku baadhi ya watu wakitarajia angemtimua Makonda, Magufuli akatufanya sote mabwege kwa kumtetea Makonda huku akidai yeye hapangiwi kazi, yeye ndo Rais, na kumwita Makonda mchapakazi. Yaani Mkuu wa Mkoa amevamia kituo cha habari, kitendo ambacho ni kosa la jinai, halafu Rais anamsifu kuwa ni mchapakazi?
Uswahiba wa Magufuli na Makonda umechangia mno ugumu wa kuchunguza tuhuma kuwa mkuu huyo wa mkoa amefoji jina analotumia pamoja na cheti cha kuhitimu kidato cha nne. Laiti Magufuli angekuwa mwajibikaji kama tunavyoamini basi angeamuru uchunguzi kuhusu suala hilo.

Na kwa wanaofahamu yanayoendelea ‘nyuma ya pazia,’ inadaiwa kuwa vetting aliyofanyiwa Bashite ilionyesha bayana mapungufu yanatajwa kumhusu yeye, na ‘Bwana mkubwa’ akashauriwa kuchukua hatua stahili lakini hakufuata ushauri huo.

Hili la Bashite limeendelea kuwakera watu wengi sana, hasa ikizingatiwa kuwa mtu huyo anatumia ipasavyo upendeleo anaopewa na Magufuli, na kufanya dharau za wazi kama ile ya kupigiwa saluti na vingozi wa ngazi za juu wa jeshi la polisi huku amevaa kapelo. Hiyo ni dharau ya hali ya juu kwa vyombo vyetu vya dola.



Na Magufuli ataingia kwenye vitabu vya historia kwa serikali yake kulifungia gazeti la kila wiki la Mwanahalisi kwa miaka mitatu, na siku 10 baadaye akalifungia gazeti jingine la kila wiki la Raia Mwema kwa siku 90. 

Na kama kuna gazeti lilijitahidi mno 'kumnadi' Magufuli ni Raia Mwema. Nakumbuka makala nyingi katika gazeti hilo wakati wa kuelekea kwenye uchaguzi zilisheheni habari 'nzuri' kuhusu Magufuli.

Pengine si vibaya nikitumia fursa hii kueleza kuwa sababu hasa iliyonifanya niache uandishi wa makala katika gazeti hilo ni kwamba lilihojiwa na 'vijana wa Magufuli' kuhusu mie lakini wahusika hawakuona umuhimu wa kunieleza wala kuandika kuhusu habari hiyo.


Na kilichopelekea bwege huyo kudadisi kuhusu mie ni TWEET...Yes, just a tweet, a #FutureTweet to be precise. 

Kanuni muhimu katika chombo cha habari ni kwamba unyanyasaji wa taasisi yoyote ile dhidi ya mwenzenu ni unyanyasaji dhidi yenu nyote. Gazeti hilo lilipaswa kunijulisha kuhusu kilichotokea au kukiandika kama habari gazetini. Lakini bahati nzuri mie mzoefu wa 'dark arts' nikafahamu mapema kilichokuwa kinaendelea.

Hata hivyo, kitendo cha gazeti hilo nilikiona kama usaliti, nikaamua kuachana nao. Hata hivyo, mie sina kinyong'o nao na ndio maana jana nililaani na kupiga kelele kuhusu hatua hiyo ya serikali.

Haya yanatokea wakati Tanzania bado ipo kwenye mshtuko kufuatia jaribio la kumuua mwanasiasa ambaye amekuwa mpinzani mkubwa wa Magufuli, mbunge wa Chadema Tundu Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria cha TLS. Chuki inayopandikizwa dhidi ya wapinzani imepelekea takriban asilimia 99 ya viongozi wa CCM kuogopa kwenda kumjulia hali Lissu huko Nairobi alikolazwa.

Lakini pengine kipimo halisi cha mambo kwenda kinyume na matarajio ya baadhi yetu kuhusu Magufuli ni kwamba tangu aingie madarakani, zaidi ya viongozi na wanachama 400 wa Chadema wamekamatwa na polisi. Imefika mahala, wakuu wa wilaya wanakamata viongozi wa Chadema kila wanapojisikia. Na pengine kibaya zaidi ni ukweli kwamba taratibu jamii inaanza kuzowea kuona viongozi na wanachama wa upinzani – hususan Chadema – wakidhalilishwa na kukamatwa kiholela.

Jambo jingine la kusikitisha kuhusu utawala wa Magufuli ni utitiri wa sheria kandamizi kuhusu uhuru wa habari. Licha ya sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo ni kazi ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, tayari kuna sheria ya Huduma za Habari, ambayo ‘shujaa Nape’ alihusika kwa kiasi kikubwa, na sasa kuna kinachoitwa ‘Kanuni za Maudhui ya Mitandao ya Kijamii,’ ambayo laiti zikipitishwa zitakuwa balaa kubwa.

Na huku Chadema ikishuhudia viongozi na wanachama wake wakinyanyaswa ovyo ovyo, kuna kila dalili kuwa mgogoro unaoendelea ndani ya chama cha CUF una mkono wa serikali hasa kwa kuzingatia mwenendo wa ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa (taasisi ya serikali) kuibeba waziwazi kambi ya mwanachama aliyejiuzulu kwa utashi wake Prof Lipumba, ambaye from nowhere alirudi chamani na kudai yeye bado mwenyekiti.

Majuzi, Magufuli katumwagia siri kwamba kuna siku aliombwa ushauri na Spika Ndugai kuhusu uteuzi wa wajumbe wa kamati ya bunge. Hiyo ina maana kuwa bunge limewekwa mfukoni na mhimili wa serikali. Kadhalika, kauli za Jaji Mkuu ‘mpya’  baada ya jaribio la mauaji dhidi ya Tundu Lissu zinajenga taswira ya mhimili wa mahakama nao kuwekwa mfukoni na mhimili wa serikali.

Katika kuhitimisha makala hii ndefu ninarudia swali lililobeba kichwa cha habari: nini kilichomsibu Magufuli hadi kubadilika kiasi hiki? Kauli yake kuwa alisukumwa kuchukua fomu ya urais inazidi kuleta mkanganyiko kwamba labda alikuwa anafahamu fika hana uwezo wa kuongoza taifa letu lakini akakubali tu kutokana na shinikizo hilo, ambalo hata hivyo hatujui limetoka kwa watu gani.

Dalili kwamba ‘Magufuli atabadilika’ (kurejea kuwa yule tuliyemwona ni mkombozi wetu) ni finyu. Kwa vile maamuzi yake mengi yanamtengenezea maadui zaidi ya waliopo, kuna kila dalili kwamba atazidi kuwa mkali ili ‘kujilinda.’ Tutegemee uhuru wa kujieleza/habari uendelee kubinywa zaidi kadri bwana mkubwa anavyozidi kutukumbusha yeye ndio Rais, asiyeambiwa nini cha kufanya, anayejua siri zote na nchi yetu, na vitu kama hivyo.

Nimalizie kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuhusu rai ya mara kwa mara ya Rais Magufuli kuwataka Watanzania tumwombee. Na tufanye hivyo kwa bidii kubwa ili Mwenyezi Mungu amwonyeshe njia sahihi ya kuliongoza taifa letu kwa kuzingatia haki na usawa. Tumwombee aondokane na 'fear of the unknown,' apate muda wa kupumzika badala ya kukesha macho akihofia 'the unknown.' Aachane na chuki dhidi ya kila anayemkosoa hata kama kukosoa huko ni kwa nia njema. Tumwombee awe na busara ya kutokitumia 'kitengo' kama kampuni yake binafsi. Ajiulize, kwanini licha ya ulinzi wake wa 'kufa mtu' bado siri zinavuja? Jibu jepesi: ukiwafanya watu wazima tena wenye utaalamu nyeti kuwa kama watoto, inakuwa 'mwaga ugali nimwage mboga.' Na asije kukasirishwa na makala hii...

Ni wazi kuwa ndoto za kuikomboa Tanzania yetu kiuchumi haziwezi kufanikiwa katika hali ya sasa ya siasa za vitisho, kunyanyasa wapinzani, “watu wasiojulikana,” na vitu kama hivyo. 

Mungu ibariki Tanzania


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.