7 Apr 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-57

Asalam aleykum,

Wakati naelekea mtamboni kuandaa makala hii,hatimaye Rais wa Iran ametangaza kuwaachia huru wanajeshi 15 wa Uingereza ambao walikuwa wakishikiliwa mateka na jeshi la Iran.Mgogoro huu ulikuwa umetawala mno kwenye vyombo vya habari vya hapa Uingereza na nchi nyingine za Magharibi.Kwa namna mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni vigumu kutabiri nini kingefuatia iwapo Iran ingeendelea na msimamo wake wa kuwashikilia wanajeshi hao.Tayari baadhi za sauti zenye msimamo mkali hapa UK zilishaanza kumtaka Waziri Mkuu Tony Blair “kufanya kitu flani” kuhakikisha kuwa mateka hao wanaachiwa.Nadhani akilini mwao,watu hao walikuwa wakijaribu kuchochea matumizi ya nguvu za kijeshi ili kutatua tatizo hilo.Hata hivyo,kiongozi yoyote mwenye busara angelazimika kufikiria mara mbilimbili kabla ya kuchukua uamuzi mzito kama huo hasa ikizingatiwa kuwa Iran “imekamilika” kijeshi bila kusahau karata yake turufu ya mafuta.Hadi muda huu haijafahamika ni lini hasa mateka hao watarejea hapa lakini lililo wazi ni kuwa wameachiwa kwa kile Rais wa Iran alichokiita “zawadi kwa watu wa Uingereza.”Pengine alikuwa anamaanisha zawadi ya Pasaka.

Tukiachana na hilo,ningependa kuungana mkono na wito uliotolewa na mwanasiasa mkongwe,mbunge wa Mtera na Makamu Mwenyekiti wa CCM,John Malecela,ambaye amenukuliwa hivi karibuni akiomba ifanyike semina kwa wabunge kuhusu ugonjwa wa homa ya bonde la ufa (Rift Valley Fever-RVF).Naamini madhumuni ya mkongwe huyo wa siasa ni katika jitihada ya kulipa kipaumbele janga hilo katika namna ambayo Taifa zima kwa kupitia wawakilishi wao Bungeni litawekwa katika tahadhari ya kupambana na ugonjwa huo.Nadhani licha ya semina kwa wabunge,jitihada za haraka zinahitajika kuuelewesha zaidi umma wa Watanzania kuhusu namna ya kuukabili ugonjwa huo.Japo si ugonjwa mpya lakini hii ni mara ya kwanza ambapo unaelekea kuchukua taswira ya kitaifa.Inatupasa kukumbuka kuwa hadi muda huu bado gonjwa jingine tishio la kipindupindu linaendelea kutesa katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu.Haimaanishi kuwa serikali haifanyi jitihada zinazopaswa bali sote tunafahamu kuwa ni rahisi kukumbwa na ugonjwa kuliko kuutokomeza.Kwa mantiki hiyo,kinga dhidi ya RVF itakuwa ni jambo la muhimu zaidi kuliko kuanza kuhangaika na tiba pindi utakapotapakaa.

Labda la kukumbushana hapa ni ile tabia ya semina juu ya semina kujadili kitu flani.Yayumkinika kusema kwamba laiti semina lukuki dhidi ya majanga kama ukimwi zingeishia kutafsiriwa kwa vitendo basi tungeweza kuwa tumepiga hatua kubwa zaidi ya hapa tulipo sasa.Hivyohivyo,kwenye maeneo kama vita dhidi ya umasikini na tatizo sugu la rushwa.Semina ni kitu kizuri kwa vile lengo ni kuelimishana kuhusu suala husika.Lakini semina ambazo zinaishia kwenye posho tu ilhali fedha hizohizo za posho zingeweza kuelekezwa kwenye utatuzi wa matatizo yanayojadiliwa katika semina hizo ni jambo ambalo linapaswa kuepukwa.


Jambo jingine nalopenda kuligusia ni kipigo cha Taifa Stars huko Senegal.Aliyekuwa akijidanganya kuwa tungeweza kuibika na ushindi kirahisi katika mechi hiyo atakuwa haijui vizuri dunia ya soka.Yayumkinika kusema kipigo cha mabao manne kilikuwa ni halali yetu japo hakuna mpenda soka ambaye yuko tayari kuridhika na kipigo.Tulitegemea nini tulipopambana na timu ambayo wachezaji wake wote 11 wanacheza soka la kulipwa nchi za nje.Na hapo tunawazungumzia watu kama Elhadj Diouf ambao wana majina makubwa hadi kwenye ligi ya hapa Uingereza.Senegal ni moja ya timu zenye hadhi kubwa ya soka duniani na ndio maana timu za taifa za nchi zinazotamba kwenye dunia ya soka hupendelea kuomba mechi za majaribio na Simba hao wa Teranga.Wenzetu hawahitaji ziara ya sehemu kama Brazil kujiandaa kwa mechi zao kwa vile mechi ngumu katika klabu wanazochezea wanasoka wao ni majaribio tosha ya kukabili timu kama Taifa Stars.

La msingi hapa ni kujiandaa kwa mechi ijayo.Ni mechi ngumu kweli,na sote tunapaswa kutambua ukweli huo.Ni rahisi kuishi kwa matumaini kuliko kuikabili hali halisi.Kwa namna hiyo hiyo,ni rahisi kuamini kuwa tunaweza kuwatoa Wasenegali hao watapokuja kwenye mechi ya marudiano Dar,lakini kuwa na imani pekee hakutoshi.Kunahitajika maandalizi ya hali ya juu.Nadhani kwa mtizamo wangu,zile fedha zinazotafutwa kwa ujio wa ziara ya timu ya Real Madrid zinaweza kuelekezwa kwenye maandalizi ya mechi dhidhi ya Senegal.Na pengine kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaua ndege wawili kwa jiwe moja.Yayumikika kusema kuwa timu ya taifa ya Senegal ina umaarufu unaokaribiana na Real Madrid.Na kama suala ni kulifanya tukio la uzinduzi wa uwanja mpya wa taifa kuwa la kihistoria basi hakutakuwa na historia au zawadi kubwa kama kuufungua kwa mechi ya marudiano na Senegal na kuwafungasha virago siku hiyohiyo.Naamini kabisa kuwa pesa ambazo zinatafutwa kuwagharamia mastaa wa Real Madrid zinaweza kuwa changamoto tosha kwa wachezaji wetu iwapo kwa mfano wataahidiwa hata nusu ya posho ya siku ambayo taifa letu litawajibika kuwalipa “wageni wetu kutoka Madrid.”Unadhani kama wanasoka wetu wataahidi shilingi milioni 1 kila mmoja iwapo wataibuka na ushindi kwenye mechi hiyo,hawatajituma katika namna ya “kuua mtu”?

Kingine ni pongezi zangu kwa kituo cha redio cha Clouds FM kwa kuanzisha huduma ya matangazo yake kwenye mtandao.Nilijiskia raha isiyoelezeka wakati nafuatilia “laivu” kwenye mtandao uzinduzi wa albamu ya “ndege tunduni” ya Juma Nature na wenzake hapo Diamond Jubilee.Sijui kama wenyewe walikuwa wanafahamu kuwa uzinduzi huo ulikuwa ukisikika sehemu mbalimbali duniani kwa kutumia teknolojia ya internet.Kwa hilo,nawapongeza sana Joseph Kusaga na timu yake nzima ya Clouds FM.Kwa hakika wamefungua njia mpya katika sekta ya habari.

Hata hivyo,kwa vile sasa matangazo ya stesheni hiyo yanasikika ulimwenguni kote ni muhimu kwao kuhakikisha kuwa utendaji wao unakuwa na hadhi ya kimataifa.Wikiendi iliyopita nilikuwa nasikia kipindi flani (sikijui jina lake) ambacho kilirushwa hewani alfajiri kwa saa za hapa na kilipitia habari za kimataifa.Naomba niseme kwamba mtangazaji (wa kiume) aliyekuwa akiendesha kipindi hicho alikuwa “anajiumauma” sana kana kwamba habari hizo zinatoka kichwani mwake badala ya kuzisoma mahala flani.Lengo langu sio kumuumbua bali nachofanya ni sawa na changamoto kwake na kwa watangazaji wengine hususan katika kipindi hiki ambacho wasikilizaji wao wako zaidi ya mipaka ya Tanzania.Na hilo halimaanishi kuwa “kulipua” matangazo yaliyo ndani ya mipaka ya nchi yetu ni suala linalokubalika.Raha ya kusikiliza habari ni pamoja na umakini wa mtangazaji.

Mwisho nitoe pongezi kwa “mdau” mmoja mwenye blogu ya haki-hakingowi.bogspot.com.Blogu yake ina mkusanyiko wapicha kutoka sehemu mbalimbali hasa za huko nyumbani.Na ukiwa huku ughaibuni,kila picha ya nyumbani inaleta kumbukumbu flani za kuvutia.Kazi anayofanya ni ya kuvutia hasa ikizingatiwa kuwa inahitaji jitihada flani kutumia muda binafsi kwa ajili tu ya kuwafurahisha watu wengine.Napenda pia kutumia fursa hii kutoa changamoto kwa watu wa fani mbalimbali kuanzisha blogu zao.Ni eneo ambalo linapanuka kwa kasi sana hasa kwa vile linafanikiwa kuwaunganisha watu walio sehemu mbalimbali duniani pasipo vikwazo vilivyozoeleka katika vyombo vya kawaida vya habari.

Pasaka njema.

3 comments:

 1. Yesss Ahmadinejad nadhani ni aina ya kiongozi anayehitajika katika ulimwengu huu wa kibabe ambapo kila mtu anataka ajionyeshe mbabe na anataka anyakue cha mwingine Ahmadinejad tunahitaji kama yeye na washikaji zake kina Hugo Chavez, Luda Da Silva, na wengineo huraa, Bush na Blair wanaboa sana wanarutubisha uranium halafu wanakataa wengine wasirutubishe ni ujinga.

  Kuhusu hiyo semina ya mzee Malechela anayopendekeza ni michosho tu kwani watatumia mamilioni ya fedha za walipa kodi kushibisha matumbo na bado RVF itaendelea kutesa hivyo cha maana kufanya ni kuzitumbukiza pesa zote kudhibiti RVF.

  Anyway mambo vipi habari za siku tele nimefurahi sana kukupata mzee, maana ni miaka mingi tangu tupoteane pale Mlimani. Vipi Sospeter unawasiliana naye, Gheto na washikaji wengine vipi???

  ReplyDelete
 2. ah mkuu heshimaa yakooo sanaa..
  mbona kimyaa snaaaa....
  nafanya mpango nikuweke kwenye
  front page yangu soon..
  sasa fanya mambo ya ku update bloh yetu hiyoo
  kila mara...
  mimi nakuhakikishia ntaitangaza kwa
  nguvu zangu zotee mpaka kieleweke..
  wakatabahu

  haki-hakingowi.blogspot.com

  ReplyDelete
 3. Unaongelea ya Rift Valey Fever mapema hivi? tunashangaa au wewe ndiyo umekuja nayo? Maana zamani haikuwepo!
  Karibu na makala zako, ujue wanablogu sio wasoma makala ndefu kwa jinsi technologia yetu ilivyo, tunaogopa kukikodolea macho muda mrefu hiki kioo kinachotoa maandishi na zile picha...
  Karibu

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube