8 Sept 2017



Jana, Septemba 07, 2017, majira ya mchana, zilipatikana taarifa kwamba Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Mbunge wa Singida Mashariki, Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, na Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), amepigwa risasi kadhaa na kujeruhiwa vibaya.

Tukio hilo la kutisha lilitokea jijini Dodoma, wakati Mbunge huyo aliposhuka nyumbani kwake eneo la Area D, inakoelezwa alienda kwa ajili ya kujipatia mlo wa mchana.

Kabla ya kuingia kiundani kwenye makala hii, nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwa Lissu, na kumwombea apone haraka. Salamu za pole pia kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema, chama ambacho Lissu amekuwa akikiwakilisha kwa ufanisi mkubwa.

Pia ni vema nitahadharishe mapema kwamba intelijensia sio sayansi timilifu kwa asilimia 100, kwa kimombo wanasema “intelligence is not an exact science.”

Okey, sasa tuingie mtamboni. Hadi muda huu kuna dhana za msingi tatu ambazo zinatokana na‘mchujo’ wa dhana mbalimbali.

Dhana ya kwanza na ambayo pengine ni maarufu zaidi ya zote ni kwamba jaribio hilo la mauaji ya Lissu lina mkono wa dola. Kwamba sio siri kuwa Lissu amekuwa ‘akiisumbua mno’ serikali, ambapo wafuasi wake wanamwona kama jasiri asiye na uoga wa kusema ukweli, ilhali wapinzani wake wakimwona kama mchochezi.

Yayumkinika kuhitimisha kwamba kama kuna mwanasiasa wa upinzani ambaye amekuwa ‘mwiba mchungu’ kwa serikali ya Rais John Magufuli basi si mwingine bali Lissu.

Na pengine kinachoongeza uzito kwenye dhana hii ni ukweli kwamba Agosti 18 mwaka huu, Lissu aliwaeleza wananchi kwamba anafuatiliwa.

Namnukuu "Naomba kabla sijaanza Mazungumzo yangu nimuombe Mkuu wa idara ya Usalama wa Taifa anaitwa Kipilimba au Inspekta Generali wa Polisi Simon Sirro, wale vijana ambao wamewatuma na kwa wiki tatu mfululizo wananifuata kila nilipo wanaotembea na gari ya Toyota premio namba T460CQV, jana niliwakaba Kanisani St. Peter's.



Kwa upande mwingine serikali ya Magufuli ni kama ilikuwa inatafuta ‘kulaumiwa bure.’ Kwa sababu, Hadi muda huu hakuna sababu moja ya msingi kwa serikali hiyo kuyafanya maisha ya wanasiasa wa upinzani yawe magumu kiasi hiki. Magumu kwa maana ya kuwanyima kila aina ya fursa ya kufanya siasa (political space).

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, zaidi ya viongozi na wafuasi 400 wa Chadema wameshakamatwa tangu Magufuli aingie madarakani. Mtu atayedai kuwa kiongozi huyo ‘anawachukia wapinzani’ hatoonekana mtu wa ajabu japo huenda akatupwa jela.

Katika hotuba zake mbalimbali, Rais Magufuli ameshindwa kuficha hisia zake dhidi ya upinzani na wapinzani. Juni 12 mwaka huu, Rais Magufuli alimweleza Spika Job Ndugai maneno yafuatayo

“Tumia mbinu hiyohiyo ya kuwafanya wasiropokee Bungeni, waropokee nje na kule tutadili nao vizuri kwasababu wanapokua kule ndani wana kinga wanaweza wakatukana chochote, sasa kinga wanayoitumia vibaya bungeni kainyooshe wewe. Wawe wanatoka kule bungeni, ukishamfukuza hata mwezi mzima… atakuja aropokee huku, na mimi nakueleza waache waropokee huku nitadili nao, wala siwatishi lakini hatuwezi kuwa kwenye vita wewe unaanza kugeuka kupiga wale wanaokwenda mbele…. ni nafuu unyamaze ukalale.”

Kwa kuangalia jinsi watendaji wa serikali ngazi za mkoa na wilaya wanavyochuana na polisi kuwanyanyasa wapinzani, hususan wa Chadema, dhana kuwa serikali ina mkono katika jaribio la mauaji ya Lissu ni kama ‘ready-made.’

Hata hivyo, pamoja na ‘dalili zote’ kuashiria uwezekano wa mkono wa serikali katika jaribio la kumuua Lissu, dhana hii inakosa mantiki kiuhalisia. Ni kwamba hakuna tija kwa serikali kumuua Lissu. Sawa, sio siri kuwa uhusiano kati ya serikali na Lissu/ wapinzani sio mzuri, lakini haitokuwa na tija yoyote kwa serikali ya Magufuli kumuua Lissu.

Na hata kama ingekuwa lazima ‘aondoke,’ basi kuna ‘njia mwafaka zaidi’ za mauaji ya watu maarufu (assassination), huku 'kifo cha ajali' ikiwa maarufu na rahisi zaidi.

Halafu kinachotatiza katika tukio la jana, na kinachopunguza zaidi nguvu ya dhana kwamba ‘kuna mkono wa serikali,’ ni jinsi waliofanya shambulio hilo walivyoonekana kama wanahitaji publicity ya kutosha. Kwanini? Jibu lipo kwenye uchambuzi wa dhana ya tatu.

Dhana ya pili ni dhaifu kuliko nyingine mbili. Hii inahusisha mbio za urais mwaka 2020. Kwamba kila siku Lissu amekuwa akijitengenezea mazingira ya mgombea mwafaka wa Chadema/Upinzani katika uchaguzi mkuu ujao, wala halina mjadala. Sio kwamba Lissu amekuwa hodari katika masuala mbalimbali kwa vile anataka urais (hajawahi kutamka nia ya kugombea nafasi hiyo) lakini umahiri wake bungeni na katika masuala ya kisheria na kitaifa kwa ujumla, unamfanya kuwa kipenzi cha takriban kila mfuasi wa Chadema.

Dhana hii dhaifu inasema kuwa jaribio hilo la mauaji ni kazi ya wapinzani wa kisiasa wa Lissu, hususan ndani ya chama chake.

Udhaifu wa dhana hii ni kwamba, kama ambavyo kwenye dhana ya kwanza, hakuna tija katika kumdhuru Lissu hadharani. Kwamba hata kama kungekuwa na lundo la wapinzani wa kisiasa wa Lissu huko kwenye chama chake, kwanini wafanye ‘operesheni’ hiyo waziwazi badala ya kuandaa mkakati wa siri?

Na kama ilivyokuwa kwenye dhana ya kwanza, hata kama wapinzani wa kisiasa wa Lissu ndani ya chama chake wangekuwa wahusika, kwanini basi tukio hilo lifanyike katika mazingira ya ‘kusaka publicity kwa nguvu’?

Hiyo inatuacha na dhana moja, ya tatu, na ya mwisho. Ya mwisho lakini sio haba katika mantiki. Dhana hii inaeleza kwamba jaribio hilo la mauaji limefanywa makusudi na kile wajuzi wa mambo wanaita ‘rogue elements.’  Hizi zilitusumbua sana katika utawala wa Awamu ya Nne wa Rais Jakaya Kikwete. Rogue elements hizi zinajumuisha watumishi halali wa vyombo vya dola wanaofanya shughuli zisizo halali. Nani anawatuma? Hiyo ni habari nyingine.

Kuna kitu kinachofahamika kama ‘Deep state.’ Kila nchi ina tafsiri yake kuhusu ‘deep state’ lakini tafsiri nyepesi kwa mazingira yetu ni ushirika wa watu wenye nguvu katika serikali na jamii – mfano vigogo (hususan wa zamani) wa vyombo vya dola, wafanyabiashara wenye uwezo mkubwa na wanasiasa kutoka upande wowote ule, lakini zaidi chama kilichopo madarakani.

Dhana hii inaliona tukio la kujaribu kumuua Lissu kama njia rahisi ya kuichafua serikali ya Rais Magufuli, ambayo kwa bahati mbaya/makusudi ilishajitengenezea mazingira ya kulaumiwa pindi la kutokea likimtokea mwanasiasa wa upinzani kama Lissu. Rais anaposhindwa kudhibiti ‘chuki zake’ dhidi ya wapinzani, anawapa nafasi nzuri ‘wabaya wake’ kutenda kitu kisha ikawa rahisi tu lawama kuelekezwa kwake.

Ndio maana dhana ya kwanza – kwamba kuna mkono wa serikali ya Magufuli kwenye jaribio la kumuua Lissu – inaonekana kama yenye uzito kwa vile "kuna sababu ready-made.”

Dhana hii inapata uzito kutokana na ukweli kwamba Magufuli amejitengenezea maadui wengi, wenye nguvu, na baadhi yao wakiwa viumbe hatari. Kuna watu waliozowea kuishi maisha ya kifalme ambao sasa wanalazimishwa kuishi maisha ya kawaida. Hawa watu wakipata upenyo wa kumdhuru Magufuli, hawatosita kufanya hivyo.

Lakini kwa vile ni ‘vigumu mno’ (angalau kwa wakati huu) kufanikisha jaribio la kumdhuru kiongozi huyo, njia nyepesi inaweza kuwa katika ‘kuua character yake,’ ambayo bahati nzuri kwa ‘wabaya wake,’ sio nzuri sana.

Kumekuwa na malalamiko kadhaa hasa kutoka upande wa upinzani kumtuhumu Magufuli kuwa ni dikteta. Na ukifuatilia mwenendo wa siasa zetu kwa muda huu, sio siri kwamba kuna chembe chembe za udikteta. Kwahiyo, ni rahisi kwa ‘wabaya wa Magufuli’ kutumia mwanya huo kujenga picha ya “serikali ya dikteta yamuua mpinzani wake mkubwa.”

Na hilo linatuleta kwenye suala la publicity. Kwamba jaribio la mauaji hayo liwe na mwangwi wa kutosha ndani na nje ya Tanzania. Mwangwi huo ni wa makusudi ili uakisi taswira inayojengeka kuwa ‘Magufuli ni dikteta. Na madikteta hunyanyasa wapinzani wao, na ikibidi hata kuwaua.’

Kwahiyo, kama kuna funzo kubwa kwa Magufuli katika tukio hili ni kuepuka mazingira yaliyopo ya uhasama mkubwa dhidi ya upinzani hususan Chadema. Kiongozi huyo anatambua fika kwamba kuna watu wapo radhi kufanya lolote lile kumng’oa, na kwa vile ‘njia za kawaida’ sio rahisi, basi inakuwa ‘anything goes,’ liwalo na liwe.

Na dhana hii ya tatu inaleta uhusiano kati ya tukio la jana la jaribio la kumuua Lissu na lile la hivi karibuni la kuchomwa moto kwa ofisi za kampuni ya uwakili wa IMMA. Kama hili la Lissu, tukio la moto nalo lilifanyika katika mazingira ya kuvutia publicity, yaani kama kulikuwa na jitihada za makusudi za kuushawishi umma kwamba “mnaona huyu dikteta Magufuli anakoelekea? Sasa anachoma hadi ofisi wa ‘wabaya’ wake.”

Nihitimishe uchambuzi huu kwa kueleza bayana masuala mawili matatu. Kwanza, lengo la uchambuzi huu mfupi sio kuingilia kazi za vyombo vya dola vinavyoendelea na uchunguzi kuhusu jaribio la kumuua Lissu. Nimefanya uchambuzi huu kama mtu mwenye uelewa wa masuala ya intelijensia na siasa za Tanzania yetu, ikiwa ni pamoja na “yanayojiri nyuma ya pazia.”

Pili, lengo la uchambuzi huu sio kumshawishi mtu yeyote abadili mtazamo wake kuhusu “nani ana/wanahusika.”

Mwisho, kama nilivyotanabaisha awali, tasnia ya intelijensia sio sayansi kamilifu kwa asilimia 100 (intelligence is not an exact science). Kwa maana hiyo, japo uchambuzi huu ni karibu kabisa na hali halisi, sio rahisi sana kufikia hali halisi yenye uhakika wa asilimia 100.

Nimalizie kwa kumtakia afya njema Bwana Lissu huku nikiamini kuwa malaka husika zitafanya kila jitihada kuwanasa wahusika, sio tu kwa minajili ya serikali kujinasua bali ili Bwana Lissu atendewe haki.

9 comments:

  1. Nimependa sana ulivyofanya chambuzi hii ndugu yangu. Kwanza inatoa picha na wanga juu ya jaribio la kuuwawa kwa lisu ila katika nyanza nyingi ikiwemo hizo tatu ulizo ongelea. Nimejifunza vyema kabisa

    ReplyDelete
  2. Nakubaliana na uchambuzi huu kwa asili mia mia moja. Hakuna serikali duniani inayoweza kufanya kitendo hiki kwenye mazingira yale yaliyofanyika nyumbani kwa Lissu. Isitoshe Lissu has never been a threat neither to the Government nor to the president. Why should the government have a hand in this? Nina amini kabisa kuwa wahalifu hao watakamatwa na ukweli utajulikana tu maana ninajua jinsi serikali yetu inavyo fanya kazi yake. Natoa pole kwa Lissu (na familia yake yote), na pia kwa Raisi wetu na wananchi wote wa Tanzania. Nakuomba Raisi usikatishwe tamaa na dhana hizi.

    ReplyDelete
  3. Ahsante kwa uchambuzi bwana Chahali

    ReplyDelete
  4. Tukio hili linafanana na tukio la kuuwawa kwa mwanaharakati malcom x 1964

    ReplyDelete
  5. "Deep state" "Killing JPM character" nimeBold key words. ila kwanini Binadamu tu katili hivi? the shooter was proffesional Sniper either hired from external or local bandit group.

    ReplyDelete
  6. Ahsante sana kaka kwa uchambuzi yakinifu, naomba kuongeza moja, jana Dola ilikuwa inapokea ripoti ya kamati ya Bunge kuhusu Almasi na Tanzanite, hawa wawekezaji wetu wanaweza kuwa hawafurahishwi na utendaji huu wa Serikali haswahaswa kwa kupokea hizo ripoti wazi na media zote zikarusha. Zile athali walizopata Barrick na Accasia zingeweza kuwapata nao pia,kwa maana hiyo wangeweza kutengeneza tukio ambalo lingiweza kuzima ripoti hizo kutacle media za ndani na nje. Naona mpaka ABC TV wamerusha tukio la Lissu ukiachia BBC , Aljazeera na CNN.

    ReplyDelete
  7. Umechanganua vizuri ila kama ulivyo kometi mwanzo kuwa haiwez kuwa asilimia mia! Hapo kwenye dhana ya pili haipo poa, sababu kuu hii hapa. Kama ni chama chake basi ilikuwa rahisi sana kwa serikali kubaini na kitu kigne ambacho kinatia ukakasi ni sehemu aliyopigiwa, wlinzi wa pale wasinge mute! Mkuu njugu 38 zinapigwa mfurulizo neighbors security never showed their face kweli,ata mbwa koko hayupo hivyo!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.