10 Oct 2006

Mbona mambo!?

1 comment:

  1. Lowassa hajawaziba mdomo Wabunge!

    • Vikao vya Wabunge wa CCM ni kwa mujibu wa kanuni zao
    • Hawaumbui Watendaji wilayani ila wanajiumbua wenyewe kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo
    • Agizo lake la elimu limeingiza wanafunzi wa ziada 50,000 Sekondari katika miezi mitatu

    Nimesoma kwa mshangao mkubwa makala yenye kichwa cha habari “Lowassa: Kuwaziba midomo Wabunge ni sawa na kuwaziba midomo wananchi”. Makala hiyo imeandikwa na Evarist Chahali, kutoka Scotland, kwenye gazeti lako la KULIKONI la Novemba 3-9, 2006 katika ukurasa wa 7 wa safu ya “Habari kutoka Ughaibuni”.

    “Anachoogopa ni nini kuhusu Wabunge kujadili suala la mgao wa umeme?” iliandikwa katika nyongeza ya kichwa cha habari cha makala hiyo. Nyongeza hiyo ya kichwa cha habari imeendelea: “Kuna ugumu gani kwa Lowassa kuwaita ofisini kwake au kuwapigia simu au hata kuwaandikia barua kuwaonya watendaji anaowaona wanakwenda ndivyo sivyo badala ya kutumia mikutano ya hadhara kuwaumbua?”

    Siyo busara kuziacha hoja hizo bila kujibiwa. Kwanza, kuna hoja mbili zinapingana. Ya kwanza ni kwamba eti Waziri Mkuu anajaribu “kuwaziba midomo Wabunge” kwamba wasipate hata nafasi ya kukutana na kukubaliana msimamo wa pamoja. Ya pili, Waziri Mkuu “anawaumbua watendaji hadharani” na, kwa mujibu wa mwandishi, afadhali angewaita ofisini kwake na kuongea “faragha ki-utu uzima…”. Isitoshe, hoja ya tatu ni ile ya kukebehi agizo la Waziri Mkuu, ambalo Chahali analiita “amri zake (Waziri Mkuu) anazotoa kwa namna ya zimamoto”, kwamba kila mwanafunzi aliyefaulu mtihani wa elimu ya msingi mwaka jana awe ameingia sekondari, limebadilisha vipi maisha ya Watanzania.

    Ni dhahiri kwamba kwa kutoa hoja hizo mbili zinazopingana – “kuwaziba mdomo Wabunge” na “kuwaumbua hadharani watendaji” na kuhoji mafanikio ya agizo kuhusu kuwapeleka wanafunzi wengi sekondari, bila ya kuwa na uelewa wa hoja zenyewe na bila ya kufanya utafiti na kuwa na takwimu sahihi, dhamira ya mwandishi iko wazi: ni kutaka kumsakama bure Waziri Mkuu Edward Lowassa.

    Kwa nini? Kwa sababu, kwanza, Waziri Mkuu hajawahi, hatawahi na wala hawezi kuwaziba mdomo Wabunge. Hicho kilichobuniwa na kuandikwa kuwa ni “kuwaziba mdomo Wabunge” siyo ukweli bali ni upotoshaji uliotokana na tafsiri mbovu, ya makusudi au kwa kutokujua, au yote hayo mawili, ya mwandishi wa gazeti alilolinukuu Chahali. Ni dhahiri Chahali anawadhalilisha Wabunge kwa

    …/2
    kusema wanazibwa midomo. Laiti angelijua, aina ya Wabunge waliopo, sio watu
    wa kuzibwa midomo na mtu yeyote.

    Pili, Waziri Mkuu Lowassa kamwe hawaumbui wala kuwakemea watendaji hadharani. Kinachotokea ni kwamba baadhi ya watendaji hao huwa wanajiumbua wenyewe kwa kudhihirisha mbele ya kadamnasi ya watu kushindwa kwao kuwajibika ipasavyo pale wanapojibu kero za wananchi zinazotolewa katika mikutano ya hadhara. Kwa mfano, Ofisa Elimu, anaposhindwa kutoa takwimu za shule katika Wilaya yake!

    Tatu, agizo la Lowassa alilolitoa Januari mwaka huu kuhusu wanafunzi waliofaulu kuingia kidado cha kwanza, limeleta mafanikio makubwa na ya ajabu: jumla ya wanafunzi 50,715 wameongezeka na kuingia sekondari katika kipindi cha miezi mitatu tu na kuvusha kutoka asilimia 45.9 ya wanafunzi waliokuwa wamechaguliwa awamu ya kwanza mwezi Desemba na kufikia asilimia 62.5 ilipofika Machi mwaka huu. Na kama ingekuwa shule zinaandikisha wanafunzi bila ya kufuata mihula maalum, basi leo hii asilimia hiyo ingekuwa juu zaidi. Ni vigumu kwa Chahali kutambua haya maana yeye, tunafahamu, anafaidi elimu nje ya nchi kwa gharama za maskini wa nchi hii ambao Waziri Mkuu ndio anawahangaikia wafanane na watu wengine duniani.

    Kwa hoja ya kwanza, kwa mfumo wetu, haiwezekani kuwaziba mdomo Wabunge. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wote wa chama kinachotawala na wa vyama vya upinzani, wako huru, tena kwa kiwango cha juu, kuikosoa Serikali katika utendaji wake. Ukiacha kutunga sheria, kuihoji serikali ni moja ya wajibu wa Wabunge. Kama ada, wanauliza maswali ambayo Mawaziri wanayajibu, wanachangia hoja mbalimbali zinazowasilishwa Bungeni na kwa jumla wana uhuru mpana wa kuzungumza, kwa mujibu wa sheria na kanuni za Bunge.

    Hicho kinachoitwa “kuwaziba mdogo Wabunge” ni tafsiri tu potofu ya mwandishi kuhusu kikao cha Kamati ya CCM ya Bunge, kilichofanyika Dodoma Jumapili Okt. 29, mwaka huu, siku mbili kabla ya Mkutano wa tano wa Bunge, ulioanza Jumanne Okt. 31. Kama kawaida kabla ya mkutano rasmi wa Bunge kuanza, kamati mbalimbali za Bunge, ikiwa ni pamoja na Kamati za Vyama vinavyowakilishwa Bungeni, hukutana kwa nyakati tofauti. Katika kikao hicho Waziri Mkuu Lowassa aliwaeleza Wabunge wa CCM masuala kadhaa, lakini moja lilikuwa ni kuwapa maelezo ya kina kuhusu Serikali inafanya nini kukabiliana na suala la umeme, ili hoja ya aina hiyo ikizuka Bungeni, Wabunge wa CCM waelewe nini kinachotokea. Kwa jumla ni jambo la kawaida na limo katika taratibu za Bunge. Wabunge wa chama fulani hukutana kuwekana sawa au kupata na kuwa na msimamo na uelewa wa pamoja kuhusu masuala fulani fulani yanayoibuka Bungeni.
    …/3
    Katika Bunge la Tanzania, suala hili la Kamati ya Chama ya Bunge na nafasi ya kujadili masuala mbalimbali lipo katika kanuni 83.A na kanuni 84.-(1) na (2), katika kitabu cha Kanuni za Bunge. Kanuni ya 83.A inasema na nanukuu:
    “Wabunge wa kila Chama cha Siasa kinachowakilishwa Bungeni wanaweza kuunda Kamati ya Wabunge wote wa Chama hicho kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na Taratibu za Chama kinachohusika…”. Kanuni ya 84.-(1) inasema: “Kila Kamati iliyoundwa kwa mujibu wa Kanuni ya 83.A, itajiwekea taratibu zake kwa ajili ya kuendesha shughuli zake. (2) Majadiliano yote katika mikutano ya Kamati iliyoundwa kwa mujibu wa kanuni ya 83.A, pamoja na mambo mengine yote yanayohusu Kamati hiyo yatakuwa na hadhi, kinga na nafuu zote zinazotolewa kwa mujibu wa sheria kuhusu majadiliano, kumbukumbu na mambo mengineyo ya Bunge na vikao vyake.

    Na suala hili la Kamati za Chama katika Bunge, kwa Kiingereza “Party Caucus”, lipo katika Bunge la Uingereza na Mabunge ya Jumuiya ya Madola na hata Marekani. Sasa kwa Waziri Mkuu kukutana na Kamati ya CCM ya Bunge na kuzungumzia suala la umeme, nani amezibwa mdomo? Kwa bahati mbaya, Chahali alipata maelezo yake kutoka gazeti moja litolewalo kila siku, lililokikariri kile kilichoitwa “habari za uhakika”. Gazeti hilo lilisema, katika kichwa chake cha habari, “Lowassa awaangukia wabunge CCM Dodoma” na kuweka tafsiri yake kuwa kwa Lowassa kukutana na Wabunge wa CCM na kuzungumzia tatizo la umeme ni “kuwaziba mdomo Wabunge”. Gazeti limepotosha, likamfanya Chahali naye apotoke. Naye, kwa kuwa amepotoka, anapotosha zaidi. Lipo tatizo hili la kupotosha, ama kwa makusudi ama kwa kutojua, linalofanywa na baadhi ya vyombo vya habari nchini, hasa magazeti.

    Kuhusu kile Chahali anachokiita “kuwaumbua watendaji hadharani”, inawezekana mwandishi huyo haelewi anachokisema. Mikutano ya Waziri Mkuu Lowassa hasa huko vijijini inashangiliwa sana na wananchi. Badala ya Waziri Mkuu kuanza kuhutubia, huwa anawaomba wananchi watoe kero zao. Na kero hizo zinajibiwa pale pale na wahusika – kuhusu Mtendaji wa Kijiji anajibu Mtendaji huyo, kuhusu Diwani anajibu Diwani mwenyewe, kuhusu Mkuu wa Wilaya anajibu mwenyewe, na kadhalika. Pale ambako watendaji hao wanafanya kazi zao vizuri na bila ya wasi wasi, huwa wanatoa majibu ya uhakika. Pale ambako kuna ubabaishaji, watendaji wanababaika, hawana majibu ya kweli. Majibu ya ubabaishaji huwa ni sehemu ya ushahidi wa udhaifu kuhusu utendaji wao. Ukipatikana na ushahidi mwingine wa kutosha, na baada ya uchunguzi zaidi, baadaye watendaji hao huwa wanawajibishwa. Hili ni jambo zuri. Sasa utapimaje utendaji wa watendaji hao kama hukushirikisha wananchi waseme kero zao na jinsi wanavyohudumiwa? Je kama mtu anababaika kujibu kwa sababu anashindwa kutekeleza mambo yake vizuri, ndiyo Waziri Mkuu anamuumbua, au mtu huyo anajiumbua mwenyewe? Mfano mzuri ni mtendaji mmoja katika Wilaya ya Same, ambaye alikabidhiwa jukumu la kusimamia ugawaji wa chakula cha njaa kilichotolewa na serikali. Lakini wakati watu wanahitaji chakula, ikachukua zaidi ya mwezi mzima anaendesha semina za
    …/4
    namna ya kugawa chakula. Chakula chenyewe hakijawafikia walengwa. Katika mkutano mmoja wa hadhara, wananchi walisema, tena kwa uchungu mkubwa, hawajakiona chakula cha njaa ambacho serikali imekipeleka. Alipoulizwa mtendaji huyo akasema ni kweli bado chakula kiko makao makuu ya wilaya na hakijasambazwa vijijini kwenye watu wanaotaabika na njaa. Sababu, anasema: “kwanza naendesha semina, bado sijapata magari ya kufikisha huko”!. Huu ulikuwa sehemu ya ushahidi ambao ulipelekea kusimamishwa kazi kwa mtendaji huyo. Hakika utaratibu huu wa kuwawajibisha mara moja watendaji wasiotimiza wajibu wao ipasavyo ni mzuri. Unakwenda sambamba na falsafa ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya!. Hakuna muda wa, kama alivyosema Chahali, “kuitana ofisini na kuongea faragha ki-utu uzima”. Mnaongea nini?

    Na hiyo Chahali anayoiita “kuumbuana” imezaa matunda. Sasa hivi ripoti za Ma-DC na Ma-RC hazina mzaha, huwa zinafanyiwa kazi kweli kweli. Na Waziri Mkuu anapokwenda kwenye ziara, watendaji hawadiriki tena kutaka kumdanganya, kwa sababu wanajua wataulizwa maswali na watatakiwa wawe na majibu sahihi kama inavyopasa.

    Kuhusu elimu, Januari mwaka huu takwimu zilizotolewa zilionyesha kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Shinyanga,Tabora, Singida, Mtwara na Kigoma haikufanya vizuri katika kuwapatia nafasi wanafunzi waliofaulu elimu ya msingi kuingia elimu ya sekondari. Kati ya waliofaulu Desemba mwaka 2005 hata asilimia 50 walishindwa kupata nafasi ya sekondari. Ndipo Waziri Mkuu Lowassa Januari hiyo hiyo alipoagiza kuwa kila mkoa, lazima uwaingize sekondari wanafunzi waliofaulu elimu ya msingi, siyo chini yasilimia 50, kwa kuhakikisha kuwa madarasa yanaongezwa na walimu wanapatikana.

    Katika utekelezaji wa agizo hilo, ilipofika Machi mwaka huu, mkoa wa Dares Salaam, kwa mfano, ambao Desemba ulipeleka wanafunzi asilimia 21.7 tu ya waliofaulu kuingia sekondari, ukawa umepeleka wanafunzi 10,660 zaidi na kufikia kiwango cha asilimia 70.2 ya waliofaulu. Dodoma uliopeleka asilimia 47,8 uliongeza wanafunzi 3,520 na kufikia asilimia 75.2 na Singida uliopeleka asilimia 39.8 uliongeza wanafunzi 4,141 na kufikia asilimia 85.6! Hivyo, kwa takwimu za ile mikoa minane tu iliyokuwa chini, jumla ya wanafunzi 50,715 wameongezeka na kuingia sekondari. Nyongeza hiyo ya wanafunzi, ambao kwa kawaida wangekosa nafasi ya kuingia sekondari, imefanya idadi ya wanafunzi walioingia sekondari katika kipindi cha miezi mitatu tu kutoka asilimia 45.9 ya waliofaulu hadi kufikia asilimia 62.5.! Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 ilisema ifikapo mwaka 2010, asilimia 50 ya watoto wanaofaulu elimu ya msingi lazima waingie sekondari. Lengo hilo, kwa takwimu hizi, kwa hakika, tayari limevukwa, miaka minne kabla ya 2010! Lakini Chahali anadiriki kuhoji, “amri anazotoa (Waziri Mkuu) kwa namna ya zimamoto, zimebadilisha vipi maisha ya Watanzania?”. Ukweli ni kwamba maagizo ya Waziri Mkuu, na siyo “amri za zimamoto”, kama hili la elimu ya sekondari, yamefanikiwa mno. Huo ndiyo ukweli na anayetaka kuthibitisha atathibitisha.
    …/5







    Ndiyo maana inaonekana dhahiri kwamba labda Chahali ana lake jambo. Amekurupuka kulalamika na kutoa maoni yake, bila ya kufanya utafiti na kutafuta
    na kupata takwimu sahihi.Hivyo basi ni dhahiri kuwa maelezo ya Chahali katika safu ya “Habari kutoka Ughaibuni” katika gazeti la KULIKONI la Novemba 3-9 mwaka huu yalikuwa ni maoni tu na siyo habari za kweli na sahihi. Taarifa sahihi zipo na Chahali angeweza kuzipata, kama angetaka, badala ya kutegemea baadhi ya maelezo potofu anayoyasoma kutoka katika baadhi ya magazeti. Sana sana maelezo hayo ya Chahali ni maoni binafsi ambayo, kitaaluma, kama ilikuwa ni lazima kuyachapisha, yalistahili kuwekwa kwenye safu ya “Barua za Wasomaji” badala ya safu ya habari.



    (mwisho)





    Saidi A. Nguba
    Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu
    S.L.P. 3021,
    DAR ES SALAAM

    Barua pepe: [email protected]
    Simu: 0754 388418

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.