13 Nov 2006

KULIKONI UGHAIBUNI-34:


Asalam aleykum,

Waziri Mkuu Tony Blair anatarajiwa kung’atuka mwakani.Ataondoka huku Waingereza wengi wakimwona kama kiongozi ambaye anapaswa kuingia katika vitabu vya historia kwa mambo mbalimbali,mazuri na mabaya.Pengine baya zaidi ni jinsi ambavyo wengi wanamwona kama kibaraka wa George W. Bush.Hata hivyo,wapinzani wa Blair wanakubali bila ubishi kwamba huyu Bwana akipewa fursa ya kujieleza huwa hafanyi makosa.Ukubaliane nae au upingane nae bado atasimamia hoja yake na kuielezea kwa umakini sana kiasi kwamba hata asieafikiana nae anaweza kukubali yaishe kwa kukubaliana kistaarabu kutokubaliana nae.Na kwa kiasi kikubwa ndio siasa za hawa wenzetu zilivyo.Hoja inawekwa mezani,inajadiliwa kiutu-uzima,mwafaka ukipatikana inakuwa poa.Mwafaka usipopatikana watu wanakubaliana kwamba hawajaafikiana na kutafuta namna nyingine ya kutatua linalojadiliwa.Mambo ya kuzibana mdomo ni adimu sana katika siasa za hapa.

Nimesoma gazeti moja la huko nyumbani lililobeba habari kwamba Waziri Mkuu Edward Lowassa anajaribu kuwaziba midomo wabunge wa CCM wasilishupalie suala la mgao wa umeme kwenye kikao cha bunge.Naomba kwanza nimjadili Mheshimiwa Lowassa kwa marefu na mapana.Moja ya mambo ambayo yanawafanya baadhi yetu tusimwelewe Waziri Mkuu wetu ni tabia yake ya kuwaumbua watendaji wake hadharani.Wapo wanaoona vitendo hivyo kama namna ya kutafuta umaarufu kuliko kurekebisha matatizo.Kuna ugumu gani kwa Lowassa kuwaita ofisini kwake au kuwapigia simu au hata kuwaandikia barua kuwaonya watendaji anaowaona wanakwenda ndivyo sivyo badala ya kutumia mikutano ya hadhara kuwaumbua?Sidhani kama yeye atafurahi iwapo atateleza na bosi wake JK akaamua kumshambulia kwenye hotuba zake za kila mwisho wa mwezi.Ukweli ni kwamba wataongea faragha kiutu-uzima na kupeana maelekezo ambayo mwisho wa yote ni kwa manufaa ya Taifa zima.Ndio maana (kama lilivyoripoti gazeti la Mwananchi) JK aliwahi kumpigia simu Lowassa saa saba usiku kumweleza masononeko yake kuhusu suala la umeme,badala ya kufanya hivyo kwenye mkutano wa hadhara.Pengine Lowassa anapaswa kuelewa kwamba wanachohitaji wananchi sio kuwalambisha peremende kwa kuwaumbua viongozi hao (ambao ni sehemu ya serikali anayoongoza yeye kama Waziri Mkuu) bali kuwapatia tiba ya matatizo yao lukuki ambayo yanaelekea kutokuwa na mwisho.Nakumbuka wakati flani aliomba aletewe orodha ya wadaiwa sugu wa maji ili awashughulikie.Sasa kwanini hakutumia njia hiyo alipokuwa waziri kwenye wizara hiyo?Au haoni kuwa kwa kufanya hivyo alikuwa akiuambia umma kuwa wenye mamlaka ya kukusanya madeni ya maji wameshindwa kutekeleza majukumu yao hadi inambidi yeye kama Waziri Mkuu kuingilia kati?Na pengine awaambie Watanzania kuwa hizo amri zake anazotoa kwa namna ya zimamoto zimebadilisha vipi maisha ya Watanzania,kwa mfano agizo lake kwamba kila mwanafunzi aliefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana awe ameingia kidato cha kwanza.Wapo walioanza kumfananisha Lowassa na marehemu Sokoine,lakini nadhani Sokoine alikuwa mwingi wa vitendo kuliko maneno.

Ila kinachonifanya nisimwelewe huyu bwana ni hii tabia yake ya kuwaziba mdomo wabunge wa CCM ambayo ni namna ya kistaarabu ya kulea uzembe na maovu yanayowaumiza Watanzania.Kwenye kikao cha Bunge la bajeti alijitokeza kuwa mwokozi wa mawaziri waliokaliwa kooni na wabunge,na sio mwokozi kwa kutoa ufumbuzi wa yaliyokuwa yakiwakera wabunge bali kuwalinda wasiumbuke.Sasa iweje yeye awe anapenda kuwaumbua baadhi ya watendaji wa ngazi za chini lakini anakuwa mwepesi kuwatetea mawaziri wanaochemsha kwenye utendaji wao?Hivi vikao vya kuwekana sawa kati ya Lowassa na wabunge wa CCM ni kwa manufaa ya nani?Wabunge wanaingia bungeni kuwakilisha mamilioni ya Watanzania ambao haiwezekani kwao kuingia kwenye jengo hilo kwa mkupuo kuihoji serikali waliyoiweka madarakani.Kuwaziba midomo wabunge ni sawa kabisa na kuwaziba midomo wananchi,na hilo linapaswa kukemewa kwa nguvu zote.

Niliandika hivi karibuni kuwa Waziri Karamagi ana wakati mwepesi katika kujibu maswali magumu yanayohusiana na tatizo la umeme sambamba na sakata la kampuni ya Richmond.Jibu jepesi nililotabiri na ambalo inaelekea ndio atakalokuwa akilitumia kila atapohojiwa ni kwamba yeye ndiyo kwanza ameingia wizarani hapo na hakuwapo wakati mikataba ya kampuni hiyo ikisainiwa.Hilo ni jibu la kisiasa na linalengwa kukwepa kuwajibika kwa wananchi.Ningeweza kumwelewa Karamagi kama Waziri Msabaha angekuwa amehamishiwa wizara ambayo iko nchi kama Irak ambako mawasiliano ya simu ni ya kubahatisha na ambako sidhani kama mawaziri wa “serikali” ya nchi hiyo wanapata muda wa kubadilishana mawazo nyakati za jioni au wikiendi.Msabaha yuko Dar es Salaam,simu yake inafanya kazi,na ni suala dogo tu kwa Karamagi kumdadisi mwenzie kwamba hivi haya ambo yakoje?Na kama kweli anataka Watanzania wamuelewe vizuri ni lazima awe na majibu ya wakati uliopo na sio kutupiana mpira na mtu ambaye kwa sasa sio mhusika katika wizara hiyo.Kwa kifupi,yeye ndiye mwenye dhamana ya kutujulisha ni lini tatizo la mgao wa umeme litaisha (au pengine awasiliane na viongozi wa dini kufahamu ni lini “mitihani ya Mungu” itamalizika).

Turudi kwa Lowassa.Ni vema akafahamu kuwa kama yeye hahitaji mjadala kuhusu suala la mgao wa umeme,waliomweka madarakani (yaani Watanzania) wana kiu kubwa mno ya kufahamu kulikoni.Anachoogopa ni nini kuhusu wabunge kujadili suala hilo?Kuna nini ambacho hataki Watanzania wakifahamu?Pamoja na kuwa msemaji sana tangu aingie madarakani hajaweza kabisa kugusiana utata uliojitokeza kuhusu kampuni ya Richmond.Kwanini sasa asiwaache Watanzania kupitia kwa wabunge wao wajadili kwa undani suala hilo na kufahamu nani aliyetufikisha hapa na pengine cha muhimu zaidi ni lini nchi yetu itarejea kwenye kanuni za jiografia za mchana kuwa mchana na usiku kuwa usiku badala ya sasa ambapo inaelekea usiku ni mrefu kuliko mchana kutokana na “giza la kulazimisha” linalosababishwa na mgao wa umeme.Tunafahamu kuwa mgao huu unawaumiza wale wasio na uwezo wa kununua jenereta na sio vigogo ambao hawajui hata bei ya mafuta ya taa kwa vile muda wote umeme upo maofisini na majumbani mwao.Pia ni dhahiri kuwa baadhi ya watu wananufaika na mgao huu hasa wale wenye biashara ya majenereta,na si ajabu hili wazo la kununua mitambo ya umeme kutoka nje ikawa kwenye mlolongo huohuo.Kama kweli serikali ilikuwa na nia ya kupunguza makali ya mgao wa umeme kwa kununua majenereta basi ingeweza kuomba msaada kwa balozi za nchi kama Japan,Marekani,Uingereza,nk kuwasaidia kupata kampuni ambazo naamini ndani ya mwezi mmoja zingekuwa zimetekeleza walichoagizwa.Tumeanza kusikia tetesi kwamba iwapo serikali itavunja mkataba na kampuni ya Richmond,inaweza kujikuta inatakiwa kulipa fidia kubwa.Yaleyale ya IPTL.Hivi hawa jamaa wa Richmond wanatoa msaada wa bure au wanatakiwa kutekeleza mkataba halali wa kibiashara ambao unawalazimisha kutekeleza matakwa ya mteja (serikali) ndani ya muda maalum badala ya kuleta mitambo kwa mafungu (na hatuna uhakika lini mitambo hiyo itaanza kazi,kama kweli itaweza kufanya kazi “kutokana na joto la Tanzania”,na iwapo itakongoroka basi wahandisi kutoka Marekani hawatakuja kwa mafungu kama mitambo hiyo).

Mwisho,nawaomba sana wawakilishi wetu huko bungeni wasikubali kuwasaliti Watanzania wanaowawakilisha.Hakuna dhambi kwa kukubaliana na Lowassa kuwa hawataibua hoja hiyo lakini wakamgeuka na kuiibua wakati wa kikao cha bunge.Huko sio kukosa nidhamu bali ndio kuwajibika.Wabunge wetu wafahamu kuwa siku zote serikali itatetea matendo yake hata yakiwa mabaya,na ni jukumu la wabunge kuikosoa na kuiwajibisha pale itapolazimika.Wabunge msituangushe safari hii,mnapaswa kuikalia kooni serikali bila uoga ili muwasaidie mnaowawakilisha angalau wafahamu wahusika wakuu katika hili sakata la mgao wa umeme na mikataba ya utata.Na kwa Waziri Mkuu,wito wangu kwako ni kukuomba uwaruhusu Watanzania kupitia kwa wawakilishi wao watumie haki yao ya kikatiba kufahamu ni lini hiyo ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania itatimia kwa kuanzia na suala la umeme.

Alamsiki

http://chahali.blogspot.com
http://chahali.livejournal.com

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.