17 Jan 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-42

Asalam aleykum,

Natumaini wengi wenu mko katika maandalizi ya sikukuu ya Krismasi.Uzuri wa Bongo ni kwamba sikukuu za kidini zinakuwa kama za kitaifa na ndio maana inapokuwa siku kama Idd utaona Wakristo wakijimwayamwaya sambamba na Waislam kama ambavyo kwa wakati huu Waislam nao wanajumuika na wenzao Wakristo kwa maandalizi ya Krismasi.Na ndivyo inavyopaswa kuwa na kudumishwa milele.Sikukuu ni furaha na furaha hiyo inapaswa kuwa kwa wote bila kujali dini zao.

Hapa maandalizi ya Krismasi huanza takriban miezi miwili kabla ya sikukuu yenyewe.Usishangae kukuta duka flani linatangaza “seli” ya Krismas wakati ndio kwanza mwezi Oktoba umeanza.Katika makala yangu flani huko nyuma niliwahi kuzungumzia suala la dini hapa Uingereza na nikatoa mifano ya jinsi majengo yalikuwa yakitumika kama makanisa yanavyoishia kuwa kumbi za starehe baada ya makanisa hayo kuishiwa na waumini.Sasa hii Krismasi inayoanza Oktoba kwa kiasi flani ni kama haina uhusiano na ile siku alozaliwa Yesu Kristo.Hii ni Krismasi inayohusiana na mambo ya fedha.Huu ni msimu wa kutengeneza faida,na hawa jamaa wanajua sana kuwavutia wateja hasa kama kuna tukio au siku flani maalumu.Hapa kuna namna mbili ya kutengeneza faida.Kwanza kuna wale ambao wanatoa ofa za dhati,yaani kama kitu ambacho bei yake ya kawaida ni pauni 100 basi kwenye seli kinashuka bei hadi pauni 50.Lakini wapo wale “wasanii” ambao ofa zao ni kama za kukupa ahueni muda huu lakini baadae unajikuta unalipa fedha sawa na bei ile ya siku zote.Yaani unaweza kukuta kitu cha pauni 500 ambacho unaweza kukinunua bila kutoa hata senti kwa miezi 12 halafu baada ya hapo unaanza kulipa.Na pengine ukaishia kulipa zaidi ya hiyo pauni 500.Ila kwa ujumla seli nyingi za hapa ni za dhati na ndio maana mitaa yenye maduka inafurika sana kipindi hiki.

Uingereza ni nchi ya Kikristo,na “mkuu” wa nchi,yaani Malkia Elizabeth wa Pili ndiye “Mlinzi wa Imani” (defender of the faith) wa Church of England.Lakini ni ukweli usiofichika kuwa mahudhurio ya hawa Waingereza huko makanisani ni hafifu sana,na kuna idadi kubwa tu ya watu ambao wanajitambulisha kuwa hawaamini katika mambo ya dini japo wakati huu wa Krismasi wako bize kununua maua na kadi za sikukuu hiyo.Kwa namna flani,Krismasi kwa hapa ni siku ya familia,siku ambayo watu wanajumuika pamoja na kula mlo unaochagizwa na nyama ya bata mzinga.Huu ndio wakati ambao baadhi ya vibabu na vibibi “vilivyosahaulika” kwenye nyumba za kulelea wazee (care/residential homes) vinapata wasaa wa kutembelewa na watoto na wajukuu wao.Usishangae kusikia kuwa kuna watu wanajifanya wako bize mwaka mzima na wakati pekee wanaopata kuwatembelea wazazi wao ni huu wa Krismasi pekee.

Ila pamoja na kinachoweza kuonekana kama “unafiki” kwa taifa linalojitambulisha kuwa linafuata utamaduni wa Kikristo lakini baadhi ya makanisa yake yanaishia kugeuzwa kuwa sehemu za biashara kutokana na uhaba wa waumini,ukweli unabaki kuwa watu ni wakweli.Ni hivi,kuna umuhimu gani wa kwenda kanisani kila jumapili au msikitini kila ijumaa huku mtu anaendeleza zinaa,anakula rushwa kama hana akili nzuri na pengine anaiamini bia kuliko muumba wake?Na hapa ndipo napopenyeza salamu zangu za Krismasi kwa wasomaji wapendwa wa makala hii na gazeti hili kwa ujumla.Makanisa na misikiti yetu inafurika zinapofika siku za ibada,lakini idadi inakuwa kubwa maradufu siku ya sikukuu kama Krismasi au Idd.Tuambiane ukweli,hivi tunapokwenda kwenye nyumba hizo za ibada tunafanya hivyo kwa vile ni wajibu wetu kama waumini au ni kwa sababu tu ya “mazowea ni kama desturi” ?Mie nadhani waumini wa dhati ni wengi kuliko wale wa “bora liende” na hawa ndio naotaka “kuwashikia bango.”

Nimeshawahi kutamka huko nyuma kuwa japo nafanya sala binafsi kila siku bado mahudhurio yangu kanisani sio mazuri,na sijisifu kuhusu hilo hasa kwa vile ninatoka katika familia inayoshika sana dini.Najiona kama “kondoo ninayehitaji kurejeshwa zizini” na naamini nitajirekebisha hivi karibuni. “Ugomvi” wangu uko kwa wale ambao wanashika ibada kwa kuhudhuria nyumba za ibada kama ratiba inayowataka lakini maisha yao nje ya nyumba hizo za ibada yametawaliwa na yale yasiyompendeza Mungu.Unajua ulaji rushwa ni sawa kabisa na wizi,na dini inakataza kuiba.Kwa maana hiyo muumini ambaye hakosekani kanisani au msikitini lakini kazini kwake ni mla rushwa alobobea huyo afahamu kuwa anajiandalia tu kuni za kumuunguza motoni.Dini zote zinasisitiza upendo,na ukiwa na upendo huwezi kuwa “mlafi” wa kuminya misaada inayotolewa na wafadhili kwa ajili ya wenye mahitaji na badala yake ukaitumia kwa manufaa yako binafsi.Ukiwa na upendo wa dhati kama dini zinavyotutaka tuwe huwezi kuelekeza nguvu kwenye nyumba ndogo badala ya familia yako.Na kama unafuata dini ya dhati huwezi kuendelea kumwombea mwenzio mabaya badala ya mafanikio hasa ikizingatiwa kuwa mafanikio ya huyo unayemwombea mabaya yanaweza kuja kuwa mafanikio yako siku zijazo.

Wakati nawatakia wasomaji wangu salamu za heri na Baraka ya sikukuu ya Krismasi nawajibika kupeleka salamu kali kwa wezi,majambazi,wala rushwa,wabadhirifu,waendekeza zinaa,matapeli,mangimeza na wale wasiojali hatma ya vizazi vijavyo kwa vile wanaendekeza maslahi yao binafsi.Pia salamu hizo kali zinaelekezwa pia kwa “mumiani” wanaoingiza na kuuza unga ambao unaishia kuwaua Watanzania wenzao (wazungu wa unga wanavunja waziwazi amri inayosema “usiue”),bila kuwasahau wale ambao aya flani katika Biblia inawakumbusha kwamba “wajikwezao watashushwa na wajishua watakwezwa” na wanafiki wengine ambao wanachoongea hadharani ni tofauti kabisa na wanayoyafanya kwa siri.

Naamini kabisa kuwa kwa vile tofauti na hapa ambapo watu wengi hawana habari na mambo ya dini (ukiondoa sie wachache ambao mara nyingi tunaogopa kusema “haki ya Mungu” au “Masafi ya Mtume” huku kinachosemwa ni cha uongo),huko nyumbani suala la imani bado ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku na watu wengi wanatemtegemea Mungu katika kila wanalolifanya,na kwa maana hiyo imani katika dini inaweza kabisa kusaidia kuwarejesha “kondoo waliopotea.” Lakini pia ni muhimu kwa viongozi wetu wa dini kuishi kama Maandiko Matakatifu yanavyosema na kuachana na maneno kama “fuata nachosema usijali nachofanya.”

Natumaini ujumbe umefika,atakayenuna shauri yake lakini huo ndio ukweli.Kwa wanaofuata dini kwa dhati,ombi langu ni kuendelea na maombi kwa wale ambao bado hawajakaa kwenye mstari.Kwa wale ambao wanafuata dini wakiwa makanisani au misikitini lakini wakiwa maofisini au mitaani wanakuwa waumini wa shetani nawakumbusha kuwa huko mbele kuna moto wa milele,na njia pekee ya kuukwepa ni kutenda yale yanayompendeza Mola wetu pamoja na kuwapenda wenzetu kama tunavyojipenda wenyewe.Penye upendo hakuna uzembe,majungu,fitna,rushwa,ubabaishaji,uzinzi,uuzaji na utumiaji wa unga,ulevi na madhambi mengine.

Heri ya Krismasi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.